nmb-4Jumapili iliyopita Oktoba 25, mwaka huu ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa Watanzania waliojitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu hapa nchini kwa kuwachagua viongozi wanaowataka katika nafasi ya rais, ubunge na udiwani.

Uchaguzi huu umetawaliwa na matukio mengi ambayo yanatoa majibu kwa kukua kwa demokrasia na ushindani mkubwa wa hoja kwa wanasiasa tofauti na chaguzi zilizopita tangu nchi yetu ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Katika makala  zilizopita, niliandika kwamba “NEC, Polisi na hawaaminiki” na hiyo inatokana na taasisi hizo kuonesha kutafuta namna ya kukinufaisha chama kimoja cha siasa.

NEC hii haiwezi kuaminika kwa sababu si tume huru. Ndio maana imekuwa ikiingiliwa mara kwa mara na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye amehusika kutoa maagizo mbalimbali kwa kuhodhi madaraka ya tume ya mwenyekiti wa tume.

Tume hiyo pamoja na madudu mengine yaliyojitokeza ikiwemo vituo vingi kuchelewa kufunguliwa na vingine kukosa vifaa vya kupigia kura karatasi za kura za Rais na wabunge.

Pia kasoro nyingine ni kukosekana kwa daftari la wapigakura kwa madai kwamba limesahaulika katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo. Kasoro hiyo ilijitokeza katika kituo cha uchaguzi cha Msingwa shule ya msingi Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima alipohojiwa kuhusu kuibuka kwa kasoro hizo zilizosababisha wananchi kushindwa kuitumia haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wawatakao amesema zimesababishwa na baadhi ya wasimamizi waliokuwa wakilalamikia posho zao.

Katika Manispaa ya Kinondoni amesema wasimamizi hao walifanya fujo kwa kuchana karatasi za kura, kuharibu masanduku ya kura kwa kuyakanyaga na kutupa vifaa vingine walipokuwa wanakabidhiwa vifaa vya kupigia kura katika ofisi ya Msimamizi wa Jimbo.

Amesema vurugu hizo zilianza saa 9 usiku. Kwa ujumla kumeibuka kasoro nyingi katika majimbo mbalimbali nchini na lawama zaidi zimeelekezwa tume ya uchaguzi ambayo si huru na kutoa upendeleo kwa chama tawala.

Nilieleza kwa kutoa mfano wa timu za soka za watani wa jadi Yanga na Simba zinapoingia katika mchuano huku timu moja ikimweka mwamuzi na washika vibendera wake ni lazima timu hiyo ishinde hata kwa “bao la Nape”.

Huu ni ubabe, hakuna ushindani wa kweli na haki hapa. Kama nchi zinakosa kuruhusu demokrasia ya kweli isiyokuwa na mashaka kwa kung’ang’ania tume kama hii tuliyonayo ndio chanzo cha vurugu na machafuko.

Nawashukuru wasomaji wengi wa safu hii ambao wamekuwa wakiniunga mkono na baadhi yao wachache walioporomosha matusi wakidai kwamba nimehongwa na mgombea urais wa Chadema.

Wakati wote huwezi kuhubiri amani bila haki, na hivi ni pacha hivyo wakati matokeo ya kura yakitangazwa wananchi hatuhitaji kuona vurugu na machafuko vinavyohamasishwa na baadhi ya viongozi wanaofikiri kikundi cha watu wachache ndio chenye dhamana ya kuwaongoza iwe kwa njia halali au haramu.

Kama NEC na ZEC zitaleta ubabaishaji wa kutangaza matokeo kwa haki na kweli, viongozi wake watakuwa wamefuata nyayo za aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK), Joseph Kivuitu aliyefariki kwa saratani ya koo jijini Nairobi.

Marehemu Kivuitu alivuma sana mwaka 2007 baada ya matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Kenya yaliyotangazwa na ECK wakati huo yeye akiwa ni mwenyekiti, matokeo hayo yalipelekea hisia tofauti na kusababisha machafuko makubwa kuwahi kushuhudiwa Kenya huku watu 1,133 wakipoteza maisha na zaidi ya 600,000 kuachwa bila makazi.

Chonde chonde NEC msiwe chanzo cha kuvuruga amani ya nchi yetu. Nasema haki, ukweli na uwazi vikikosekana amani itapotea na kuirejesha upya ni kazi kubwa sana.

Mungu ibariki Tanzania. Wabariki watanzania wote, haki na amani vitamalaki nchini kote.

1104 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!