MAANDIKO YA MWALIMU NYERERE

Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (7)

Wiki iliyopita tulichapisha sehemu ya sita katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, ambapo Mwalimu Nyerere anasema wazi kuwa baada ya kushauri ikashindikana, alirejea kijijini Butiama na kuamua kuandika utenzi. Leo, Mwalimu anasimulia nini kilimsukuma kuwaza kuwa uongozi wa CCM ulikuwa umepwaya wa kiwango cha kuhitaji nahodha mpya. “Hawawezi kutetea sera ya Chama ya Serikali Mbili wala mwelekeo wa Chama wa Serikali Moja. Watatumia uwezo walionao kutokana na hadhi walizonazo kuvuruga sera ya Chama na mwelekeo wake. Tutahitaji kiongozi mpya wa Serikali na kiongozi mpya wa Chama.” Endelea…DODOMA 12/11/1993

Nadhani uamuzi wa kuitisha kikao cha mchanganyiko ulifanywa na viongozi wetu katika kikao cha Dodoma II. Nimesema awali kwamba Waziri Mkuu alipohisi kuwa baadhi ya mawaziri wenzake walikuwa wanaunga mkono hoja ya Utanganyika na yeye kwa wakati huo alikuwa hajui aiunge mkono au aipinge, alipendekeza ifanyike semina ya viongozi wote ili jambo hili lizungumzwe na lipingwe nje ya Bunge.

Viongozi ambao wangehudhuria katika semina hiyo ndiyo walioalikwa kuja katika kikao cha mchanganyiko cha Dodoma.

 

Lakini shabaha ya kuwakutanisha ilikuwa imebadilika. Kama semina ya awali ingefanyika, shabaha yake ilikuwa ni kupinga hoja ya wabunge na mimi niliombwa niende nisaidie.   Kamati Kuu ya CCM ikaamua kuwa hapakuwa na haja ya kufanya semina hiyo.

 

Lakini baada ya kuona msimamo wa Halmashauri Kuu ya Taifa na ugumu wa kushawishi wajumbe wake wakubali hoja ya Serikali Tatu, viongozi wetu walifufua tena lile wazo la semina.

 

Huenda waliona wanahitaji msaada, na kwa kuwa sasa hoja ni ya wabunge wote, walihisi kuwa itafaa itafutwe njia ya kuikutanisha Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na wabunge wote.

 

Na kwa kuwa isingetoa sura nzuri kuita wabunge peke yao, ikapendekezwa kuwa Serikali ya Mapinduzi na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nao waitwe!

 

Mazungumnzo na maamuzi ya kikao hicho cha mchanganyiko yanafahamika vizuri zaidi, na hayana haja ya kuelezwa sana. Inatosha kusema kuwa wote walikubaliana, na baada ya mjadala wa wazi wazi, kwamba sera ya Serikali Mbili ni sera ya Chama Cha Mapinduzi, wakapendekeza kuwa suala hili lizungumzwe na wanachama wa CCM ili tupate maoni yao.

 

Ni aina ya referendamu; lakini badala ya kutafuta maoni ya wananchi wote, waulizwe wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kama wanataka:

(i) Tubaki na Sera ya Serikali Mbili;

(ii) Tuibadili na kuwa na sera ya Serikali Tatu; au

(iii) Tuibadili na kuwa na sera ya Serikali Moja.

 

Jambo hili yafaa lisisitizwe. Viongozi wetu, kama kawaida yao, walipachika maneno “haja ya kuwa na Serikali ya Tanganyika,” katika mapendekezo ya kikao cha pamoja.

 

Hizo ni hila; maelewano sivyo yalivyokuwa. Mapendekezo ni kwamba sera ya Serikali Mbili, izungumzwe ndani ya Chama ili kuona kama pana haja ya kuibadili.


Kikao kile hakikusema kuwa endapo wanachama wetu wataamua kubadili sera ya Serikali Mbili, basi wazingatie hoja na haja ya kuwa na Serikali Tatu. Kwa bahati njema maswali waliyoulizwa wanachama wa CCM yanazingatia na kuheshimu uhuru wao, bila kujali hila hizi za viongozi.


Hapo ndipo tulipo hivi sasa. Mimi nitashangaa kabisa ikiwa wanachama wa CCM watasema kuwa wanataka Serikali ya Tanganyika. Iwafanyie kazi gani ambayo haiwezi kufanyika hivi sasa? Nakuvunja Muungano kutawafaa nini, wao na raia wenzao? Na Wana uhasama gani na Wazanzibari? Au wamewafanyia nini hata waseme wamechoka nao?

 

III. HAJA YA KUWAJIBIKA

Kabla ya kuondoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ambako nilionana na watangazaji wa habari baadaye, nilipata nafasi ya kuzungumza na Rais kuhusu matokeo ya mkutano wa pamoja na nini la kufanya. Nilimweleza maoni yangu. Kwa kuwa mazungumzo haya yanayotakiwa yafanywe na wanachama wa CCM ni ya kusukumizwa na hayana maelezo si busara kufanya haraka. Ilikuwa imetangazwa kuwa Rais atateua kamati ya kuratibu maoni ya wananchi.


Nilitazamia kuwa badala yake atateua kamati ya kusimamia utaratibu wa kupata maoni ya wanachama.


Nilishauri ateue kamati ya watu makini; iongozwe na mtu mwenye busara, iandae maelezo yatakayokuwa mwongozo wa mazungumzo yatakayofanywa na wanachama wa CCM.


Wanachama hawana budi waelezwe kwa nini tunataka wazungumze muundo wa Muungano. Lazima tueleze tena asili ya muundo wa Serikali Mbili. Tuwasaidie wanachama na wananchi kwa jumla kuelewa sababu za muundo huo; uzuri wake na upungufu wake.


Lazima tueleze ni upungufu gani tunadhani unatokana na muundo wenyewe, na ni upungufu gani unaotokana na utekelezaji tu. Lazima tuchambue namna mbalimbali za kuendesha Muungano; jinsi ya kurekebisha muundo wa SerikaIi Mbili, na jinsi ya kuondoa upungufu unaotokana na utekelezaji.

 

Kamati hiyo ingeweza kusaidiwa na kazi ambayo imeanzwa na kamati mbali mbali za Chama na SerikaIi. Kama itaonekana kuwa muundo wa Serikali Mbili lazima uachwe, hatuna budi tuchambue na kueleza faida na hasara za miundo mbali mbaIi: muundo wa Serikali Moja, na muundo wa SerikaIi Tatu.

 

Tunaweza, tukipenda, kuchambua na kueleza pia faida na hasara za kuwa na muundo wa Serikali zaidi ya Tatu.


Kinachopendekezwa na washabiki wa Serikali Tatu ni Muundo wa Shirikisho. Wako watu wanaoamini kwamba ni rahisi zaidi kuwa na Shirikisho la Zanzibar yenye Serikali Moja na Tanganyika yenye Serikali zaidi ya moja, kuliko kuwa na Shirikisho la Zanzibar yenye Serikali Moja na Tanganyika yenye Serikali Moja.


Yote haya yanatakiwa yachambuliwe na kuelezwa vizuri kabisa. Na wakati huo huo maelezo hayo hayana budi yasisitize historia na mwelekeo wa nchi yetu na Chama Cha Mapinduzi. Historia yetu na mwelekeo wetu mpaka sasa umekuwa ni wa kuimarisha Muungano.


Kama tunaona kuwa inafaa kuacha muundo wa Serikali Mbili hatuna budi tuseme wazi wazi katika Mwongozo huo, kwamba kwa maoni ya uongozi wa Chama muundo unaoweza kuendeleza historia na mwelekeo wa nchi yetu, ni muundo wa Muungano wa Serikali Moja. Uongozi wa Chama hauwezi kusema kuwa hauna maoni yake, ila unasubiri maoni ya wanachama! Kuongoza ni kuonesha njia.


Baadaye wanachama wa CCM walipoombwa watoe maoni yao kuhusu suaIa hili hapakuwa na maelezo wala mwongozo kama huo. Sababu zinazotolewa ni kwamba viongozi wetu hawakutaka waonekane kama wanawashawishi au kuwalazimisha wanachama kufuata msimamo fulani.


Nadhani ukweli ni kwamba viongozi wetu walidhani kuwa sera ya Chama isipokuwa na mtetezi wake na uwanja ukaachwa wazi kwa washabiki wa Serikali Tatu, basi wanachama wa CCM watakubali hoja ya Utanganyika. Lakini hata bila maelezo hayo na mwongozo huo siamini hata kidogo kwamba wanachama wa CCM watakubali hoja ya Serikali Tatu.


Ilikuwa ni dhahiri kwamba kazi hii haiwezi kufanywa chini ya usimamizi wa viongozi waliopo. Hawa sasa wanaona kuwa heshima yao na “nyuso” zao, na labda baadaye zao, zinawadai watetee msimamo wa Serikali Tatu. Hawawezi kutetea sera ya Chama ya Serikali Mbili wala mwelekeo wa Chama wa Serikali Moja. Watatumia uwezo walionao kutokana na hadhi walizonazo kuvuruga sera ya Chama na mwelekeo wake. Tutahitaji kiongozi mpya wa Serikali na kiongozi mpya wa Chama.

MAANA YA MANENO: kisanduku 3

Neno la Kiingereza “resign”, lina maana mbili: .

 

(i) to give up or surrender (one’s job or property or claim etc.). Ni kuacha au kuachia; kama kuacha au kuachia, (kazi, au mali au haki, au madai n.k.). Maana ya “give up”; to cease (doing something); to part with; to surrender; to abandon hope; to declare a person to be incurable or a problem to be too difficult for oneself to solve.


Ni kuacha (kufanya jambo); kuachia au kuachana na; kusalimu amri; kukata tamaa; kusema kuwa mtu hatibiki au tatizo fulani linakushinda kutatua.


Maana ya “surrender”: (1) to hand over, to give into another person’s power or control, especially on demand or under compulsion.


Ni kutoa kwa, au kumwachia mwingine uwezo au mamlaka, hasa kwa kudaiwa au kulazimishwa.

 

(2) to give oneself up, to accept an enemy’s demand for submission.

Ni kusalimu amri, kukubali amri ya adui ya kujitolea. Hayo ndiyo maelezo ya maana ya kwanza ya neno “resign,” yaani “jiuzulu”.

 

(ii) Maana ya pili: “Resign onself to”: to be ready to accept or endure, accept as inevitable.

Ni kuwa tayari kukubali na kustahimili; kukubali kuwa jambo fulani ni lazima liwe, halizuiliki. Ni kukubali kuwa umeshindwa au utashindwa, na kuwa tayari kustahimili matokeo ya kushindwa. Ni kukubali kusalimu amri ya adui au mpinzani wako na kuwa tayari kustahimili matokeo yake. Ni kukubali kutekwa na kuwa tayari kustahimili matokeo ya kuwa mateka. Ni kukubali kushindwa; ni kubwaga silaha.


Mkazo katika maana hii ya pili ni kule kukubali kustahimili matokeo ya kukata tamaa na kubwaga silaha.