Aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, anaishi kwa wasiwasi. Hana uhakika uchunguzi unaoendeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) utaishia wapi.

Wiki mbili tu zilizopita Lugola alikuwa miongoni mwa watu wachache nchini ambao angeweza kusema lolote bila ya kujali athari zake. Wakati huo Lugola alikuwa anaweza kufanya lolote, kwa mtu yeyote bila kujali athari zake. 

Lugola alikuwa miongoni mwa watu wachache nchini ambao hawakujali sana wengine watafikiria nini kutokana na kile atakachokisema au kukifanya.

Lakini leo hii Lugola anaishi kwa wasiwasi, akisubiri kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma ambazo zinaweza kusababisha akae rumande kwa muda mrefu sana. Haitashangaza iwapo kati ya mashitaka atakayoshitakiwa litakuwemo la utakatishaji fedha, shitaka ambalo kwa mujibu wa sheria za nchi halina dhamana.

Lugola anapotazama uwezekano wa kuwekwa ndani kwa muda mrefu, wapo watu wengine wanaanza kumfikiria kuhusiana na zile mbwembwe zake wakati akiwa waziri, tangu kuvaa mavazi yenye rangi za Bendera ya Taifa, kukatika mauno hadharani, sifa alizokuwa anammwagia rais hadharani hadi kauli za kutishia na kashfa alizokuwa anazitoa kwa wale walio chini yake na wapinzani.

Lakini hizo ni mbwembwe tu, jambo kubwa ni hoja kuwa Lugola na wenzake wametenda jambo ambalo ni kinyume sana cha sheria kiasi cha kumkasirisha rais hadi kufikia uamuzi wa si tu kuwaondoa katika nyadhifa zao, bali kutangaza hadharani. 

Naamini yapo madudu mengi yanayofanywa na wasaidizi wake, lakini rais anayavumilia, wala hayatangazi hadharani.

Hapa mtu unaweza kujiuliza, Lugola alikuwa na ujasiri wa namna gani hadi kufikia hatua ya kufanya jambo hilo wakati yeye akiwa ni mmoja wa watu ambao wanamfahamu kiundani Rais Magufuli (kumbuka Lugola aliwahi kuwa mwanafunzi wa Rais Magufuli). 

Ukiachilia mbali kumfahamu tangu akiwa mwanafunzi, lakini kama mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri, Lugola alipaswa kuwa mmoja wa watu ambao wanamfahamu bosi wao kwa undani. Ilikuwaje afanye hivyo?

Jibu la swali hili kwa kiasi fulani linapatikana katika kauli ambayo Rais Magufuli ameitoa kuhusiana na sakata zima lililomhusisha Lugola na viongozi wengine wizarani na kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Inaonyesha kuwa ni taarifa za kiintelijensia ambazo zilikuwa zinapatikana jinsi mchakato wa kusaidia mkataba uliomtia matatani Lugola na wenzake ulivyokuwa unaendelea. Kama ni hivyo, upo uwezekano kuwa wakati wa mchakato wa mkataba, kuna watu walikuwa wanafahamu kuwa mchakato huo unatazamwa kwa kina na taasisi nyingine. Kwa nini watu hao hawakumjulisha Lugola kuwa anachokifanya kinafuatiliwa na watu kutoka taasisi nyingine?

Je, inawezekana kuwa Lugola aliachwa afanye alivyofanya kama mtego ili baadaye mtego huo umnase na aondolewe kirahisi madarakani kukiwa na sababu za kuhalalisha kuondolewa kwake?

Lakini kwa nini Lugola ambaye anaifahamu Serikali ya Awamu ya Tano kwa karibu na anamfahamu Rais Magufuli na hulka zake kwa karibu, ajiingize kwenye jambo ambalo alipaswa kufahamu kuwa lisingemfurahisha rais?

Iwe alitegewa au vipi, lakini Lugola anapaswa kujilaumu mwenyewe, kwa sababu kama waziri wa moja ya wizara nyeti nchini alipaswa kuwa na weledi wa kubaini mitego inayowekwa kwenye njia anamopita.

Lugola alijua kuwa anaongoza wizara ambayo taasisi za kiuchunguzi zimo ndani yake. Labda uwaziri ulimtia upofu kiasi kwamba akajiona ana kinga ya yeye kutoguswa na taasisi hizo za kiuchunguzi. 

Lakini Lugola anafahamu kuwa taasisi za kiuchunguzi hazimo tu kwenye wizara yake. Hivi alidhani pia hizo taasisi nyingine za kiuchunguzi zisingeweza kumgusa pia?

Labda kujuana kwake kwa karibu na Rais Magufuli kulimfanya ajiamini kiasi cha kudhani kuwa kiongozi huyo mkuu wa nchi asingeweza kumwondoa katika wadhifa wake kwa sababu tu wanafahamiana kwa karibu.

Vyovyote iwavyo, Lugola asimlaumu mtu yeyote kwa haya yaliyomkuta.

Labda ana utetezi utakaomwezesha kumweka nje ya tuhuma zilizosababisha rais amfute kazi. Lakini hilo litakuwa jambo la ajabu sana, kwa sababu haiyumkini kwa rais kutamka hadharani kuwa (Lugola) amefanya makosa wakati Lugola hajafanya hivyo. Haiwezekani kuwa rais alifikia hatua ya kumfukuza kazi Lugola bila ya kuwa na uhakika wa tuhuma alizozisema hadharani.

870 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!