Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa amezidi kujiimarisha kisiasa baada ya kuongeza idadi ya wenyeviti wa Kamati za Kisekta za Bunge wanaomuunga mkono.

Uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati hizo uliofanyika mwishoni mwa wiki, umeonesha kuwa kambi ya Lowassa kuelekea kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015 imepata ushindi mkubwa.

 

Asilimia zaidi ya 80 ya wabunge wanaopingana na Lowassa katika mpango wake wa kuelekea 2015 ama wameshindwa kutetea nafasi zao, au kuchagulika kuongoza Kamati za Kisekta.

 

Lowassa alipoulizwa na JAMHURI kuhusu hilo, amesema kwa kifupi, “Namshukuru Mungu.” Hakufafanua iwapo idadi kubwa ya wenyeviti waliochaguliwa kuongoza Kamati hizo wanamuunga mkono au vinginevyo.


Waliochaguliwa mwishoni mwa wiki kuongoza Kamati za kisekta za Bunge ni Anne Makinda (Kanuni za Bunge), Hassan Ngwilizi (Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge), Lediana Mung’ong’o (Masuala ya Ukimwi), Edward Lowassa (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) na Andrew Chenge (Bajeti).


Wenyeviti wengine na kamati zao zikiwa katika mabano ni Pindi Chana (Sheria na Utawala), Mahmoud Mgimwa (Uchumi, Viwanda na Biashara), Anna Abdallah (Ulinzi na Usalama), Margaret Sitta (Huduma za Jamii), Jenista Mhagama (Maendeleo ya Jamii) na Profesa Peter Msolla (Kilimo, Mifugo na Maji).


Wengine ni Peter Serukamba (Miundombinu), Kabwe Zitto (Hesabu za Serikali), Rajab Mbarouk (Hesabu za Serikali za Mitaa), Dk. Hamis Kigwangalla (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini) na James Lembeli (Ardhi, Maliasili na Mazingira). Walioshindwa katika kinyang’anyiro hicho na wanaodaiwa kuwa kinyume na mtazamo wa Lowassa ni Christopher ole Sendeka, Anne Killango Malecela, Profesa David Mwakyusa, Idd Azam, John Cheyo na Augustine Mrema.


By Jamhuri