maradona-hand-of-god_1fd1vx1cfzhd51a5rqhvjozib1Mashabiki 114,580 walishuhudia Ali Bin Nasser kutoka Tunisia akirudi katikati ya dimba baada ya kupuliza filimbi katika dakika ya 51 kwenye Uwanja wa Azteca Juni 22, 1986 nchini Mexico, katika mchezo wa robo fainali Kombe la Dunia kuruhusu bao la mkono la Diego Armando Maradona.
  Mashabiki wa Argentina walilipuka kwa shangwe kushangilia bao hilo kwa sababu kubwa mbili – kupata ushindi uwanjani lakini ilikuwa ni kama kisasi cha kivita katika vita ya Falklands dhidi ya Uingereza, iliyodumu kwa miezi miwili na wiki moja –  miaka minne iliyopita kabla ya fainali hizo. Vitani, Uingereza ilishinda.
  Waargentina walikuwa na shauku ya kulipa kisasi cha kichapo cha vita hiyo ya kuwania Kisiwa cha Sandwich. Morali ya kivita iliwaingia wachezaji katika mishipa ya damu na kapteni wa Argentina, Maradona, ndiye aliyekuwa mwenye hasira zaidi kuhitimisha vita hiyo.


  Mabao mawili ya Maradona likiwamo lile la ‘Mkono wa Mungu’ yalitosha kuiondoa England katika hatua hiyo ya robo fainali kati ya Argentina na England. Diego Maradona alikuwa shujaa wa Argentina siku hiyo maana alifunga mabao ya kusisimua akianza na lile la ‘Mkono wa Mungu’ kisha alifunga bao la pili kwa kupiga chenga mabeki wanne na kipa kisha kutikisa nyavu za Waingereza kwa mara ya pili na kuhitimisha mchezo kwa jumla ya mabao 2-1 na kumfanya Kocha wa Argentina, Carlos Bilardo, kuwa shujaa.


  Waingereza walilia sana, lakini kilio chao hakikuwa kule kutolewa robo fainali pekee bali waliona wametolewa isivyo halali kwa kufungwa bao la mkono. FIFA walimpa Diego Maradona kiatu cha dhahabu kama mchezaji bora wa mashindano hayo ambayo Argentina iliibuka mabingwa.
  Bao la mkono likaitwa ‘Mkono wa Mungu’ na mfungaji wake kupewa kiatu cha dhahabu, lakini unaweza kujiuliza kwanini huyu aliyetenda hila alipewa kiatu cha dhahabu na shirikisho linalotangaza ‘fair play’?


  Siku ya Jumanne kama leo, Juni 2002 katika Uwanja wa Daejeon jijini Daejeon, soka likaingia katika mtihani mwingine wa ‘fair play’. Alikuwa ni refa Byron Aldemar Moreno Ruales aliyezaliwa Quito, Ecuador Novemba 23, 1969 aliporuhusu bao lililofungwa katika muda wa nyongeza na Ahn Jun-hwan na kujipatia umaarufu katika vyoo vya umma kule Italia.


  Picha ilikuwa hivi; watazamaji zaidi ya 42,000 walikuwa uwanjani wakitazama mechi ya kukata tiketi ya kwenda robo fainali kati ya wenyeji Korea ya Kusini dhidi ya Italia iliyosheheni vipaji.
  Siku hiyo ulimwengu wa soka uliamini Wataliano wangeing’oa Korea Kusini na kutinga robo fainali. Wataliano walionesha wameimarika kila idara, timu iliyosheheni wafumania nyavu kama Alessandro De Piero, Christian Vieri, Francesco Totti, Pippo Inzaghi kisha beki kama Fabio Cannavaro, Alesandro Nesta na mkongwe Paolo Maldini, mbavu ya kushoto, huku langoni kukiwa na kipa ghali duniani, Gigi Buffon, ilikuwa ngumu kuamini kuwa itatolewa na Korea Kusini katika hatua kama hiyo.  


  Mambo yalianza kwa Moreno kuruhusu penalti dhidi ya Italia, penalti ambayo Korea Kusini walikosa. Christian Vieri akapeleka kilio Korea kabla Korea Kusini hawajasawazisha katika dakika za lala salama na muda wa ziada ukaongezwa wakati huo sheria ya goli la dhahabu ikiwa katika uhai wake.
  Katika kile kilichoonekana Moreno amepanga kuwabeba wenyeji; Damiano Tommas alifunga bao lililoaminika kuwa ni safi, lakini yeye alikataa. Wataliano wakiwa bado hawaelewi nini kimetokea, Totti akapigwa kadi ya njano ya pili na kutolewa nje na ndipo “shujaa” wa Korea Kusini alipotekenya nyavu kwa bao la kichwa ambalo lilionekana kuwa ni la kuotea.


  Mfungaji Ahn Jun-hwan akapigiwa simu na Luciano Gaucci, mmiliki wa klabu ya Perugia, kuwa hahitajiki tena klabuni hapo kwa kuwa bosi huyo hayupo tayari kumlipa mshahara mtu aliyeitia aibu nchi yake isivyo halali. Wataliano wakacharuka na kuviita vyoo vya umma vya nchini mwao kwa jina la Aldemar Moreno kwa hasira waliyokuwa nayo.
  Wakina Berlusconi walichukia sana lakini waliweka akiba ya maneno kwa heshima ya refa wa Kiitaliano, Luigi Collina, na walisema waziwazi kuwa Italia haioni thamani ya michuano ile kama si refa wao kuwapo, ambaye alichezesha mechi ya fainali kati ya Brazil na Ujerumani iliyohitimishwa kwa Brazil kuibugiza Ujerumani mabao 2-0.


  Aldermar Moreno aliporudi kwao Ecuador pamoja na madudu mengine akatimuliwa kazi na shirikisho la soka nchini humo. Kocha wa Korea Kusini wakati huo, Mholanzi Guus Hiddink, hakuonesha kutetea bao lile na Sepp Blatter alipoulizwa alisema kuwa hata yeye aliona ni bao la kuotea na akasema lawama zote ni kwa mshika kibendera.


  Rais huyo wa FIFA alikiri, lakini haikuwa na faida yoyote kwa machozi ya Wataliano na wala hakukuwa na namna yoyote ya wao kupata haki yao iliyodhulumiwa na refa mwenye beji ya FIFA. Hakukuwa na majibu na hata leo hakuna majibu “aliyepewa kapewa” ndiyo “fair play” ya mpira wa miguu.
  Ukitafakari mambo hayo na mazonge mengine katika soka, unaweza usiipate maana halisi ya “fair play” kwenye kamusi labda kwenye moyo wa aliyefaidika na tukio husika. Kuna sheria na kanuni nyingi za mpira zenye utata ikiwapo ile ya kuzuia mtu aliyetendwa ubaya na kukosa haki katika shirikisho la soka kwenda mahakamani.
  Unaweza kujiuliza maana ya hii “fair play” ukakosa majibu zaidi ya lile la kufunika kashfa za kifisadi za FIFA. “Fair play” ya kuwa lililoamuliwa limeamuliwa kwamba haliwezi kutenguliwa wala kuhojiwa katika mamlaka za juu hata kama si halali, ndiyo “fair play” inayonishangaza.
 
Baruapepe: [email protected]
Simu: 0715 36 60 10

 

By Jamhuri