Jumapili Agosti 3, mwaka huu, ilikuwa ni siku ya kuvunja rekodi na pengine kumaliza ubishi uliodumu kwa muda mrefu. Timu ya soka ya Azam maarufu kama Wanalambalamba walibeba Kombe la Kagame bila kupoteza mchezo.

 Kadhalika, bila kuruhusu bao hata moja katika mechi yoyote ndani ya dakika 90 za mchezo. Swali la kujiuliza je, Azam FC walistahili? Jibu ni rahisi, “walistahili.”

Hakuna ubishi kwamba Azam imewekeza vya kutosha kwenye miundombinu kwa miaka kadhaa sasa na usajili wao wa wachezaji hasa wa nje umekuwa makini. Katika kipindi ambacho Stewart Hall amerejea katika benchi la ufundi kama kocha mkuu kwa mara ya tatu, ilitarajiwa afanye makubwa.

Huku nyuma tulikwisha kuandika kuhusu Azam kwamba imekuzwa katika falsafa ya kocha huyo raia wa Uingireza, hivyo kurejea kwake kulimaanisha “upele kupata mkunaji.”

Wameleta kombe nyumbani, wametupa heshima na furaha lakini wametuachia funzo na wamejibu maswali kadhaa yaliyotawala katika vichwa vya wanamichezo wengi.

Wametufunza kuwa usajili wa wachezaji wa nje ni muhimu ila ufanywe kwa tija na si kujaza nafasi maadamu zipo saba; kila mtu ameona shughuli ya Pascal Wawa, Baptist Mugiraneza ‘Migi’ na  Kipre Tchetche ilivyokuwa muhimu katika kuipa Azam ubingwa.

  Pia wametujibu kuwa inawezekana kwa klabu isiyo kongwe wala mashabiki wengi kupata ubingwa katika si tu mashindano ya ndani, bali pia mashindano makubwa kama haya ya Afrika Mashariki na Kati.

Azam wamevunja rekodi kwa kuonesha kuwa wapo kimkakati zaidi kwa kukabidhi pesa ya zawadi ya ubingwa, zaidi ya milioni 60 za Kitanzania, kama zawadi kwa wachezaji wao kwa kutwaa ubingwa huo.

Hii ni wazi kuwa Azam wana malengo makubwa zaidi na ndiyo maana wamefanya haya yote. Walau klabu kongwe kubwa na zile zinazopanda na kushuka daraja zinaweza kujifunza hapo kimikakati na hata miundombinu ya viwanja vya mazoezi. 

Kimbinu, Stewart Hall alikuwa makini na alikuja na mfumo mpya wa 3-5-2 ambao umemfanya Aishi Manula asiokote mpira katika nyavu mpaka mashindano yanamalizika. Walistahili.

  Jumapili hiyo hiyo kule katika jiji la London, England, kulikuwa na pambano la ngao ya hisani kati ya Arsenal na Chelsea za nchini humo. Kilichovutia katika mchezo huo ni kukutanisha makocha wenye uhasama mkubwa – Jose Mourinho na Arsene Wenger – ambao wamekuwa hawapikiki chungu kimoja na msimu uliopita “walishikana mashati” katika pambano lililowakutanisha katika Ligi Kuu.

Mechi ilikwisha kwa Arsenal kupata ushindi wa bao moja bila majibu na kumfanya Wenger kushinda mechi ya kwanza dhidi ya Mourinho katika mechi 14 walizowahi kukutana. Pengine hii ilituliza dharau za Mourinho aliyemtania Wenger kwa kumwita ‘Mfalme wa kushindwa.’

Dharau na kejeli za Mourinho hazijamalizwa maana amesikika (siku chache baada ya mechi hiyo) akisema, “Ni rahisi kuipita Arsenal ikiwa imekutangulia pointi 9 mbele kuliko kuipita Manchester United ikikutangulia pointi moja katika Ligi.”

Hii inaashiria kuwa uhasama bado utaendelea maana ‘Domokaya’ hajatulizwa bado ila amechokozwa tu. Pamoja na maneno na dharau za Mourinho lakini ukweli unabaki kuwa rekodi imeshavunjwa.

Ushindi wa Azam hapa nyumbani na ule wa Arsenal kule England una neno la kutwambia wanamichezo wote hapa nchini, kwamba historia haichezi mpira na hakuna lisilowezekana kukiwa na dhamira.

Kuchoshwa kudhalilishwa na Mourinho ndiko kulikomfanya Wenger ajipange na kupindua historia. Na kuchoshwa na kukosa mataji ya Ligi na UEFA ndiko kulikowafanya wamiliki wa klabu hiyo kumkabidhi Wenger paundi milioni 200 afanye usajili wa mchezaji anayemtaka kwa gharama yoyote.

Shaka yangu ni utayari wa bahili Wenger kuingia sokoni na hilo fungu lote la pesa. Muda utasema lakini kama atakuwa ametumia hata robo tatu ya fungu hilo atakuwa amevunja rekodi yake mwenyewe ya ubahili.

Kupewa fungu hilo nono ambalo lilisababisha Mourinho kuweweseka na kusema “Klabu zinatumia pesa nyingi kununua ubingwa”, kumetokana na juhudi zilizofanywa na Wenger za kupata ushindi katika ukata. Amechukua Kombe la FA mara mbili mfululizo na amezindua msimu kwa kumchapa bingwa mtetezi Chelsea.

Baada ya kushuhudia rekodi zikivunjwa hapa Bongo na kule England, sasa ni zamu ya Taifa Stars kuvunja rekodi kwa kuifunga Nigeria katika kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika jijini Libreville, Gabon, Jumamosi Septemba 5, 2017.

Historia kamwe haichezi soka na uamuzi wowote wa kuchoshwa na kuporomoka katika viwango vya FIFA mpaka nafasi ya 140 na kuwa wasindikizaji, utatusaidia kupata matokeo mazuri uwanjani.

Hii nafasi ni kwa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kuwaonesha Watanzania walioibua morali kwa Taifa Stars kwamba wamefanya jambo sahihi na kwa wakati sahihi.

  Wachezaji watambue kuwa morali hii haitokani na matokeo yoyote waliyotupa, bali ni uwekezaji wa imani na matumaini yetu kwao. Kwa maandalizi haya ya mapema ni wazi kuwa dhamira ya kusaka ushindi ipo, maana ni nadra kwa Taifa Stars kufanya maandalizi ya mapema na ya uhakika namna hii.

Tumemsikia Mkwasa akitangaza kikosi cha wachezaji 29 walioingia kambini Jumapili iliyopita katika Hoteli ya Tansoma  Dar es Salaam. Baada ya kambi hiyo fupi ya jijini, vijana hao wa Mkwasa wanatarajiwa kuweka kambi ya siku 10 jijini Istanbul, Uturuki, na huko watacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu za taifa za Libya na Kuwait kisha kurejea nchini kuwamaliza Super Eagles.

Wachezaji walioitwa ni makipa Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam); mabeki wa pembeni: Shomari Kapombe (Azam), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Juma Abdul, Mwinyi Haji (Yanga) na Abdi Banda (Simba).

Walinzi wa kati; Hassan Isihaka (Simba), Nadir Haroub na Kelvin Yondani (Yanga) wakati viungo wakabaji ni Himid Mao, Frank Domayo na Mudathir Yahya (Azam); viungo washambuliaji ni Salum Telela (Yanga) na Said Ndemla (Simba).

Washambuliaji wa pembeni; Orgenes Mollel (Aspire-Senegal), Abdrahman Mbambi (Mafunzo), Deus Kaseke, Saimon Msuva (Yanga), Ramadhani Singano, Farid Musa (Azam) huku washambuliaji wa kati wakiwa ni John Bocco, Ame Ally (Azam) na Rashid Mandawa (Mwadui).

Wachezaji wa kimataifa waliojumuishwa katika kikosi hicho ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngassa (Free State, Afrika Kusini), Hassan Sembi (Santos FC, Afrika Kusini) na Adi Yussuf (Mansfield Town, Uingereza).

Kwa upande wa uteuzi wa wachezaji na aina ya maandalizi ni wazi timu itakuwa imeandaliwa kushinda na tunastahili hivyo kama Azam, Arsenal na sasa ni zamu ya Taifa Stars.

 

Baruapepe: amrope@yahoo.com

Simu: 0715 36 60 10 

1891 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!