De geaNi mkono wa kwa heri kila kona; huku tunaagana na Mart Nooij kule katika Jiji la Manchester, ambalo linakuwa na anga nyekundu mara bluu, kuna kuagana na David De Gea.
Presha imekuwa kubwa na haizuiliki tena watu kurudi katika asili yao. Wahispania wamekuwa wakibeba makombe katika timu ya Taifa kwa kutumia asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza ligi ya ndani; hili linafahamika na kila mtu pale kwao kuanzia kwa Perez wa Madrid, mawakala wa wachezaji wa Kihispania na hata mashabiki.


Mchezaji wa Kihispania anayecheza timu ya taifa ataruhusiwa kuondoka Hispania mara uwezo wake wa kuisaidia timu ya Taifa utakapopungua, au atakapohitajika kwenda kukuza kiwango nje ya nchi yao na akipata ubora unaostahili atanunuliwa haraka kurudishwa. Kufunguliwa milango ya kuondoka kwa Xavi na sasa Iker Cassilas si bahati mbaya na kuruhusu Fabregas kwenda kukua pale Arsenal na leo kufufua kipaji chake pale Chelsea si makosa, ile ni falsafa.
Wahispania ni walafi sana wa vipaji bora. Wanaumia kimya kimya kumkosa Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar kwa sasa kama walivyoumia huko nyuma kuwakosa Ricardo Kaka, Ronaldinho, Zinedine Zidane na Luis Figo katika timu yao ya Taifa. Pamoja na hayo wanafaidika na changamoto za magwiji hao wa soka katika soka la timu yao ya taifa.


Wanafurahia rekodi za magwiji wakubwa wa soka duniani kukipiga pale Santiago Bernabeu na Catalunya kwa kuwa wachezaji wale mbali na kuipa Hispania hadhi na mataji ya UEFA, lakini wanawapa changamoto kubwa wachezaji wa Kihispania waliopo ndani na nje ya Hispania.
Mashabiki wa Manchester United wanakosa kuhuzunika wanapomuona De Gea anarudi kwao, baada ya kupata ubora pale England ni kama mashabiki na viongozi wa Yanga wanapohuzunika kumuona Charles Mkwasa ‘Master’ akiteuliwa kuwa kocha wa Taifa Stars.


Katika kipindi hiki ambacho wapenda soka wengi wametamani kuwa na kocha mzawa; tunahitaji kupata kocha mwenye weledi na soka letu, anayejua kusimamia nidhamu na mwenye nidhamu binafsi, mwenye rekodi nzuri ya kutumikia Taifa hili na mwenye moyo wa kizalendo na aliye tayari kujituma na kusimamia malengo. Tunahitaji kocha atakayesimamia haki, uwezo, ukweli na nidhamu katika soka letu — tena awe mtu wa kazi na si mtu wa maneno mengi yaliyojaa unazi.
Anahitajika mtu anayeheshimu kipaji chake kama taaluma maalum inayompa heshima binafsi na taasisi anayoifanyia kazi. Ungeniuliza mwaka jana nani anafaa ningekujibu Mkwasa na hata leo ukiniuliza tena nitakwambia ni huyo huyo kwa kuwa tunahitaji mtu wa kutuunganisha tena na si kututenganisha lakini mwenye rekodi nono.


Katika kipindi hiki cha mpito, tunahitaji mtu mwenye nidhamu binafsi hasa katika matamshi yake ili asitugawe katika usimba na uyanga ambao nao ni sumu kubwa katika soka letu.
Tatizo la soka letu haliwezi kumalizwa na Mkwasa pekee, bali wadau wote wa soka na hususani TFF ambao watapaswa kumuheshimu kocha mzawa kama walivyofanya kwa wageni. TFF wanajua kuwa pale ofisini kwao hakuna kocha ndiyo maana wakamteua Mkwasa, hivyo haitakuwa busara wao kuingilia majukumu ya kocha ambayo walijua pasipo shaka kwamba hawayawezi. Wadau wote wa soka ni wakati wa kumuunga mkono mgonga pasi huyu na kocha wa zamani wa Twiga Stars.


Yanga wanaumia kumuona akienda Taifa Stars na maumivu yao si kama hawamtakii mema Mkwasa, au hawalitakii mema Taifa hili, bali ni kwa kuwa wanaujua ubora wa Mkwasa.
Yanga lazima mkubali kuwa ubora mliouona ninyi ndiyo huo tunaouhitaji kwa ajili ya Taifa zima ambalo Yanga ipo ndani ya Taifa hilo. Kama hamtaki Mkwasa aende Taifa Stars mlitaka nani aende? Inawauma kwa kuwa Mkwasa ni bora, sasa kama ni bora lazima apewe nafasi ya kutumika kutupa mwelekeo bora.
Tukubaliane kuwa kukubalika kwa Mkwasa mbele ya Pluijm mpaka akamuhitaji hata nje ya Yanga, ni wazi kuwa Mkwasa ni bora hata mbele ya wageni ambao mara nyingi hawawakubali makocha wasaidizi wazawa huwa huwakubali kwa kinyongo, ni ishara kuwa Mkwasa yupo katika ubora kwa kiwango cha nchi yetu.
Katika kipindi hiki cha mpito tunahitaji kuwa na nidhamu ya Kiitaliano, tabia ya Kihispania na uvumilivu wa Kiholanzi ili kupata timu bora ya Taifa letu. TFF imeruhusu wachezaji wa kigeni sababu wakati timu ziliomba wachezaji kumi wa kigeni.


Katika idadi hiyo sina ugomvi nayo lakini jambo muhimu ni kuwa na tabia ya Kihispania kwa maana ya kufanya soka letu kuwa bora ili hata mchezaji mzawa akiwa huko nchi jirani katika ubora atamani kurudi nyumbani kusakata kandanda kama inavyotokea kwa Wahispaniola.
Pili, uwepo wa wachezaji wa kigeni uimarishe vipaji vyetu kama vile Gerad Pique anavyoimarika kwa kukabana na Christian Ronaldo mara kwa mara. Hakuna mshambuliaji atakayemsumbua Pique kama kila mara anakabana na mchezaji bora wa dunia. Kuna faida hapa kwetu Cannavaro anapohaha kumkaba Okwi au Isihaka anapomkaba Tambwe lakini kuna hasara Kapombe anaposema kumkaba Coutinho ni kazi nyepesi sana.


Wachezaji wakipenda na kuona soka la nyumbani lipo juu, basi wakirudi baada ya kupandisha viwango vyao huko nchi jirani tuwe na nidhamu ya kuwatumia kama Waitaliano wanavyofanya. Mara nyingi Waitaliano wamehusudu sana wachezaji wanaocheza ligi ya ndani kwa kuwa wanajua wachezaji wale wanacheza katika falsafa moja katika ligi yao, jambo ambalo halimpi tabu kocha wa timu ya taifa.


Lakini tunahitaji uvumilivu wa Kiholanzi pia ili kuruhusu wachezaji chipukizi na falsafa ya kocha kuiongoza timu kuliko kila mtu kuwa kocha wa timu. Shabiki anataka mchezaji wake, TFF mchezaji wake na kocha mchezaji wake, hapo tusitarajie kupata timu tunayotamani tuipate na ilete ushindani.
Chonde chonde timu zetu acheni kutuletea wageni wasioleta changamoto yoyote, maana inakuwa ni matumizi mabovu ya fursa ya kukutana na wageni ambao wangetuimarisha kama Tevezi alivyowaimarisha mabeki wa Kiitaliano.
Wasajilini wakina Pogba na Hazard ambao watafanya wachezaji wetu kuwa bora kuliko kusajilli wakina Yahya Sanogo kila kukicha.

Baruapepe: amrope@yahoo.com
Simu: 0715 36 60 10

 
1997 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!