Leo kwa makusudi nimeamua nijadili mada hii sambamba na mada iliyotangulia hapo juu. Pamoja na matukio yanayoendelea ya uhalifu niliyoyajadili kwa kina kwenye safu yangu ya Sitanii, nimeona yaende sambamba na suala la Haki ya Kupata Habari.

Nimefuatilia mijadala ya mabaraza ya Katiba katika sehemu mbalimbali nchini, lakini ukiacha Baraza la Wanahabari lililoundwa chini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) hakuna mtu anayezungumzia suala la haki ya kupata habari. Hapa naona wananchi na wajumbe wa mabaraza wanafanya kosa kubwa.

 

Inawezekana kuna dhana potofu kuwa Haki ya Kupata Habari inadaiwa na Waandishi wa Habari kwa ajili ya magazeti, redio na televisheni. Kama yupo anayefikiria hivyo anafanya kosa la msingi. Haki ya Kupata Habari ni haki ya msingi inayowezesha upatikanaji wa haki nyingine.

 

Kwa mfano, kiwango cha uhalifu nchini kinachoendelea iwapo vyombo vya dola vingekuwa vinashurutishwa kisheria kutoa habari tungeweza kufahamu chimbuko la wimbi la uhalifu huu. Inawezekana polisi wameishiwa fedha za kufuatilia wahalifu, hivyo kama sheria ingekuwa inalazimisha viongozi wangetupatia taarifa hizi.

 

Inawezekana mwananchi akienda mahakamani, hospitalini, polisi, TRA au sehemu yoyote ya kupata huduma wanadaiwa rushwa. Ikiwa haki ya kupata habari haijatolewa kikatiba, basi ni wazi wataendelea kunyimwa huduma na hakuna lolote wanaloweza kufanya.

 

Historia inaonesha kuwa haki ya kupata habari imesaidia mataifa mengi duniani kupiga hatua kubwa kiuchumi haraka kuliko mataifa mengi yenye ukiritimba wa kutoa habari. Nchi kama Marekani, Japan, Uingereza, Finland, Ujerumani, Denmark na nyingine zimepiga hatua kubwa kiuchumi kutokana na kuendesha serikali kwa uwazi.

 

Tanzania ilianzisha utaratibu huu kwa kuchapisha kiasi cha fedha zinazotumwa kwenye halmashauri mbalimbali kama ruzuku, lakini hakika utaratibu huu haujaeleweka vyema kwa Watanzania walio wengi.

 

Kimsingi, utaratibu huu ingawa fedha zinachapishwa kwenye mtandao wa Wizara ya Fedha, hakuna sababu zinazotolewa juu ya kwanini kiasi kinachotolewa ni kidogo ikilinganishwa na bajeti iliyotengwa.

 

Ndio maana kwa mfano, Mkoa wa Kagera katika mwaka wa fedha 2010/2011 Kilimo Kwanza kilitengewa wastani wa Sh bilioni 10, lakini wakubwa wakaishia kutoa Sh bilioni tatu. Kiasi hiki ni sawa na asilimai 30 ya bajeti iliyotengwa, lakini iwapo Katiba ingekuwa inatamka bayana juu ya haki ya kupewa maelezo, basi zingeelezwa sababu za msingi na kuepusha tatizo kama hili kurejewa siku za usoni.

 

Kwa upande wa vyombo vya habari vinahitaji haki hii kuliko wakati wowote. Mara kadhaa tumeshuhudia katika wizara, taasisi na mashirika mbalimbali baadhi ya watendaji wamekuwa wakigoma kutoa taarifa kwa vyombo vya habari hali inayozifanya taasisi hizi kujiendesha kwa ubabe.

 

Mashirika binafsi na kampuni kubwa nazo zimegeuka kero. Wapo watu wanafanya biashara kubwa, wanakwepa kodi, lakini bado huwezi kuwagusa maana Katiba haitoi uhuru huu. Ndio maana leo vyombo vya habari haviwezi kwenda kuzilazimisha kampuni za madini, simu au nyinginezo kueleza mapato yao kwa usahihi.

 

Kinachotokea ni wananchi kuendelea kurundikiwa kodi na watu wanaopaswa kulipa kodi hawalipi. Haya yote yanawezekana ikiwa wananchi wanaojadili mambo mbalimbali kwenye mabaraza ya Katiba iwapo watagundua kuwa ikiwa hawatatetea haki ya kupata habari kuwamo kwenye Katiba, hata haki hizo wanazozitetea zinaweza kutolewa lakini zisifanye kazi.

 

Hakika ninasema chondo chonde wajumbe wa mabaraza, kwa nia ya kuwezesha hayo mnayoyadai kuwamo kwenye Katiba na yakafanya kazi vizuri, tafadhali daini na Haki ya Kupata Habari, kwani bila hivyo tutapata Katiba nzuri iliyozibwa midomo.

 

Haki ya kupata habari ni haki ya msingi inayowezesha haki nyingine. Nimeona nilikumbushe hili, kuepusha wajumbe wa mabaraza kujadili siasa zaidi na kusahau suala la msingi kama hili la haki ya kupata habari. Nawatakia mjadala mwema.

 

1097 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!