shukuru kawambwa 222

 

Umbali mrefu kati ya shule za sekondari za kata na makazi ya wanafunzi unachangia kwa kiasi kikubwa ‘anguko’ la wanafunzi katika matokeo ya mwisho ya wahitimu wa kidato cha nne kila mwaka.
 Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda wa miezi mitano umebaini kuwa ufaulu hafifu wa wanafunzi hao husababishwa na umbali mrefu uliopo kati ya shule na makazi ya wanafunzi.
Kadhalika, sababu nyingine ni uteuzi holela wa wanafunzi wa mijini wanaojiunga na shule za sekondari za kata.
Mwalimu Khalifani Gora wa Shule ya Sekondari Mikese, katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, anasema, “Hali hii ikiendelea inaweza kulikwamisha Taifa kuifikia Dira ya Maendeleo ya Milenia mwaka 2025.”  
Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni, Gora anasema, “Mimi ni mwalimu pekee ninayeishi hapa shuleni. Ufaulu hafifu hapa shuleni upo. Ila fahamu ufaulu hafifu una sababu zake na sababu nyingi.
“Kwanza kuna mazingira yasiyo rafiki kielimu. Kama unavyoona mwenyewe. Hapa hakuna umeme wala maji na la pili au kubwa ni umbali kati ya makazi ya wanafunzi walio wengi na shule hii ilipo.”
Anasema kwamba, “Umbali unasababisha uwepo wa matatizo mengine. Mazingira haya yanafanya wanafunzi wengi kushindwa kuhitimu elimu ya sekondari. Wanaohitimu, wengi wanaambulia kufeli kila mwaka.”
Mwalimu huyo aliyekuwa akizungumza kwa tahadhari, anasema Mwalimu Gora huku akionekana kusikitikia hali hiyo, “Mahudhurio nayo ni hafifu. Wakati nahamia hapa mahudhurio yalikuwa si chini ya wanafunzi 800 kwa siku. Siku zinapozidi mahudhurio yanashuka.
Yakawa wanafunzi kati ya 700 na 720 kwa mwaka jana. Kwa sasa hawazidi wanafunzi 500. Wanafunzi wengi hawafiki shule.
Anaendelea kusema, “Wanafunzi wanaofika shuleni, nao wanakuwa wamechoka. Hali zao za kujifunza zimeshuka. Mara nyingi huchelewa. Kiutaratibu tunawapatia adhabu. Tunafanya hivi ili uchelewaji usijirudierudie.  Kuna wanafunzi ambao hawafiki shuleni kabisa. Wamejiingiza katika shughuli nyingine za kujipatia kipato. Hivyo mahudhurio yao ni mabaya.”
Anasema kwamba wasichana ndiyo wameathirika zaidi kwa sababu umbali unawalazimisha kuingia katika ‘mtego’ wa kurubuniwa kingono kwa urahisi.
Nani anarubuni? Katika hilo, Mwalimu Gora anafunguka, akisema; “Hapa kwetu tuna waendesha bodaboda. Wamewarubuni wasichana wengi. Wengine wameharibiwa maisha. Kuna waliopata ujauzito.”
Hali ikoje shule? Mwalimu Gora kwa haraka anasema, “Taarifa zilizopo shuleni zinaonesha, si chini ya wasichana watano kila mwaka wanaripotiwa kupata ujauzito. Kuna matukio mengine kama haya ambayo hayaripotiwi. Wengine wanapopata ujauzito hutoweka shuleni kimyakimya na kwenda mbali kwa ndugu zao. Taarifa zake hufichwa.”
Anasema kwamba wengi wa wanafunzi huja shule na kurejea makwao kwa miguu na kwa mwendo wa umbali mrefu. Na kutokana na hali za uchumi na wazazi au walezi wao, wanafunzi hao wanakosa akiba katika mifuko yao hivyo kushindwa kumudu gharama ndogo za vyakula vinavyoandaliwa na wakazi waishio jirani na shule hiyo.
“Kwa bahati mbaya hapa shuleni hatuna huduma yoyote ya chakula wala maji ya kunywa. Hata huduma ya maji ya bomba hapa shuleni hatuna. Shule nayo iko mbali na makazi ya watu. Hali hii inawafanya wanafunzi kutozingatia masomo.
“Wanafunzi hawa wanatoka majumbani kwao usiku bila ya kuweka chochote tumboni ili kuwahi shule. Wanapofika hapa wanakaa hadi jioni bila ya kuweka chochote tumboni,” anasema.
Anasisitiza kwamba maisha ya kiuchumi ya wazazi wa wanafunzi ni magumu kwa sababu wengi hutegemea mapato ya msimu kutokana na mavuno ya kilimo.
 “Ndiyo, wanapata pesa zao kwa msimu. Kuna wanafunzi hawafiki shuleni mwezi mzima. Ukimwadhibu mwanafunzi ikatokea akapatwa na tatizo mzazi anakuchukulia hatua za kisheria. Kuna walimu watano wameshafikishwa polisi,” anaeleza.
Anasema, adha hizo husababisha wanafunzi wengi kuacha masomo kabla ya kuhitimu elimu hususani ya sekondari, japo changamoto hiyo ipo kwa wanafunzi wa shule za msingi waliopevuka.
 “Wahitimu  wengi huambulia ufaulu hafifu. Athari ya ufaulu hafifu ni kubwa. Kwanza wahitimu hawa wanakosa fursa katika sekta rasmi. Kuna wengine wanakosa kabisa sifa ya kupokelewa katika taasisi za juu za elimu na mafunzo. Hii inatokana na matokeo yao kuwa hafifu sana. Athari hizi zinawaandama wahitimu hawa katika maishani yao yote,” Mwalimu Gora anaeleza.
 Licha ya ufaulu hafifu wa ujumla kwa wanafunzi wote kuikabili shule hiyo, Mwalimu Gora amesema kuwa Shule ya Mikese ndiyo pekee katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini iliyotoa mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza mwaka 2013. Shule nyingine zote katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini hazikufua dafu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, katika shule hiyo umbali si tatizo pekee linalowakabili wanafunzi pekee bali pia uhaba wa walimu.
  Walimu wafundishao katika shule hiyo akiwamo Mwalimu Mkuu, Stanslaus Mbiliza, na walimu wengine wote wanaishi mbali na shule hiyo kwa sababu ya kukosa makazi rafiki. Ni Mwalimu Gora pekee ndiye anayeishi hapo.
Walimu wa shule hiyo wanaishi Manispaa ya Morogoro Mjini. Wanafika Shule ya Sekondari Mikese iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini kufundisha kisha wanarejea mjini kwenye makazi yao.
Gazeti hili lilifika katika kijiji cha Lubungo, Kitongoji cha Mgama, kata ya Mikese kwenye Halmashauri hiyo ya Morogoro Vijijini na kuzungumza na Mzee Mohamed Sintenda.
 Mzee Sintenda ni baba wa Juma Mohamed Sintenda. Juma ndiye mhitimu bora wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mikese mwaka 2013. Kwa sasa anasoma kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Kibiti.
  Yeye ndiye mhitimu pekee wa kidato cha nne mwaka 2013 katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini aliyepata daraja la kwanza. Gazeti hili lilitaka kujua siri ya mafanikio ya Juma.
  Mzee Sintenda amesema, “Umbali ni tatizo. Hivyo mimi na mke wangu, Bi. Mariamu Shabani tulijitahidi sana kuhakikisha tunagharamia usafiri wa kumpeleka shule na kumrejesha nyumbani mwanetu katika kipindi chote alichosoma Mikese.  
 “Shule ya Sekondari ya Mikese ni mbali kutoka hapa tunapoishi sisi. Iko zaidi ya kilomita 10 kutoka hapa nyumbani. Tulilazimika kumpatia baiskeli. Baiskeli hiyo nayo ilikuwa ikiharibika mara kwa mara kutokana na ubovu wa njia. Tumeifanyia matengenezo mara kwa mara kuhimili mikimiki ya safari ndefu ya kila siku.”
Wakati baba yake, akisema hayo, Juma kwa upande wake anasema “Mafanikio ya mwanafunzi yanachangiwa na mahudhurio mazuri darasani.
“Ufuatiliaji makini wa kinachofundishwa nalo ni jambo la msingi. Mwanafunzi ni lazima ahudhurie masomo darasani na kuzingatia kile anachojifunza darasani. Vinginevyo ni vigumu kufaulu mitihani.”
 Abuu Abdallah, mwanafunzi wa shule ya sekondari Tomondo iliyopo kata ya Mkuyuni kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini amezungumza na JAMHURI na kusema kuwa, ameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya umbali na michango.
Ameongeza kuwa, “Gharama za elimu ni tatizo. Michango ni mingi. Inafanya gharama ya elimu kuwa kubwa.”
Gharama za usafiri pekee ni Sh. 6,000. Ukiondoa usafiri, michango nayo imekithiri. Kuna mchango ya kila aina shuleni. Sh 40,000 mchango wa madawati. Mchango wa ulinzi Sh. 10,000. Kuna michango ya maabara. Michango mingine midogo midogo nayo ni mingi. Tatizo michango hii inahitajika kila mwaka,”  anasema Abuu.
Kauli ya Abuu inaakisi hali halisi ya gharama za shule za kata. Azimio na tamko la Serikali la mwaka 2001 ni kutoa ruzuku kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Serikali ilijiwekea mipango miwili muhimu; Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES). Mipango hii inadaiwa inatekelezwa hadi leo.
Katika mipango hiyo Serikali inatoa Sh 10,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya sekondari.
Serikali kupitia Sera mpya ya Taifa ya Elimu ya mwaka 2014 imeainisha kuwa Serikali inagharimia elimu na mafunzo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu wa ndani na nje ya nchi.
Ainisho hilo linaeleza kuwa jamii pia inachangia katika ugharamiaji wa elimu na mafunzo kwa njia mbalimbali.
Hii ni baada ya kukiri kutokuwepo kwa ugharamiaji endelevu kutokana na mifuko ya elimu kutokukidhi mahitaji ya elimu katika ngazi zote.
  Hata hivyo, sera ya elimu haijaainisha wazi ni njia zipi hizo mbalimbali ambazo jamii itachangia katika kugharamia elimu na mafunzo. Hali hii inawafanya wazazi na walezi wengi wa wanafunzi kama vile mzazi wa Abuu kushindwa kumudu hizo gharama mbalimbali ambazo kwao ni mzigo usiobebeka.
  Bibi Khadija Ramadhani Kiluma mkazi wa kijiji cha Fulwe kilichopo kata ya Mikese kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ambaye ndiye mlezi wa Amina Dunia amesema, “Kwangu mimi naona mimba ndio tatizo.”
“Ufaulu wa wanafunzi si mzuri kwa sababu wengi wamejiingiza kwenye mapenzi (ngono). Mjukuu wangu alibebeshwa mimba akiwa mwanafunzi. Hii inatokana na vishawishi alivyokutana navyo huko njiani. Lakini hata tabia za watoto wetu wa siku hizi nazo si nzuri. Ni za ajabu ajabu. Mtoto akisoma shule, akamaliza unamshukuru Mungu. Wamejiingiza katika mambo ya hovyo yanayowaharibia masomo.”
Mwalimu Mary Richard wa Shule ya Sekondari ya Nelson Mandela akizungumza na JAMHURI amesema, umbali na mazingira wanakoishi wanafunzi na shule ni chanzo cha kufeli.
  “Wanafunzi wanatembea umbali mrefu kufika shuleni. Wanakuja shule hata chai hawajanywa. Hali hii inasababisha utoro. Wengine wanaaga wanakuja shule, lakini wanaishia njiani,” anasema.
Anafafanua, “Hapa kwetu baada ya kubaini tatizo hili shule ikaamua kutoa huduma za chakula (makande) wakati wa mapumziko. Angalau sasa wanafunzi wanaonekana. Wakati wa kande ndipo wanafunzi wengi huonekana.”
Mwalimu Mary anasema, “Hali ya ufaulu katika hapa shuleni siyo nzuri. Katika matokeo ya Kidato cha nne ya mwaka 2013 hatukuwa na daraja la kwanza wala la pili. Tulikuwa na wanafunzi wachache waliopata daraja la tatu na la nne. Wanafunzi wengi walipata sifuri.”
Salehe Mwanji, mkazi wa Kata ya Mikese ambaye pia ni Mlezi wa Amina Msafiri ameiambia ,” anaelezea Mwalimu Gora huku akionekana kusikitikia hali hiyo. Tatizo lilelile la umbali kwani linasababisha mwamko wa elimu kukwama.
“Mdogo wangu, Amina Msafiri ametushangaza. Ameshindwa kuhimili adha hii. Akiwa kidato cha kwanza alianza kudai kuwa haoni. Akatuambia ni bora asitishe masomo. Madai hayo tukayakataa,” anasema.
Anasema kwamba baadaye, alipofika kidato cha pili akalazimisha kuwa haoni na kuacha shule licha ya kubembelezwa angalau ahitimu kidato cha nne, ikashindikana.
Anasema kwamba walikoma kumlazimisha kwani waliona kuwa wanapoteza fedha na muda kwani “Msomi Amina” alisisitiza kuwa haoni, lakini cha ajabu anasoma ujumbe mfupi wa maneno unaotumwa kwenye simu yake.
JAMHURI imebaini kuwa uteuzi holela wa wanafunzi wanaojiunga na shule za sekondari za kata ni tatizo. Uteuzi huu holela unafanywa na mamlaka za elimu nchini kwa wanafunzi wanaojiunga kwenye shule za sekondari za kata unaendelea kuididimiza elimu ya Tanzania.
Gazeti hili umebaini, ufaulu hafifu unaotokea kila mwaka katika shule za sekondari za kata ni matokeo ya uteuzi  huo holela.
“Mchezo” huo ukiendelea utakwamisha sekta ya elimu. Uteuzi holela unavyofanywa ni: Mamlaka husika kuwateua  wanafunzi kutoka kata moja wanaohitimu elimu ya msingi kwenda kusoma shule za sekondari za kata zilizopo kata nyingine tena zilizo mbali na wanakoishi ilihali kata wanazotoka zina shule za sekondari za kata.
Mwalimu Mary anasema kwamba uteuzi huu ni sawa na kuwachimbia wanafunzi kaburi kielimu kwani “Hali hii inasababisha na kuendeleza ufaulu hafifu kwa wanafunzi wa shule za sekondari za kata.”
Mbali ya umbali na uteuzi holela kuididimiza elimu katika shule za kata lakini pia JAMHURI limebaini hata hali za shule nyingi za kata si za kuridhisha.
Shabani Juma mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Kiloka iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini akizungumza na JAMHURI hivi karibuni amesema, umbali wa kutoka nyumbani hadi shule ilipo, “ni shughuli.”
Anasema, “Mazingira yenyewe ya shule ni mabovu. Shule haina vitabu, haina maktaba, haina viwanja vya michezo na haina madarasa yanayoridhisha.”
“Madarasa mengi yaliyopo hayana hata sakafu. Ni vumbi tupu. unakwenda shule msafi unarudi mchafu. Upepo ukipiga, vumbi lote linaishia mwilini.
“Wakati nikiwa kidato cha kwanza hali hii ilinisumbua sana. Safari tu ya kuelekea shule, ukifika akili yote inakuwa imechoka. Wakati wa mvua ndio shida zaidi…unaingia darasani ukiwa umechoka na kulowa mwili mzima,” anaeleza Shabani.
Ukiachana na tatizo la umbali linalokwamisha ufaulu wa wanafunzi walio wengi lakini pia hata mazingira ya shule hizi za kata ni duni na yasiyo salama.
Kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Serikali imekiri kuwa “Mazingira katika baadhi ya shule na vyuo nchini ni duni na hayana usalama wa kutosha.”
JAMHURI ilifika katika shule ya sekondari Kiloka na kumtafuta Mkuu wa Shule hiyo; Anna Mbaga.
Hata hivyo Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Frank Bankwistu, akasema kwamba bosi wake yuko likizo ya uzazi, lakini shuleni kwake kuna ufaulu haba.
“Kuna baadhi ya madarasa hayana sakafu. Sisi viongozi kazi yetu ni uendeshaji wa shule tu. Suala la uteuzi wa wanafunzi na ujenzi wa majengo ya shule ni jukumu la watu wengine,” anasema.
Akizungumzia changamoto zinazosababisha ufaulu hafifu, Mwalimu Bankwistu anasema, changamoto ni nyingi hasa katika shule yao na kwamba changamoto hizo zinawaathiri zaidi wasichana kuliko wavulana.
Anasema kwamba wanaoacha masomo hapo Kiloka kutokana na changamoto mbalimbali ni wengi. Kwa mwaka 2013 wanafunzi walioacha masomo wanafikia 33. Idadi hii inajumuisha na wale waliopata mimba.
Bankwistu anasema, ufaulu hafifu unaitesa Kiloka kwani mwaka 2013 wanafunzi 44, kati ya 62 walipata sifuri na zaidi ya hapo hawakuwa na wanafunzi waliopata daraja la kwanza wala la pili.
“Ni sita tu walipata daraja la tatu.  Wengine 12 walipata daraja la nne,” anasema na kuongeza: “Umbali ni chanzo kikuu cha ufaulu hafifu. Tumejaribu njia nyingi. Lengo likiwa kumkwamua mwanafunzi asifeli.”
Anasema kwamba kutokana na wanafunzi wengi kutoka mbali ya maeneo wanaoishi na shule, walianzisha kambi shuleni kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha nne.
  “Madhumuni yalikuwa kupandisha ufaulu. Hata hivyo zoezi hili nalo lilikabiliwa na changamoto. Tukaamua tena, kambi hizi ni maalumu kwa wanafunzi wa kike tu,” anasema Mwalimu Bankwistu.
  “Tulilazimika kufanya hivi kutokana na wasichana waliokuwa wakipangiwa vyumba karibu na shule kujiingiza katika tabia hatarishi. Wanafanywa wake za vijana na wanaume waishio mitaani.
 Hali hiyo inasababishwa na wazazi wengi kushindwa kugharamia gharama za wanafunzi. Kuna wazazi waliokuwa wakiwapa watoto wao Sh. 2000 kwa mwezi kama gharama ya kujikimu.
“Sasa hapo ndugu mwandishi unatarajia nini kitafanyika kwa mwanafunzi huyo? Wa kiume maamuzi yaliyotolewa ni kuwa, wanatakiwa waishi makwao,” anaeleza Mwalimu Bankwistu.

>>ITAENDELEA TOLEO LIJALO

Makala hii imepatikana kwa ufadhili wa Taasisi ya Kusaidia ruzuku kwa vyombo vya habari katika mradi wa kuendeleza habari za uchunguzi katika Gazeti la JAMHURI.

By Jamhuri