Wiki iliyopita ilikuwa ya majonzi makubwa kwangu, na naamini kwa Taifa letu kwa jumla.

Tumempoteza mwanasheria mahiri, Dk. Sengondo Edmund Mvungi, aliyevamiwa na majambazi nyumbani kwake Kibamba na kucharangwa mapanga. Baada ya Dk. Mvungi kucharangwa mapanga, alipelekwa Hospitali ya Mifupa Muhimbili (MOI) na baadaye akakimbizwa nchini Afrika Kusini, alikofia.

Mwili wake ulirejeshwa nchini siku ya Ijumaa, ukaagwa kwenye viwanja vya Karimjee Dar es Salaam siku ya Jumamosi na hadi tunakwenda mitamboni, mazishi yake yalitarajiwa kufanyika nyumbani kwao Moshi jana jioni.

Kwa wiki karibu yote tangu kifo chake kimetokea, nimebaki kinywa wazi. Sikujua niandike nini niache nini, nimesoma makala za watu mbalimbali, ila nikasema basi nami nieleze japo kidogo kile nikijuacho.

Nimemfahamu Dk. Mvungi rasmi mwaka 1999 tulipoanza kufanya kazi wote. Hapa Dk. Mvungi alikuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Marafiki zake wa karibu walikuwa Dk. Harrison Mwakyembe, wakati huo akifundisha Sheria za Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, Dk. Aggrey Mlimuka. Na mara kadhaa tulikuwa tukikutana na Profesa Chris Peter Maina.

Watano hawa tumefanya kazi kubwa ajabu. Moja ya kazi ninayoikumbuka ni mjadala wa Komandoo, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, alipotaka kubadili Katiba kugombea urais kipindi cha pili. Nakumbuka Dk. Mwakyembe alikuwa akitupakia katika Benzi lake la Kijerumani, linaloendeshewa mkono wa kushoto na kupiga muziki kwa kiwango cha juu tukielekea Pugu Road.

Watano hawa walinipa habari za kutosha hadi Komandoo Dk. Salmin Amour akabwaga manyanga. Nguzo ya habari zenyewe ilikuwa ni mpango wa Dk. Salmin kuongeza muda wa urais Zanzibar ifikapo mwaka 2000, kwamba alitaka apewe kipindi cha tatu.

Nakumbuka nilimhoji Dk. Mvungi baada ya Dk. Salmin kuwa ametoa kauli kuwa Zanzibar ni nchi na ina jeshi lake, na bila woga Dk. Mvungi akasema:

“Kama Dk. Salmin anatangaza kuwa Zanzibar ni nchi, na ina jeshi ndani ya Muungano, ni lazima akamatwe, ametangaza uasi dhidi ya mamlaka halali.”

Hii ilikuwa habari kubwa. Harakati hizi nilizianzia kwenye Gazeti la Majira, baadaye nikazihamishia Mwananchi. Kichwa cha habari kilisomeka, “Dk. Mvungi: Komandoo Salmin akamatwe.”

Siku iliyofuata tulikutana kama jopo na niliowataja hapo juu isipokuwa Profesa Maina, na wakafafanua Dk. Mvungi alimaanisha nini. Wakasema ili nchi itambulike kuwa ni nchi, kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna, lazima  iwe na watu, ardhi, jeshi na uwezo wa kusaini mikataba ya kimataifa. Wakasema Zanzibar ina watu na ardhi, lakini haina jeshi wala uwezo wa kusaini mikataba ya kimataifa. Hii pia ilikuwa habari kubwa.


Mambo yaliendelea na kimsingi niseme mahojiano na magwiji hawa wa sheria ndiyo yaliyonishawishi kusoma sheria hasa baada ya wao kunijuza kuwa nao walianza kama waandishi wa habari, baadaye wakasoma sheria na sasa (wakati huo) wanafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nikikumbuka enzi hizo, machozi yananibubujika.


Kama hiyo haitoshi, pamoja na kwamba muda wote tuliendelea kufanya kazi wote, tangu mwaka 2010, mimi Wakili Dk. Kapinga, James Mbatia, Wakili Mohamed Tibanyendera, Dk. Mvungi, waandishi Beatrice Bandawe na Frank Mdimu, tumekuwa tukienda mahakamani kila baada ya miezi mitatu hivi kulingana na muda alionao Jaji Aboud, kuendesha kesi ya Mbatia dhidi ya NBC Limited ya Mwaka 2003.


April 6, 2012 nikiwa Ikulu, Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alitangaza majina ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Lilitajwa jina la Dk. Mvungi. Nilipotoka Ikulu nikafika ofisini, nilimpigia simu Dk. Mvungi kupata maoni yake juu ya kuteuliwa kwake, alipopokea simu akasema: “Balile unasema kweli, wala mimi sijapata hizi taarifa, ndiyo unanijulisha. Unasema kweli? Basi kama ni kweli hii ni kazi ya kitaifa, na tutaifanya kwa moyo mmoja.”

Tangu wakati ameingia kwenye Tume ya Marekebisho ya Katiba, tumekuwa tukikutana tunajadiliana masuala mbalimbali na hata tunapokutana mahakamani kwenye kesi ya Mbatia, bado alikuwa akinieleza nini cha kufanya ili hatimaye kuwa mwanasheria mzuri. Yote haya sasa ni historia. Vibaka wamekatisha maisha yake kwa tamaa ya fedha zisizoenea hata kwenye kiganja.

Imeelezwa kuwa wamekamatwa watu 10 hadi sasa, mwingine kakamatwa na simu ya mkononi aliyokuwa akiitumia, mwingine kakamatwa na bastola yake, na wengine wametajana. Ni katika mazingira haya nasema kifo cha Dk. Mvungi tukitumie kama mbegu iliyopandwa, iote kuimarisha usalama wa Taifa hili.


Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuwa mjinga alipoamua kwa makusudi kuwa kuanzia nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961, wageni wote lazima wafahamike wanapofika katika familia fulani. Mfumo wa mabalozi wa nyumba kumi unapaswa kurejeshwa haraka. Amani ya Tanzania ambayo Mwalimu Nyerere aliijenga kwa utaratibu huu inapotea kwa kasi kubwa.

 

Mfumo huu wala hauna gharama, hauna itikadi za kisiasa. Hakuna itikadi katika usalama wetu. Hatuwezi kuwa na itikadi katika kuteteresha amani. Nasema wakati sasa umefika, Serikali ipeleke bungeni waraka maalum kurejesha mfumo huu. Tayari wananchi tunatumia gharama kubwa. Watanzania wengi kila jioni tunalala magerezani bila kuhukumiwa na Mahakama.


Nyumba nyingi zimezungushiwa magrili, mageti ya chuma mithili ya magereza. Hata ikitokea ajali ya moto ndani, ni vigumu mtu kutoka kwa kupitia dirishani. Kwa wenzetu Ulaya na Marekani, unakuta dirisha la futi 6 x 6 ni kioo kitupu bila nondo hata moja. Ndiyo, wanatumia kamera za usalama, lakini huwezi kupangishwa nyumba bila kuwa na barua ya mamlaka husika.


Ukienda kupangisha nyumba lazima uwe na ama hati ya kusafiria au barua ya utambulisho, itakayoonesha wewe ni nani, umekwenda pale kufanya nini, utakaa muda gani na nani anagharimia maisha yako kwa muda unaokuwa nchini mwao. Wadhamini wako lazima wafahamike, lakini hapa kwetu tumeachia tu.

Zipo nyumba nyingi, ambazo wenye nyumba hawafahamiani na wapangaji. Madalali na watu wa kati ndiyo waliogeuka wapangishaji, na matokeo yake majambazi, vibaka na wezi wa kutupwa kutoka mataifa mbalimbali wamemwagika hapa nchini. Polisi nao wana vitendea kazi duni, gari linawekewa lita 10 kisha anamwambia afukuze majambazi yenye V8 iliyojaza lita 200!

 

Watanzania tuache utani na maisha yetu. Wala hakuna gharama yoyote kurejesha mabalozi wa nyumba kumi. Sheria inaweza ikatungwa na kuweka kiwango cha kila mkazi wa mtaa mmoja au mwingine kuchangia gharama za ulinzi kwa mwezi, badala ya kukaba nyumba na magrili, hadi hapo Serikali itakapopata uwezo wa kugharimia ulinzi wa wananchi wake.

Nasema kifo cha Dk. Mvungi kituamshe sasa. Tufanye uamuzi waraka upelekwe bungeni, turejeshe mabalozi wa nyumba kumi kuimarisha ulinzi. Tukipuuza hili, magaidi wapo milangoni kwetu na hata majambazi wanatunyemelea. Tuchukue hatua. Tanzania ni yetu sote, tukizembea hakuna atakayepona.


1554 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!