Tujisahihishe: Mwalimu Nyerere

 

UMOJA wa kundi lolote ni sawa sawa na umoja wa viungo mbalimbali vya mwili au mtambo. Viungo vya mwili havina budi vitii kanuni zinazoviwezesha kufanya kazi yake sawa sawa. Lakini haviwezi kutii kanuni hizo kama haviko katika hali ya afya njema. Mara kiungo kimoja kinapokuwa hakina afya safi, huanza kuvunja kanuni za kazi na mwili mzima hupata taabu.

Umoja wa binadamu na kadhalika, hauwezi kutimiza madhumuni yake bila viungo vyake kutii kanuni zinazouwezesha umoja wa binadamu kufanya kazi zake sawa sawa. Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake.

 

Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi n.k, matatizo yao mengi hutokana na unafsi. Unafsi ni wa aina nyingi. Swali ambalo twalisikia mara kwa mara, hali yetu ya baadaye itakuwaje? Ni swali ambalo sina shaka kuna watu wanaouliza kwa nia safi kabisa. Lakini mara nyingi linalotokana na unafsi.

 

Mtu anayeuliza unafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi basi TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tunzo, anasahau kabisa kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla. Lakini kwa mtu wa aina hiyo hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya jumuiya ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake, huu ni unafsi.

 

Kama wanachama wa TANU, na hasa viongozi, hawatakihukumu chama chetu kwa mahitaji ya jumuiya, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu na wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama.


Dalili nyingine ya unafsi na ambayo ni ugonjwa mbaya sana ni fitina. Kanuni moja ya TANU inasema hivi: “Nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko.”  Lakini bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua. Ni wa aina mbalimbali.


Wengine humwona mwenzao anafanya kosa, badala ya kumwabia pale pale kijamaa kwamba atendalo ni kosa, watanyamaza kimya. Lakini hawanyamazi kabisa! Watakwenda kumteta katika vikundi vya siri siri. Mateto haya si ya kumsaidia mwenzao, ni ya kumdhuru. Hii ni aina mojawapo ya fitina. Wengine hugawa watu katika mafungu.

 

“Fulani” japo akifanya kosa kubwa sana hasemwi. Lakini “fulani” wa pili akifanya kosa japo dogo, kosa lile hukuzwa likawa kama Mlima Kilimanjaro. Hawa hutafuta sababu za kumtetea “fulani” wa kwanza au za kumlaumu “fulani” wa pili ambazo hazifanani kabisa na ukweli.

 

Kwa watu wa aina hii, ukweli ni jambo ambalo hutegemea mtu-si kitu kinachojitegemea chenyewe bila kujali mtu. “Fulani” wa kwanza akisema katika majadiliano kuwa mbili na mbili ni tano, wao watakubali. Lakini “fulani” wa pili akisema sivyo, mbili na mbili nne watamwona ni mtu mbaya kabisa ambaye hastahili hata kusikilizwa. Hawa hawajali ukweli, hujali nafsi tu. Kwao, ukweli ni maono yao na matakwa yao.

 

Hatuna budi, hasa katika majadiliano na mazungumzo yanayohusu jumuiya, tujifunze kusikiliza hoja zenyewe zinazotolewa na wenzetu, na kuijibu zile hoja kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali kama aliyezitoa ni rafiki au si rafiki. Pia wanaopingwa hawana budi wakubali kuwa kinachopingwa ni zile hoja zao, siyo wao wenyewe. Bila mazoea haya, mazungumzo hayana maana; yanakuwa ni kupoteza wakati maana huwa tumekwisha kuzihukumu hoja za mtu hata kabla hajazitamka! Kadhalika, hoja zetu zikijibiwa kwa kupingwa halafu tukawakasirikia waliozipinga tunafanya mazungumzo yasiwe na maana, kwa sababu tunapenda hoja zetu zikubaliwe tu hata kama si hoja safi.


Ukweli una tabia moja nzuri sana, haujali mkubwa wala mdogo, hujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa. Ukiniona nataka kupiga teke jiwe kwa kuwa unafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa.


Wakati mwingine mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunaotoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake. Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha. Ni kweli mbili mara tatu ni sita, lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu, au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana. Huu ni mfano wa upuuzi, lakini mara nyingi hoja tunazotumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda, au kukubali mawazo yetu huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayoyajadili.


Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni unafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine  twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake.

 

Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kamba demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi. Lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi.


Kadhalika, matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na mazungumzo. Bila wale wachache kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana maana.Wakati mwingine hata baada ya majadiliano, wachache-japo wamekubali kutii uamuzi wa wengi- wanaweza kuendelea kuamini kwamba mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka. Demokrasi inawapa haki na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka wengi waone kuwa ni ya kweli. Bila hivyo maendeleo katika mawazo hayawezekani, kwani mara nyingi wazo zuri hutokana na mtu mmoja tu. Mwanzo laweza likapingwa, pengine kwa nguvu kabisa, na walio wengi, lakini hatimaye wengi hulikubali. Huu ndio msingi wa maendeleo katika mawazo ya binadamu.


Makosa ni makosa na dhuluma ni dhuluma, japo watendao makosa hayo au dhuluma ile ni wakubwa au ni wengi. Chama kinachopenda ukweli na haki hakina budi kiwape wanachama wake uhuru na nafasi ya kusahihisha makosa na kuondoa dhuluma. Wanachama hawana budi waone kuwa ni wajibu wao kutumia uhuru huo na nafasi hiyo. Wanachama wasiotumia uhuru huo na nafasi kwa sababu ya kuogopa kuchukia au kupoteza nafasi zao, wanafanya kosa kubwa la unafsi, ambalo ni adui wa haki na ukweli.


Kosa jingine linalotokana na unafsi tunalifanya wakati wa kuchagua viongozi. Wakati mwingine hufanywa na wanachama; wakati mwingine hufanywa na viongozi wenyewe, au wale wanaotaka uongozi. Nimesema mahali pengine kwamba viongozi wetu hawana budi watokane na WATU. Viongozi wa TANU. hawana budi watokane na wanachama wa TANU wenyewe, bila hila,vitisho, rushwa au ujanja wa aina yoyote. Lakini mara nyingi wanachama huchagua viongozi bila kufikiri kwa makini kama viongozi hao wanaweza au hawawezi, kazi wanayochaguliwa kufanya.


Wanachama wetu watafanya makosa makubwa sana ikiwa watachagua viongozi wao ovyo tu. Hii ni jambo la hatari kwa demokrasi na chama chetu, na maadui wa TANU wanaweza kusema kwamba demokrasi haina maana kwa sababu haizai viongozi wanaoweza kazi zao! Hii si kweli, maana wote twajua kwamba demokrasi inaweza kuchagua viongozi wazuri. Lakini ni wajibu wetu katika kuhifadhi demokrasi kuona kuwa inachagua viongozi ambao wanaziweza kazi zao.

 

Kazi ya kuchagua viongozi ni kazi ya wanachama wetu; kwamba jambo hili ni kubwa sana. Haifai kuchagua kiongozi kwa sababu ni mjomba, au binamu au ana sauti au sura nzuri. Wala haifai kuacha kumchagua mtu kuwa kiongozi kwa sababu kama hizo. Jambo kubwa ni kuchagua kiongozi mwenye tabia nzuri na anayeweza kazi. Hatuna budi tutii kanuni hii katika kuajiri wafanya kazi katika TANU au serikalini. Hawa pia hawana budi wachaguliwe kwa sababu wanaiweza kazi wanayoajiriwa kufanya, na ni watu wenye tabia nzuri.


Kosa jingine ni kutojielimisha. Kanuni yetu moja inasema: “Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu wote na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.” Wengi wetu hufikiri kuwa kujielimisha ni kwenda Kivukoni, au kupata nafasi kwenda kusoma katika nchi za nje. Wengine hufikiri kuwa kujielimisha ni kujua kusoma na kuandika. Hilo ni kosa, lakini si kubwa kama la pili, wengi wetu hasa baadhi ya viongozi hufikiri kuwa tunajua kila kitu na hatuna haja kujifunza jambo lolote zaidi. Mtaalamu mmoja wa zamani alisema kuwa mwanzo wa elimu ni kutambua kuwa hatujui kitu.

 

 

By Jamhuri