Mfanyakazi wa Kampuni Ikolo Investiment Ltd, Joseph Ludovick (31), aliyekamatwa na Polisi akihusishwa kwenye sakata la utekaji na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, anatajwa kuwa ni mtu muhimu katika upelelezi wa tukio hilo.

Hadi tunakwenda mitamboni, Ludovick anakuwa mtuhumiwa wa pili kukamatwa baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Kagera, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare.

 

Ludovick alikamatwa Ijumaa iliyopita mjini Iringa, ambako maelezo ya awali yanasema alikwenda kwa shughuli binafsi akiwa mgeni wa mwanablog maarufu, Majid Mjengwa. Jina moja la “Ludovick” linatajwa kwenye mkanda wa video unaodaiwa kuwa na sura ya Lwakatare na watu wengine wasiofahamika waliokuwa wakipanga njama za kuwadhuru baadhi ya waandishi wa habari na wanasiasa.


Ludovick alisafirishwa kwa helikopta ya Jeshi la Polisi hadi Dar es Salaam ambako anaendelea kushikiliwa. Kukamatwa kwake, ingawa hakujawekwa bayana na Polisi, kunahusishwa na taarifa za kiintelijensia, na pia namna alivyodai kutokea na tukio la kutekwa usiku huo huo ambao Kibanda alitekwa.

 

Kibanda, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, alitekwa usiku wa kumakia Machi 6, mwaka huu wakati akirejea nyumbani kwake Goba Kunguru, Kata ya Mbezi Juu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Anatibiwa katika Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini hivi sasa.

 

Ludovick anatajwa kama mmoja wa vijana wasomi walio karibu na viongozi wa Chadema, ingawa amekuwa hajioneshi moja kwa moja. Historia yake fupi inaonesha kuwa alizaliwa Februari 25, 1982. Alisoma katika Seminari ya Mtakatifu Francis wa Sales mkoani Morogoro, na baadaye alijiunga na masomo ya Falsafa na Teolojia katika Taasisi ya Wasalvatori ya Morogoro. Baadaye alijiunga katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Chang’ombe (DUCE). Amemuoa Digna Swai. Pia kuna habari kwamba ameshafanya kazi katika makazi ya Papa mjini Vatican.

Wasiwasi wa Ludovick kuhusika

Polisi wanamtuhumu Ludovick kwamba ameweza kujipenyeza na kuwa karibu na wanahabari wengi, lengo likiwa ni kuwachunguza, kurekodi nyendo zao na kusiwalisha kwa genge ambalo halijafahamika. Inaelezwa kuwa mwaka jana, na mwaka huu amekuwa akiwasiliana na wanahabari na watu mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza azma hiyo.

 

Polisi wamesema wamepata ushahidi usio na shaka kwamba mtuhumiwa amekuwa akiwasiliana na baadhi ya waandishi wa habari, akiwadadisi kujua wanakoishi na wanakopendelea kwenda baada ya kazi. Inadaiwa kuwa mkakati ulilenga kuwadhuru baadhi ya waandishi wa habari na watu wengine, ili kuwajengea hofu na wakati huo huo kuibua chuki kati ya jamii na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.


Duru za uchunguzi wa Polisi zimebaini kuwa mmoja wa walengwa wakuu kwenye mkakati wa kuumizwa alikuwamo Kibanda, na kwamba mwaka jana mwishoni mtuhumiwa huyo alihamia Ubungo Kibangu na kuishi karibu na Kibanda.

Inadaiwa kuwa, Kibanda akiwa hajui mpango huo, alihamia Goba Kunguru; na ndipo Ludovick naye alipoanza mipango ya kutafuta chumba maeneo ya Mbezi. Hata hivyo, kwa mujibu wa habari kutoka Polisi, hadi tukio hili linatokea, alikuwa hajahamia huko.

Madai ya Ludovick ya kutekwa yaliyoibua shaka

Ludovick alituma taarifa ifuatayo kwenye mitandao ya kijamii saa 11:09 alfajiri ya Machi 6, 2012 akidai kwamba alitekwa. JAMHURI inachapisha maelezo hayo kama yalivyo bila kuyahariri. Yanasomeka hivi:


Leo usiku yapata saa tano na nusu niliachana na Maggid Mjengwa maeneo ya Shekilango tukitokea Rose Garden.yeye alielekea hotelini alikofikia,sehemu fulani kariakoo,nami nikasubiri kigari kuelekea nyumbani kwangu.hapo shekilango,magari yalichelewa kidogo,pembeni ilipaki bajaji ikiwa na watu 2 na dereva.ndipo wakaniambia twende tuchangie mia tano tu kwenda ubungo mataa.nikakaa katikati ya hao jamaa.


Ghafla wakakata kona na kuanza kuelekea mabibo na wakiulizana kama wako kamili,na mwingine kujibu yuko kamili.nikajua tayari niko mikononi mwa majambazi na sikujua wako kamili namna gani,kwa hiyo nikaamua kuwa mtulivu.Tulipofika relini karibu na mabibo,wakanipokonya begi lakini hawakulifungua. (ndani yake kulikuwa na laptop,toshiba kubwa,na chaja yake,kamera ndogo ya digital na USB yake,modem ya zantel na card reader.).tulipofika maeneo ya loyola sekondari nikawasihi wanishushe ili nirudi mwenyewe,wakaniambia safari ile inaishia jangwani.nikaingiwa na wasiwasi mkubwa na nia yao hasa.maana wameshanipokonya begi,kwa nini wasiniachie? lakini niliendelea kuwa mtulivu ili kutowa provoke.


Tulipovuka kigogo mwisho kwenye giza karibu na msikiti,wakasimama pembeni ya barabara na kuniamuru kushuka.nikashuka na kuanza kuwadai begi langu.ndipo mmoja akasema wamekuwa wastaarabu mimi naanza kuwadharau.Ghafla akanivuta kwa nguvu kunirudisha kwenye kibajaji,akamwambia mwenziye wanisachi kama nina vitu vingine.wakanisachi na kuchukua pesa (nilikuwa na elfu 35) na simu mbili ndogo za nokia.moja yenye line mbili.kisha mmoja akatoa order nivuliwe nguo.Nikavuliwa viatu,T shirt na suruali.nikabaki na nguo za ndani pekee.wakanishusha na kuniacha hapo.


Kurudi nyuma kama hatua kumi tu ndipo kituo kidogo cha polisi Kigogo.nikaanza kutoa maelezo hapo kwa zaidi kama ya saa 2 nikiwa uchi na nguo za ndani tu.Nikiwa hapo nikasikia polisi wakiwasiliana juu ya tikio la kupigwa vibaya ABSALOM KIBANDA kwenye redio calls.ilikuwa yapata saa nane.baada ya kuchukuliwa maelezo,polisi walinipatia gari nikaelekea hotelini kwa Maggid,ambaye saa kumi aliamshwa na kunichukulia chumba hapo nikapumzika.ameniazima nguo zake ndizo nimevaa bado hadi sasa.naelekea kituo cha polisi Magomeni kwenda kupewa mpelelezi wa kesi yangu.namba ya case yangu kigogo ni KIG/RB/318/2013 (WIZI KUTOKA MAUNGONI).


Namshukuru Mungu hawajanijeruhi wala kunipiga.namshukuru Maggid kwa msaada wake hadi sasa.MUNGU NI MWEMA: LUDOVICK

Taarifa ya Maggid Mjengwa baada ya madai ya Ludovick

… Na Msaidizi Wa Mwenyekiti naye alitekwa na majambazi jana usiku! “Kijana Ludovik Joseph. Tulikula wote na kuongea pale Rose Garden jana usiku. Tuliondoka kwenye saa tano usiku. Nikamfikisha mpaka kona ya Shekilango na Morogoro Road. Hapo aliniambia angepata daladala la kumfikisha nyumbani kwake. Nilimwuliza jambo tu; “ Ni salama hapa kukuacha?” Akanijibu ni salama maana amesafiri mara kadhaa katika muda huo. Masikini, akafikwa na balaa la kutekwa na majambazi kwenye bajaji. Nilikofikia Dar nikaamshwa saa kumi za usiku. Mlinzi akaniambia kuna ndugu yako amekuja na teksi hata nguo hana. Amebaki na nguo ya ndani tu. Amekabwa na majambazi. Nikamsaidia Ludovik. Na kwa vile yeye ni Yanga, basi, nikahakikisha nampa suruali na jezi ya Simba! Naam, iko siku, kila mtu ataishabikia Simba!

Watilia shaka kutekwa kwa Ludovick

Wadau mbalimbali waliochangia kwenye majukwaa ya kijamii wameonesha hofu juu ya kutekwa kwa Ludovick. Mmoja wa wachangiaji katika Jamiiforums kaandika hivi: Ndugu Ludovick, sijakuelewa vizuri. Usiku saa 5.30 unatembea na vitu vyote hivyo, Sheikilango/Manzese? Hauwezi kuwa serious. Ukapanda bajaji usiku wote huo, ukakaa katikati yao. Mhhhhh! Jambo la kufikirika.


Mabibo relini wakakunyang’anya begi lenye vitu vya thamani, hawakulifungua. Hivi unadhani watu wote ni mabwege, kwani shida yao kubwa ilikuwa nini?


Kigogo mwisho walikushusha ukaanza kuwadai begi lako. Wewe mwendawazimu. Yaani mamba kakutema kisha mwenyewe unarudi tena mdomoni kwake!!!!!!!!!


Ukarudi nyuma kama hatua kumi tu ndipo ukakuta kituo kidogo cha polisi Kigogo. Yaani hawa vibaka wamekutoa sehemu ambayo hakuna kituo cha polisi, wakaenda kukushusha kituo cha polisi, du basi nchi hii hatuwezi kusalimika. Acha upuuzi, yaani hatua kumi, ushindwe kumwita polisi ama kukimbilia kituoni hadi unavuliwa nguo??? Polisi walikupa gari ukaelekea hotelini kwa Mjengwa. Ina maana vituo vidogo siku hizi vina magari? Kwa nini haukuenda nyumbani kwako? Dogo unajifunza usanii sio!!!

Maswali  muhimu:

1: Ludovick anasema polisi walimpatia gari, Mjengwa anasema Ludovick alifika na teksi hotelini kwake. Mbona kuna mkanganyiko?

2:  Ludovick anasema aliibiwa kila kitu (zikiwamo fedha), kama alikodi teksi fedha alizipata wapi za kumlipa dereva? Mjengwa hajasema kama ndiye aliyelipia teksi.

3:  Kigogo hadi Kariakoo ni umbali wa kilomita 4. Ilikuwaje Ludovick akatoka Kigogo Polisi saa 8 usiku akafika Kariakoo saa 10 alfajiri.

4:  Simu ya Ludovick iliwasiliana na nani kati ya saa 5 usiku na saa 10 alfajiri?

5:  Kutoka Shekilango hadi Sinza ofisini alikokuwa Kibanda kuna umbali wa kilomita 2 tu. Bashe anasema wamewahi kuviziwa nje ya geti. Je, kuna uhakika kuwa Ludovick aliposhushwa Shekilango hakwenda Sinza Kijiweni alipokuwa Kibanda?

6: Kibanda anaishi Goba (Mbezi Juu) na si Mbezi Beach kama ilivyoripotiwa. Je, kati ya saa 5 usiku na saa 7 usiku simu ngapi zilipigwa kutoka minara ya Sinza kwenda minara ya simu ya Goba?

7:  Je, kati ya saa 5 usiku na saa 7 usiku, hakuna simu ya mfanyakazi yeyote wa ofisini kwa Kibanda iliyofanya mawasiliano na watuhumiwa?

8: Je, polisi hawawezi kuchukua simu zote za wafanyakazi wa New Habari (2006) Limited, na hasa waliokuwa kazini siku hiyo na kuangalia nani aliwasiliana na nani kati ya saa 1:00 jioni na saa 6:30 usiku kisha wakachambua pumba na mchele?

9:  Je, ni kweli hakuna mfanyakazi ndani ya New Habari aliyeshiriki mpango huu?

10: Ludovick anasema alipoachiwa na waliomteka, aligeuka na kutembea hatua 10 akaingia polisi. Je, kwanini watekaji waende waache maeneo hatari kama ya kuelekea Mabibo, badala yake wakaamua kwenda polisi?

Kauli ya Mjengwa baada ya Ludovick kukamatwa

Ndugu zangu,

Usiku huu nikiwa kwenye shughuli ya shule ya watoto wangu pale Highlands Hall Iringa nilifikiwa na habari kuwa Kijana Ludovick amekamatwa na polisi kuhusuana na tuhuma za kuhusika na kuteswa mwandishi Absalom Kibanda.


Namfahamu kijana Ludovik tangu akiwa Chuo Kikuu (DUCE). Ni mmoja wa Watanzania wengi walionifahamu kupitia kazi zangu za magazetini.


Kwangu Ludovick ni kijana mtaratibu na mpole sana, na hata niliposikia habari hizi kwa namna fulani nimeshtushwa nazo. Ludovick ambaye amekuwa akiishi Dar ni mmoja wa vijana waliokuwa wakinisaidia kwa kujitolea kwenye kazi zangu za mitandaoni, hususan kwenye Mjengwablog na website ya Kwanza Jamii.

 

Amekuwa na mchango mkubwa, na hata katika miezi ya karibuni ndiye yeye aliyekuwa akifanya kazi ya kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog kila asubuhi. Akiwa Dar na mimi nikiwa Iringa, Ludovick hakuwa mwajiriwa wangu kama wanavyodhani wengine, bali amekuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa tayari kunisaidia kwa kazi za hapa na pale ikiwamo kunipelekea invoice kwa watangazaji kwenye Mjengwablog. Mara nyingi nimekuwa nikimtambulisha kama ‘ Msaidizi wa Mwenyekiti’.


Na jana nilimwomba aje Iringa aniletee vitabu vyangu vya invoice na risiti kwa vile nilitarajia ugeni wa kutoka TMF- Mfuko wa Ruzuku kwa vyombo vya habari. Kwamba huenda vitabu hivyo vingehitajika wakati wa mazungumzo na watendaji wa TMF yaliyofanyika leo asubuhi.


Hata hivyo, katika hili lililomtokea, siwezi hapa kumtetea wala kumtia hatiani. Maana, naye ni binadamu kama wengine, siwezi kusema kuwa ninamfahamu sana. Kwa vile yuko mikononi mwa vyombo vya usalama, nina imani, kuwa vyombo hivyo vitafanya kazi yake ili kutusaidia katika kupata ukweli wa jambo zima.

 

Na kama ni kweli kwa namna yoyote ile itathibitishwa kuwa ameshiriki njama za kupanga mikakati hiyo ya kigaidi, basi, ahukumiwe kwa dhambi hiyo. Na jamii, ikiwamo mimi, itamlaani vikali. Hapa chini ni maelezo niliyoyaandika kwenye ukuta wangu wa facebook, siku ile Ludovick alipopatwa na mkasa wa kuvamiwa usiku (maelezo hayo ndiyo yamewekwa hapo juu).

Mwana JF akosoa “mkanda wa Lwakatare”

Jambo lolote unaloambiwa, kuliona au kulisikia ni lazima ushughulishe akili kufikiri ili ujiridhishe kama ni la kweli au laa. Utakuwa unakubaliana na jambo ambalo si la kweli.

 

Jaribuni kuipa nafasi akili yenu kufikiri. Bahati mbaya sana katika siku za hivi karibuni imeonekana Watanzania wengi sana wana tatizo la kutoipa akili nafasi ya kufanya uamuzi na kung’amua, na mmoja wao ni Pasco ….wachache wanaipa akili nafasi ya kufikiri.

 

Kuna matukio mengi sana na mengine wengi hamyafahamu ambayo yanalenga kuichafua “image” ya Taifa na kwa kuwa matumizi ya teknolojia nchini yamekuwa yakikua kwa kasi, hasa matumizi ya simu na intaneti na kwa kuwa teknolojia inakuwa kwa kasi, na hivyo wengi wanashindwa kwenda sambamba na ukuaji wake na hivyo wanajikuta wanakubaliana na kila kitu wanachokiona au kusikia.


Katika mkanda huo ambao wewe Pasco unauita ni ‘’bonafide and genuine’’ nimefanikiwa kuuona jana mchana na mimi na wenzangu tumekaa na kuupitia kwa makini kabisa na kwa njia za kisasa zilizotusaidia kujua uhalisia wake.

 

Mkanda huo ni “fake” (umeghushiwa) na tayari taarifa imeshatolewa. Hata wewe Pasco ukijipa muda wa kukaa na kuipa akili yako nafasi utagundua kuwa mkanda ule ni “fake”, vinginevyo utakuwa unasumbuliwa na ‘’Invincible ignorance’’


Chini hapa nitakusaidia kidogo ili walau upate picha ya kuwa mkanda ule ni “fake”:

00:01…Sauti inaanza kwa kutamka “MIC’’ na kisha kuuliza, “HAPO?’’- maana yake watu hawa wanajiandaa kuanza kujirekodi na wakati wa nafanya editing (uhariri) waliyaacha maneno hayo.

00:15…Sauti ya mtu wa pili inasikika ikisema “TUTA-NOTE TENA HAPO’’-inaelekea watu hawa kuna mahali walikosea na kusema watarudia mahali hapo.


00:28…Binti anaonekana akija dirishani na kisha anaondoka baada ya maongezi mafupi na mwenzake aliyoko upande wa pili wa dirisha.


01:45…Sauti ya mtu mwingine ambaye baadaye alikuja kutambulika kama Rich inasikika akiwasalimia, lakini aliyesalimiwa (Lwakatare) kulingana na picha na mdomo wake inaonekana si yeye aliyeitikia “marahaba’’.


Kuthibitisha hilo, mara baada ya salamu, msalimiwa hakugeuka kumwangalia anayesalimia ila aliendelea na shughuli zake na papo hapo kijana anayeonekana na kupewa maelezo mara moja anaanza mazungumzo na kijana (Rich) aliyekuwa anasalimia na ndipo anamwita jina hilo “Rich’’ na wanapeana pole za matatizo na habari za sikukuu, na kadhalika.

 

Katika mazungumzo mtu anayeonekana kwenye clip (Lwakatare) bado hageuki kumwangalia huyo Rich, badala yake anaendelea kutoa maelezo namna ya kudhuru watu.

 

03: 15…Wakati mazunguzo na melekezo kutoka kwenye “clip” ya Lwakatare yakiendelea, kwa mbali anasikika binti anayemkaribisha mtu mwingine na pia anasikika akisema “napanda maua’’ na anamalizia na neno “karibu, ingia ndani’’ (Ili kumsikia binti umakini unahitajika kidogo).

 

03:20…Inasikika sauti mtu akikoroga chai kwenye meza yalipokuwa yanafanyika mazungumzo na anarudisha kijiko kwa kugonga meza, lakini picha inayoonekana haimuoneshi mtu huyo na wala hakuna dalili za kuwa kwenye meza ya Lwakatare kulikuwa na kikombe cha chai na kuwa chai ile ilikorogewa pale; na pia kwa kufuatilia kwa makini mtu anayekoroga chai si yule aliyekuwa anapewa maelekezo.

Kitu kingine ni kwamba “clip” nzima quality (ubora) ya sauti ya Lwakatare haisikiki sawa sawa kama sauti ya mtu wa pili (kijana anayepewa maelekezo).


05:35…Sauti inasikika ikitamka “Unaelewa lakini?’’ Lakini ukiangalia kwa makini mdomo wa Lwakatare hakutamka neno hilo , badala yake mdomo unaonesha ametamka “Umeliona hili?’’ Ni sawa na pale alipokuwa akisalimiwa na “Rich’’ hakutamka neno “marahaba” na badala yake neno alilotamka kulingana na mdomo ulivyoonekana alitamka, “Yote muhimu’’ na ndiyo maana hakugeuka kumwangalia yule aliyekuwa anasalimia kama ilivyoeleza hapo juu.


05:57…Sauti inasikika ikitamka kuwa “Kama tulivyofanya hii ya Morogoro kisha kwenda Igunga’’. Swali la kujiuliza hapa ni mauaji yapi yalitangulia, ya Morogoro au Igunga? Bado ushahidi unaonesha video hii ni ya kupika.


07:36…Sauti inasikika ikisema, “Dawa aina mbali mbali, vidonge, unga ama liquid form fanya utafiti ujue zinapatikana wapi na ni bei gani, ni rahisi mno kama tulivyofanya utafiti wa Mgongolwa tukapata ile kitu’’. Hapa pia kunachanganya inawezekanaje kijana anapewa jukumu la kutafuta bei na upatikanaji wa dawa wakati huo huo akikumbushwa namna walivyopata “ile kitu’’ kwa Mgongolwa ambapo kijana alishiriki? Maana yake kijana anajua bei na wapi zinapatikana. (Huyu Mgongolwa ni nani?)


15:59…Sauti inasika ikisema, “Unamuweka kwenye dilemma hajui adui ni nani yaani anakuja hapa anakukuta wewe ‘LUDOVICK’ ndiye unamfuatilia’’ Huyu Ludovick ni nani? Yawezekana ni mmoja wa vijana waliokuwa wanajirekodi na hili ni jina lake halisi na wametajana pasi kujua au ni code name?


17:10…Kijana anayepewa maelekezo (Ludovick) anauliza, “Kwa hiyo kama kila kitu kitaenda ‘well’ inakwenda mpaka lini?’’ Lakini katika kujibu “clip” inayomuonesha Lwakatare akijibu swali hilo akisema, “Bahati mbaya umekuja na majibu yasiyojitosheleza’’ Katika majibu haya kuna mkanganyiko mkubwa, maana hakuna uhusiano wa swali lililoulizwa na jibu lililotolewa. Tangu dakika ya 15 ya “clip” hii maelezo ya sauti zinazosikika hayana mpangilio wa maana. Mengi yalilenga kufuatisha ishara na vitendo vya Lwakatare alivyokuwa akiongea na ukitizama kwa makini hakuna uhusiano kati ya maneno yenyewe na mdomo wa Lwakatare.


19:20…Lwakatare anaonekana akiongea kwa mdomo na vitendo (kuchezesha mikono) huku kichwa chake na macho vikielekea kwa kijana (Ludovick) aliyesimama/kukaa mbele yake, mara ghafla kitu kinadondoka chini na kijana anainama kukiokota, lakini bado Lwakatare akiongea kichwa na macho vikiangalia juu alipo kijana na kijana anaitikia, “Mmmh, mmmh” mara ghafla “clip” inakatwa na kuishia hapo. Hapa pia kuna mkanganyiko mkubwa. Hakuna uhusiano wowote wa maneno yale na picha inayoonekana na tukio la kudondoka kitu chini. Binafsi naamini “clip” ingeendelea kuanzia hapo sura ya mtu wa pili ingeonekana hasa mara baada ya kuokota kitu kilichodondoka na ndiyo maana clip imeishia hapo.

(Mhariri amehariri dosari ndogo ndogo za uchapaji)

Ben Saanane alimrekodi Lwakatare?

Kada wa Chadema, Ben Saanane, anatuhumiwa kuwa ndiye aliyemrekodi Lwakatare. Saanane aliwahi kugombea kiti cha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), lakini jina lake liliondolewa katika mazingira ambayo hayakuwekwa wazi. Moja ya tuhuma ni kwamba yeye Afisa Usalama wa Taifa, na kwamba amekuwa akianzisha na kuratibu mipango ya kukihujumu chama hicho.


Mwanasiasa huyo kijana ameshaingizwa kwenye tuhuma nzito za mauaji, akidaiwa kula njama za kumtoa uhai kwa sumu Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto. Saanane amekuwa akikanusha tuhuma zote zinazoelekezwa kwake.


Kwenye mtandao wa Facebook imeandikwa kwamba Saanane ndiye anayehusika na kurekodi mkanda.


“Inaaminika hakurekodi ili autoe hadharani ila baada ya kufanikiwa kurekodi baada ya muda kupita alikwenda kumwonesha Lwakatare na kudai kiasi cha Sh milioni 5 ili kutunza siri hiyo. Lwakatare alimlipa hela hiyo na kumsihi sana asiutoe na kuomba auharibu. Jamaa alikubali.

“Baada ya miezi miwili kupita alienda tena kwa Lwakatare na kusema anaomba tena Sh milion 5 ili aendelee kuficha siri, Lwakatare alipogoma kijana huyu akaona ‘tape’ hiyo ni mtaji wa kisiasa ndipo alipoamua kwenda kuuza kwa mahasimu wa kisiasa wa Chadema kwa Sh milioni 5,” amedai mmoja wa watumiaji wa mtandao huo.


Saanane hakusita kujibu tuhuma hizo kupitia Facebook. Amesema, “Nimesikitishwa sana na taarifa za uongo zinazosambazwa kwamba nimekamatwa na niko Kituo cha Polisi nahojiwa kuhusu sakata la Kamanda Lwakatare na hiyo video ya kutunga iliyosambazwa.” Alipoulizwa na JAMHURI, alijibu, “…Wewe unanijua vizuri kwamba sina price tag (sinunuliki). Msimamo wangu kuhusu CHADEMA unaujua, niko principled (mtu wa msimamo) na sinunuliki. Hizo tuhuma ni malicious fabricated (zimetungwa) kama ilivyo kwa hiyo video. Kijana wa CCM anapokuja kuleta tuhuma kama hizo maanake ni nini. Ni gutter politics tu (siasa chafu). Ni za kupuuza.”

Maelezo ya awali ya Kibanda

Akizungumza kwa tabu alipokuwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), hospitalini Moi, Kibanda alisema, “Nilifika nyumbani kwangu kama saa sita usiku nikitokea kazini na nilipofika kwenye lango la kuingia ndani nilipiga honi ili mlinzi anifungulie. Lakini ghafla nilivamiwa na kundi la watu ambao walivunja kioo cha gari langu upande niliokuwa nimekaa. Nilitokea kupitia mlango wa abiria lakini sikuweza kuwakimbia watu wale kwani walinikamata na kuanza kunishambulia kwa vitu vizito.


“Baada ya kutoka kwenye gari, nahisi nilikanyaga sehemu mbaya, nikateleza na kuanguka wakanifuata…niliona kama watu watatu hivi wakaanza kunishambulia. Sikuwa nafahamu kilichojiri, lakini nilisikia mwingine akimwambia mwenzake afande ‘mshuti… mshuti’ huyo alipoelekeza mtutu na kujaribu ‘kushuti’ (kupiga risasi) ilikuwa kama vile imegoma.


“Nikiwa bado niko chini, wakanipiga kwa kitu cha ncha kali kwenye jicho la kushoto, wakaning’oa meno na kucha katika vidole vya mkono wa kulia, walinipiga sana na nilipata maumivu makali. Baada ya kunipiga na kunijeruhi waliniburuza hadi bembeni ya nyumba yangu na kunitupa na wakaondoka, baadaye majirani na wasamaria wema walikuja kuniokoa.

Matukio ya kutia shaka

Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe, siku chache baada ya Kibanda kutekwa na kuumizwa, alisema, “Kabla ya tukio hilo kumkuta Kibanda wiki tatu kabla, tulitoka ofisini saa 5:00 usiku na kwa muda mrefu nje ya ofisi lilipaki gari la polisi aina ya gofu lililokuwa na namba za usajili PT 180.”


Alisema kwa kuwa yeye na Kibanda wanaishi Mbezi, walipotoka walifuatana, lakini cha ajabu gari hilo lililokuwa limepaki nje ya ofisi yao na kuelekea upande wa Shekilango, liligeuza na kuwafuata.


“Gari lile liligeuza likatufuata nyuma mpaka eneo la makaburini, mbele ya Mwika Baa, likazuia gari yangu na baadaye kupaki mbele ya gari yangu. “Hawakushuka lakini baada ya dakika tatu, nne hivi akashuka askari mmoja nikawasha taa za gari ndani kwa sababu nilikuwa na mwenzangu nikamuuliza unataka nini? Akasema tunalitilia shaka gari lako, nikamwambia nimewaona ofisini na sasa mnatufuata, mnataka nini? Lile tukio tuliripoti polisi,” alisema Bashe.

 

Alisema wakati hayo yanatendeka, Kibanda alikuwa ameegesha gari lake upande wa kulia wa barabara na kwa kuwa naye aliona tukio zima, alimpigia simu na kumpa tahadhari ya kutoshuka kwenye gari. Alisema pamoja na mambo mengine alimjulisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuhusu tukio hilo ambaye aliahidi kulifuatilia.


Please follow and like us:
Pin Share