Kinana

 

Mwandishi mmoja mkongwe aliwahi kuandika kuwa ukimwona mbuzi juu ya mti jua kapandishwa. Lakini pia ukimwona mbwa koko anabweka jua yuko nyumbani kwao.
  Si mara moja kusikia na kusoma vituko vya Waziri Lazaro Nyalandu. Madudu yake yamewekwa hadharani kwa ushahidi si mara moja wala mbili.


 Wengi wameonesha kushangazwa na ukimya wa aliyemteua! Imefikia wengine kuhoji endapo Nyalandu ana kismati (bahati) tu au kuna kingine zaidi!
 Wengine wameenda mbali zaidi kudai kuwa kama ni msaada wa ‘mganga’, basi huyo ‘mganga’ wake ni kiboko. Haiwezekani madudu yote ya kutisha ya Nyalandu eti bado leo ni waziri na  anaendelea kutamba tena kwa kiburi! Kiburi hiki kinatoka wapi?

 
 Nyalandu sasa anaitafuna TANAPA kweli kweli. Anafanya hivyo kwa sababu haina Bodi tangu mwanzoni mwa mwaka jana. Hakuna wa kumzuia kuchota fedha. Jamani, ina maana wabunge hadi Rais wa nchi hawalijui hili jambo? Au tuamini kuwa kuna mkono wa wakubwa kwenye mtandao huu wa kuimaliza TANAPA na Ngorongoro?


  Si nia yangu kurejea madudu ya Nyalandu. Kama wewe ni mfuatiliaji, naamini utakuwa unajua Nyalandu ni mtu wa namna gani na kwamba yote yaliyowahi kuandikwa kumhusu yeye hakuna hata moja alilosingiziwa. Na ndiyo maana hata waandishi walimshauri kuwa kama anaona kuwa hatendewi haki aende mahakamani.
 Baada ya kubanwa sana Nyalandu aliandaa taarifa kwa umma aliyodai kuwa inatoka wizarani. Taarifa hiyo ambayo watendaji wakuu wizarani kwake wanadai walishangaa kuiona magazetini (kwa maana kwamba haikuandaliwa wizarani) haikujibu hoja yoyote zaidi ya kulalamika kuwa eti “Tuhuma dhidi ya Waziri Nyalandu zililenga kumchafua, kumuondolea heshima mbele ya jamii na kupunguza kasi na dhamira yake ya kupambana na ujangili!”


 Eti majibu haya yalitosha kujibu hoja nzito zenye ushahidi za yeye kuhamishia ofisi hotelini; kulala Arusha na kuamkia Dar es Salaam kila siku awapo nchini kwa gharama na ndege ya Serikali; kwenda kuzurura Marekani na vimada kwa gharama za Serikali; kujilipa posho tatu kwa safari moja; kugawa kinyemela vitalu vya uwindaji kwa rafiki zake na matumizi mabaya ya leseni ya rais kuua mamia ya wanyama kinyume cha sheria.


  Pia kuna tuhuma za kurefusha msimu wa uwindaji ili kuwafurahisha rafiki zake; kuhusika na ujangili; kutishia walinzi kwa silaha huko Singida na kuvunja vizuizi pale walipotaka kukagua gari lake; kuwashauri wenye hoteli kuishtaki Serikali kugomea tozo; kusaidia baadhi ya kampuni za utalii kukwepa kulipa kodi za Serikali; kufukuza kazi watumishi waadilifu na kuwaweka watuhumiwa wa ujangili; kula njama na Wakenya ili kufungua mpaka wa Bologonja; kuhusika katika kashfa ya kuagiza ndege chakavu iliyoua marubani wazalendo watatu; na jaribio la kuuza mbuga zetu akishirikiana na James Lembeli.


  Kashfa hizi zimeandikwa mno kwenye magazeti na hata kujadiliwa bungeni. Hakuna majibu au utetezi wa maana uliotolewa, lakini Nyalandu bado anapeta! Ni dhahiri kuwa hapo mtini (wizarani) alipo kapandishwa na aliyempandisha anajua kwa nini kafanya hivyo na ndiyo maana hata ingenyesha mvua ya mawe hawezi kumshusha.
  Kama tembo wataisha waishe, lakini Nyalandu hang’oki ng’o! Watu wote wanaoonekana kikwazo kwa Nyalandu watang’oka ili Nyalandu abaki afanye vitu vyake. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Dk. Cyril Chami, Khamis Kagasheki, Maimuna Tarishi, Profesa Alexander Songorwa, Profesa Jafari Kideghesho na Aloyce Nzuki.


Nyalandu, zaidi ya vituko amekuwa akidhihirisha kiburi hadharani kwa yeyote anayehoji tabia zake, hata kwa mawaziri wenzake.  Rejea majibu yake dhidi kauli ya William Lukuvi ambaye alilalamikia Nyalandu kutopatikana ofisini kwa ajili ya kutolea suluhu migogoro ya uhifadhi ikiwamo ile ya Jumuiya ya MBOMIPA; majibu yake kwa Ole Telele juu ya mgogoro wa Loliondo na kauli dhidi ya Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru juu ya maoni yake kuhusu wagombea urais.


  Na karibuni zaidi ni kejeli zake dhidi ya Katibu Mkuu wa chama chake, Komredi Abdurahman Kinana. Kiburi hiki na kejeli kwa wazee hawa kinatokana na imani yake kuwa hawezi kushuka mtini na kwamba yupo mwenye mamlaka zaidi anayemlinda.
Itakumbukwa kuwa katika mkutano wake hivi karibuni na wanaCCM huko Kondoa, ambako kuna mgogoro mkubwa kati ya wananchi na Pori la Akiba la Mkungunero, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana alionesha kukerwa na tabia ya uzururaji na ubabaishaji ya Nyalandu kwa ziara ambazo hazina tija. Akataka Nyalandu atoe mfano wa mgogoro gani amewahi kuutatua katika migogoro lukuki inayohusu watu na wanyamapori.


Majibu ya Nyalandu kwa hoja hii, badala ya kujirekebisha yakawa kijembe au kejeli kwa bosi wake huyu wa chama. Kwamba eti sasa atakuwa anazururia angani (kwenye ndege)! Na zaidi kikundi cha viongozi wa dini wanaojiita Kamati ya Amani ya Madhehebu ya dini wakajitokeza kumponda Kinana kwa kumtaka achunge kauli zake dhidi ya ‘mchapakazi’ Nyalandu!
Sitashangaa kusikia kuwa tamko la viongozi wa dini aliliandaa Nyalandu mwenyewe! Viongozi hawa ni wale ambao amekuwa akiwaandalia ziara mbugani na hafla kadhaa kwenye hoteli za kitalii kwa kile anachowalaghai watu kuwa eti ni juhudi zake za kupambana na ujangili!
Wewe ujangili unafanyika Iringa au Serengeti viongozi wa dini unaowatumia kupambana unawatoa Dar es Salaam! Kwani Iringa na Serengeti hakuna viongozi wa dini? Mtu atakosea wapi akisema kuwa viongozi hawa wanaganga njaa na Nyalandu anawatumia kwa malengo yake? Itoshe kusema kuwa misikiti na makanisa yetu yameingiliwa na matapeli!


  Labda sifa moja kubwa ya Nyalandu ni ujasiri wa kufanya mambo ya hovyo. Kubwa ni hili la uthubutu wa kununua watu kufanikisha malengo yake na kuwatumia vilivyo.  Kwani hatukuona Peter Msigwa, Waziri Kivuli wa Maliasili, alivyoufyata na kuanza kujianika katika vyombo vya habari kusafisha kashfa za Nyalandu japo kwa hoja zilizochoka huku akisema mwenyewe kuwa Nyalandu anamshirikisha kwenye mambo yake ndiyo maana hasemi tena?
 Msigwa anayejiita mchungaji atapata wapi ujasiri wa kukemea madudu ya Nyalandu wakati anaalikwa kwenye vikao vyenye posho nene na siku hizi na yeye anajua ilipo Dubai au Marekani kwa udhamini wa Nyalandu?


 Kwa Msigwa, maneno yaliyo kwenye kumbukumbu la Torati 16:19 kwamba  “Usikubali rushwa, kwa maana rushwa hupofusha watu wanaoona vizuri” hayana maana tena na pengine angepewa fursa kufuta baadhi ya vifungu vya Biblia angeviondoa vifungu vyote vinavyokemea rushwa kama Ezekiel 22:12; Amosi 5:12; Mika 3:11 na 7:3; Kumbukumbu la Torati 10 na 16:19; Muhubiri 7:7; Kutoka 23:8; Ayubu 15:34; Mithali 17:23 na 29:4 na Isaya 1:23.


Tumeshuhudia Nyalandu mwaka jana akithubutu kuwanunua baadhi ya wabunge ili kukwamisha bajeti yake yeye mwenyewe kama shinikizo ili uamuzi wake wa kufukuza wakurugenzi na kuweka wa kwake kinyume cha sheria uheshimiwe; tumeona alivyogomea uhamisho wa wateule wake kwenda vituo vingine na hatimaye baada ya kukwama kukimbilia ubalozi wa Marekani kuishtaki Ikulu! Na kwamba mpaka sasa hivi bado anashinikiza wateule wake hao warudi idarani.


  Ni Nyalandu huyu huyu ambaye ametuingiza mkenge na Wakenya baada ya kuwahakikishia kuwa angefungua mpaka wa Bologonja. Baada ya kukwama akawashauri Wakenya kuzuia magari ya watalii kutoka Tanzania kuingia Jomo Kenyatta International Airport kushinikiza mpaka ufunguliwe!
  Na hata baada ya hali kuwa mbaya akavunja itifaki na kwenda kukutana na mawaziri wa Kenya bila hata Balozi wetu huko kuwa na taarifa! Kama si msimamo wa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhusu hili sijui hali ingekuwaje!


Nyalandu, bila kumshirikisha Mkurugenzi wa Wanyamapori, kaandaa Tangazo la Serikali kurefusha msimu wa uwindaji. Hii kaifanya kwa kupuuza taarifa za utafiti za TAWIRI, tamko la Waziri Kivuli wa Maliasili (japo sasa kimyaa!) na ushauri uliotolewa bungeni mwaka jana. Kwa nia ya kuwafurahisha waliomtuma (kampuni za uwindaji) Nyalandu mwenyewe kavujisha siri za Serikali kwa kuwapa rasimu ya nakala ya Tangazo la Serikali (GN) na hivyo kuwafanya wauze safari za uwindaji nje ya nchi. Ni baada ya kukwama, Nyalandu anashirikiana na wenye kampuni kumlaumu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba amekwamisha GN hiyo, akidai kuwa hii ingeiletea nchi hasara kubwa kiuchumi na kidiplomasia.


Nyalandu huyu huyu akasahau kuwa Julai alishirikiana na kampuni hizo hizo za rafiki zake kumnyang’anya kwa dhuluma Mtanzania vitalu na kumfutia vibali vyote vya kufanya biashara ya uwindaji hapa nchini.
Makosa aliyomtuhumu nayo mzawa akayaruhusu yafanywe na rafiki zake Wamarekani siku chache baadaye, tena kwa kutumia vibaya vya Leseni ya Rais! Akasahau kuwa wageni wa mzawa huyu wenye hadhi ya ukuu wa nchi walishafika nchini na kulazimika kurejea kwao baada ya Nyalandu kuwanyima vibali.
Mungu hamfichi mnafiki. Magari ya kampuni hizo za TGTS yamekamatwa yakiwa na shehena kubwa ya bangi. Hii ilitosha kuzifutia leseni, lakini kwa sababu ni za rafiki zake Wamarekani, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Wanafiki kina Msigwa wamekaa kimya.


Jambo la kushukuru ni kuona kwamba kumbe hata Chama kinamuona Nyalandu kama tatizo na kimethubutu, japo kimechelewa, kumkemea. Lakini je, chama hiki kina meno na uwezo wa kuiwajibisha Serikali yake? Sitashangaa kama kauli ya Kinana haitamgharimu yeye mwenyewe akaondoka akamwacha Nyalandu akitamba!
Aliyempandisha mbuzi mtini anajua kwa nini hataki ashuke! Na mbwa koko anapobweka anajua kuwa yuko salama kwa kuwa yuko nyumbani. Alamsiki!

tomojwuku@gmail.com

2636 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!