Usiku wa Alhamisi ya Oktoba 15, nikiwa jijini Mwanza nilipata taarifa za ajali ya helikopta. Taarifa hizi mwanzo zilitaja viongozi wanne waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa walikuwamo. Moyo wangu ulikwenda mbio. Nilimtafuta mmoja wa viongozi wa juu wa CCM usiku huo huo. Nilimpigia simu hakupokea, nikamtumia ujumbe mfupi (sms). Alinijibu, ila nasikitika majibu yake yalipungukiwa uungwana.

Kiongozi huyo aliishia kunitumia ujumbe unaosema: “Tupunguze uzushi.” Kwa muda mrefu kiongozi huyu nimemchukulia kama mtu makini, lakini naona kadri muda unavyokwenda siasa zinapunguza uwezo wa baadhi ya watu kufikiri. Nilimtumia ujumbe mwingine kumweleza masikitiko yangu kuwa yeye kama kiongozi mwandamizi anafahamu fika kuwa kazi yangu ni Mwandishi, kumuuliza kamwe haiwezi kuwa uzushi.

Sitanii, nilimtakia usiku mweka, na kumweleza faraja yangu kuwa hakuwa mmoja wa waliokuwa kwenye helikopta, akahitimisha kwa ujumbe mwingine akisema: “Asante.” Sikulala. Niliendelea kuusaka ukweli. Katika mitandao ya kijamii, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, akaandika ujumbe kuwa helikopta zote nne zinazotumiwa na CCM ziko salama. Hajafuta kauli yake hadi leo.

Baadaye zilianza kupatikana taarifa kuwa Deo Filikunjombe alikuwamo kwenye helikopta iliyoanguka. Ikatajwa kuwa helikopta hiyo ilikuwa imeungua na kubaki majivu. Nilipiga simu ya Filikunjombe, mbunge kijana aliyekuwa Mwandishi wa Habari mwenzetu miaka mitano iliyopita kabla ya kugombea ubunge Jimbo la Ludewa na kupita bila kupingwa baada kura ya maoni ndani ya CCM. Muda wote ilionekana inatumika.

Mengine ni historia. Akili yangu imepata uchungu wa aina yake. Namfahamu Deo kitambo sasa. Huyu tulikuwa tukiitana kwa utani ‘Wajina’, kwa maana mimi ni Deodatus na yeye ni Deogratias. Mdogo wake Dominic Haule, ndiye aliyekuwa mpiga picha siku ya harusi yangu. Tulikuwa na urafiki wa dhati. Sitaji harakati nyingine, bali nikumbushie tu siku ya Julai 10, mwaka 2015.

Sitanii, kwa wenye kumbukumbu mtakumbuka hii ndiyo ilikuwa siku ya kihistoria katika mchakato wa kumpata mgombea wa CCM pale Dodoma. Nilikwenda Dodoma. Majira ya saa 4 asubuhi tulikutana na Deo katika Hotel ya St. Gasper. Tulikaa mimi, Deo Filikunjombe, Manyerere Jackton na Denis Msaky, kisha walikuja vijana wengine waliokuwa katika harakati za kufahamu nani anakuwa mgombea wa CCM.

Deo alitueleza bila kificho, kama ilivyokuwa kawaida yake kutoficha mambo. Kwamba aliitwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kama walivyokuwa wanaitwa wabunge wengine kupata maoni yake. Kinana akamuuliza kati ya John Magufuli na Edward Lowassa anadhani nani anafaa kuwa mgombea wa CCM. Deo alitueleza majibu aliyompa Kinana, ila kwa sababu za kimaadili nayahifadhi.

 Niliujua msimamo wa Deo kisiasa na hamu yake ya kutumikia wananchi. Hakuwa mwanasiasa waruwaru. Hakufanya siasa za kuganga njaa. Alishiriki maendeleo ya wananchi kwa dhati. Alishirikiana na wananchi si kwa kuchangia michango tu, bali kwa kukata visiki, kubeba magogo, kuchimba mitaro, kubeba zege na mengine mengi.

Hakika Watanzania wengi tumebubujikwa na machozi kwa kuondokewa na Deo Filikunjombe. Tunasikitika na tutaendelea kusikitika kwa kukosa utumishi wake. Nilifika kwao Ludewa. Tulikwenda wote Mchuchuma, Liganga na Ngaka kwenye chuma na makaa ya mawe. Hakika, Deo ni taa iliyozimika kabla ya wakati na Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake.

Sitanii, kichwa cha makala hii namuaga Deo Filikunjombe na kusema  Lowassa anakamilisha historia. Nafahamu fika kuwa wiki hii ni ya majaribu makuu kwa taifa letu. Wapo walioaminishwa au wasioamini katika chama tawala na wapo wasioamini katika upinzani. Naangalia juhudi kubwa za kuanza kupuuza hata maneno ya kweli ya mwasisi wa taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwalimu Nyerere alisema: “Upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM.” Sina sababu ya kulithibitisha hili. Uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na miaka iliyotangulia. Historia inaonyesha kuwa duniani kitu pekee kisichozuilika ni mbadiliko (change). Na inaaminika kuwa mabadiliko ni suala la kudumu. Leo tunashuhudia wagombea wote wanazungumza mabadiliko.

Naomba nieleweke hapa, na hili nimekuwa nikilisisitiza kuwa Dk. John Magufuli si mgombea au mtumishi mbaya. Anao uzuri wake. Ni mtendaji. Anaweza kufanya uamuzi. Ana siha njema. Anayafahamu maeneo mengi ya nchi hii, isipokuwa lipo wasilopenda kulisikia wafuasi wake au chama chake, kwamba amegombea katika kipindi ambacho upepo wa mabadiliko unavuma kwa kasi.

Dk. Magufuli analitambua hili na ndiyo maana hata yeye anaeleza kuwa hayo mabadiliko basi wampe yeye ayafanye. Wapo wanaoona Magufuli angeweza kuyaleta hayo mabadiliko kama anavyoeleza mara kwa mara, lakini wanakumbuka maneno aliyosema Waziri Mkuu mwenye historia ya pekee ya kushikilia cheo hicho kwa miaka 10 mfulululizo, Frederick Sumaye aliyesema kuwa MFUMO NDANI YA CCM ni vigumu kuubadilisha.

Sifa alizonazo Magufuli za kiutendaji, hazitofautiani na za Lowassa. Wapo wanaokumbuka utendaji wa Lowassa katika kusimamia idara au wizara alizopata kushika na kuona huyu ndiye kiongozi sahihi. Wanakumbuka alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alivyoagiza kuvunjwa kwa uzio uliokuwa umezungushiwa viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

Wafuasi wa Lowassa wanakumbuka jinsi alivyoweza kuvunja mkataba wa Kampuni ya maji ya City Water ikakimbilia mahakamani London Uingereza na kampuni hiyo ikashindwa kesi. Wapo wanaokumbuka jinsi alivyokuwa Waziri wa Maji alivyosimamia uvutaji wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Shinyanga na Kahama, huku akipuuza vitisho vya aliyekuwa Waziri wa Maji wa Misri, Dk. Mohamed Abu-Zaid aliyetishia kuwa iwapo maji hayo yangechukuliwa Misri ingeipiga vita Tanzania.

Wanakumbuka alivyosimamia ujenzi wa shule za Kata kwa kipindi cha miaka miwili alipokuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. Wanakumbuka alivyosimamia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na mengine mengi. Kubwa zaidi, wanakumbuka muda wote alivyokuwa akihubiri ‘maamuzi magumu’ na jinsi Julai 28, mwaka huu alivyofanya uamuzi wa kuihama CCM na kujiunga CHADEMA.

Sitanii, nazungumza na watu wa kada mbalimbali. Wapo waliokunywa maji ya bendera za upinzani na wapo waliokunywa maji ya bendera ya CCM. Hawa hawasikii cha Mhazini wala Mteka Maji Msikitini. Hawa hata ukiwaletea jiwe watalichagua tu, ilimradi limesimamishwa na chama anachokubaliana nacho kiitikadi.

Kwa kuyakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere juu ya upinzani wa kweli, najaribu kuangalia kuondoka kwa Lowassa CCM na madhara yanayoweza kujitokeza. Naanza kuiangalia CCM kuanzia ngazi ya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, Mkutano Mkuu na hatimaye wanachama wote. Nimeandika mara kadhaa juu ya suala hili, ila kwa umuhimu wa wiki hii naomba kulirudia.

Kwamba kati ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM 378, Lowassa alikuwa na wafuasi 316. Nguvu hii ya aina yake ndani ya CCM ndiyo iliyomwezesha kuwambia waliokuwa wafuasi wake wasimpigie kura Bernard Membe na ikawa. Hadi mtu kama Dk. Asha Rose Migiro kwa agizo la Lowassa kati ya wajumbe 378 alipata kura 280, lakini aliposimama mwenyewe kuomba kura katika mkutano mkuu uliokuwa na watu 2,400 akaambulia kura 50.

Sitanii, hofu ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ilionekana wazi. Sina uhakika kama alitoa maelekezo juu ya nani ashinde kati ya Migiro, Amina Salum Ali na Magufuli. Kilichonitisha ni kumtaka Spika wa Bunge, Anna Makinda kumuonyesha matokeo kwanza, kisha yeye akayaangalia na kusema: “Ehee haya ndiyo yenyewe, sasa tangaza.” Sijui yapi hayakuwa yenyewe!

Mchakato ndani ya CCM, ingawa wanatumia nguvu kubwa kuuhalalisha, uliacha maswali mengi kuliko majibu. Matokeo yake ndiyo tunayoyashuhudia. Leo waasisi akina Frederick Sumaye, Kingunge Ngombale Mwitu, Balozi Juma Mwapachu na wenyeviti wa mikoa wameondoka na kujiunga na upinzani. Pamoja na kuondoka kwao, bado wapo watu wanaoendelea kutoa kauli za vijembe wakisema waliohama ni oili chafu.

Baadhi ya wana-CCM wametumia nguvu kubwa katika kipindi cha kampeni kuuaminisha umma kuwa Lowassa ni mgojwa. Sihitaji kutana majina, lakini wanasiasa 7, waliokuwa na siha njema wamekufa wamemuacha. Mungu azilaze mahala pema roho za hawa Watanzania wenzetu. Yanayotokea ni onyo na ushuhuda wa wazi kuwa milele tusijikabidhi kazi ya Mungu na kutoa hukumu kwa wanadamu wenzetu.

Sitanii, nimesafiri kila mkoa wa nchi hii kati ya Januari na sasa. Nimeangalia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, na takwimu zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Na si takwimu tu, wewe angalia katika familia, kijiji au mtaa unapoishi watu wenye umri wa kuanzia miaka 40 kwenda juu ni wangapi? Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 12.

Taarifa zinaonyesha kuwa wapigakura wa mara ya kwanza ni asilimia 60. Kama mtafiti, nimeona kuwa hadi vijijini kuna redio, simu za mkononi, televisheni na magazeti yanafika. Ukiwa kwenye kumbi za starehe uulize nani atachaguliwa kuwa Rais Jumapili hii, kisha utapata majibu. Najua kuna vyama vinategemea wapigakura wa vijijni, lakini taarifa nilizonazo si wa kutegemea sana. Najua hata wewe msomaji unafahamu utampigia nani na hiyo ni haki yako, itumie.

Sitanii, naomba kuhitimisha makala hii kwa kuwaomba wapigakura, vyombo vya dola, wananchi wa kawaida na viongozi wetu watusaidie kuimarisha amani. Utaratibu tuliouzoea wa kupiga kura na kukaa umbali wa mita 200 miaka yote haujawa na dosari, tusijenge hofu isiyo ya lazima kwamba hata ambaye atashindwa kihalali akapata kisingizio.

Ni jukumu letu sote kutunza amani ya nchi hii. Tanzania amani ikivurugika, tufahamu hatuna sehemu yoyote ya kukimbilia. Tanzania hii ni yetu sote, na tunapaswa kudumisha amani kwa masilahi ya kizazi chetu na vizazi vijayo. Kwa vyote iwapo, haki ikitendeka itadumisha amani na tuhakikishe inatendeka. Jumapili tukapige kura, tutulie kwa amani na kusubiri matokeo bila kufanya fujo na viongozi wetu wawe tayari kupokea matokeo yatakayotoka kwenye sanduku la kura. Mungu ibariki Tanzania. Nawatakia uchaguzi mwema.

By Jamhuri