Tutakwama, tusiendelee kujidanganya

Wakati Madagascar ikifanya maajabu katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika iliyomalizika hivi karibuni nchini Misri, wengine tulijidanganya kuwa tupo kundi gumu.

Si kujidanganya tu, bali pia tulijipa matumaini kwamba lazima tupate uzoefu ili tuweze kufikia malengo halisi tunayoyataka. Tukaitolea mfano Uganda.

Eti katika michuano ya mwaka huu walifika raundi ya pili, baada ya ‘kufanya vibaya’ katika michuano iliyopita, ambapo waliaga katika hatua ya makundi.

Madagascar ambao hawajawahi kuonja utamu ama uchungu wa michuano hiyo, wakiingia kwa mara ya kwanza, wakafanikiwa kuingia hatua ya robo fainali.

Watu hawa ambao kwa miaka mingi tulidharau soka lao, kama tulivyoidharau Cape Verde, wakatinga hatua ya robo fainali wakiwa na wababe ambao ‘tunawaogopa’. Wababe hao ni Afrika Kusini, Algeria, Benin, Ivory Coast, Nigeria, Senegal na Tunisia.

Kabla Madagascar hawajaonyesha kile ambacho tulipaswa kukiona, tuliendelea kujifariji kwa kuona tuliondolewa kihalali katika michuano hiyo. Umefuzu, udhaifu wako upo wapi?

Tukaona wanasiasa walivyoitumia ‘fursa’ vizuri kwa Taifa Stars kushiriki michuano hiyo, pale walipoamua kujibebesha jukumu hilo wao, wakawaacha Watanzania, wakaenda kuishangilia huko Misri kwa ‘ka-mechi kamoja’ wakisema ni wawakilishi wa Watanzania.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nao wakaifanya kama timu yao pekee, wakawaacha Watanzania nyuma. Hivyo haikuwa vibaya wengine kuisema vibaya Taifa Stars.

Lakini kwa kujidanganya tena, tunaendelea kujipa matumaini kwamba tutafanya vema na kufuzu katika michuano inayokuja. Tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeshapanga makundi na tunajijua tupo na Equatorial Guinea, Libya na Tunisia.

Pamoja na kufahamu tupo kundi gani na tunapambana na kina nani ili kufuzu, bado tunaendelea kuchukulia mambo kwa urahisi zaidi. Tunawaona kama vibonde. Kumbe katika kundi hilo tunaojivika kilemba cha ukoka ndio vibonde halisi.

Serikali nayo inaona jukumu kubwa la kufanya vema limo mikononi mwa TFF, wao wakipiga debe la kuichangia timu haina shida. Wanajua fedha zitafanya kila kitu, kumbe haiko hivyo. Pia wakisaka wenye ‘mdomo wa kuongea’ wanaowaita watu wa hamasa mambo yamekwisha. Haiko hivyo.

Tunakwama wapi?

Hapa nachanganya soka na michezo yote. Tumeitenganisha michezo na elimu na tumeigeuza michezo ni siasa. Tunaifanya michezo kama ni starehe badala ya ajira. Hiki ni kiwanda kikubwa zaidi, chenye kuajiri watu wengi lakini tumekitupa.

Wanasiasa wanaitumia michezo ili kufikia malengo yao binafsi na wanamichezo kwa kutojua hili wameendelea kutumika, huku wakiona ni sifa kubwa kwao kutumiwa na wanasiasa.

Tunakaribia kipindi cha uchaguzi, kuanzia  ule wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu na wa rais, wabunge na madiwani mwishoni mwa mwaka ujao, tumekwishaanza kuona harakati za wanasiasa kufikia mafanikio yao kupitia wanamichezo.

Hakuna binadamu asiyetaka kufikia lengo lake hata iwe kwa ‘njia za panya’, lakini katika michezo lazima tufuate misingi halisi inayotakiwa. Lazima tufuate kanuni sita za msingi kama tunataka kutoka hapa tulipo.

Tunatokaje?

Kwanza, lazima tukubali michezo ni elimu na elimu ni michezo. Hatuwezi kuitenganisha michezo na elimu hata siku moja, huu ni sawa na uji na mgonjwa. Tatizo kubwa tunaanza kukwama kuanzia hapa. Tulipoamua kuifanya michezo si elimu.

Michezo lazima ipitie njia sita zilizo sahihi kama vile mtoto anavyoanza kupata elimu yake. Yaani kuanzia kindergarten, nusery, primary, secondary, high school na university. Hili la university, linahusisha chuo chochote atakachopita. Hii ndiyo njia sahihi, ambayo inaweza kututoa tulipo. Eneo hili ni pana sana kulizungumzia, kuna siku nitalielezea kwa kina zaidi.

Swali jingine la kujiuliza, tunazalisha makocha wangapi kwa mwaka? Tuna shule au vituo vya michezo vingapi? Hapa pia ndipo tatizo jingine linapoanzia, na Uganda wataendelea kutuburuza zaidi. Sitaki kutoka mbali, twende hapa Afrika Mashariki. Uganda wanazalisha makocha wangapi? Wana vituo au shule ngapi za michezo?

Nenda kaone kile kinachofanyika Uganda International Sports Academy, pitia National Sports Academy, ISSAK au Kids for Africa Sports Academy, hivi ni vituo vichache kati ya zaidi ya mamia vilivyotapakaa ndani ya nchi hiyo. Nazungumzia vinavyotambulika, hapa ukiondoa vingi ambavyo vipo kienyeji.

Tuje kwetu, tunazalisha makocha wangapi kwa mwaka? Tuna vituo vingapi ambavyo vinatambulika rasmi? Tunataka tushindane na nani ili tufikie malengo yanayotakiwa?

Ushauri

Serikali na wanasiasa waache siasa katika michezo. Serikali pia haiwezi kukwepa jukumu lake na kujiondoa katika michezo. Inahusika moja kwa moja badala ya kuviachia vyama na kuviona ndivyo vyenye jukumu la kuhakikisha tunafanikiwa katika medani hiyo.

Kwa kuanzia tu, tungekuwa na shule moja katika kila mkoa na kuanzisha kanda, huku tukihakikisha tunazalisha pia makocha wengi ambao mwisho wa siku watakuja hata kwenye mitaa wanayoishi. Ila kwangu, naona tutaendelea kujidanganya.