Matukio ya ugaidi yanayoendelea sehemu mbalimbali hapa nchini, yanathibitisha pasi shaka kuwa kundi la al-Shabaab la nchini Somali tayari lina makazi yake hapa nchini Tanzania.

Oktoba 7, mjini Mtwara walikamatwa vijana 11 wakifanya mafunzo ya ugaidi katika Mlima wa Makolionga wilayani Nanyumbu, na walikutwa wanamiliki silaha za moto, mapanga na DVD 25 zenye miongozo ya mafunzo ya al-Shabaab. Hii ilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen.

“Moja ya DVD waliyokutwa nayo ilikuwa na programu yenye jina Zinduka Zanzibar,” Stephen alisema.

“Inafundisha namna ya kuua kwa haraka na kutoa mafunzo kwa wanamgambo. DVD nyingine zilikuwa na mafunzo yanayohusu ugaidi yanayohusiana na al-Shabaab.”


Mohammed Makande mwenye umri wa miaka 39 alitajwa kuwa kiongozi wa watuhumiwa waliokamatwa. Naye alitiwa mbaroni. Watuhumiwa wengine walibainishwa kuwa ni Said Mawazo (miaka 20), Ismail Chande (miaka 18), Abdallah Hamisi (miaka 32).


Wengine ni Ramadhani Rajabu (miaka 26), Salum Wadi (miaka 38), Hassan Omary (miaka 39), Fadhili Rajabu (miaka 20), Abbas Muhidini (miaka 32), Issa Abeid (miaka 21) na Rashid Ismail (miaka 27).


Wakati hayo yakitokea Mtwara, Oktoba 28, wilayani Kilindi huko Tanga, Jeshi la Polisi limekamata watuhumiwa 69 wanaodaiwa kujihusisha na ugaidi. Katika msako huo, watoto 74 na wanawake 32 walikombolewa. Hadi sasa watoto 20 bado wapo kwenye kambi maalum ya kuwarejesha kwenye utu baada ya kuwa wamepewa mafunzo ya imani kali kwa kiwango cha kukana wazazi wao kuwa si Waislamu halisi.

DC wa Kilindi asimulia

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa, ameiambia JAMHURI kuwa msako wa kwanza uliwawezesha polisi kukomboa wanawake 32 na watoto 54 waliounganishwa na familia zao.

Ilibainika kuwa watoto hao walikuwa wanatoka maeneo ya Singida, Lushoto, Tanga na Dar es Salaam.

 

“Ilibidi tuwawezeshe nauli kuwarejesha nyumbani kwao,” anasema Liwowa.

Anasema baada ya kuwapata watoto hao kutoka katika msitu wa Lwande, waliitisha mkutano mkuu wa Kijiji cha Lwande, lakini kutokana na hali waliyokuwa nayo watoto hao na mafunzo waliyokwishapata ya ugaidi, wanakijiji waliwakataa watoto hao.

 

Nao walipoulizwa maeneo ambayo wangependa kwenda, kina mama na watoto wao walisema wanataka kurejea katika vijiji vya nyumbani kwao kwani wengi walikuwa wahamiaji, hivyo ulifanywa utaratibu wa kuwarejesha makwao.

 

Ukiacha watoto hawa na wanawake waliokombolewa kwenye eneo la Lwande, wapo watoto wengine 20 waliokombolewa kwenye eneo la Madina. “Hawa walikuwa afya zao zimedhoofika, maana wengine walikuwa na kichocho na minyoo,” anasema Liwowa.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua jukumu la kuwaweka watoto hawa katika Kituo cha Usawi wa Jamii jijini Tanga, kwa nia ya kuwapa matibabu na ushauri nasaha kwani hali zao zilikwishakuwa mbaya kutokana na mafunzo ya ugaidi waliyopewa.

 

“Watoto hawa walikuwa na mafunzo ya jinsi ya kutumia visu, mapanga na hata kupambana bila silaha. Kati yao wamo watoto wenye umri wa miaka saba. Unashangaa walifikaje mikononi mwa watu hawa kufundishwa ugaidi,” anasema Liwowa.


Awali, baadhi ya wazazi walivieleza vyombo vya dola kuwa watoto wao walipelekwa hapo

kwenye Msikiti wa Madina kufundishwa Korani Tukufu, lakini kinyume na matarajio, madaftari yao yamejaa maandishi yenye kufundisha mbinu za kivita.

 

“Wameandika kabisa jinsi ya kucheza kareti, judo, kungful, kuua, kupambana na mtu mwenye silaha au asiye na silaha, nini unapaswa kufanya hatua ya kwanza, akikuzidi nguvu na kama hajatumia silaha umpige wapi.

 

“Na hata tulipowahoji mafundisho haya yana malengo yapi, watoto hawakuficha. Walisema kuwa walimu wao walikuwa wanawafundisha kuwalenga ‘makafiri’ ambayo wanadai yametawala Afrika Mashariki. Wanafundishwa kabisa mbinu za kuhujumu uchumi na mambo mengi ya ajabu,” anasema Liwowa.

Al-Shabaab walifika lini Kilindi?

Kwa mujibu wa DC Liwowa, watu wanne ambao ni wafuasi wa al-Shabaab walifika wilayani Kilindi mwaka 2008. Walifikia katika Kijiji cha Lwande. Kwa muda waliishi na wanakijiji wa Lwande, na wanakijiji wakawa wamewapokea kama Waislamu wenzao.


Baada ya muda walianza kutoa mafundisho ambayo hayaendani na utamaduni wa Kitanzania. Kutokana na hali hiyo, Liwowa anasema walifarakana na wanakijiji wakajitenga na kununua eneo lao kisha wakajenga msikiti unaitwa Madina. Eneo hili walilojenga msikiti sasa linafahamika kama Answar Sunni.


Viongozi wa msikiti huu mpya sasa waliendelea kuongezeka na wengi wakitoka Dar es Salaam, Kigoma na Singida. Kiongozi Mkuu wa walimu hawa wa wanafunzi alifahamika kwa jina la Ayubu, lakini ndani ya Kilindi alijulikana kwa jina la ‘Master.’ Huyu, alipopata taarifa za ujio wa polisi kwenye msikiti wa Madina, kwa kutumia mazoezi na mbinu za kigaidi alitokomea porini na hadi sasa hajapatikana.


Msaidizi wake aliyekamatwa, naye alifahamika kwa jina moja la Jumanne. Jumanne ni mwenyeji wa Singida, alikuwa ameoa ana mke na watoto watatu hapo Kilindi.


Ukiacha mgogoro huo uliowaondoa katika msikiti wa awali, pengine wananchi wa Kilindi waliwaamini kutokana na kwamba walijitambulisha kama wachimba madini (dhahabu) katika eneo la Kilimamzinga. Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa walimu wengi waliokuwa wanafika hapo Midelo ulipo msikiti wa Madina si wenyeji wa Kilindi, bali wanatokea Bagamoyo, Somalia na Mombasa.


Walifahamika ni magaidi waliponyanyasa wenyeji

Taarifa za watu hawa kuwa magaidi zilianza kuvuja baada ya kuanza kunyanyasa wenyeji wa Kilindi. Walizidi kuongezeka na kuwa wengi, na kila mara walianza kuchukua mashamba ya wenyeji bila fidia. Maelezo yao kwa wenyeji ilikuwa ni kwamba ardhi ni mali ya Mungu, na wao wametumwa na Mungu hivyo ni haki kwao kuichukua bila fidia.


Idadi ya wageni katika kambi hii iliongezeka zaidi mwaka jana wakati Sheikh Ponda Issa Ponda alipokamatwa na polisi na baadhi ya wafuasi wake wakawa wanasakwa, anasema Liwowa.  Anasema wengi wa wafuasi wa Ponda walikimbilia eneo hili la Madina.


Katika msitu wa Dibungo, katikati ya Kilindi na Bagamoyo, wakubwa hawa walianzisha kambi. Waliteka ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 na katikati ya eneo hili wakajenga uwanja wa mazoezi. Kwa nje walijenga vibanda kuzunguka eneo hili, na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia katikati ya msitu huu.


“Pia walijenga msikiti katika msitu huu, na walikuwa wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku. Walikuwa wanafanya mazoezi saa 11 jioni na saa 11 alfajiri,” anasema Mkuu wa wilaya.


Bahati mbaya kwao na bahati nzuri kwa Serikali, uhusiano kati ya wafuasi hawa wa al-Shabaab na wanakijiji wa maeneo yaliyozunguka kambi yao hii ulizorota. Wenyeji wengi ni wafugaji, lakini wafuasi hawa wa al-Shabaab walianzisha utaratibu wa kutoza kodi ya mifugo au faini ya mifugo kwa ng’ombe wanaoingia kwenye msitu huu.


“Ilikuwa ng’ombe wakiingia kwenye msitu huu kula majani, basi watu hawa wanawateka ng’ombe na kuwatoza faini ya ng’ombe wawili. Ilikuwa mfugaji akibishi, basi wanachukua kundi lote la ng’ombe na hapo ndipo mgogoro ulipofumka na siri ikavuja na kuvifikia vyombo vya dola kuwa kuna watu wanaishi porini,” anasema Liwowa.


Hatari iliyo kubwa zaidi, kambi hii imetumika kutoa mafunzo kwa vijana ambao inaelezwa kuwa wamekuwa wakisafirishwa kutoka Kilindi, kupitia Mombasa na kwenda Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab.


“Tuliwakuta na mikanda minane, baadaye tulivyofanya upekuzi tukapata mikanda mingine minne hivyo ikawa jumla mikanda 12. Mikanda hii ina mafundisho ya al-Shabaab, yenye kusisitiza kuwa Afrika Mashariki imekamatwa na makafiri, hivyo wanafundishwa namna ya kuikomboa kijeshi,” anasema Liwowa.

Taarifa za awali

Wakati wafuasi hawa wa al-Shabaab inaelezwa kuwa kuna siku walikuwa wanafanya mazoezi ya kutumia majambia, mmoja wa wanafunzi wao akakatwa na jambia utumbo ukatoka nje. Baada ya kuumia, walimbeba wakaenda kumtelekeza porini, wananchi wakati wanapita walimuona na kujiuliza kulikoni, kisha wakambeba na kumpeleka kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimamba.

 

Mwenyekiti wa Kijiji aliwaambia wampeleke Handeni polisi akapewe PF3, watu hao mwanzo waligoma kumpeleka polisi, ila baadaye wakakubali. Hata hivyo, mtu huyo alifia njiani kabla hawajafika polisi. Baada ya hapo, Mwenyekiti aliwasisitiza wampeleke mtu huyo polisi kwa ajili ya kuandikisha repoti, ila wao walikataa wakasema ni mtu wao watakwenda kumzika, kisha wakatokomea naye porini.


“Sasa huyu kijana alikuwa anasema alitokea Kilimanjaro, akaenda Zanzibar halafu ndiyo akaja Kilindi, kwa hiyo hii nayo ilianza kuleta wasiwasi kwa wanajamii maana tangu afariki haikujulikana amezikwa wapi na iwapo ndugu zake wanafahamika. Taarifa zikaanza kufika serikalini,” anasema Liwowa.


Anasema baada ya polisi kupekua vibanda vyao, walikuta maelezo binafsi (CV) za walimu waliokuwa wanafundisha watoto hao, kuna vitabu vya utabibu na matumizi ya mitishamba kwa mtu anayeumia akiwa porini, vizibo vya modem za mtandao wa Internet, hali inayoashiria kuwa watu waliokuwa pale ni wasomi waliobobea. Anasema watu 65 wamekamatwa na wote walipelekwa Handeni polisi.

DC Halima Dendego anena

Halima Dendego, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga na Kaimu Mkuu wa Mkoa, ameiambia JAMHURI kuwa watoto 20 waliotolewa kwenye Msikiti wa Madina, wamewekwa chini ya Ustawi wa Jamii kwenye kituo kimoja jijini Tanga (hakukitaja), kwa ajili ya kuwapa matibabu na ushauri nasaha kwani walikwishapandikizwa msimamo mkali.


“Hawa watoto wote 20 ni wa Kilindi. Wengine wanasema jinsi gani walivyokuwa wanafundishwa, ila kinachoshangaza unakuta mtoto ana miaka minne naye yumo kwenye kundi la mafunzo haya. Sasa unajiuliza mzazi wake aliridhia kweli, yupo kweli huyu mzazi? Napata tabu kweli kuwaelewa,” anasema.


Anasema watoto hawa watapewa ushauri nasaha kwa wiki tatu na ikithibitika kuwa wamerejea katika hali ya kawaida na kuondokana na kuwakana wazazi wao kuwa si Waislamu wa kweli, basi wataunganishwa tena na familia zao.


“Ukiwauliza wanasema ‘tuliambiwa tunaenda kusoma Korani’. Dunia ya leo kweli unaacha kukumbatia elimu? Nadhani wazazi wanapaswa kuelezwa sasa kuwa tatizo kubwa tulilonalo ni elimu, na bila kuwapa elimu watoto wetu itakuwa rahisi mno kutumika kwa kuchotwa akili sawa na ilivyowatokea watoto hawa,” anasema Dendego.


Amewataka Watanzania kuungana kupinga matendo ya ugaidi kwa maelezo kuwa hayana faida kwa mtu binafsi au Taifa, zaidi ya kupandikiza chuki isiyo ya lazima na kuondoa amani katika Taifa hili. “Tusikubali kuelekea huko,” anasema.

Kamanda Massawe aonya

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, aliiambia JAMHURI kuwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita walikuwa wamekamatwa jumla ya watu 69 na uchunguzi bado unaendelea. Alisema matendo hayo kwa sasa hayavumiliki na watu wote wanaoyafanya watakutana na mkono wa dola bila huruma.


Kamanda Massawe amesema polisi wameamua kutumia ulinzi shirikishi katika Wilaya ya Kilindi, na anaamini kuwa hao polisi jamii wanayafahamu vyema maeneo husika, hivyo itakuwa rahisi kuwadhibiti watu wanaofanya vitendo vya ugaidi.


Pia aliwataka wananchi kutokubali kupokea wageni wasiofahamu wametokea wapi na wana malengo yapi, kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujikuta wanaliingiza Taifa katika matatizo makubwa pasipo ulazima. Alisema uchunguzi bado unaendelea.


Robert Manumba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai kabla ya kustaafu wiki iliyopita, alipohojiwa na JAMHURI juu ya Tanzania inafanya nini kukabiliana na tishio la al-Shabaab linaloonekana kuongezeka, alisema polisi wanashirikiana na mashirika mengine ya usalama kupambana na tatizo hilo.


“Tumeunganisha idara zote za usalama kuunda timu maalum. Timu hiyo inahusisha maofisa usalama kutoka polisi, jeshi, Usalama wa Taifa, Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania, ambao wanafanya kazi kwa kushirikiana kutafuta suluhisho la kudumu,” Manumba alisema.


Oktoba 31, pia polisi Tanga walimkamata mfanyabiashara Juma Abdallah Kheri akishukiwa kwamba alikuwa akijihusisha na kugharimia makundi ya kigaidi nchini Tanzania na washirika wa al-Shabaab nchini Kenya. Kheri hadi sasa yuko rumande. Matukio haya ni ishara mbaya ambayo wachunguzi wa mambo wanasema hata nchi zilizoko kwenye matatizo makubwa kama Somalia, yalianza kidogo kidogo na kulifikisha taifa lao kuwa vipande.


Pendekezo kubwa linalotolewa kama njia ya haraka ya kuimarisha usalama na kumaliza ugaidi, ni kurejesha mpango wa mabalozi wa nyumba kumi kumi wanaoaminika kuwa wataandikisha wakazi wote wa mtaa husika na kuweka kumbukumbu za nani anaishi wapi na anafanya nini.

2082 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!