Lissu njia panda

Ofisi ya Bunge inakusudia kutangaza hatima ya ubunge wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), baada ya kutokuwapo bungeni kwa miezi 16 sasa.

Uamuzi huo ukisubiriwa kutoka kwa Spika Job Ndugai, mwanasiasa huyo amekataa kuzungumzia lolote kuhusu madai kwamba ofisi yake inataka kuchukua uamuzi wa kumtangaza Lissu kuwa si mbunge baada ya kukosa mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, hivyo kupoteza sifa ya kuwa mbunge.

Msaidizi wa Spika, Said Yakubu, amesema: “Suala hilo kuhusu Tundu Lissu litatolewa majibu na Spika ndani ya Bunge katika mkutano ujao wa Bunge Januari hii.” Mkutano huo ulitarajiwa kuanza leo jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Masuala ya Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema, amesema: “Tunajua kuna hizo taarifa, lakini tunawakumbusha kuwa Lissu alikuwa kwenye matibabu. Lakini Lissu si wa kwanza kutibiwa kwa muda mrefu. Aliwahi kutibiwa kwa muda mrefu mzee Mark Mwandosya kwa zaidi ya mwaka, hakuna hatua zilizochukuliwa, na wapo wabunge wengine wako kwenye matibabu kwa muda mrefu sasa.”

JAMHURI limewasiliana na Lissu, na haya ndiyo majibu yake: “Taarifa gani ya maandishi wanahitaji wakati nilishambuliwa nikiwa kwenye vikao vya Bunge.

“Nilipelekwa Nairobi nikitokea Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kikao kilichomshirikisha Katibu wa Bunge wakati huo, Dk. Thomas Kashilila, Spika Ndugai na Naibu Spika Tulia Ackson.

“Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Katibu Mkuu wake, Dk. Ulisubisya Mpoki, walikuwepo kwenye kikao hicho; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alikuwepo, na nilisindikizwa mpaka Nairobi Hospital na daktari kutoka Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma.

“Wakati wote ambao nimekuwa kwenye matibabu wamewasiliana kwa maandishi na mwakilishi wa familia yangu kuhusu matibabu yangu. Wametoa matamko mengi hadharani kuhusu kushambuliwa kwangu na kuhusu matibabu yangu.

“Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, amekuja kuniona nikiwa hospitalini Nairobi; Balozi wa Tanzania Ubelgiji, Joseph Sokoine, amekuja kuniona hospitalini Leuven mara mbili.

“Spika Ndugai na uongozi wote wa Bunge, akiwemo Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai, na maafisa wake hawajawahi kukanyaga hospitalini kuja kumwangalia mgonjwa wao, aliyeumizwa vibaya akiwa bungeni.

“Hawajawahi kujihangaisha na mimi kwa namna yoyote ile, zaidi ya kuninyima haki zangu za matibabu kinyume cha Sheria ya Uendeshaji wa Bunge.

“Katika mazingira haya, ni kitu gani ambacho hawakifahamu kuhusu kushambuliwa na kuumizwa kwangu ambako kunahitaji waandikiwe barua?

“Na waandikiwe barua gani zaidi ya barua nne au tano ambazo wamekwishaandikiwa na kaka yangu, Wakili Alute Mughwai?

“Ninachoona ni hiki: walitaka nife kwa risasi. Imeshindikana. Wakataka nife kwa kukosa matibabu na huduma nyingine kama mgonjwa. Ikashindikana. Sasa wanataka kunifuta ubunge kwa mabavu tu. Itashindikana vilevile.

“Badala ya kuona aibu na kukaa kimya, wanataka kuzima moto kwa kuumwagia petroli. Hautazimika, utawaka zaidi. Na, kwa kufanya hivyo, watajianika hadharani ili dunia nzima ishuhudie uovu wao!”

Hali jimboni kwa Lissu

Miezi 16 tangu Lissu ashambuliwe kwa risasi 16, JAMHURI limebaini siri ya nguvu za kisiasa za mwanasiasa na mwanasheria huyo machachari.

Katika uchunguzi wa gazeti hili uliohusisha mahojiano na wananchi kadhaa wa jimbo hilo na viongozi mbalimbali, nguvu za kisiasa za Lissu zimejikita katika taaluma yake ya sheria na huruma yake iliyomfanya atoe bure msaada wa kisheria kwa wananchi wanyonge.

Kwa upande mwingine, udhaifu wake kisiasa umejikita katika namna ya kushindwa kupanga safu ndogo ya wasaidizi wake wenye utaalamu mahususi kwa kadiri ya mahitaji ya shughuli za uzalishaji jimboni humo.

Hata hivyo kwa ujumla, uchunguzi wa JAMHURI kwa njia ya kuhoji wananchi, kufuatilia matukio mbalimbali na hata kuchambua maelezo ya wananchi jimboni humo namna walivyoishi miezi 16 bila Lissu, uhusiano wa mbunge huyo na sehemu kubwa ya wananchi umezidi kuimarika kwa mambo mawili; kwanza, nguvu zake za kisiasa za awali; pili, huruma ya wananchi baada ya shambulio la risasi dhidi yake kiasi cha uhai wake kuwamo hatarini.

Uimara wa kisiasa

JAMHURI limejiridhisha kuwa, uimara wa Lissu kisiasa umejikita katika taaluma yake ya sheria, akiwa wakili wa Mahakama Kuu, sambamba na ujasiri wa kupigania haki za wanyonge kupitia taaluma hiyo.

Wananchi waliozungumza na gazeti hili wamesema uonevu wa muda mrefu dhidi ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kubambikiwa kesi, ulimjenga zaidi Lissu ambaye alitumia taaluma yake ya sheria kuwatetea katika kesi bila malipo, na kazi hiyo aliianza kabla ya kuwa mbunge na kisha kuiendeleza kwa nguvu zaidi katika kipindi cha ubunge wake wa takriban mihula miwili.

Diwani wa Mang’onyi, Emily Mjengi, anathibitisha hili akisema moja ya athari za moja kwa moja za kukosekana kwa Lissu jimboni katika kipindi cha matibabu yake ni kukosekana kwa huduma yake ya kisheria kwa wananchi wenye matatizo.

“Mbunge amekuwa msaada mkubwa wa kisheria kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo, kukosekana kwake kumeathiri kwa kiasi gani wananchi wa kawaida,” anasema.

Katika kuzidi kuthibitisha hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ighuka, jimboni Singida Mashariki, Venance Dule, anasema: “Lissu amekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa vijijini na mjini, amewaokoa wananchi na jinamizi la kukamatwa mali zao mara kwa mara kwa sababu ya kulazimishwa kutoa michango isiyokwisha kila wakati, na hili la kutetea wananchi alilianza kabla ya kuwa mbunge.”

Dule anasema ushindi wa kishindo wa viti 47 vya serikali za vijiji jimboni Singida Mashariki dhidi ya viti vitatu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa mwaka 2014, kwa kiasi kikubwa ulitokana na nguvu ya Lissu kusaidia wananchi moja kwa moja kisheria; huduma ambayo awali wananchi hawakuipata bila malipo.

Na kwa hiyo, Diwani Mjengi anazungumzia athari za kukosekana kwa Lissu jimboni kwa miezi hiyo 16 akisema: “Athari za kukosekana mbunge wetu kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja ni kubwa ingawa viongozi wengine wapo, moja ya athari kubwa ni kukosekana kwa msaada wake kwa wale wenye shida, hasa msaada wa kisheria. Hata sisi wenyeviti wa serikali za vijiji baadhi yetu tumebambikiwa kesi na kufanyiwa matukio mengine kinyume cha taratibu kama kusimamishwa uenyekiti, lakini hatujui namna ya kupigania haki zetu katika mkondo wa kisheria, Lissu alikuwa akitusaidia sana.”

Dule anasema katika Kata ya Ikungi, wenyeviti wawili wa serikali ya kijiji waliswekwa rumande kwa saa 48 kwa sababu ya kutokuhudhuria mkutano wa mkuu wa wilaya ambao anadai walijulishwa dakika za mwisho wakiwa katika shughuli nyingine.

 

Hamahama ya wanasiasa

Katika kuthibitisha nguvu zake za moja kwa moja za kisiasa, wimbi la uhamaji wa viongozi wa vyama vya upinzani kwenda CCM halikuiathiri Singida Mashariki. Hakuna wenyeviti wa mtaa au vitongoji waliohama. Gazeti hili limeelezwa kuwa pamoja na kile kilichoitwa “njaa” za wananchi na viongozi wao jimboni, lakini wameshindwa kumsaliti mbunge wao wakionyesha kulipa fadhila za msaada wake kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) Kata ya Ikungi, Bernard Swai, anasema jimboni humo viongozi wengi ni wa Chadema, lakini hakuna aliyejiondoa katika chama hicho; siri kubwa ni kuungana kwa Lissu katika kipindi chake kigumu cha maumivu na matibabu.

Katibu wa Jimbo la Singida Mashariki wa Chadema, Ibrahim Ikhalla, anasema kwa namna mambo yanavyomwandama, Lissu angeweza kuachana na siasa, lakini hafanyi hivyo kutokana na ujasiri wake.

“Hapa jimboni kinachofurahisha ni kuwa Lissu alipanda mbegu ya ujasiri, ukakamavu na kujiamini. Wananchi wa jimbo hili wamekuwa na ujasiri mkubwa ndiyo maana katika wimbi la kuhamia CCM – hakuna aliyehama. Wananchi na viongozi waliona ni dhambi kukimbia chama wakati mbunge anauguza maumivu ya mashambulizi ya risasi. Waliona huo ni usaliti kwa mbunge aliyewaokoa kutoka kwenye michango isiyo na manufaa kwao.

“Tunalipa fadhila kwa Lissu ambaye kabla hajawa mbunge alitumia taaluma yake ya kisheria kupinga uonevu kwa wananchi jimboni hadi wakamchagua kuwa mbunge, aliwapa elimu ya sheria kuhusu haki zao msingi na hasa hili la michango ya masuala ya maendeelo wakati miradi inayolengwa haipigi hatua na fedha zinaliwa,” anasema Ikhalla.

Anasema, awali kina baba walikuwa wakikimbia makazi kukwepa kukamatwa na mgambo, lakini kwa sasa anayefanya biashara ndiye anayelipa ushuru.

“Mgambo waliweza kufanya chochote, lakini leo tuko huru. Tunamwombea mbunge wetu arudi salama, na sisi tunasema uwezo wake wa kuongoza kwa kupigania haki za wananchi ni mkubwa, na Mungu amezidi kumpa uhai maana yake ni kwamba Mungu ameonyesha Lissu bado anahitajika kwa malengo maalumu kwa wananchi na taifa hili,” anasema.

Mawasiliano, wanavyom- ‘miss’

Diwani Mjengi anasema: “Kumkosa mbunge kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja imekuwa changamoto kubwa kwa kuwa mbunge wetu alikuwa anafika jimboni mara kwa mara.

“Wananchi wamepata athari kubwa, kwanza zile taarifa za awali kwamba amepigwa risasi na maisha yake yako hatarini wakati wote wa matibabu, kisaikolojia ni jambo gumu sana.”

Anasema pamoja na changamoto hiyo wamekuwa wakiendelea na shughuli za maendeleo huku wakielekeza sala kwa mbunge wao.

Lakini; je, ni kwa namna gani pengo la kutokuwapo kwa Lissu jimboni na hasa uwakilishi wa wananchi wake bungeni limekuwa ‘likizibwa?’

Diwani Mjengi anajibu: “Wabunge wa Chadema kutoka sehemu nyingine walikuwa wakifika hapa na kuwakilisha wananchi wa hapa huko bungeni. Hatuwezi kumpa maoni yetu mbunge wa chama kingine…kwa hiyo tulikuwa tunawakilishwa hisia na maoni yetu kupitia kwa wabunge wengine”.

Wamekuwa na mawasiliano na Lissu kwa simu kwa kipindi chote alicho kwenye matibabu.

Anaamini kuwa tukio la kushambuliwa Lissu kwa risasi na kuendelea na matibabu kwa muda mrefu halijateteresha nguvu zake za kisiasa, badala yake limeimarisha nguvu hizo jimboni na kwenye ngazi ya taifa.

“Tumesikia akionyesha utayari wa kutaka urais kama chama kitamchagua kuwa mgombea, kwa sababu ya hulka yake ya kusaidia wananchi wa kawaida kila wakati kwa maana ya msaada wa sheria na hata fedha kwa kadiri ya uwezo wake na ni mpigania haki asiyekubali hata kidogo uonevu, tunaamini kwa moyo huo wa mapenzi kwa wananchi ataumudu urais,” anasema diwani huyo.

Anajigamba kwa kusema CCM hawataambulia ushindi wowote katika Uchaguzi Mkuu mwakani.

Anatoa mwito kwa wananchi wa Singida Mashariki na Tanzania: “Licha ya shambulio la risasi nyingi dhidi ya Lissu lakini bado yu hai, huu ni muujiza wa Mungu na ni ushahidi kuwa Mwenyezi Mungu bado ameona umuhimu wa Lissu katika kupigania wananchi wake. Akigombea urais aungwe mkono.”

Naye, Venance Dule kuhusu hilo anasema: “Wananchi wetu na sisi viongozi tumekuwa tukijisikia ukiwa kwa kukosekana kwa Lissu, lakini tumepokea kwa furaha taarifa za kupata kwake nafuu kiasi cha kuruhusiwa kutoka hospitalini.

“Wananchi wanasubri kwa hamu atarudi lini nchini na hapa jimboni kwake.”

Kwa upande wake, Stella Mpembee, ambaye ni mkazi wa jimboni humo anasema: “Baada ya shambulizi dhidi ya Lissu tulikosa amani kabisa, tuliumia na kujiuliza maswali mengi, tumeathirika sana, lakini kwa sasa wananchi tunasubiri kwa hamu kumwona, tunampenda mbunge wetu. Kutokana na uhai wake licha ya kupigwa risasi, tafsiri yetu ni kwamba Mungu ametutia moyo tusonge mbele. Mimi kama mama nazidi kuitia moyo familia ya Lissu, mkewe na watoto. Tunajua wamepitia kipindi kigumu.”

Charles Zefania anasema taarifa za awali za Lissu kupigwa risasi ziliwashitua mno, hawakuamini, na mara baada ya taarifa hizo wananchi walijikuta wakijikusanya katika makundi kujadiliana na kutiana moyo.

“Wananchi wamekuwa wakifuatilia sana habari zake kuhusu mwenendo wa afya yake. Na niseme wazi maadui zake wa kisiasa hawakufaidika na shambulizi hilo lililomfanya kuwa nje ya jimbo na bungeni kwa zaidi ya mwaka mmoja,” alisema Zefania.

Akisimulia anachokumbuka na namna mambo yanavyokwenda, Bernard Swai wa BAVICHA, kama alivyoelezea masuala mengine kumhusu Lissu, anakumbuka namna taarifa za Lissu kupigwa risasi akisema: “Nilikuwa nyumbani nafanya kazi za kawaida, lakini baada ya taarifa hizo nilishindwa kuendelea na kazi.

“Tulikusanyika katika makundi na wengine walihangaika kwenda Dodoma (kwenye tukio). Tuliwaombea waliosafiri naye kwenda kwenye matibabu. Wazee wa hili jimbo waliwatuliza vijana. Tulikuwa tukijipa moyo – akifikisha kesho atakuwa amenusurika.”

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Ikungi, Hussein Msandae, ambaye amepata misukosuko ya ‘kushughulikiwa’ akiamini kwamba ni “kushughulikiwa kisiasa” ili ahame chama hicho katikati ya wimbi la wanasiasa wa upinzani kukimbilia upinzani lililoshika kasi mwaka jana, anasema: “Nilihusishwa na tuhuma za matumizi mabaya ya mali za serikali, lakini katika kesi nilishinda na waliponipeleka TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) waliona hakuna jambo la maana. Nilisimamishwa uenyekiti kinyemela bila kufuata mchakato wa kisheria.”

Kuhusu Lissu kukosekana jimboni, anasema fedha za maendeleo kwa miradi ya maendeleo zimekuwa zikielekezwa kwenye majimbo mengine, hasa Singida Magharibi. Anatolea mfano wa ujenzi wa hospitali. Wilaya ya Ikungu ina majimbo mawili – Singida Mashariki na Singida Magharibi.

Lakini Ibrahim Ikhalla, anazungumza tena na gazeti hili akisema moja ya athari za kutokuwapo kwa Lissu ni madiwani kukosa ujasiri wa kuhoji kwa kiwango kilichokuwapo awali, akisema wengi wanahofu kubambikiwa kesi.

“Madiwani wanahofia kuhoji zaidi kuhusu fedha za maendeleo. Wanaohoji wanaitwa halmashauri, wanaburuzwa kamati ya maadili, wengine wanatiwa ndani kwa saa 24, yote haya yanafanyika kisiasa,” anadai.

Nini kimekuwa kikitokea wakati Lissu akiwa kwenye matibabu? Katibu huyu anasema: “Tumekuwa tukiwasiliana naye kwa simu, tunatumia njia ya video live (video call). Na sasa matumaini yetu ni kuwa atarajea salama nchini na jimboni, na usalama wake hautakuwa wa shaka.”

Spika na Lissu

Ikhalla anazungumzia ukaribu uliopo kijamii kati ya Spika Ndugai na Lissu; akisema: “Spika ni kijana wa huku kwetu, amesoma Shule ya Msingi Matare, Kata ya Unyahati ambayo kwa zamani wakati anasoma iliitwa Kata ya Ikungi. Amekulia huku, ni kijana wa nyumbani, Ndugai ni ndugu yetu, naye Lissu ni wa huku amesoma Shule ya Msingi Mahambwe.”

JAMHURI limezungumza na mama mdogo wa Lissu, Felista, kuhusu tukio la kijana wao kupigwa risasi, walivyopokea taarifa hizo na namna maisha yao yalivyokwenda katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja cha matibabu ya mtoto wake nje ya nchi.

“Tumechukizwa na tukio la mtoto wetu kupigwa risasi, lakini tulimuomba Mungu amponye na hadi sasa tunaendelea kumwomba Mungu. Mimi naamini Lissu amekuwa kama Yesu wa pili kwa kuwa ameshinda mauti. Tulilia sana mwanzoni, ilikuwa kama tupo msibani. Tuliona picha za kushambuliwa kwake kwa risasi mitandaoni, majirani walituletea picha hizo za mitandaoni na kila taarifa iliyokuwa inatolewa, taarifa nyingine zilikuwa za kweli na nyingine si za kweli, hali ilikuwa ngumu,” anasema mama huyo mkulima wa Kijiji cha Mahambwe lilipo boma la Mzee Mughwai Lissu (marehemu mumewe – yeye akiwa mke wa pili wa mzee Lissu, mke – mama mzazi wa Lissu alifariki dunia mwaka 2010).

Mdogo wa Tundu Lissu, Alu Lissu, anasema: “Tunaamini serikali itachukua hatua kuhusu tukio hili baya kwa kaka yetu.”

Mwanafamilia mwingine wa Lissu ambaye ni mdogo wake anasema: “Familia imepitia katika kipindi kigumu sana, lakini hatukuwahi kupoteza matumaini yetu kwa Mwenyezi Mungu.”

Muro Mughwai aliyesoma darasa moja na Spika Ndugai na enzi zao za shuleni akiwa kiranja mkuu na Ndugai akiwa kiongozi wa darasa (monitor) katika Shule ya Msingi Matare, anasema Ndugai ni mwenzao.

Anakumbuka siku Lissu alipopigwa risasi. Anaanzia mbali kueleza namna ambavyo mwanafunzi mwenzake wa shule ya msingi (Ndugai) amekuwa Spika wa Bunge.

“Tulijiunga katika Shule ya Msingi Matare kwa nyakati tofauti sote tukiwa darasa la tano, tulimaliza shule mwaka 1977, tulipenda masomo yote na michezo, mwenzetu (Ndugai) alikuwa akikaa kwa mwalimu shuleni, sisi wengine tulikuwa tunahangaika kupita njia yenye wanyama wakali kuelekea shuleni au kurejea nyumbani ingawa wakati mwingine Job alikuwa akilala nyumbani kwetu hasa tunapotoka kwenye michezo ya shule maeneo mengine nje ya kijiji – ulikuwa mwendo wa hadi nusu saa.

“Maisha yake ya shule yalikuwa mema, alikuwa mwanafunzi muungwana, alishiriki shughuli zote za shuleni ikiwamo usafi, hakutamba kuwa asifanye kwa kuwa anaishi kwa mwalimu ambaye alikuwa ndugu yake, hapana. Alifagia hata uwanja wa shule kama wanafunzi wengine. Hakujitenga na wenzake.

“Mimi nilikuwa kiranja wao mkuu shuleni, yeye alikuwa ‘class monitor’… bosi wake…kazi yake ilikuwa kukusanya madaftari darasani (anatania), lakini alikuwa rafiki yangu. Miaka mingi ilipita sikuwa najua yuko wapi.

“Siku moja nikiwa mahabusu natazama televisheni (aliwekwa mahabusu kwa tuhuma za mauaji ya kijana aliyedhaniwa mwizi, lakini Lissu alimtetea katika kesi hiyo na kushinda)… sasa wakati natazama TV nikaona Bunge linaelekea kuanza kikao chake cha siku, namwona Ndugai amevaa kanzu (joho) ilikuwa mwaka 2011 (Ndugai akiwa Naibu Spika), nikawambia wenzangu pale mahabusu, ‘huyu (Ndugai) tumesoma naye shule ya msingi’. Wakanicheka, wakasema mwenzako yuko kule anatumikia nchi wewe uko mahabusu.

“Nilipomaliza kesi yangu nilimweleza Tundu Lissu kwamba nafahamiana na Ndugai, naye akasema atamweleza, na akamfikishia salamu zangu. Tuliongea na Ndugai, tukapanga kupitia Tundu Lissu niende kumtembelea bungeni. Bahati mbaya, kuna mambo mengi yalipita katikati kikiwamo kifo cha Mbunge Christina (mdogo wake Tundu Lissu), baada ya matatizo mengi kupita, Septemba 2017 tulizungumza na Lissu akiwa Dodoma, nami nikiwa hapa Ikungi, tukakubaliana siku iliyofuata niende Dodoma, lakini baadaye mchana (baada ya kupanga safari na Lissu) taarifa zilivuma kwamba Lissu amepigwa risasi, ndipo safari ya kwenda kumwona rafiki yangu wa zamani Ndugai ikaishia hapo hadi leo,” anasema Muro.

Bado anaamini atakutana na rafiki yake (Ndugai), akisisitiza kuwa Lissu na Ndugai ni watu wenye nasaba na Jimbo la Singida Mashariki.