Wapenzi wa muziki wa kizazi kipya duniani, hasa Afrika, kundi la P-Square si geni masikioni mwao kutokana na kazi zake kukubalika katika makundi mbalimbali.

Vijana hao wawili, ambao ni mapacha kutoka nchini Nigeria, Peter Okoye na Paul Okoye, wanaunda kundi maarufu linalojulikana kama P-Square. Mapacha hao nje ya muziki wanafanya biashara.

Peter na Paul wamezaliwa jijini Lagos, nchini Nigeria, miaka 36 iliyopita. Wamesoma elimu ya sekondari katika Shule ya Mtakatifu Murumba, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki huko Jos, nchini Nigeria.

Mapacha hao kwa wakati mmoja walijiunga na shule ya muziki pamoja na maigizo ambapo walikuwa wakiimba na kucheza kwa kuwaiga kina Michael Jackson, MC Hammer na Bobby Brown.

Mwaka 1997 walianzisha kundi lililoitwa Smooth Criminal ambapo walikuwa wanacheza ‘Break Dance’. Kundi hilo lilianza kama genge la mtaani lililojulikana kwa majina ya MMMPP (M Clef a.k.a. Itemoh, Michael, Melvin, Peter and Paul).

Mwaka 1999 vijana hao Peter na Paul, wakaingia rasmi katika masomo ya muziki kuongeza ujuzi wao na kujifunza kupiga gitaa pamoja na ngoma.

Kazi zao za muziki zilianza kuingizwa katika filamu kama Tobi, Mama Sunday, Moment of Bitterness pamoja na Evas River.

Mwaka huo wa 1999, wakajiunga na Chuo Kikuu cha Abuja kusomea masuala ya uongozi wa biashara. Baada ya kujiunga na masomo ya elimu ya juu, kundi lao la Smooth Criminal, liliathirika na hatimaye kusambaratika kwa sababu M Clef, Michael na Melvin walisoma vyuo tofauti na wao.

Lakini vijana hao Peter na Paul hawakukata tamaa, wakaamua kuunda kundi lao jingine la watu wawili lililojulikana kama ‘Double P’, ambalo nalo baadaye walibadili jina mara mbili na kuwa ‘P&P’ na ‘Da Pees’ na kundi ilo lilipotulia zaidi ndipo likajiita P-Square, ambalo liliongozwa na Promota Bayo Odusami a.k.a Howie T.

Mwaka 2001 P-Square walijishindia katika mashindano yaliyojulikana kama ‘Grab Da Mic’, kitendo ambacho kiliwavutia watu wengi mpaka Benson & Hedges iliyoamua kuwadhamini katika albamu yao ya ‘Last Night’, ambayo iliachiwa na lebo ya Timbuk2 music.

Mwaka 2003 walishinda tena katika mashindano ya Amen, kama kundi bora la muziki wa R&B. Mwaka 2005 wakaachia albamu yao ya pili ya Get Squared chini ya lebo yao, Square Records.

Albamu hiyo ilisambazwa kimataifa na TJoe Enterprises, ingawa walikuwa bado wanaongozwa na Howie T na video ya albamu yao ya pili ikachukua nafasi ya kwanza katika MTV Base kwa wiki kadhaa. Kundi lao likaweza kuwashirikisha wasanii wengine wa kimataifa kama Ginuwine, Sean Paul, Akon and Busola Keshiro.

 Mwaka 2007 wakaachia albamu yao, ‘Game Over’ ambayo iliwaingizia pesa nyingi baada ya kuuza nakala milioni 8 kimataifa. Mwaka 2009 wakaachia albamu yao ya nne ‘Danger’ ambapo katika albamu hiyo waliweza kuwashirikisha kina 2Face Idibia, J Martins pamoja na Frenzy.

Aprili, 2010 wakaitwa wasanii wa mwaka katika KORA All Africa Music shughuli za utoaji tuzo hizo zilifanyika katika mji wa Ouagadougou, Burkina Faso. Ambako walijishindia dola za Marekani milioni 1.

P-Square waliweza kurekodi video pamoja na mwanamuziki machachari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Awillo Longomba.

Mapacha hao wa kufanana, Peter na Paul Okoye, wametangazwa kushika nafasi ya pili kwa utajiri nchini Nigeria. P-Square walifanikiwa kuuza kila albamu waliyotoa kwa mauzo ya juu yakichagizwa na maonyesho mbalimbali wanayofanya na kusababisha kujulikana zaidi duniani.

Vijana hao wana utajiri unaokisiwa kufikia dola za Marekani milioni 3, zaidi ya Sh bilioni 6 za Tanzania, huku wakimiliki eneo lenye thamani kubwa nchini Nigeria la Square Vile.

Wanamiliki mali zenye thamani kubwa yakiwemo magari, ndege aina ya Airbus, waliyoinunua kwa ajili ya kusafiria, kutoka katika moja ya kampuni za Arabuni.

Peter na Paul Okoye, wanamiliki mali mbalimbali katika miji ya Jos na Port Harcout, likiwemo jumba la kifahari lenye thamani ya Naira milioni 400 lililopo katika mji wa Lagos.

Mapacha hao wametajwa kuwa ndio wanamuziki tajiri kuliko wote nchini Nigeria kwa sasa, wakiwa wamerekodi na kuuza albamu kadhaa sehemu mbalimbali duniani. Wameingizwa kwenye klabu ya mabilionea wa Nigeria.

Please follow and like us:
Pin Share