Emmanuel Amunike! Alipata sifa sana wakati akiwa mchezaji lakini amejikuta akiwa garasa katika kazi ya ukocha. Sitaki kuzungumzia huko alikotoka, lakini ndani ya Taifa Stars ameshindwa kufikia malengo ya waajiri wake, nao wamemtoa kafara.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, akaamua kuitisha mkutano, lakini ‘wababe’ wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakatuma wawakilishi. Nao walikuwa na ‘kikao kizito’.

Walikuwa na haki ya kususa kikao chake, kwani serikali inakumbuka ‘mambo mwishoni mwishoni’.

Katika hili, nikamkumbuka Dk. Mshindo Msolla. Unaweza kushangaa, ni huyu huyu Msolla wa Yanga – ni bonge la kocha, nilishawahi kuwa naye karibu zaidi ‘miaka ya nyuma’ wakati tulipokuwa wote Rwanda.

Nikamkumbuka Charles Boniface Mkwasa. Huyu ambaye ametoka karibuni kuwa Katibu Mkuu wa Yanga. Nilimfahamu vizuri zaidi wakati nilipokuwa naye Rwanda.

Nikamkumbuka marehemu Syllersaid Mziray. Mungu ampunguzie adhabu ya kaburi, lakini pia nilikutana naye Rwanda na tukafahamiana vizuri zaidi, tena sana.

Nikamuwaza Bukhard Pappe. Kocha ambaye aliamini katika darasa, lakini wachezaji wakawa hawaamini hilo wakisema mpira ni kipaji, si kuingia darasani. Naye tulikutana Rwanda.

Nikawaza zaidi juu ya Muhidin Ndolanga. Mbabe ambaye wakati unakwenda kufanya naye mahojiano lazima uwe umejiandaa kwa data mpaka vielelezo. Nilimfahamu vizuri zaidi tukiwa Rwanda.

Nikamkumbuka Ismail Aden Rage. Mtu ambaye anajiamini kwa kila jambo na anaweza kutetea kile anachokiamini. Mpaka leo napenda sana kumfuatilia, nilimjua na kumfahamu zaidi hata kabla ya kwenda Rwanda.

Nimewakumbuka watu hawa na kukikumbuka kikosi kilichoshiriki michuano ya Chalenji zaidi ya miaka 18 iliyopita na vile wananchi wa Rwanda pamoja na mashabiki wa nchi nyingine walivyokiogopa.

Ndolanga akiwa na wajumbe wenzake wa CECAFA alikuwa akitamba sana juu ya benchi lake la ufundi, Mziray akikutana na makocha wenzake anatamba kwamba benchi lote wote ni ‘madokta’. Waliogopa. Ila timu haikutwaa taji.

Mpaka leo nitaendelea kusimamia hilo kwamba hakuna benchi la ufundi bora kabisa ndani ya timu ya taifa lililowahi kutokea kama hilo. Pappe, Dk. Msolla, Mkwasa, marehemu Mziray. Huku kukiwa na viongozi wenye misimamo kama Ndolanga na Rage. Nitasimamia hili.

Kukumbuka huko kulinifanya nizidi kuitafakari Stars hii ya Amunike, ambayo ‘ilipangwa kundi gumu’ kama wenyewe wanavyodai katika michuano ya AFCON iliyomalizika wiki mbili zilizopita kule Misri na Algeria kutwaa taji.

Tumerogwa?

Rais mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliposema ‘Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu’ wala hakukosea. Nilishangaa tu alipoamua kuifuta kauli yake hiyo miaka ya karibuni, lakini ukweli uko palepale.

Huwezi kuwa na timu ya taifa imara kama una ligi dhaifu. Hata Amunike nilimuonea huruma pale alipoamua kuwaacha hata wale wachezaji ‘walioamua kujibebisha’ na kwenda kucheza nchi zinazotuzunguka. Walikuwa na uzoefu mkubwa, lakini hakuwaamini.

Tuje sasa! Tuukubali ukweli, inashangaza sana kuona Ligi Kuu inakosa udhamini na kuifanya izidi kuwa dhaifu zaidi. Ligi yenyewe bado inaumwa halafu inakosa udhamini, unategemea nini?

Hapa ndipo unapojiuliza, tumerogwa? Huwezi kuwa na ushindani katika ligi yenye timu zinazolia njaa, ni lazima watapatikana wababe wachache wenye ‘kuamua matokeo’.

Usitarajie ligi yenye ushindani wa Azam, Simba na Yanga pekee, huku zingine zikiwa kama zinajitutumua, halafu ukapata timu ya taifa iliyo bora. Huku ni kujidanganya. Hatuwezi kupata timu ya taifa bora kama tuna ligi dhaifu. Ndipo ninaposimamia hapo.

Hata kabla ligi haijaanza unaweza kutabiri ni timu zipi zinaweza kuwa bingwa. Hapa utazizungumzia Simba au Yanga. Azam itakuja kwa mbali, lakini kwa fitina za hawa ‘wazee’ lazima ikae pembeni.

Ni moja kati ya timu hizo mbili ndiyo itakayotwaa ubingwa na wala haina haja ya kwenda kwa mganga kupiga ramli. Huu ndiyo ukweli katika ligi iliyo dhaifu.

Kama Ndanda inalia njaa, usitarajie kuwa na ligi yenye ushindani. Iwapo Biashara haijui pa kutokea usitegemee hata kidogo, ushindani utakuwa wenye tija. Wakati Lipuli ikipiga kelele za kuombaomba fahamu inapigana kubaki Ligi Kuu tu.

Ombaomba ya Yanga si kama ile ya Ndanda au Lipuli. Yanga ina rasilimali watu, lakini hizi nyingine hazina. Wakati Azam, Simba na Yanga zinajiimarisha kwa kusajili vikosi bora, wengine ‘wanadata’ kwa kubembeleza wachezaji wa kuwasajili.

Tutoke tulipo

Ifikie hatua TFF lazima ikubali kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha Ligi Kuu inakuwa na mdhamini imara. Bodi ya Ligi Kuu pia wahakikishe wanakuwa na ligi isiyo na mizengwe ili wadhamini watie fedha zao.

Kama ratiba inakuwa haieleweki, malalamiko yasiyokwisha, kukataa ushauri wa uendeshaji wa Ligi Kuu, usitegemee kama utapata mdhamini mwenye nguvu zaidi kuingiza fedha zake.

TFF pia inapaswa kuzisaidia hasa hizi timu zinazoitwa ndogo wakati sivyo, zijue namna ya kujiendesha na kutafuta masoko. Hizi timu zimekwama kwa kiasi kikubwa.

Idara ya Masoko TFF pia mnakwama wapi? Uchawi unaanzia hapa kwa kuifanya Ligi Kuu iwe dhaifu.

371 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!