Buriani Lutumba Simaro Massiya

Lutumba Simaro Massiya aliyekuwa mtunzi na mcharazaji maalumu wa gitaa la ‘rhythm’ katika bendi za T.P. OK Jazz na Bana OK, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amefariki dunia Machi 30, mwaka huu katika Jiji la Paris, Ufaransa.

Taarifa hiyo ilitangazwa na mwanawe wa kiume, Simon Lutumba, kutoka jijini Paris, kwamba baba yake Lutumba alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81.

Baada ya taarifa ya kifo chake kusikika, baadhi ya wapenzi wa muziki wa rhumba Afrika Mashariki na Kati, wameingiwa simanzi kubwa kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Lutumba alipelekwa huko kwa ajili ya matibabu ya maradhi ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa kipindi kirefu yaliyosababisha kustaafu kupiga muziki mwaka jana, baada ya kuutumikia kwa miaka 60.

Aidha, alisema kuwa umri wake wa miaka 80 ulikuwa umemtupa mkono sambamba na maradhi ya miguu yaliyokuwa yakimsumbua.

Mara baada ya kutangaza kustaafu muziki, Lutumba alibisha hodi Ikulu ya Kinshasa akiwa amebeba gitaa lake ambako alimkabidhi Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kong (DRC) kwa wakati huo, Joseph Kabila, ikiwa ni kielelezo cha kustaafu kwake.

Kwa kuthamini mchango wake kwa taifa kupitia muziki, Serikali ya DRC Machi 19, 2018 ilimuenzi Lutumba Simaro kwa kubadilisha jina la Barabara ya Avenue Mushi kuwa Simaro Lutumba Avenue.

Aidha, kuliandaliwa muziki maalumu katika Ukumbi wa Dancing Bar 1, 2, 3 uliopo kwa Mama Kulutu, Mtaa wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ikumbukwe kwamba hii si mara ya kwanza kwa serikali hiyo kuenzi wanamuziki wake.  Ilitokea wakati wa gwiji la muziki nchini humo, Franco Luambo Makiadi, serikali hiyo ilijenga mnara wa kumbukumbu yake katika Jiji la Kinshasa. Aidha, ilibadilisha majina ya barabara Jean-Bendel Bokassa kuwa Franco Makiadi Avenue.

Bakossa alikuwa rais wa Afrika ya Kati na rafiki mkubwa wa Mobutu Sese Seko, aliyekuwa rais wa Zaire (DRC) kabla ya kupinduliwa na Laurent Desire Kabila.

Lutumba kwa kipindi kirefu alikuwa akienda Paris kuhudhuria matibabu ya moyo, pamoja na maumivu kwenye miguu.

Ilikuwa vigumu kuendelea kukaa jijini humo kwa kuwa ‘visa’ yake ya miezi mitatu ilikuwa imefikia kikomo.

Lutumba alirudi DRC Februari 18, 2015 akitokea Ufaransa kushughulikia ‘visa’ nyingine.

Wakati akiwa nchini mwake madaktari walimtaka alirudi haraka Paris kuendelea na matibabu ya uhakika.

Lutumba Simaro wakati wa uhai wake alinukuliwa akisema kuwa uamuzi wake wa kustaafu ungekamilika mara baada ya kutoka rasmi kwa ‘album’ yake ya mwisho ya ‘Ma Prière’ ambayo kwa lugha yetu ya Kiswahili ni ‘Dua Yangu’ iliyokuwa na nyimbo sita.

Licha ya hali yake kiafya kuwa tete, mkongwe huyo alifanya onyesho lake la mwisho katika Ukumbi wa Show Buzz uliopo Colonel Mondjiba Avenue, Ngaliema Commune, Machi 23, mwaka jana.

Lutumba Simaro amepiga muziki wa rhumba kuanzia mwaka 1958 akiwa katika bendi za Micra Jazz, Congo Jazz mwaka 1959 hadi 1960 na T.P. OK. Jazz mwaka 1961 hadi 1993.

Nguli huyo alikuwa mmoja kati ya waanzilishi wa bendi ya Bana OK. mwaka 1994 ambako alitunga na kupiga muziki hadi Machi mwaka jana.

Simaro amekuwa mashuhuri kwa kupiga gitaa la ‘rhythm’ katika bendi za T.P.O.K. Jazz na Bana OK.

Wajuzi wa muziki walimuelezea Simaro Lutumba kuwa ni mwalimu ndani ya T.P.O.K. Jazz.

Aliweza kuwafundisha vijana wengi muziki ambao ni pamoja na Youlou Mabiala na Malage de Lugendo.

Baadhi ya nyimbo alizotunga ni ‘Maya’ ulioimbwa na Carlyto Lassa, ‘Mabele’ ulioimbwa na Sam Mangwana, ‘Dati Petroli’ alioimba Madilu System; ‘Mbongo’, ‘Mandola’ na ‘Kadima zilizoimbwa na Djo Mpoyi na nyingine nyingi.