Moja ya mambo yanayosababisha mrundikano mkubwa wa mahabusu magerezani, ni tatizo la watu kushitakiwa mahakamani halafu wanakosa dhamana au kushindwa kutimiza masharti magumu.

Tumesikia mara kadhaa kutoka maeneo tofauti nchini, mahabusu wakigoma kushuka kutoka kwenye magari au mabasi ya Jeshi la Magereza wanapofikishwa mahakamani, na pia kuna wengine hugoma hata kula wakilalamikia upelelezi wa kesi zao kutokamilika kwa muda mrefu.

Wapo wanaolalamika kwamba wamekaa mahabusu kwa miaka mitatu, minne, mitano, sita au zaidi huku kila wanapokwenda mahakamani polisi wanazidi kudai kuwa “upelelezi wa kesi haujakamilika”.

Sitetei uhalifu wala kulishutumu Jeshi la Polisi au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kukamata, kuhoji na kuwafungulia kesi watuhumiwa wa makosa mbalimbali kwa niaba ya Jamhuri. Kazi zinafanywa na vyombo hivyo vya dola kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi hii.

Pamoja na ukweli huo, bado sikubaliani kwa namna zote na hatua ya Polisi na Takukuru ya kuwashitaki watu mahakamani wakati upelelezi wa tuhuma dhidi yao bado haujakamilika.

Ni ajabu kwa mtu kushitakiwa wakati ndiyo kwanza amepata mtoto juzi, halafu kesi hiyo ikadumu hadi mtoto wake anaingia darasa la kwanza, akafika hadi darasa la saba huku shauri hilo likiwa bado linaendelea kunguruma mahakamani.

Mtoto huyo ananyonya hadi anaachishwa ziwa la mama yake, anaanza shule ya chekechea na kuhitimu, anaingia darasa la kwanza au la pili huku upelelezi wa kesi ya baba yake bado haujakamilika na haielezwi utakamilika baada ya miezi au miaka mingapi!

Sielewi kinachosababisha watu kushitakiwa mahakamani wakati bado upelelezi wa kesi zao haujakamilika katika upande wa kwanza. Pia ninashangazwa na udhaifu mkubwa wa Polisi na Takukuru kuchukua miaka mingi kufanya uchunguzi wa tuhuma ambazo kuna nyingine hata sungusungu wasingechukua hata mwezi mmoja kuzichunguza.

Fikiria, kwa mfano, kwamba mtu anaua kisha anakamatwa katika eneo lilelile alipofanyia mauaji akiwa na zana zake zote, na pia kuna wengine hujisalimisha katika vituo vya polisi. Lakini cha ajabu ni kuona kesi zao nazo zikichukua miaka mingi kwa sababu “upepelezi bado haujakamilika!”

Mtu alikamatwa katika eneo la tukio akiwa na kisu mkononi alichotumia kufanyia mauaji, alikutwa na damu ya marehemu mikononi hadi kwenye nguo alizovaa wakati akitekeleza unyama huo, ikathibitishwa kitaalamu na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutumia vipimo vya kutambua vinasaba (DNA), lakini anapopelekwa mahakamani uchunguzi wa kesi yake unachukua miaka saba kukamilika ili mashitaka hayo yaanze kusikilizwa.

Mbali na hao, wapo watuhumiwa wanaofanya mauaji mbele ya halaiki kama sehemu za baa, barabarani au mahali pengine na kukamatwa palepale na wananchi.

Kutoka hapo hupelekwa na kukabidhiwa moja kwa moja mikononi mwa polisi na mashahidi wote huandikisha maelezo wakianzia majina yao kamili, jinsi, umri, makazi, namba za simu na kadhalika; halafu huwaongoza askari eneo la tukio ili kuchukua ushahidi mwingine unaotakiwa kwa mujibu wa sheria za uchunguzi wa makosa ya jinai.

Pamoja na kufanya hayo yote, ajabu ni pale kesi hizo zinapopelekwa mahakamani inaanza danadana ileile ya kila mwezi kwa miaka mingi kuwa “upelelezi bado haujakamilika”.

Mbali na udhaifu unaofanywa na Polisi, Takukuru nao katika upande wao wameathiriwa na tatizo hilo hilo. Zipo kesi nyingi zinazodumu miaka mingi kukamilika upelelezi, ilhali kuna mwingine unakuwa wazi hata kwa mtoto wa chekechea.

Mathalani, mtuhumiwa aliyetoa rushwa anaweza kukamatwa katika kile kinachoitwa “ready handed” na mbele ya ushahidi uliokamilika, lakini cha ajabu Takukuru wakimfungulia kesi mahakamani nao huanza upelelezi usiokwisha!

Hali hiyo husababisha baadhi ya mahakimu kutumia sheria zilizopo kwenye vitabu vyao kuzifuta, lakini inaweza kuchukua miaka mingi kama nilivyobainisha mapema.

Nimewahi kuandika katika moja ya makala zangu huko nyuma kuwa mchezo huu wa kuwakamata watu, kuwadhalilisha mbele ya halaiki, kuwaweka mahabusu, kuwapotezea muda na kushindwa kuwafikisha mahakamani ni utendaji dhaifu na ni kushimdwa kazi kwa vyombo vya dola.

Siamini kama Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema, au Mkurugenzi Mtendaji wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, ndiyo wazembe kiasi hicho au wanafurahishwa na hali hiyo. Sikubaliani kabisa na utetezi eti kwamba inawezekana hawajui chochote kuhusu hali hii.

Endapo kweli hawafahamu kitu chochote, basi ni tatizo jingine kubwa katika taasisi hizo za dola, lakini pia inawezekana udhaifu ukawa katika Idara za Upelelezi na hivyo uozo wote uliopo ndani ya Polisi na Takukuru unasababishwa na ofisi hizo.

Lakini hata ikiwa namna gani, ukweli bado unabaki palepale na vilevile kuwa vyombo hivyo vya dola katika ujumla wake ni dhaifu sana, jambo ambalo ni hatari kwa sababu vimepewa madaraka yote ya kuzuia, kupambana na kudhibiti uhalifu wa jinai kwa niaba ya Serikali.

Sioni sababu yoyote ya msingi kwa Polisi au Takukuru kutokamilisha upelelezi hadi wa kesi ambazo hata mtoto wa shule ya msingi angeweza kuutolea jawabu katika kipindi cha miezi miwili tu.

Kinachoudhi zaidi ni kuona kwamba hata matukio ambayo watuhumiwa hukamatwa wakiwa katika eneo la uhalifu, wale ambao pia ushahidi dhidi yao hupatikana palepale unakuta nao upelelezi wa kesi zao unakuwa “bado haujakamilika”.

Hapa ndipo ninapojiuliza kama kuna haja ya vyombo hivi vya dola kuendelea kuheshimiwa. Hali hii inakuja kwa sababu hakuna ubishi kwamba vyenyewe vimeshinhdwa kuthibitisha uhalali wake, badala yake siku zote vinaonyesha kuwa vimelemewa na shughuli zake na kusababisha watu wengi kuonewa, kupotezewa muda, kuporwa haki zao na kuteswa kwa miaka mingi mahabusu.

Ili hali hii isiendelee, nadhani inabidi sheria zote zinazohusu upelelezi wa makosa ya jinai na hatimaye mashitaka dhidi ya watu ziangaliwe upya na kwa makini, zichambuliwe kwa ujuzi na utaalamu wa hali ya juu kuliko mwanzo, kisha zirekebishwe ili zifanane au zikidhi matakwa na mahitaji yote yaliyopo hivi sasa.

Ni vizuri sasa zikisema kuwa hakuna mtuhumiwa anayeweza kupelekwa mahakamani au kuwekwa mahabusu kama upelelezi wa shauri lake haujakamilika.

Vinginevyo Polisi na Takukuru wataendelea kukamata kwa visasi, uonevu na kukomoa watu kwa vile wanajua hakuna sheria yoyote inayowabana – ama wao wenyewe au taasisi zao – kutokana na uzembe wanaofanya kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibarika Afrika.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0762 633 244 na 0719 822 344

1797 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!