Mzee wa Kiraracha aliposhinda uchaguzi mdogo wa ubunge wa Temeke mwaka 1996 alisema ameanza kuichukua nchi kirejareja. Lyatonga Mrema alikuwa ndio ametoka kushindwa uchaguzi wa rais na William Benjamin Mkapa, ndipo ‘kihiyo’ akatokea pale Temeke akachukuliwa na maji ya fitna za kisiasa na uchaguzi ukaitishwa.

Nakumbuka hali hiyo, kwa sababu nilikuwa likizoni baada ya kuwa nimehitimu udaktari wangu huu wa magonjwa ya binadamu. Nilipenda magazeti yalivyoandika, maana nilikuwa nimeshapata joto la siasa pinzani za nusu kwa nusu hapa kwa Malkia, tofauti na tisini kwa kumi au thamanini kwa ishirini za hapo Tanzania.

 

Urejareja huo na huu wa wanasiasa wa Labour si sawa, maana huu una uhai zaidi kama nilivyokuandikieni pale uchaguzi wa serikali za mitaa Labour ilivyoongoza. Itakuwa vyema wana Jamhuri wenzangu kukumbuka kwamba Uingereza inaongozwa na serikali ya mseto, kwa sababu hakuna chama kilichopata kura za kutosha.

 

Laiti Liberal Democrat (chama cha Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg, kidogo kama cha akina Cheyo Mapesa hapo) kingekubali kuungana na Labour baada ya uchaguzi ule, tungekuwa tunazungumzia mengine. Hiki ndicho chama kilichokuwa kama mkata mzizi wa fitna, kwani kiliambulia viti vichache katika nafasi ya tatu baada ya Conservative cha Waziri Mkuu David Cameron na Labour ya Ed Miliband na Ed Balls.

 

Kwa hiyo, Clegg akaamua kuwaunga mkono Conservatives, ndipo wakaunda serikali chini ya Cameron. Ndoa yao imekuwa ya masumbufu katika muda wake mfupi, angekuwa mke, tungesema anapigwa, mradi si Mkurya, basi ni tatizo. Leo serikali imefikia mahali Waziri Mkuu (PM) na naibu wake wanatofautiana mpaka naibu analikimbia Bunge, anapokuja kuulizwa kulikoni anasema aliona ngumu kuongea tofauti na PM pale pale hivyo akakitoa mjengoni.

 

Chaguzi ndogo zimekuja tatu na kama kumsukuma mlevi vile, Labour imechukua viti vyote, kitu ambacho ni pigo kubwa kwa watawala walio madarakani. Kama hiyo haitoshi, Liberal Democratic wameanguka vibaya mpaka nafasi ya nane kwenye Jimbo la Rotherham, matokeo mabaya kabisa kwa chama kikubwa.

 

Wabunge walioshinda na viongozi wao wamejenga hoja kwa wananchi kwamba Liberal Democrats wanaelekea kaburini kwenye Uchaguzi Mkuu ujao na Conservative watabaki tu kama mashahidi wa ushindi wa Labour.

Wapiga kura waliwaadhibu vibaya watawala, ambapo baada ya kuwapa Labour nafasi ya kwanza, ya pili waliitoa kwa UK Independence Party (Ukip).


Kwenye chaguzi mbili kati ya hizo tatu, ushirika unaoitawala Uingereza ulionja aibu ya karne kwa kupata pungufu ya asilimia tano ya kura. Conservative walishika nafasi ya tano hapo Rotherham na ya nne pale Middlesbrough

Waingereza wameanza kusema kwamba wanataka mabadiliko, ambapo vyama vidogo kama Ukip na Peace vimepewa kipaumbele baada ya Labour.


Haikosi watoto wa Malkia wameanza kuchoshwa na mchemko wa serikali wa kuwakatia marupurupu yao ya kujikimu, ambapo Cameron anasema ananyanyua uchumi. Wamesema ni heri enzi zile za Tony Blair na Gordon Brown walipokuwa 10 Downing Street kuliko leo Cameron anavyowabania paundi.

 

Mabadiliko wakati mwingine ni magumu, lakini wananchi wakianza kutonya, bora uwe kama unapoona mwenzako ananyolewa, anza kutia maji usilie mkubwa mzima bure.

[email protected]


By Jamhuri