Lowassa: Ninayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu

Lowassa copy

 

Hakuna ubishi kwamba minong’ono juu ya matamanio ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, au kutajwa kuwania urais, imeshika kasi.
 Lowassa, Mbunge wa Jimbo la Monduli (CCM), amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye nguvu kubwa na matamanio ya kuiongoza nchi baada ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
 Kutokana na kutajwa huko kwa Lowassa mara kwa mara, amekwepa kutangaza hadharani japo nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu.
Wakati Lowassa akiwa kimya, yamejitokeza mambo mawili kwa harakaharaka.


Kwanza Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameagiza wanachama na wadau wa masuala ya utawala kushawishi watu wanaodhani kuwa wanafaa kuwania nafasi mbalimbali.
Bila kutaja majina, Rais Kikwete alisema kwamba kuna waliotangaza nia, kadhalika ambao wako kimya hadi sasa. Alitaka wale ambao hawajatangaza, washawishiwe.


Jambo la pili lililojitokeza ghafla ni kwa wadau hao kuanza kujitokeza hasa kwa makada watatu wa CCM wakiwashawishi kuwania urais. Makada hao ni Lowassa; pia Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalum pamoja na Mbunge Mteuliwa wa Rais aliyepata kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Makundi hayo ya watu mbalimbali yamekuwa yakijitokeza zaidi kwa Lowassa kumtaka kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Masheikh kutoka Bagamoyo
Masheikh wapatao 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Machi 21, mwaka huu walimkabidhi Lowassa Sh. 700,000 ikiwa ni mchango wao wa kumshawishi kuwania urais 2015.
 Masheikh hao wakiongozwa na Yussuf Sururu na Ally Mtumwa, walimkabidhi fedha hizo nyumbani kwake mjini Dodoma na kushuhudiwa na Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya.
 Masheikh hao wanaeleza katika salamu zao kuwa wameona mtu pekee anayefaa kumrithi Rais Kikwete ni Lowassa, hivyo wanamsihi atangaze nia na achukue fomu ya kugombea na wapo nyuma yake katika dua.
  Kuona hivyo, Lowassa akasema kuwa makundi mbalimbali ya jamii yamekuwa yakimuomba kutangaza nia kiasi cha kumfanya ashawishike kufanya hivyo wakati ukifika.


“Ila nataka kuwaahidi, naheshimu sana maneno yenu na nayakubali kwamba siku ikifika nitaweza kutafakari na kwa taratibu za chama nitachukua maamuzi, ila bado sijakuwa na maamuzi mpaka sasa.
“Natambua ya kuwa mna maono yenu na mapenzi mema kwangu, ila tusubiri huku tukimuomba Mwenyezi Mungu, maana hilo mnaloniomba ni suala kubwa ambalo linahitaji nguvu ya Mungu.
  “Nitaendelea kutafakari na kumuomba Mungu aniongoze, ila ni vyema pia tukaendelea kuiombea pia nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, nawashukuru kwa moyo wenu wa upendo mlionionyesha.”
 
Wajumbe wa Baraza la Wazazi CCM
Likafuata kundi la baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wazazi la CCM, walifunga safari mpaka nyumbani kwa Lowassa mkoani Dodoma wakimuomba wakati wa kuchukua fomu aweze kuchukua fomu na kugombea urais wa nchi.
Wajumbe hao walieleza kuwa wanayo matumaini makubwa na Lowassa kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa uongozi, hivyo wataendelea kumshawishi na kumtia moyo ili aweze kugombea nafasi hiyo ambapo wanaamini kuwa anao uwezo mkubwa wa kuongoza nchi.
Wajumbe hao ambao walikuwa wakitoka katika mikoa mbalimbali, walimkabidhi Sh. 600,000 zimsaidie katika Safari ya Matumaini muda utakapokuwa umefika.


Kutokana na hayo, Lowassa akawajibu: “Mmenipa nguvu mpya, nilipokuwa jimboni kwangu Monduli nilipokea wageni wengi, ambao walikuwa ni baadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, Movement for Change, wamachinga na hata viongozi wa dini. Jana nimepokea masheikh kutoka Bagamoyo. Hawa wote waliongea na kunishawishi ikiwa ni pamoja na kuniombea.


“Hoja nimeielewa na Mwenyezi Mungu akinijaalia nitaweza kufanya maamuzi. Ukweli ni kwamba bado namuachia Mungu aweze kuniongoza. Mmenipa faraja, tumuombe Mungu atuongoze.
“Kazi ninayowaombeni si tu kunishawishi bali washawishini Watanzania waweze kujiandikisha katika daftari ili wapate haki yao ya msingi ya kupiga kura. Mshikamano ni muhimu katika nchi,” anasema.
 
Wamachinga, bodaboda na wanafunzi
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya mkoani Dodoma, wafanyabiashara ndogondogo na waendesha pikipiki (bodaboda) waliunganisha nguvu ya pamoja na kwenda nyumbani kwa Lowassa ili kukutana naye na kumtaka awanie nafasi ya urais.
Mwakilishi wa kundi la wamachinga, Robert Mwakaselo, anasema kuwa, “Tunakuomba utangaze nia ya kugombea kwa sababu wewe ni mchapakazi, na kauli yako kuhusu vijana katika ajira ni kauli sahihi maana ukiwa Ikulu tunaamini viwanda vyetu utavifufua, ajira zitapatikana nchi nzima nasi tutaacha kukimbizana na polisi kama ilivyo sasa.”


Mwakilishi wa waendesha pikipiki (bodaboda), Bakari Ngalama, anaeleza kuwa, “Tupo tayari kukupigania maana wewe ni kiongozi wa vitendo na maono kwa nchi yetu ambayo imetutelekeza.”
  Rais wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Fredrick Lutengano, anasema kuwa; “Tupo na wewe mahali popote na wakati wowote, tunakuhakikishia kuwa muda ukifika kachukue fomu nasi tutakusindikiza na kuhakikisha fomu hiyo iko mikononi mwako. Tuna matumaini makubwa na wewe, tutaendelea kukushawishi.”
Azan Baraka Nkya kutoka Chuo cha Madini anaeleza kuwa; “Tutaacha kukushawishi pale utakapojitoa lakini si vinginevyo, tunakuhakikishia kuwa hizi mbio zetu zitakoma pale tu utakapoingia katika Ikulu ya Magogoni. Utakapokuwa nasi tupo, sisi ndiyo tunaokuhitaji wewe, hivyo tunakuomba usisite.”
Mwakilishi wa Chuo cha Mipango, Julius Mavele, anasema, “Tunaamini kwako, hatujaja hapa kwako kwa kubahatisha, tunakuomba usisite. Kupanga ni kuchagua, tumepanga na kuchagua kuwa na wewe mahali popote na wakati wowote.


Naye, Mhadhiri Profesa Kopoka anasema, “Tunakuomba utangaze nia na uchukue fomu, utendaji kazi wako unafahamika kwani siyo wa shaka. Tunayo imani kubwa na wewe, tunakuomba ukubali ombi letu, tunahitaji kiongozi mwenye dira, mwelekeo na uchungu wa nchi yake.
“Kwako ni Monduli, lakini siku utakapokuja kuchukua fomu tutakuwa na wewe kwa vyovyote vile, tunakupatia kiasi kidogo cha fedha ya kununulia mafuta ya gari kutoka Monduli mpaka Dodoma kuja kuchukua fomu 150,000.”
 
Kauli ya Lowassa
“Mmenishtua kwa faraja. Sikutegemea nyumbani kwangu kujaa watu kiasi hiki, huu ni moyo wa upendo. Zamani nilipokuwa nikiulizwa nilikuwa nikisema nitavuka mto nitakapofika darajani, hoja imejengwa nimeielewa.
“Wakati ule chama cha Labour walikuwa wanakosea, lakini akatokea Tony Blair alikipaka rangi chama chake, alipojitokeza aliulizwa utafanya nini, alijibu moja elimu, mbili elimu na tatu elimu. Naamini njia pekee ya kuokoa Taifa ni lazima kuwekeza katika elimu kwanza, baadhi yenu hapa ni matunda ya shule za kata. Nilizijenga kwa moyo wangu wote, na wale waliozembea wanajua  nini kiliwapata.
“Mambo yakienda vizuri nikishawishiwa vya kutosha nitakuwa na la kusema, ninachojua uchaguzi huu utakuwa uchaguzi mgumu sana, wenye mambo mengi, uchaguzi ni hesabu, hivyo kila Mtanzania aliyetimiza umri wa kupiga kura analo jukumu mbele yake, jukumu la kujiandikisha kupiga kura ili kuwachagua viongozi anaowahitaji.
“Nendeni mkawashawishi vijana wenzenu watimize haki yao ya msingi ya kupiga kura na hatimaye kuchagua viongozi wa nchi yao.”
 
Wachungaji wa Kipentekoste
Kufumba na kufumbua, wakaibuka Wachungaji kutoka katika ikoa na wilaya mbalimbali nchini waliofika nyumbani kwa Lowassa. Kiongozi wa msafara huo, Mchungaji Bernedict Kamzee, kutoka Katavi anasema kuna kitu kimewasukuma na kwamba kipo ndani ya maisha yao.
  “Tumejigharimia kuja kukutia moyo na kukueleza kuwa tupo nawe, tunaamini nchi yetu ya Tanzania kupitia wewe tutakuwa salama. Hakuna aliyetushawishi, tumesukumwa na Mungu tufanye hivi, tunaamini sauti ya wanadamu ni sauti ya Mungu.
  “Tumekuja kwako tufanye maombi ya pamoja maana tumeambiwa tuombe bila kukoma, tunakutia moyo, songa mbele katika kazi, tunakuomba uchukue fomu ugombee urais maana unaweza,” anasema.


  Kamzee akasema, “Sasa imani bila matendo imekufa, tutakuombea mpaka mwisho wa safari yako, tunaamini Mungu tunayemtumikia, tunamwambia Mungu tunamtaka rais atakayetokana na maombi, maandiko yanasema mtu mwema akitawala hata wadudu watapata nafuu.”
 
Mwenyekiti wa CCM Shinyanga
Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Hamis Mgeja, anasema kwamba licha ya Uislamu wake, lakini ni viongozi wachache nchini wenye hulka na tabia kama zake.
“Siyo mdini, anayependa na kuheshimu uhuru wa kuabudu, siku zote anaiangalia nchi yake Tanzania. Ni kiongozi anayeweza kuwaunganisha Watanzania wote.
 “Na mimi kama kiongozi na utashi wangu katika lile ninaloliamini najua nchi yangu inahitaji kiongozi wa aina gani. Nguvu kubwa za maombi haya ni kubwa sana, wanaotubeza kuwa tumepewa pesa wameishiwa na wanatapatapa,” anasema.
 
Lowassa akajibu
“Hii ni siku ya kipekee katika historia ya maisha yangu, asanteni mmeandika jambo kubwa katika maisha yangu. Nimekuwa nikipokea watu wengi kuja kunishawishi, wanakuja watu wenye nia moja, nia njema; jambo hili ni kubwa tuingie kwenye sala tupige magoti tuombe,” anasema.
“Ninayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu, tuendelee na sala hatimaye Mungu akubali. Kuna mtu mmoja katika magazeti amesema maneno ya hovyo, siwezi kumjibu kwani nitakuwa nampa ujiko.”


Mbali ya hao, pia Lowassa alipokea kundi la watu wapatao 60 waliofika nyumbani kwake kutoka Mbarali mkoani Mbeya, wakiongozwa na Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Wilaya na mfanyabiashara Ibrahim Ismail Mwakabangaz.
Mwakabangaz anasema, “Kazi yetu kubwa iliyotufikisha hapa ni kumueleza na kumuomba Lowassa awasikilize hasa wapenzi wake, wanaomuunga mkono achukue fomu agombee urais. Sisi tumetoka Mbarali kwa basi na wenzetu wamekuja kwa pikipiki, yote haya ni kutokana na kuwa na imani kubwa na wewe. Tunaamini ya kuwa utatuongoza. Hizi changamoto unazozipata ni kutokana na uwezo wako, zisikutishe. Ukiona mchezaji anakabwa na mabeki zaidi ya watatu ujue huyo ni tishio kwa timu hiyo, wewe ni tishio kwa baadhi ya watu lakini sisi tutaendelea kukuunga mkono”.
 
Mwenyekiti wa Bodaboda
Yahya Katagara, Mwenyekiti wa Bodaboda, anasema; “Tumetumia siku mbili kutoka Mbarali, tumekuja tukiendesha bodaboda zetu, nia ya kuja na usafiri huo ni kukuomba uchukue fomu maana wewe ni mwanzilishi wa bodaboda. Tunaamini juu ya usafiri huu ulioutoa, ndiyo maana tumeutumia.”
 
Kauli ya Lowassa
“Nimeambiwa mmesafiri kilometa 600 kutoka Mbarali mpaka hapa, nimefarijika sana maana si jambo la kupuuza hata kidogo. Bodaboda wanafanya kazi kubwa nchini, wanahitaji kusaidiwa nami binafsi nitaendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono.

 

“Nasikitika wanasema nimewaiteni, nawapeni pesa, nawapikieni chakula. Ni vibaya kumdhalilisha mwenzako kwa kufikiria tumbo muda wote. Watu wamekuja hapa kwa utashi wao wenyewe na gharama zao lakini yanasikitisha sana, sintokata tamaa.
“Mimi binafsi ni vigumu kuyazuia mafuriko kwa mikono, lakini niwaombe wengine ambao wanataka kuja kuniona ambao hawajafika hapa wasubiri kwanza maamuzi ya chama. Wale ambao hawajaja tusiingize mgogoro kwenye chama, natambua mapenzi yenu kwangu lakini nawaombeni mtulie na muendelee kuhamasishana kujiandikisha kupiga kura.”
 
[email protected]
0715 446 194