Kama kuna mwanamuziki ambaye hawezi kusahaulika katika kumbukumbu za wapenda muziki ni Dk. Remmy Ongalla. Desemba 13, 2018 alitimiza miaka minane tangu afariki dunia.

Alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu ya Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa ni siku ya majonzi kwa wapenzi wa muziki wa dansi Tanzania, Afrika Mashariki na ulimwenguni kwa ujumla baada ya kusikia taarifa za kifo chake.

Majina yake kamili ni Ramadhan Mtoro Ongalla, aliyekuwa kipenzi cha watu. Remmy aliwaacha wapenzi wake na wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kufuatia tungo za nyimbo zake zenye maudhui maridhawa, ambazo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini hata nje ya mipaka.

Yapo mambo kadhaa aliyoyafanya ambayo yanasababisha watu wengi kutomsahau nguli huyu.

Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo ‘Mambo kwa Soksi’. Lakini jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye viongozi wa serikali, vyama na dini na wengine kwa ujumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy, wakaanza kuhubiri majukwaani  tahadhari hiyo.

Ramadhan Mtoro Ongalla alizaliwa akiwa na meno mawili ya mbele kinywani mwake na akaonekana kana kwamba ni  mtoto wa ajabu. Aidha, hakuwahi kunyolewa nywele zake kwa miaka yote hadi alipokuja kuokoka akiwa hapa nchini Tanzania.

Alijipatia umaarufu katika Jiji la Dar es Salaam, hususan maeneo ya Sinza, kufuatia gari lake dogo ‘saloon’ ambalo  popote lipitapo watu walilishangaa. Lilikuwa na maandishi nyuma ya gari hilo yakisema ‘Mkweche, mkweche, baba yako analo’?

Historia ya maisha ya Dk. Remmy Ongala yaelezwa kwamba mara alipozaliwa, wazazi  wake walimuita Ramadhani. Alizaliwa mwaka 1947 katika Mkoa wa Kivu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu, eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani mwa Tanzania.

Baba yake alikuwa ni mwanamuziki, baada ya kuzaliwa haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji wa Kisangani huko DRC.

Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake, mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, mtoto alifariki dunia. Alipopata ujauzito mara ya tatu alikwenda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asifariki dunia.

Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia safari hii asiende kujifungulia hospitalini, bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake.

Yote hayo yalitendeka na ndicho kisa cha Dk. Remmy Ongala kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyomsababisha kuokoka ndipo aliponyoa nywele zake akiwa hapa nchini Tanzania.

Mwenyewe aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na nywele ndefu namna ile. Lakini baadaye jina na taswira ya mfalme wa ‘reggae’ ulimwenguni, hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Kongo, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari.

Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele, kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama ‘Doctor Remmy Ongalla.’

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangu akiwa mdogo kabisa. Jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, walimu, wakulima n.k, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.

Kwa bahati mbaya baba yake huyo mwaka 1953 alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita, akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia ada ya shule, Remmy aliacha masomo.

Ilipofika miaka ya 1960, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa.

Mwaka mmoja baada ya kifo cha baba yake mzazi, mwaka uliofuatia – 1964 ulikuwa si mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi naye alifariki dunia, jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake, kwani yeye sasa ndiye alikuwa mkuu wa familia, licha ya umri wake kuwa mdogo.

By Jamhuri