Februari Mosi Mwaka huu, Jiji la Arusha limezindua kampeni ya kudumu ya usafi wa mazingira. Tayari baadhi ya mitaa ya jiji hilo imeanza kupendeza.

Mradi huo unaohusisha ukarabati wa barabara, mitaro, dampo, taa za barabarani na za kuongoza magari unahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa ujumla.

Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (CHADEMA), amesema hatarudi nyuma katika kushirikiana na madiwani kutafuta maendeleo ya wananchi.


Kwamba ushirikiano huo ni pamoja na kuhakikisha Jiji la Arusha linadumu katika usafi wa mazingira, na eti kampeni hiyo itakuwa ya CHADEMA.


Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mara, Amani Golugwa naye akasema mazingira yakiwa machafu chama hicho ndio kitaonekana kimeshindwa kuwajibika.


Kauli za viongozi hao zimeibua hisia kwa wananchi na miongoni mwao wanaamini sasa siasa za Arusha huenda zikachukua sura mpya ya kutambua umuhimu wa ushirikiano.


Lakini nikiwa mmoja wa wadau wa usafi katika uzinduzi wa kampeni hiyo nilishangaa kutowaona viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na mbunge Lema.


Nanajiuliza mambo kadhaa juu ya uongozi wa Lema. Je, anadhani anaweza kufanya jambo la maendeleo bila kushirikiana na viongozi wengine wa CHADEMA, chama tawala – CCM na Serikali?


Lema anapaswa kutambua kuwa yeye si msafi kwa kila eneo chini ya jua kiasi cha kugoma, au kuamini kwamba hawezi kushirikiana na wengine kutafuta maendeleo ya wananchi wa Arusha.


Kwa muda mrefu sasa Lema amekuwa mkosoaji wa kila jambo linalofanywa na viongozi wengine lakini hatuoni cha maana alichokifanya yeye.


Hivi karibuni tumeshuhudia akikurupuka kufunga Shule ya Sekondari ya Korona. Nilitegemea angetafuta njia ya kusaidia badala ya kuifunga kwani kitendo hicho ni sawa na baba kukimbia majukumu ya familia yake.


Wito wangu kwa mbunge Lema ni kwamba aanze kujirekebisha ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi maneno anayozungumza jukwaani.


Nanaamini kinachomsumbua sasa ni jinsi ya kujitokeza kushirikiana na viongozi wengine wakiwamo wa Serikali katika kuwaletea wananchi wa Arusha maendeleo kwani tayari ‘alishatukana mamba kabla hajavuka mto’. Wazo la kampeni ya usafi wa Jiji la Arusha amelianzisha yeye lakini ameshindwa kujitokeza kulifanyia kazi kwa vitendo badala yake ameishia kujiona yeye ni ‘Mkatoliki kuliko Papa’.


By Jamhuri