Msanii wa kizazi kipya, Diamond Platnumz (pichani), ambaye ‘nyota’ yake inaendelea kung’aa kwa kuingiza pesa lukuki kutoka katika maonyesho yake amekuwa akipata mialiko mingi ndani na nje ya nchi, ambako hulipwa ‘kitita’ kizuri cha pesa.

Mara baada ya kuzaliwa Oktoba 2, 1989 katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, alipewa majina ya Nasibu Abdul Juma.

Kwa bahati mbaya hakupata malezi ya baba na mama yake kwa pamoja kwa kuwa wazazi wake walitengana akiwa na umri mdogo.

Nasibu akatelekezwa na baba yake pasipo msaada wowote, ikabidi mama yake ampeleke kwenda kuanza maisha mapya maeneo ya Tandale Magharibi kwa bibi yake mzaa mama.

Historia yake ni ya kusikitisha kama alivyoelezea kwenye wimbo wa ‘Binadamu Wabaya’.
Mwaka 1995 alianza kupata elimu ya awali (nursery) katika Shule ya Chakula Bora iliyopo Tandale Uzuri hadi alipomaliza na kujiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Tandale Magharibi iliyopo jijini Dar es Salaam mwaka 1996.
Mwaka 2000 Nasibu akiwa darasa la tano alionekana kuanza kupenda muziki, hivyo alianza kukariri baadhi ya nyimbo za wasanii waliokuwa katika kilele cha umaarufu ndani na nje ya nchi.

Katika kipindi hicho Diamond akawa anaimba katika maeneo tofauti ikiwa ni njia ya kujitangaza.
Mama yake aliweza kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Nasibu kwa kuwa mara nyingi alikuwa akimnunulia kanda za albamu za wasanii mbalimbali waliokuwa wakitamba kipindi hicho.

Wakati mwingine mama huyo alikuwa akimuandikia baadhi ya nyimbo za wasanii hao ili mwanaye aweze kuzishika na kuimba kwa urahisi.

Mama Diamond ilifikia siku zingine alikuwa akimpeleka mwanae katika matamasha tofauti ya vipaji (talent show) ili apate nafasi ya kuimba.

Kitendo hicho baadhi ya ndugu wa familia waliona ni sawa na kumpotosha na kumharibu mtoto huyo ambaye waliamini mwelekeo ulipaswa kumhimiza katika masomo.
Kwa kweli hali ya maisha yao ilikuwa ngumu, Mama Diamond hakuwa na njia ya kumuingizia kipato cha ziada kuweza kumlea na kumsomesha mwanaye.

Ilimbidi atumie kiasi kidogo anachokipata kutoka kwenye kodi ya vyumba viwili alivyopewa na mama yake, yaani bibi yake Diamond na biashara zake ndogondogo za mtaji unaotokana na mikopo. Walilazimika kulala chumba kimoja na bibi yao ili vyumba hivyo viwili viwapatie kodi.
Baada ya kuhitimu shule ya msingi mwaka 2002 akataka kuanza masomo ya sekondari mwaka 2003, mama yake alimwambia aachane na muziki kabisa na azingatie masomo.

Mama Diamond alikuwa akimsisitiza mwanaye ili aweze kupata elimu itakayomsaidia hata kwenye muziki kwa kuwa asingeweza kushika vitu viwili kwa pamoja muda huo.
Akiwa sekondari, Diamond aliendelea kufanya muziki kwa siri bila mama yake kujua, ilipofikia mwaka 2004 taratibu akaanza kujifunza kuandika nyimbo zake mwenyewe.

Baada ya kuhitimu elimu yake ya sekondari mwaka 2006, mwaka uliofuata wa 2007 alijikita rasmi katika shughuli za muziki ili kujaribu kutimiza ndoto zake.
Haikuwa safari rahisi kama alivyokuwa akitarajia. Ilifikia wakati mwingine akaanza kutafuta vibarua ilimradi aweze kupata riziki.

Diamond alikuwa akifanya hivyo ili kuepuka hali ya kushinda nyumbani, alifanya shughuli mbalimbali kama kuuza mitumba, kibarua kituo cha kuuza mafuta (petrol station), kupiga picha, kupigisha simu, kazi za viwandani hata wakati mwingine kuingia kwenye makundi ya kucheza kamari mitaani ili aweze kupata pesa ya kuingia studio kuredi nyimbo zake lakini bila kufanikiwa.

Diamond alilazimika kuuza pete ya dhahabu ambayo alipewa na mama yake mzazi aivae.

Alimdanganya mama yake kuwa pete hiyo imepotea na ndipo alipofanikiwa kuingia studio kurekodi wimbo wa kwanza uitwayo ‘Toka Mwanzo’.
Kutokana na kutokuwa na mazoea ya kurekodi, hakuweza kutengeneza wimbo ‘mkali’ lakini wimbo ule ulianza kumpa mawasiliano tofauti.

Baadhi ya watu walishangazwa jinsi alivyoingia kwa mara ya kwanza studio na kuweza kutengeneza wimbo kama mzoefu.

Hali hiyo iliwafanya kuamini kuwa akipata nafasi ya kurekodi mara kadhaa angeweza kufanya kitu kikubwa.
Wimbo ule ulimfanya aweze kukutana na Chizo Mapene ambaye alijitolea kumsimamia.

Hakika wakaanza kurekodi albamu, lakini bahati mbaya wakiwa katikati ya kurekodi albamu hiyo, Chizo Mapene aliyekuwa akimsaidia, alipata matatizo ya kifedha na hakuweza tena kumsaidia.

Diamond ilimbidi kuanza upya kuzunguka katika studio mbalimbali kuomba kuingia mkataba kwenye ‘record label’, lakini kote hakuweza kufanikiwa, wote walimwambia hajui kuimba na kutotaka kumsikiliza kabisa.
Kilikuwa ni kipindi kigumu kwa Diamond kwa kuwa hata yule mpenzi wake ambaye alikuwa naye alimuacha.

Dada huyo alikuwa amekwisha kuchoshwa na ndoto hewa za Diamond ambazo alikuwa akiziota kila siku kuwa ipo siku atafanikiwa kimuziki na kuwa mwanamuziki mkubwa, wataishi maisha mazuri. Hatua ya dada huyo ilimchanganya na kumuumiza Diamond.

Please follow and like us:
Pin Share