Mmoja wa Makocha wenye heshima katika ukanda wa Afrika  Mashariki na Kati (EA), Adel Amrouche aliwahi kutoa  maoni yake juu ya kwa nini ukanda huu haupigi hatua katika soka.

Kwa wasiomfahamu, amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Burundi na baadae kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya (Harambe Stars) na  vilabu kadhaa, kama DC Motema Pembe (Congo DRC) na USM Algear (Algeria).

Kwa hiyo ni mtu anayelijua soka la ukanda huu. Mtaalamu huyo, raia wa Ubelgiji alishangaa jinsi nchi za AfrikaMashariki na Kati ambavyo zimekuwa hazipati nafasi katika mashindano ya makubwa barani Afrika kama kombe la mataifa ya Afrika (AFCON), huku  vyama vya soka katika nchi husika vikiwa havifanyi jitihada kukabiliana na changamoto hiyo.

Alishangaa kuona nchi zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara kutoa timu nne tu kwenye mashindano ya Afcon yaliyo fanyika nchini Guinea ya Ikweta mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa katika mashindano yaliyopita timu zilizofanikiwa kufuzu kwenye fainali hizi kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara zilikuwa ni Zambia, Afrika ya Kusini, Congo

DRC na Congo Brazaville huku ukanda wa Afrika Mashariki ukiendelea kuwa mtazamaji.

Kocha huyo alitaja sababu nyingi zinazoendelea kuua soka la ukanda huu, lakini moja ya sababu kubwa aliyoitaja ni siasa na  ambayo imejipenyeza kuanzia kwenye vilabu, vyama vya michezo mpaka katika timuza taifa.

Kwa mujibu wa Kocha huyo timu nyingi za ukanda wa Afrika Mashariki ya Kati zimejikuta zikifanya mambo ya ajabu kwa kuingiza siasa hata katika masuala yanayohitaji utaalamu.

Alienda mbali kwa kusema kuwa ni katika ukanda huu ambapo unakuta watu wanatumia nguvu kubwa kuanzisha mashindano ya mitaani kwa malengo ya kisiasa na si kwa malengo ya kukuza soka.

Ubabaishaji huo unaoanzia kwenye vilabu hadi ngazi ya juu  umechangia kwa kiwango kikubwa kudorora kwa timu za taifa za nchi husika huku viongozi  wasijue la kufanya.

Alisema soka katika ukanda huu limegeuka kuwa sawa na biashara za watu binafsi wenye kujali maslahi yao na kujikuta wakisahau wajibu kuliendeleza soka.

Kocha huyo alimaliza kwa kusema kuwa itachukua miaka mingi kwa ukanda huu kufikia mafanikio yanayotakiwa endapo viongozi kuanzia ngazi ya chini hadi taifa hawatabadilika.

Kauli hii iliyo tolewa na mtaalamu huyo inaashiria kuwa itachukua miaka mingi kwa soka la ukanda huu wa Afrika Mashariki  na Kati kuanza safari ya huko waliko wengine katika soka.

Ukitaka kupata ukweli wa aliyosema mtaalamu huyo jaribu kuliangazia soka la hapa kwetu Tanzania kuanzia kwenye vilabu vyetu, chama cha soka mpaka timu ya taifa.

Hebu angalia vinavyoendelea ndani ya vilabu vyetu kuanzia ligi kuu na ligi daraja la kwanza. Timu zetu hazina mipango yoyote ya maana ya kukuza soka, halafu kesho utarajie miujiza kutoka katika timu hizo.

Kwa mfano kwa hapa nyumbani hebu iangalie klabu ya Simba ndani ya miaka mitatu ya nyuma imekuwa ikisajili wachezaji vijana kwa lengo la kujenga timu ya muda mrefu mwisho wa siku wote wanapotea.

Cha ajabu ligi inapoisha timu hiyo inajikuta ikipanguliwa na kuanza usajili upya hali ambayo imeendelea kuidhofisha klabu hiyo kwa miaka mingi sasa.

Huu ni mfano mdogo wa ubabaishaji ambao umeendelea kuididimiza nchi katika masuala ya michezo mingi. Kama hiyo haitoshi, hebu jaribu kuiangalia michezo mingine kama riadha, masumbwi, kuogelea na michezo mingine kote huko kila kukicha ni migogoro isiyoisha.

Kwa kuedeleza hizi siasa ndani ya vilabu vyetu kamwe tusitarajie kupata timu ya taifa imara kwani uimara wa timu ya taifa hutegemea uimara wa vilabu.

Ukitaka kujua kuwa uimara wa timu ya taifa huanzia kwenye vilabu hebu waulize Waingereza kwa yale yanayowakumba kwenye timu yao ya taifa ni matokeo ya kuwa na vilabu vilivyodorora.

Sababu nyingine aliyeitaja mtaalamu huyo ni kukosekana kwa mipango thabiti ya kukuza vipaji vya watoto kitu kinachoendeea kuvifanya vilabu kukim bilia kunua wachezaji kutoka nje ya nchi na nyingine kubadilisha mara kwa mara makocha wao wakidhani wanachangia kushindwa kwao.

Kwa hali ilivyo katika vilabu vyetu nchini hakika tusitegemee hata siku moja kufanya vizuri kwenye timu ya taifa hata kama leo au kesho tutamleta Dunga au Ferguson kuwa kocha wa timu yetu ya taifa letu bila kujenga misingi katika ngazi ya vilabu.

1099 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!