Berlin, Germany

Mchezaji wa zamani wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, Stefan Effenberg, amesema kuna haja ya mfumo wa ligi ya nchi hiyo kufanyiwa marekebisho kwa manufaa ya klabu na timu ya taifa ya nchi hiyo.

Amesema ligi ya nchi hiyo kuendelea kutawaliwa na klabu ya Bayern Munich ni hatari kwa ustawi wa klabu nyingine na timu ya taifa, hali inayopaswa kufanyiwa marekebisho kwa haraka bila ya kuchelewa.

“Siku za  karibuni klabu ya Bayern Munich imeendelea kutawala na itaendelea kutawala kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha ikilinganishwa na klabu nyingine, hali ambayo ni hatari kwa ustawi wa mpira wa Ujerumani,” amesema Effenberg.

Mchezaji huyo wa zamani wa Bayern Munich amependekeza uundwe mfumo mpya utakaofanya Bundesliga kuwa na mvuto na ushindani kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma ambako ligi ilikuwa na ushindani.

Amesema ligi hiyo ilikuwa na mvuto katika kipindi ambacho klabu ya Dortmund chini ya kocha Jurgen Klopp walipofanikiwa kuleta ushindi, tofauti na sasa ambako Bayern inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 18 dhidi ya klabu ya Bayer Leverkusen.

Kwa kujenga hoja yake hiyo, amesema katika mfumo huo timu 18 zitagawanywa katika makundi mawili ya timu tisa kwa kila kundi na kucheza nyumbani na ugenini, halafu timu nne za juu kila kundi zitakuwa katika nafasi nzuri kuingia raundi ya pili, pamoja na timu moja yenye matokeo mazuri katika makundi hayo mawili (best loser) kwa timu tisa.

Amesema timu tisa za juu zitacheza ligi nyingine kumsaka bingwa atakayeiwakilisha nchi katika makombe mbalimbali ya kimataifa, halafu timu tisa nyingine za chini zinacheza kwa ajili ya kupigania kutoshuka daraja na timu mbili za chini zitashuka daraja.

Amesema lengo la kuja na wazo hilo ni kutafuta namna ya kurejesha ushindani ndani ya ligi hiyo na mwisho wa yote ni kuangalia jinsi ya kuzisaidia klabu nyingine na timu ya taifa katika michuano mbalimbali.

Amesema bila ya kuja na mbinu na mikakati ya namna hiyo na kuiacha klabu moja kuendelea kulitawala soka la Ujerumani, ni sawa na kulizika soka la Ujerumani na mwisho wake ni kuja kulaumiwa na kizazi kijacho.

1458 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!