Mwanamuziki nguli wa muziki wa Jazz kutoka Zimbabwe, Oliver Mtukudzi ‘Tuku’(pichani juu), amefariki dunia wiki iliyopita katika Hospitali ya Avenues jijini Harare akiwa na umri wa miaka 66. Tuku alilazwa hospitalini hapo baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kabla hajalazwa mwanamuziki huyo alikuwa katika ziara nchi mbalimbali duniani. Alilazimika kukatisha ziara yake kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.

Tuku amefariki dunia ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kifo cha gwiji mwingine wa muziki wa Jazz, Hugh Masekela, aliyefariki dunia tarehe sawa na ya rafikiye, Oliver Mtukudzi.

Tuku atakumbukwa kwa vibao vyake vingi vilivyotikisa ulimwengu wa muziki, hasa nyimbo za ‘Neria’ na ‘Todii’.

Tuku aliibeba Tuku Music kama beji ya heshima na kuipa hadhi sanaa ya Afrika, alirejea kwa Mungu Januari 23, tarehe sawa na ile ambayo rafiki yake mkongwe wa muziki, Hugh Masekela, alifariki dunia nchini Afrika Kusini, mwaka jana.

Mutukudzi maarufu kama ‘Tuku’ alikuwa ni msanii na mwandishi mashuhuri wa ngoma mbalimbali huku akiwa ni mmoja wa wasanii wenye albamu nyingi zaidi, amerekodi jumla ya albamu 60.

Mapema mwaka jana alilazwa katika hospitali moja mjini Harare kwa shinikizo la damu. Hata hivyo aliruhusiwa na hali yake ikaimarika.

Msanii huyo alikwishawahi kufanya muziki na msanii wa Bongo Fleva, Lady Jaydee, wimbo unaoitwa ‘I am who I am’ au kwa lugha yetu ya Kiswahili ‘Mimi ni Mimi’, wakiimba kwa lugha za Kishona na Kiswahili. Tuku alitembelea Tanzania mwaka 2011.Lady Jaydee anasema Oliver Mtukudzi alikuwa msanii rahisi kufanya naye kazi kutokana na tabia yake ya kumpokea mtu jinsi alivyo.

Anasema mara baada ya kukutana na Oliver Mtukudzi alimshauri vitu vingi kuhusu muziki, kitu ambacho kimempa faida.
“Baada ya hapo mambo yalibadilika kutokana na ushauri alionipa, namna ya kufanya muziki wa ‘live’ na kuhusisha vionjo vya Kiafrika kwenye muziki wangu.

“Alikuwa ni mtu wa kawaida ambaye si mgumu kufanya naye kazi, kila binadamu ana mambo yake, lakini ni mtu rahisi sana kufanya naye kazi, anampokea kila mtu anavyokuja,” ameeleza Lady Jaydee.

Kwa upande wake msanii mkongwe wa muziki nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, ameeleza kuguswa na kifo cha Oliver Mtukudzi kwa kuwa alikuwa akiupenda sana muziki wake.

“Nimeshtushwa na kifo chake; pili, imeniuma sana kwa sababu nilikuwa nampenda na napenda kazi zake,” amesema Kiki.

King Kiki anasema Afrika imempoteza mwanamuziki nguli aliyekuwa mcheshi, akiimba kwa hisia huku akilicharaza gitaa lake.

Wasifu wa Mtukudzi

Alizaliwa Septemba 22, 1952 mjini Highfield, Harare, alikuwa ni mwanamuziki maarufu kwa muda mrefu nchini Zimbabwe. Alianza kutambulika zaidi baada ya kuingia katika Kundi la Wagon Wheels mwaka 1977 akiwa na mwenzake Thomas Mapfumo.

Wimbo wake wa kwanza ulikuwa wa ‘Dzandimomotera’ ulioheshimika sana, na hapo ndipo Tuku alipotoka na albamu yake ya kwanza iliyomletea mafanikio makubwa.

Licha ya muziki Tuku alikuwa akifurahia kuogelea katika bwawa lake (swimming pool) ambalo lina umbo la gitaa.

Mwaka 2003 alitunukiwa tuzo ya heshima kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe, kwa kutambua
mchango wake katika kujenga muziki na msukumo kwa wasanii wa kizazi kipya nchini humo.

Mwaka 2009, Chuo Kikuu cha Wanawake cha Afrika kilimpatia tuzo ya shahada ya sanaa na kumwelezea mwanamuziki huyo kama mbunifu wa hali ya juu kuwahi kutokea nchini Zimbabwe katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

Mara nyingi Tuku alikuwa akiimba nyimbo katika lugha tatu tofauti za Kishona, Kindebele na Kiingereza.

Huchanganya ala za muziki wa kiasili kwenye nyimbo zake, jambo lililompa umaarufu mkubwa dunia nzima.

Tofauti na wenzake katika Kundi la Wagon Wheels waliokuwa wakimwimba vibaya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, Mtukudzi alikuwa akimsifia sana na kusababisha anufaike kwa misaada mbalimbali kutoka serikalini.

Mwaka 2010, mwanae kipenzi, Sam Mtukudzi, ambaye naye alikuwa mwanamuziki, alifariki dunia kutokana na ajali mbaya ya gari.

Baadhi ya albamu za mwanamuziki huyo ni ‘Ndipeiwo Zano’ ya mwaka 1978, ikarudiwa tena mwaka 2000, ‘Chokwadi Chichabuda’ na ‘Muroi Ndiani?’ za mwaka 1979, ‘Shanje’ na ‘Pfimbi’ za mwaka 1981, ‘Nhava’ ya mwaka 2005, ‘Wonai’ ya mwaka 2006, ‘Tsimba Itsoka’ na nyingine nyingi.

Safari yake ya muziki ilianzia mwaka 1977, alipojiunga na bendi ya Wheels. Sauti yake yenye mvuto wa kukwaruza, imekuwa ndio utambulisho mkubwa ndani na nje ya nchi ya Zimbabwe.

Mwaka 2010 alituzwa tuzo kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe, ya ‘The International Council of Africa’ na ‘Womensim Award’. Hiyo ilitokana na mchango wake mkubwa wa kuwainua wanawake kupitia sanaa ya muziki.

Mtukudzi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66, alikuwa baba wa watoto watano na wajukuu wawili.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi. Amina.

Please follow and like us:
Pin Share