MAGUFULIWiki mbili zilizopita sikuandika katika safu hii. Sikuandika kwa maana kwamba nilikuwa mbio nasafiri mkoa hadi mwingine, kwa kiwango kilichonifanya nishindwe kutimiza wajibu wangu. Lakini si hilo tu, matokeo kadri yalivyokuwa yanatoka, taarifa zinasambaa ilinilazimu kufunga breki kwanza, kwa nia ya kujua nini kinaendelea badala ya kuandika kwa sababu tu kuna kuandika.

Nimefuatialia kwa karibu mchakato wa uchaguzi, upigaji kura, kujumlisha na kutangaza matokeo na kuna mambo nimejifunza. Nimejifunza kuwa kumbe sura ya chama au nchi, si halisi tuionayo machoni. Wahenga wanasema ukitaka kujua uhondo wa ngoma, sharti uingie ucheze. Uchaguzi huu ulioisha nimeshuhudia chuki ya wazi ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete dhidi ya aliyekuwa swahiba wake, na Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa.

Nasema aliyekuwa kwa maana matendo aliyomtendea, hakika ingawa maandiko matakatifu yanasema samehe saba mara sabini, binafsi naamini msamaha huu unaweza kuwapo pale tu itakapoundwa Tume ya Maridhiano, wawili hawa wakaelezana ukweli juu ya chimbuko la chuki hii ambayo hadi kesho, hatujawahi kuelezwa ilitokana na nini.

Lowassa amepata kuuambia umma kuwa yeye na Kikwete “hawakukutana barabarani.” Hili hakuna asiyelifahamu. Kikwete, Lowassa, Rostam Aziz na Bernard Membe, mara kadhaa walikaa nyumba moja, walipanda gari moja na mikakati ya kuanzisha mtandao ndani ya CCM waliianzisha pamoja, ila mpaka kesho binafsi sijui na sitakaa nifahamu kwa nini wamefarakana kwa kiwango nilichokishuhudia katika mchakato wa kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sitanii, Rais Dk. John Pombe Magufuli hapana shaka analifahamu hili. Anafahamu chaguo la Kikwete alikuwa ni Membe, ambaye baadae aliangukia pua. Membe alisema amekufa kifo cha ghafla (sudden death). Kisha akasema “inauma sana.” Nimefanya kazi kwa karibu na Membe, sikupata kuona kama ni mchochezi au mjenzi wa fitina. Nilipata fursa ya kumfahamu Kikwete na kufanya naye kazi akiwa waziri. Sitamtaja mzee Samuel Sitta maana naye alikuwa sehemu ya mkakati.

Dk. Magufuli anajua kuwa amefika hapo si kwa kubebwa, bali kutokana na uwezo wake wa kuchapa kazi uliotukuka. Kufanya uamuzi. Kuwa muwazi, kutosifia asiyestahili sifa na kuwa tayari kutamka anachokiamini badala ya kumchekea mtu, huku akimchoma kisu mgongoni. Dk. Magufuli hana sura mbili wala utaratibu wa kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa.

Baadhi ya mambo nilikuwa nikiyaona, lakini sikuamini kuwa binadamu tunaweza kuwa wasaliti kwa sababu ya tumbo. Wapo watu walisimama na kutoa maelekezo kwa baadhi yetu wakitaka eti ‘tumsuse Lowassa kwa kiwango cha kutosalimiana naye’ kwa sababu tu katofautiana na Kikwete, ilihali hawakutueleza walitofautiana nini.

Ilifika mahala tangu Lowassa alipojiuzulu mwaka 2008, kwa sababu tu hatukutii maagizo yao, kufika mbele yao tukinawa mikono na kuapa kuwa sasa hatusalimiani tena na Lowassa, tukaondolewa katika orodha ya misafara ya Rais nje ya nchi, magazeti tuliyoyafanyia kazi yakanyimwa matangazo na hata baadhi ya waliotangaza na sisi hawajatulipa miaka minne na zaidi ikiwamo Ikulu.

Sitanii, katika utawala uliomaliza muda wake nimeshuhudia siasa za makundi na ubaguzi wa wazi. Kikwete amepanda mbegu ya kuwagawa Watanzania kwa udini, ukabila na umajimbo. Kichwa cha makala hii kinasema ‘Rais Magufuli epuka mitego ya Kikwete.’ Kikwete alianza kuonekana wazi nia yake baada ya mwaka 2008. Alianza kufanya uteuzi wenye harufu ya udini hadi nchi ikapiga kelele.

Kama kuna jambo naomba kukushauri Rais Magufuli katika hili usiingie mkenge. Usiteue mtu kwa sababu ni Mkristo, Mwislamu au Mlutheri. Nafahamu mitego aliyoacha amekutegeshea Kikwete kwa kiwango cha kufanya hata uteuzi saa chache kabla ya kwenda kuapishwa utadhani hakuamini wewe iwapo una jicho la kufahamu nani mtendaji na nasi siyo.

Najua aliunda timu na Kampeni iliyokuwa na wajumbe 32, ambao kati yao baadhi ni masalia ya Kikwete ambayo ukiyasikiliza, yatakupeleka chaka. Hawa wapo watakaokwambia, huyu ni mwenzetu na huyu siye. Wamekwisha anza kwenye mitandao ya kijamii kuchafua wanaodhaniwa kuwa watapata fursa ya kuwa Waziri Mkuu na mawaziri.

Nimeipenda kauli yako Uwanja wa Taifa, uliposema ulioshindana nao kwenye uchaguzi, hao “walikuwa washindani wako na si wapinzani wako.” Kwamba utafanya kazi na Watanzania wa kila aina bila kujali watokako, hili ni jambo jema. Ni kwa misingi hiyo utafuta makovu. Ni kwa misingi hiyo utaziba ufa uliojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu.

Nimeupenda uamuzi wa Rais Magufuli kufuta safari za nje, kuagiza wafanyabiashara wakubwa walipe kodi. Napenda kuahidi sasa kuwa tumeanza kazi. Awamu iliyopita tulikuwa tukichapisha habari za uchunguzi zinapuuzwa, ila sasa tunajua utazifanyia kazi. Usilikose Gazeti la JAMHURI. Sisi kazi yetu ni kufunua uozo, nanyi kazi yenu iwe kufuatilia na kuwadhibiti waovu.

Sitanii, lipo lisilosemwa ila ukiangalia utaliona. Kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu zimepigwa kura za ukabila na udini. Angalia CCM wameshinda mno Kanda ya Ziwa, CHADEMA, wameshinda Kaskazini – CUF wameshinda mikoa ya Pwani na Nyanda za Juu Kusini. Ukiangalia hapa ni ukabila na udini ulioshinda. Kidonda hiki Rais Magufuli anapaswa kuanza kukiponya haraka.

Ninayo masikitiko yaliyochanganyikana na furaha kwamba katika uchaguzi huu, sisi (kampuni ya Jamhuri Media Limited) tumekuwa wahanga. Kambi ya Magufuli iliamini kuwa JAMHURI linamuunga mkono Lowassa na kambi ya Lowassa iliamini kuwa JAMHURI linamuunga mkongo Magufuli.

Kuthibitisha hili pitia magazeti yote tuliyochapisha ya JAMHURI utaona kuwa hatukupata tangazo linalomhusu Magufuli au Lowassa hata moja kwa kipindi chote cha kampeni. Magazeti mengi yalipewa matangazo, ila sisi tukabaguliwa na kuachwa ‘mtu kati.’ Hakuna mwandishi wetu hata mmoja aliyezunguka na mgombea yeyote kwenye kampeni. Hii ilitupa fursa ya kufanya kazi kitaaluma zaidi.

Sitanii, uchaguzi umekwisha. Kuna maisha baada ya uchaguzi na sasa nawiwa kumshauri Rais Dk. Magufuli, mambo yafuatayo:- 1. Jambo la Kwanza kabisa, arejeshe utawala wa sheria. Vituo vya polisi vidogo vifunguliwe saa 24, badala ya sasa ambapo Kikwete na Mathias Chikawe walishauriana ‘wakawaogopa’ majambazi na kuamuru vifungwe kila saa 12 jioni kwa maana kuwa majambazi watambe usiku kucha.

Hii ni aibu. Serikali kufunga vituo vya polisi kwa kigezo kuwa majambazi wanavivamia ni kukiri kushindwa. Ni udhaifu wa hali ya juu usiokubalika. Dk. Magufuli ondoa kadhia hii. 2. Katika kurejesha utawala wa sheria, Rais Magufuli ahakikishe hakuna polisi anayembambikia kesi mwananchi. Mahakama ziendeshwe bila rushwa na watumishi wote wa hovyo wawajibishwe. Hata kama kateuliwa wiki iliyopita, ikiwa afai tengua uteuzi wake.

Katika kurejesha utawala wa sheria, Rais Magufuli aliepushe taifa hili na uongozi wa Baba, Mama na Watoto (BMW). Watanzania hawatarajii kumwona Mama Janeth akikurubia ujumbe wa NEC na kufanya mipango ya kuwa mbunge. Nasema hapana. Watoto wako wakitaka kuingia kwenye siasa waingie kwa uwezo wao na si kwa mgongo wa Ikulu. Watanzania hawatarajii kuanza kusikia habari za watoto wa Rais kuwa na uhusiano na wafanyabiashara wakubwa ghafla.

Watanzania hawatarajii, nami sitarajii, watoto wa Dk. Magufuli kuanza kutoa matamko majukwaani jinsi ya kuendesha nchi na kudiriki kuliambia taifa Rais atatokea kanda ipi baada ya uongozi wako. Watanzania hawatarajii, kuwa Rais Magufuli ataanza kuwabeba watoto wa Kikwete eti kumfurahisha. Kama unataka kuua heshima yako, basi thubutu kumteua japo mmoja tu wa watoto wa Kikwete ushuhudie.

Watanzania wameanza kuisikia minong’ono kuwa mmoja wa wanafamilia wa huyo aliyetoka madarakani atakuwamo kwenye baraza lako. Epuka mitego ya Kikwete. Usiwape watu fursa ya kuanza kutema nyongo. Hadi sasa umeanza vizuri, ila ukitaka kutia chumvi kwenye kidonda thubutu ulifanye hilo, nami nipo hapa hapa. Nitakukumbusha yakiishakufika. Futa makundi kwenye siasa. CCM iko mikononi mwako na si kwa washauri.

Jambo la tatu ni sarafu ya nchi hii. Tanzania tumefika pabaya. Kila Mtanzania anaona fahari kumiliki dola badala ya Shilingi. Rais Kikwete alidhalilisha sarafu yetu kwa kuiita madafu. Ikiwa Rais haamini katika shilingi ya nchi yake, wananchi inakuwaje? Tunahitaji biashara huria, ila si biashara holela. Kuanzia sasa, kila anayenunua dola apewe risiti na aeleze sababu za kununua dola.

Nilikuwa Afrika Kusini hivi karibuni. Nilibaki na rand kadhaa kwenye pakacha langu. Nilipokwenda kwenye Bureau de Change, wakaniambia hawaruhusiwi kuniuzia dola hata kama narejea Tanzania. Mmoja akaniambia “kwa kukusaidia utupe na hati yako ya kusafiria, tutakubadilishia fedha kisha utavituka uwanja wa ndege fedha na passport.”

Nilivyosikia kauli hiyo nikapata hofu. Nikasema ni hatari kuacha hati yangu ya kusafiria mikononi mwa mtu nisiyemfahamu. Nikawambia waache tu wasiniuzie. Nilipofika hapa kwetu, kesho yake nikaenda eneo la Posta Dar es Salaam, nikauza rand 2050 nilizokuwanazo bila kuulizwa hata neno. Nilipodai risiti ya kuwauzia hizo rand, wakasema “utatufanya tulipe kodi risiti ya nini?” Nikashituka.

Suala la nne, naomba nizungumzie suala la foleni. Rais Magufuli kama kuna kitu unapaswa kukifanya ndani ya siku 100 za kwanza ni kupunguza na kuelekea kumaliza foleni katika majiji ya Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Arusha. Foleni zinaua uchumi. Katika hili uanze na barabara za mchepuko, kisha utaendelea na barabara za juu (flyovers).

Wiki ijayo nitazungumzia umuhimu wa kuimarisha reli, hatua za haraka kwa elimu ambapo waliopata mikopo ni wanafunzi 12,000 kati ya 70,000 wa mwaka wa kwanza wa vyuo vikuu, umuhimu wa umeme katika kukuza uchumi na hapa bila kuuma maneno au kupepesa macho nakuomba tu umrejeshe Eliakim Maswi awe Katibu Mkuu wa Nishati na Madini nguzo alizosambaza zijengwe na umeme usambae kwa kasi. Ombi ni hilo pia kwa profesa Sospeter Muhongo.

Kwa ujumla yapo mambo 21 nikayotaka kumshauri Mheshimiwa Magufuli na nitaomba kuendelea kuyadadavua wiki ijayo. Nitajadili kwa kina umuhimu wa viwanda vidogo vidogo na upimaji wa ardhi, mradi aliouleta nchini Rais Benjamin Mkapa kwa kumtumia Prof. Armando de Soto (formalization of the informal sector), ila Kikwete akaupiga teke kuanzia ukumbini. Tukutane wiki ijayo.

3153 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!