Waona giza nene mbele yao, Uganda yaonya vita inanukia
DRC yazidisha mashaka kwa Uganda, Watanzania waonya

Hatua ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kukataa kusaini mkataba wa amani na kundi la waasi la M23, imepeleka kilio kwa kundi hilo, na sasa wanalia njaa uhamishoni nchini Uganda.

Uganda, nchi ambayo ni msuluhishi wa mgogoro huo, imejikuta katika wakati mgumu kwani kundi la waasi wa M23 wapatao 1,700 limekimbilia nchini humo, ilhali Uganda ikiwa na jukumu la kusuluhisha waasi hao na Serikali ya DRC.

 

Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende, mwishoni mwa wiki ametamka kuwa Serikali yake ina wasiwasi kuwa Uganda ina maslahi binafsi na waasi wa M23, hivyo hawako tayari kutia saini mkataba unaosimamiwa kwa mitego.

 

“Uganda sasa inaonekana kuwa sehemu ya mgogoro. Ina maslahi na M23,” alisema Mende.

Kauli hii ya Mende imekuja siku chache baada ya DRC kukataa kutiliana saini na waasi kwa maelezo kuwa M23 ni kundi lililotangaza kujivunja, wamekimbilia Rwanda na Uganda, na hivyo kulipa sharti kubwa wanalolikataa.


Sharti hilo ni kuwa mkataba uwe na kipengele kinachowazuia M23 milele kutoshika silaha na kuanzisha mapambano, hoja inayokataliwa na waasi, huku Uganda ikizishawishi pande mbili zitie saini mkataba hivyo hivyo ulivyo kwa maelezo kuwa yakitokea matatizo mbele ya safari utarekebishwa tena.


Masharti mengine wanayowapa waasi hao ni kuwa makamanda wapatao 100 waliokuwa wanaongoza kundi la M23, wasiruhusiwe kuingia jeshini moja kwa moja, na badala yake wapewe mafunzo ya kijeshi, huku wakiacha fursa ya kushitaki wahalifu wa kivita watakaothibitika mbele ya safari kuwa walitenda uhalifu dhidi ya binadamu.


Uganda, ambayo sasa hivi ina mzigo mkubwa wa kulisha waasi hao waliowekwa kambini nchini humo tangu Jumatatu (Novemba 4) kundi hilo lilipotangaza kushindwa vita na kuweka silaha chini, inasema hali inayoiona ikiwa waasi hao hawatahakikishiwa usalama wao, pato la fedha na kushirikishwa serikalini, kuna wasiwasi kuwa wanaweza kurejea msituni.


“Hawa ni binadamu. Njaa ikiwashika, usitarajie watasubiri kufa kwa njaa. Wanaweza kurejea msituni,” alisema afisa mmoja wa Serikali ya Uganda.


Uganda pia imetishia kwa mara nyingine mwishoni mwa wiki kuwa ikiwa suluhu haitapatikana haraka, na DRC ikaendelea kuituhumu kuwa inashirikiana na waasi wa M23, basi yenyewe itajitoa katika nafasi ya kuwa msuluhishi.


Kuhusiana na tishio la Uganda kujitoa kwenye mazungumzo, Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Uganda, Asumani Kiyingi, amesema: “Tumewasiliana na Umoja wa Mataifa kupitia kwa Balozi wetu jijini New York, kwani tunataka kufahamu iwapo kilichoandikwa kwenye vyombo vya habari ni cha kweli,” amesema.


“Ikiwa Umoja wa Mataifa utathibitisha kuwa wataalamu wake wameandika taarifa hizo za uongo [kuwa Uganda inaunga mkono M23], basi tutajitoa katika jukumu la usuluhishi wa mgogoro wa DRC na waasi wa M23.”


M23 kwa upande wao walioanza vita Aprili 2012 wanamtuhumu Rais Joseph Kabila kuwa wao ndiyo waliomsaidia baba yake, Laurent Kabila, kuingia madarakani na hata makundi ya waasi yalipokuwa yanatishia kumuondoa madarakani walimtetea, lakini alipoingia madarakani akawatekeleza.


Wataalamu wanasema kuwa nchi za Uganda na Rwanda pamoja na kukaripiwa na jumuiya ya kimataifa, zikaacha kukiunga mkono kikundi cha M23, hali iliyokifanya kichapwe kama mtoto mdogo, sasa zimehamishia nguvu kwa makundi mengine ya waasi yaliyopo kwenye misitu ya Congo.


Shutuma kubwa zinazosukumwa kwa nchi hizi ni kuwa zimekuwa zikinunua madini na mbao kutoka kwa waasi, hali inayoziingizia fedha nyingi za kigeni bila kujali kuwa zinahatarisha maisha ya Wakongo wasio na hatima, taarifa ambazo Serikali ya Uganda imeziita za ‘kipuuzi’.


Kikosi Maalum cha Umoja wa Mataifa kinachoongozwa na Mtanzania, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa, kwa kuhusisha Brigedi Maalum ya SADC, kimewachakaza M23 hadi wakasalimu amri, lakini wachambuzi wa mambo wanasema kung’olewa kwa M23 si mwisho wa matatizo DRC.


Richard Mugamba, Mhariri Mtendaji wa gazeti la the Citizen, ambaye amekuwa akiripoti habari za waasi kwa kufika Goma, anasema M23 ni moja ya makundi zaidi ya 17 yaliyoko mashariki mwa Congo.


“Kila mtu anatambua kwamba M23 kuweka silaha chini ni furaha kwa Wakongo, ila matatizo yao yana miaka 17. Tangu 1999 wamekufa watu milioni 5. M23 wamekuwapo kwa miezi 24, lakini mashariki mwa Congo kuna makundi kama FDRL, Mai Mai, RCD-Goma, ADF, kuna vikundi 17 na vyote hivi viko mashariki kwenye madini, kwenye mbao na mkaa.


“Ni vyema kwamba M23 imeshindwa, lakini haiwezi kuwa suluhisho tangu 1996 walipommaliza Mabutu [Sese Seko Kukubanga wa Zabanga], wamekuwa wakipigana. Kiongozi wa waasi Laurent Nkunda yuko Uganda (CNDD). Kuna nchi ambazo zinatuhumiwa – Rwanda na Uganda zinatuhumiwa,” amesema Mugamba. Hata kiongozi wa sasa wa M23, Kanali Sultani Makenga, amekimbilia Uganda.


“Sisi kama Tanzania tume-play role (tumetimiza wajibu) yetu. Kuna watu wanataka haya makundi yawepo kwa sababu wanafanya biashara. Makenga alikuwa ana-access dola 58 milioni mwaka jana, tuseme anapata dola milioni 10, lazima wote wanafanya biashara.


“Watu wote wanaohusika na Congo hebu wakae chini wazungumze. Mali zinauzwa nje. Nikiwa Congo niliona vitu ambavyo nasema sawa kuna tatizo, lakini mbona kuna mikono mingi tu. Kama hakuna amani Congo au kwa jirani yako, wewe huwezi kuwa na amani. Angalia hali ya usalama kwa mikoa ya Kigoma na Kagera.


“Jeshi la UN lipo Congo kwa miaka 11, watu milioni 5 wameuawa. SADC Intervention Brigade UN waliipinga awali, lakini angalia kazi iliyofanya kwa miezi sita. Dunia kama ingekuwa na nia ya dhati hawa waasi wote wangekuwa hawapo,” anasema Mugamba.


Mobhare Matinyi, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, anasema M23 kama kikundi kimekwisha kwa sababu makamanda wake wamejisalimisha, na kuna taarifa kuwa Waziri wa Mashauri ya Nje wa Marekani, John Kerry, na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, walimpigia simu Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kumwambia asiingilie aache hiki kipigo kiishe.


“M23 imepigika, haina uwezo wa kuibuka tena, lakini bado kuna hatari. Kwa kuwa Uganda viongozi wake wana maslahi binafsi nchini Congo na Rwanda ina maslahi ya kitaifa Congo, kuna uwezekano wakaanzisha insurgence groups (makundi ya waasi) kuleta shida kwa Congo waendelee kuvuna,” Matinyi ameiambia JAMHURI.


Anasema bado kuna makundi yanayopigana yenyewe kwa wenyewe, baadhi ya makundi hayo ni kama FDLR, Democratic Forces for Liberation of Rwanda, mabaki ya Interahamwe na Banyamulenge ambao bado ni tishio.


“Majeshi yetu Tanzania kihistoria ni nchi yenye msingi wa utu, usawa na haki. Ndiyo maana Tanzania imekuwa ikitoa majeshi yake kumtetea Mwafrika na kumtetea binadamu. Tulipoitikia kwenda Congo ilikuwa ni kumtetea Mwafrika, hatuwezi kukaa miaka 20, 30 watu wakiuawa sisi tunaangalia tu,” anasema.


Swali ni je, njaa ikiendelea kuwasumbua waasi wa M23 hawatarudi msituni? Wachambuzi wanasema mkataba wa amani unapaswa kuharakishwa.


 

By Jamhuri