*Wawili hawa hawagombei ubunge mwaka 2015

*Watano wajitokeza Monduli, Nape aenda Mtama

*Wamo Namelok Sokoine, Kadogoo, Porokwa

 

Ingawa pazia la kugombea urais mwaka 2015 halijafunguliwa rasmi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vigogo wawili wanaodhaniwa kukigawa chama hicho hawatagombea ubunge mwakani, uchuguzi wa JAMHURI, umebaini.

Wakati Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu (mstaafu), taarifa za kina zinasema hagombei tena wadhifa huo, Mbunge wa Mtama, Bernard Membe (wote kutoka CCM) yeye aliishatangaza kuwa hagombei tena ubunge.

Tafsiri sahihi ya wawili hao kutokuwa na nia ya kugombea tena ubunge, inazua mjadala juu ya uwapo wa taarifa kuwa wanataka sasa kugombea urais mwakani zinathibitishwa.

Wanachama kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kujitokeza kuwania ubunge Jimbo la Monduli baada ya kuwapo habari kwamba Mbunge wa sasa, Lowassa, hana mpango wa kuwania tena nafasi hiyo mwakani.

Lowassa, ambaye amekuwa Mbunge wa Monduli kwa zaidi miaka 20; anatajwa kuwa miongoni mwa wana CCM wanaotaka kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kumalizika kwa muhula wa Rais Jakaya Kikwete, Oktoba mwakani.

Kwa maelezo yaliyopo iwapo hatagombea, Lowassa ataungana na Membe, ambaye ameshatangaza wazi kuwa hatagombea ubunge mwakani. Kama ilivyo kwa Lowassa, Membe naye anatajwa kuwa miongoni mwa wana CCM wenye nia ya kuwakiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi wa Rais mwakani.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka Monduli zinasema wanachama watano wa CCM tayari wameshaonyesha nia ya kujaza nafasi hiyo endapo Lowassa atajielekeza kwenye urais.

Aliyewahi kuwa Katibu Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha na Diwani wa Monduli Mjini, Loata Sanare anatajwa kuwa miongoni mwa wana CCM wanaotaka kuziba nafasi hiyo. Sanare ambaye pia amewahi kuwa Diwani wa Lepurko, ingawa hajatangaza hadharani, lakini watu walio karibu naye wanasema amenuia kwa dhati kuwa Mbunge wa Monduli.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Namelok Sokoine, anatajwa kushika nafasi hiyo ambayo iliwahi kushikwa na baba yake mzazi, Waziri Mkuu wa zamani marehemu Edward Moringe Sokoine.

Namelok ambaye amekuwa Mbunge kuanzia mwaka 2010, anatajwa kuwa na mvuto miongoni mwa wagombea, akijivunia rekodi nzuri ya utendaji kazi uliotukuka iliyowekwa na baba yake.

Amezungumza na JAMHURI na kusema ingawa anapenda kuendelea na masuala ya siasa, hajafikia uamuzi wa kuwania ubunge kupitia mfumo gani.

“Bado sijaamua, muda ukifika nitatangaza hadharani, kwa sasa siwezi kusema kwa sababu bado tunasubiri Katiba mpya. Kuna habari ya asilimia 50 kwa 50. Nasubiri kujua mfumo gani utatumika. Kwa sasa hilo nimeliacha kwa sababu tunatekeleza Ilani ya Chama,” anasema.

Alipoulizwa endapo anajiona ana uwezo wa kuwania ubunge kupitia jimbo, anasema: “Uwezo huo ninao. Uwezo wa kuwania kiti cha jimbo ninao, ninachosema kwa sasa nasubiri tu kuona Katiba itaamua vipi ili niamue mfumo sahihi wa kugombea.”

Mwana CCM mwingine anayetajwa kuwa na mvuto wa kisiasa, kiasi cha kushawishika kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge Jimbo la Monduli ni Diwani wa sasa wa Lepurko, Julius Kalanga. Huyu amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Monduli.

Huyu ni kijana mwenye ushawishi, na kwa sasa; pamoja na kujihusisha na siasa, ni mfanyabiashara anayejihusisha na masuala ya ujenzi.

Kalanga amezungumza na JAMHURI na kusema: “Mzee (Lowassa) tunamheshimu, kwa hiyo nadhani Monduli ni kubwa zaidi ya wanaojitokeza, na ina heshima. Kuamua tu kujitokeza kugombea inahitaji uamuzi wa busara kwa sababu jimbo ni zito kwa historia ya wabunge waliokuwapo.

“Kuvaa viatu vya mtu kama huyo si rahisi. Sijaamua, itategemea maoni yake kama mbunge wa sasa, ni mtu tunamheshimu sana, ni mapema sana kuamua kama nitagombea.

“Monduli ni kubwa kuliko nafsi zetu kwa sababu jimbo limekuwa kwenye umoja na mshikamano na maelewano makubwa sana. Hoja kubwa si nani anataka kugombea, bali hoja ni kukubaliana hasa kwa kumshirikisha mbunge wetu.

“Nasita, kwanza jimbo lina heshima na tunamheshimu Mheshimiwa Lowassa na anaipenda Monduli, inategeana na ushauri wake atueleze nini cha kufanya.

“Ni demokrasia lakini nashindwa kusema kwa sababu ya historia ya jimbo. Tutaona nani anafaa kuanzia pale alipoishia yeye, karibu maeneo yote amefanya maendeleo makubwa sana. Si jambo rahisi kuvaa viatu vya Lowassa. Ukija kienyejienyeji utapwaya…viatu vya Lowassa si mchezo.”

Mwana CCM wa nne anayetajwa ni Daniel Porokwa. Kwa sasa Porokwa ni Katibu CCM Babati Mjini. Mwanasiasa huyu kijana ni mmoja wa vijana ‘waliorejea kundini’ kwani kuna wakati aliasi ‘kambi’ ya Lowassa, lakini haukupita muda, akatambua makosa yake na kutubu.

Porokwa aliwahi kumshambulia hadharani Lowassa, lakini alipoibaini kuwa alichokifanya hakikuwa sahihi, alirejea kwa Lowassa na kwa wazee wa mila akawaomba radhi; na akasamehewa.

Tangu wakati huo amekuwa bega kwa bega katika siasa za kuijenga CCM pamoja na maendeleo ya Mkoa wa Arusha. Nafasi yake kwenye ubunge inatajwa kuwa ni kubwa kutokana na ushawishi wake, na pia ni miongoni mwa watu wanaoungwa mkono na makundi ya vijana na wazee.

Katibu Uenezi Mkoa wa Arusha, Isack Joseph Kadogoo, yeye anasema hajatangaza nia, lakini anathibitisha kuwa wakati ukifika, hatasita kufanya hivyo. Pamoja na Uenezi, Kadogoo ni Diwani wa Monduli Mjini.

“Ni mapema mno. Uwezo ninao, uwezo ninao kabisa. Kwa sasa Mbunge wetu ni Mheshimiwa Lowassa. Hatuwezi kubishana na mzee wetu. Ameifanyia Monduli mambo makubwa sana. Amekuwa mbunge tangu Monduli ikiwa pamoja na Longido. Maendeleo yanayonekana kwa kila mtu.“Siwezi kutangaza sasa kuwania ubunge kwa sababu sijamsikia akisema hatagombea. Lakini wakati ufika, na kama hatagombea, sioni kwanini nisitangaze nia kwa sababu uwezo ninao. Kwa sasa naomba tusubiri,” amesema.

 

Wasifu wa Lowassa

Alizaliwa Agosti 26, 1953. Alikuwa Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1990. Alichukua nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Lepilall Naityamieng’ishu ole Molloimet.

Lowassa alisoma shahada ya kwanza katika mada ya tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, halafu shahada ya pili katika sayansi kwenye Chuo Kikuu cha Bath (Uingereza).

Amekuwa Waziri Mkuu (2005 – 2008), Waziri wa Maji na Mifugo (2000 – 2005), Waziri wa Ardhi na Makazi (1993 – 1995), Waziri wa Nchi wa Haki na Mambo ya Bunge katika Ofisi ya Makamu wa Rais (1990-1993), Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (1989 – 1990), Waziri mdogo wa Mazingira na Mapambano dhidi ya Umasini katika Ofisi ya Makamu wa Rais (1988-1990).

 

Membe naye asema ubunge basi

Wakati Lowassa akiwa hajatoa kauli rasmi ya, ama kuwania, au kutowania ubunge Membe, yeye tangu mwaka 2012 alishatangaza kwamba hatagombea ubunge mwaka 2015.

Taarifa zilizopatikana na zisizotiliwa shaka ni kuwa Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye anawania Jimbo la Mtama. Nape yeye hajathibitisha wala kukanusha alipotafutwa.

Membe alilithibitishia JAMHURI katika mahojiano maalumu, akisema kutogombea kwake ubunge ni utekelezaji wa ahadi yake ya muda mrefu, kwani alisema baada ya vipindi vitatu, hataendelea. Hata hivyo, uamuzi huo unaweza kutafsiriwa na wengi kuwa ni maandalizi yake ya kuwania nafasi ya juu zaidi, yaani urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini mwenyewe anasema amelitumikia Taifa kwa muda mrefu katika nafasi mbalimbali, hivyo kutogombea kwake ubunge kumelenga kumpa nafasi ya kukaa na familia, na ikiwezekana kuanza kuandika masuala aliyofanya kitaifa na kimataifa.

Alipoulizwa kama lengo lake ni kujiandaa kuwania urais, alisema: “Kwa sasa (mwaka 2012) ni mapema, ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba nilishatoa ahadi ya kuwatumikia wananchi wa Mtama kwa vipindi vitatu, sasa vimetimia, na lazima niheshimu ahadi yangu.”Akasema nguvu zake amezielekeza katika kumsaidia Rais Jakaya Kikwete, ili aweze kumaliza vema ngwe yake ya uongozi. “Sipo tayari kulizungumza jambo hilo (kuwania urais) kwa sasa…kwa kweli nipo bize sana kumsaidia Mheshimiwa Rais Kikwete amalize ngwe yake ya uongozi.

“Hiyo ndiyo ‘priority’ (kipaumbele) yangu ya kwanza, hiyo ndiyo ‘priority’ yangu ya pili na kwa kweli hiyo ndiyo ‘priority’ yangu ya tatu…kumsaidia amalize ngwe yake salama,” akasema Membe

 

Historia ya Membe

Bernard Kamillius Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha Rondo-Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini, akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya watoto saba wa mzee Kamillius Anton Ntanchile na mama Cecilia John Membe.

Membe alifunga na Dorcas Richard Masanche mwaka 1986. Wana watoto watatu – wawili wa kiume na mmoja wa kike.

Elimu ya msingi alisoma katika Shule ya Msingi Rondo-Chiponda (1962-1968). Shule ya sekondari alisomea katika Seminari ya Namupa (1969-1972), na baadaye akajiunga na Itaga Seminari Tabora kwa kidato cha tano na sita (1973-1974).

Membe ana shahada ya uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani mwaka 1992. Amefanya kazi katika Ofisi ya Rais na balozi mbalimbali. Kabla ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Membe amewahi kuwa Naibu Waziri katika Wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi; na Wizara na Nishati na Madini.

 

2599 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!