JKLeo naandika sehemu ya pili ya makala hii. Naomba niseme kuwa nimefarijika kutokana na mrejesho mkubwa kutoka kwenu wasomaji wangu. Nimefarijika kuona makala hii inanikutanisha na marafiki tuliopotezana miaka 30 iliyopita. Yupo mmoja wa marafiki zangu mara ya mwisho tumekutana mwaka 1985 tukiwa shule, amesoma makala ya wiki iliyopita akanipigia. Nimefurahi mno.

Si hilo tu, nimefurahi kuona jinsi Watanzania walivyo na hamu ya kuona nchi hii ikipiga hatua kubwa za kimaendeleo. Ni wazi mrejesho mkubwa na wa aina yake, unalenga katika uchumi wa nchi hii kufufuka ukaanza kuonekana mifukoni mwa watu na si kwenye makaratasi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na hotuba za wafadhili.

Nimesema kupitia makala hii, nitamshauri Rais John Pombe Magufuli mambo ya kuanza nayo katika uongozi wake. Binafsi nilikuwa nayo mambo 21. Wasomaji wangu wameniongezea matano, na wengi walikuwa wakiangukia katika orodha yangu. Niliahidi kuwa wiki hii nitazungumzia kwa kina umuhimu wa reli, na naamini nitafanya hivyo, ila kabla ya hilo ni vyema nikaonyesha kuheshimu mawazo ya wasomaji wangu.

Sitanii, yapo mengi nimeelezwa na wasomaji wangu, ila wengi wanapendekeza mambo ya haraka ambayo Rais Dk. Magufuli akiyafanya basi nchi hii itageuka kuwa ya maziwa na asali. Kama nilivyoshauri kuanzia makala iliyopita kuwa Rais Magufuli aepuke mitego ya Kikwete, yaani mtangulizi wake Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, leo naomba kuendelea kulisisitiza hilo.

Wasomaji wangu wameniambia mengi, ila yafuatayo ni yale wanayodhani anapaswa kuyapa kipaumbele. Nitarejea kwenye reli, ila nianze na ya wasomaji. Wanaomba Rais Magufuli uingilie mgogoro wa Zanzibar. Wasomaji wanasema ukitatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar, hii itakuwa fursa kwako na Watanzania kufanya maendeleo ya pamoja.

Wanasema mtangulizi wako Rais Kikwete katika anga ya kimataifa angefikiriwa kupata hata tuzo ya Mo Ibrahim hasa kwa mchango wake wa kurejesha amani nchini Kenya, ujenzi wa barabara za lami kilomita zipatazo 11 na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na mataifa ya nje, lakini yaliyomwangusha ni machache. Chuki na fitina zake.

Hakika wanasema jamii ya kimataifa inaangalia jinsi alivyoendesha mchakato wa uchaguzi ndani ya chama, kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar kufutwa, kisha wanaona haya yanampunguzia uwezekano wa kupata fursa ya kushinda tuzo ya Mo Ibrahim. Wanasema, Zanzibar usipoishughulikia wewe binafsi ukadhani bado ni jukumu la Mwenyekiti wa CCM, utaishia kupoteza wewe.

Mwenyekiti wa CCM ni raia sawa na walivyo raia wengine. Si Amiri Jeshi Mkuu. Tena wanasema hata kama ameshinda Maalim Seif Sharrif Hamad, huna sababu ya kuwa na hofu. Zanzibar haina jeshi, haina polisi wala idara ya usalama wa taifa, hivyo Seif iwapo akitangazwa mshindi hakuna siku wala saa anayoweza kuamka akaendesha Zanzibar kwa matakwa yake, bali kwa mujibu wa Katiba zote mbili.

Sitanii, nami naongeza hapa kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli ukisoma Ibara ya 64(5), 147 na 148, utaona kuwa hakuna sababu ya kuhofia kumtangaza yeyote aliyeshinda kushika madaraka ya urais wa Zanzibar. Kwako inayoweza kuwa na ukakasi kidogo ni Ibara ya 54. Najua Kikwete aliachia mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 yenye nia ya kumega madaraka ya Amiri Jeshi Mkuu, lakini mabadiliko hayo ni batili na ni bahati hakubadili Ibara ya 1 na 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).

Napenda kuamini kuwa Rais Magufuli si mmoja wa viongozi wanaoweza kushuhudia Katiba inavunjwa wakaendelea kutabasamu. Mwaka juzi, nchini China Waziri mmoja lifukuzwa kazi kwa kutabasamu (si kucheka), kutabasamu akiwa msibani. Tunapaswa kuelekea huko na si kuwa na viongozi wanaocheka muda wote hata kama kuna jambo la hatari kama hili la Zanzibar.

Jingine walilonidokeza wasomaji wangu ni Rais Magufuli kuwa muwazi. Wanapendekeza kuwa sera yako ya Hapa Kazi Tu, iambatane na Uwazi kama Rais Benjamin Mkapa alivyoanza kipindi chake cha kwanza, kabla hajaanza kuwaita baadhi ya Watanzania Malofa na Wapumbavu! Wanashauri kama ulivyosema usiwaone vyama vya upinzani kama wapinzani wako, bali washindani wako.

Wanapendekeza ujenge utamaduni wa kukutana nao na kujadiliana nao, ingawa hiyo isiyeyushe mamlaka yako kama Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Nchi. Uendelee na wajibu wa kusimamia usalama wa nchi, uchumi wa nchi na kama ulivyofanya kwa safari za viongozi nje ya nchi, iwe hivyo katika soko la fedha kwa maana ya maduka ya fedha na benki juu ya riba na uuzaji holela wa fedha za kigeni.

Kufanikisha azma yako ya kuleta ‘Mabadiliko ya Kweli’ ni lazima ubane matumizi. Wapo wafanyakazi walioko Serikalini wameniambia unavyoweza kuokoa mabilioni. Kuna wafanyakazi wanamiliki nyumba mbili za Serikali. Moja Dodoma na nyingine Dar es Salaam, lakini wanapokuwa ama Dodoma au Dar es Salaam wanalipwa posho za kujikimu.

Sitanii, wafanyakazi wazalendo wamenidokeza kuwa kama unataka maendeleo ya kweli ni lazima ufanye uamuzi wa dhati wa ama Serikali kuhamia Dodoma yalipo Makao Makuu au kufuta mpango huo na kuokoa fedha. Wakati wa kwenda Bungeni Dodoma, mashangingi yanapishana njiani na wote wanalipwa posho nono. Ni lazima uwe na Waziri wa Fedha mbunifu na mchumi aliyebobea.

Wafanyakazi hawa wameniambia uanze na ofisi nyeti zinazoshughulikia masuala yanayohusika na Bunge – zote zihamishiwe Dodoma. Hapa utakuwa umeondoa mzigo wa kuwalipa posho wakubwa hawa eti wanakwenda bungeni kwa ajili ya kile mnachokiita ‘maotea’ serikalini. Maotea ni utaratibu wa maafisa kuwapo bungeni wakisubiri kujibu maswali ya dharura wanayoulizwa mawaziri na wakawa hawana majibu ya moja kwa moja.

Kwa uchache nimeeleza maoni ya wasomaji wangu, lakini nilipokea mengi ajabu. Wiki iliyopita nilieleza juu ya ujenzi wa reli. Mwaka 1906 Mjerumani alikamilisha reli ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Mwaka 1914 alikamilisha tawi la reli la Tabora hadi Kigoma. Huko Kigoma ni kwa watani zangu ambao wote ukiwauliza wanakwambia wanatokea Ujiji, wakati kumbe treni ilipelekwa isombe mawese kwenda Bara Hindi!

Sitanii, na nisikilize kwa umakini. Nchi hii haiwezi kuendelea kwa kutegemea malori kusafirisha mizigo yake. Tunapaswa kuwaza treni za umeme. Mwaka 2006 nilizungumza na Rais Kikwete akaniambia kwamba alipanga kukopa fedha nyingi kwa dhamana ya Serikali (sovereign bond) na kujenga treni ya kisasa (umeme?). Baadae akaniambia mtikisiko wa uchumi duniani uliongeza gharama ya kukopa (riba) hivyo mpango huo aliusitisha.

Ikumbukwe Kikwete alipokea nchi hii kutoka kwa Rais Mkapa deni la taifa likiwa Sh trilioni 5.5. Miaka 10 baadae ameondoka madarakani deni la taifa sasa ni Sh trilioni 41. Najiuliza ni kipi alichokikwepa Kikwete? Amekopa fedha nyingi zikajenga barabara na madaraja, malori yanafanya kazi ya kuzibomoa na yanazaa msongamano katika miji.

Nafahamu haya wengi mliyajua tangu enzi za ujana wenu kwamba treni moja inachukua hadi makontena 100 kwa mara moja, wakati lori ni kontena moja au mawili. Ingekuwa tuna treni za umeme, ambazo gharama yake haiwezi kuzidi Sh trilioni 10 tukiamua kujenga hapa hadi Mwanza na Kigoma maana tuta lipo tayari kilichopo ni kuong’oa mataluma ya zamani kuweka standard gauge na kufunga nyaza za kusafirishia umeme inaotumia treni, uchumi huu utapaa.

Bei za usafirishaji zitashuka, muda wa kusafirisha mizigo utapungua kwa kiwango cha ajabu. Kwa mfano kama ni treni ya umeme itatumia saa 5 hadi 6 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma badala ya siku tano za lori. Barabara zinazoharibika kila baada ya miaka 10 zitadumu kwa miaka 40 hadi 50. Tutasafirisha mizigo ya majirani zetu na kupata faida kubwa, kisha kuwa na uwezo wa kurejesha deni la fedha tulizokopa kujenga reli ya umeme.

Binafsi ukiniuliza katika hili, nasema hata kwa kukopa Tanzania ijenge reli ya umeme. Nauli za ndege zitapungua, mabasi nayo  yatabaki kwa ajili ya utalii, na yeyote mwenye safari ya kweli atatumia treni. Nchi zote zilizoendelea treni ndio uti wa mgogo wa uchumi. Hata wawekezaji wakijua treni ya kisasa inafanya kazi, bandari yetu itafanya kazi hadi tutashangaa.

Jambo la tano ni umeme wa uhakika. Rais Magufuli naomba unielewe katika hili. Wakala wa Umeme Vijijini (REA) amesambaza umeme katika baadhi ya vijiji, kikiwamo cha kwetu, Nyanga Bukoba, ila nakuthibitishia sura ya vijiji imeanza kubadilika. Umeme ni nguzo ya uchumi kwa nchi yoyote. Viwanda vinategemea umeme wa uhakika.

Ukiishakuwa na umeme wa uhakika vitaanzishwa viwanda, vitazalisha bidhaa zenye ubora, bidhaa zitauzwa katika soko la ndani na nje kwa bei nafuu, zitaingiza fedha za kijenge na ajira kwa Watanzania zitakuwa nje nje. Serikali itakusanya kodi za kutosha, itapata fedha nyingi itawekeza katika ujenzi wa barabara, hospitali, maji, shule (elimu), miundombinu na kila hali.

China inaongoza duniani kwa kutumia megawati 546,000 kwa saa kwa mwaka, Marekani ni ya pili kwa wanatumia megawati 468,000, Urusi inashika nafasi ya tatu kwa kutumia megawati 102,000. Afika Kusini ni ya 16 duniani kwa kutumia megawati 54,000 na Tanzania inatumia megawati 680. Kwa vyovyote iwavyo na kwa hali hii hatuwezi kuendelea.

Sitanii, inatupasa kama nchi kuweka lengo la kuzalisha hadi megawati 20,000 kwa kuanzia ndani ya miaka mitano ijayo, kisha baada ya hapo tuangalie uwezekano wa kuuza umeme nje ya nchi na kuanzisha viwanda vikubwa vya magari na mitambo vinavyochukua hadi megawati 500 kwa kiwanda kimoja. Hapo tunaweza kukuza uchumi.

Wiki ijayo, nitaendelea na suala la maji, afya na ajira za vijana, mama ntilie na mengine. Kwa leo naomba kuishia hapo, ila naomba kukumbusha mgogoro wa Zanzibar na hali ya kuwatowachukulia viongozi wa vyama vya upinzani kama wapinzani wako, bali washindani wako. Kwa kufanya hayo, nchi itaingia kwenye msitari. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

2668 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!