Mchora katuni maarufu, Ally Masoud (Masoud Kipanya), amesema hataogopa kumchora rais wa nchi kwa kuwa havunji sheria na kwamba uchoraji wa katuni umedumu kwa muda mrefu duniani kote.

Kipanya licha ya kuwa ni mchoraji wa katuni, pia ni mtangazaji wa kituo cha redio na televisheni, amewahi kuwa mhariri msanifu wa magazeti ya katuni. Pia alikuwa mhariri na mchoraji wa Gazeti la katuni la Sanifu miaka ya 1990; lakini kwa sasa ni mtangazaji na jina la Masoud Kipanya (KP) amelijenga mwenyewe.

Fuatilia mahojiano yaliyorushwa hivi karibuni kupitia kituo cha televisheni cha Azam katika kipindi maarufu cha ‘Nyundo ya Baruani’ kinachorushwa na televisheni hiyo ya jijini Dar es Salaam.

Fuatilia maswali na majibu baina ya mwendesha kipindi Baruani Muhuza na Masoud Kipanya.

 

Muhuza: Nimefurahi sana kuwa nawe kwenye kipindi hiki wengi wakikufahamu kuwa ni mchora katuni na wachache wanakufahamu kama ‘Masoud Kipanya’ – mtangazaji wa redio na Tv kwa wakati fulani, na baadhi wakikufahamu kama mwenye mradi wa ‘Maisha Plus’, iliyokufanya ufahamike zaidi. Masoud Kipanya ni nani ukimsema wewe mwenyewe?

 

Masoud: Ni swali pana sana ukimsema Masoud Kipanya ni nani, kwa maana ya tabia, umesema Masoud Kipanya ni mchoraji, mtangazaji wa redio na Tv, mtayarishaji lakini namba moja ni mchoraji, kwa sababu ndicho kipaji, kwenye utangazaji kila mtu anaweza kutangaza akiwa na sura nzuri, sauti nzuri na maarifa kidogo lakini kwangu mchoraji anaweza kuwa namba moja.

Masoud Kipanya, baba, kaka, rafiki na mtu mmoja ambaye ana aibu sana. Nina aibu sana, ingawa watu wengi hawawezi kufikiria hilo. Binadamu ni haya, napenda sana kuwa peke yangu.

 

Muhuza: Kwa kuwa unajionea aibu hata wewe mwenyewe, ama ni nini?

 

Masoud: Labda inawezekana si mjuzi sana kwenye watu wengi. Napenda sana kuwa peke yangu, nina sababu zangu, kwa sababu inanipunguzia vitu vingi sana, kwa hiyo napenda sana kuwa peke yangu.

 

Muhuza: Wakati nakukaribisha hapa studio, nikakukaribisha kwenye chumba cha wageni, nikakuomba radhi kuwa nisubiri kidogo nakuja, ukaniambia afadhali nitachora katuni. Ni wakati gani unakaa na kufikiria kuchora katuni, ni hizo nafasi za namna hiyo au ni wakati maalumu katika siku nzima?

 

Masoud: Haina wakati maalumu ingawa kuna deadline kwenye kutuma katuni kwa mhariri kwa ajili ya kesho yake, lazima isizidi saa kumi jioni kwa sababu nao wana deadline kati ya saa tisa na kumi kwa ajili ya kukusanya ‘stories’ kwenda kuchapa gazeti, hivyo wakati wowote kwenye muda huu nami inatakiwa niwe nafikiria.

Naweza kuwa studioni kwenye kipindi redioni wakati wa mapumziko ya muziki au matangazo, mimi naweza kuwa nachora. Kwenye kuchora jambo kubwa  ni wazo, si kukamata kalamu na kuanza kuchora. Unafikiria, unalichora wazo kichwani kwanza.

 

Muhuza: Wapi unapata fikra ya kuchora hizi katuni tukitegemea ukikaa na watu ndipo unapata fikra humo humo pengine kwenye mazungumzo au majadiliano mbalimbali ndipo unapata hizo idea (mawazo) za kwenda kuchora?

 

Masoud: Mimi napenda sana kufikiria. Kwa sababu huwezi kufikiria kama uko kwenye zogo, mnapiga stori huyu kaleta hii, huyu kaleta hii; mimi napenda sana kufikiria ndiyo maana mara nyingi napenda kuwa peke yangu. Haimaanishi kwamba wakikusanyika watu basi mimi ndiyo nakimbia, hapana, lakini si mara nyingi kunikuta mimi niko na watu.

Kinachohitajika ni uwezo wako wa kuweza kufanya analysis (uchambuzi). Kwa hiyo mikusanyiko hainipi sana katuni kwa kuwa napenda sana mwenyewe kufikiria na kutafakari.

 

Muhuza: Hili la katuni ndilo limechukua nafasi kubwa ya kutambulika kwako. Je, ulianzaje kuchora katuni? Ni jambo limekutokea ama kuna mtu alikushawishi kuanza kufanya kazi hiyo?

 

Masoud: Hii 2019 unajua huu ni mwaka wa 30 nafanya kazi hiyo, inabidi nifanye sherehe. Nilianza kama watoto wengine wanavyokuwa na vipaji, ukizungumzia soka leo hii mtu atakwambia alianza akiwa mdogo kabisa anacheza.

Watoto wote wanakuwa na vipaji – huyu ufundi, huyu anachora, lakini tukifika njia panda ya kutakiwa kuchagua, chaguzi huwa zinakuwa mbili au tatu kwenye ile njia panda. Kwanza kuacha kile unachokifanya kwa maana ya kipaji na kuendelea na mfumo wa kawaida wa utoto kuelekea ujana, kwa maana ya masomo au kuacha vyote au kubeba unachokifanya.

Mimi nilipata kuungwa mkono katika umri mdogo na mzee wangu. Kuungwa mkono si kukatazwa. Juzi nakumbuka kuna mama mmoja alimleta mtoto wake akisema anapenda sana kuchora, lakini baba yake hapendi kumwona huyo kijana akichora. Najua wasiwasi wa huyo mzee ni kwamba huyo kijana hatafanya vizuri darasani. Mimi nilipata bahati kuwa ninachora na vitu vingine vikawa vinaendelea kama kawaida.

Please follow and like us:
Pin Share