TABORA

Na Moshy Kiyungi

Judith Wambura, maarufu kama Lady Jaydee, Jide, Komandoo au Binti Machozi ni miongoni mwa wasanii wakongwe wa kike nchini.

Msanii huyu ana kipaji na uwezo mkubwa wa kutunga na kuimba nyimbo zenye ujumbe mzito kwa jamii huku akipiga muziki mubashara na Machozi Band.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipotoka kwa mara ya kwanza na albamu ya Machozi, wapo waliombeza wakidhani asingefika mbali katika muziki wa Bongo Fleva.

Lakini ni wimbo huo, au albamu ya ‘Machozi’ ndiyo imembeba kwa muda mrefu, ikimpa jina la utani la ‘Binti Machozi’ na baadaye kubeba jina la kundi lake la muziki, Machozi Band.

Alizaliwa Juni 5, 1979 mkoani Shinyanga. Kwa sasa ni maarufu kwa muziki wenye mahadhi ya R&B, Zouk na Afro Pop. 

Mwonekano wake kiurembo ni tofauti na wanawake wengine wenye umri kama wake.

Kama ulimuona Komandoo Jide miaka 10 iliyopita, hakika hata leo hajabadilika au basi mabadiliko yake ni madogo sana.

Mitaani wanadai ‘udongo’ wake ni mzuri; yaani Malkia huyu wa Bongo Fleva, hazeeki!

Hakika mienendo ya Jide, aka Komandoo, unaweza kumfananisha na mwimbaji, mwigizaji, mfanyabiashara na mwanamitindo wa Marekani; Jennifer Lopez (JLo), ambaye Julai 24, mwaka huu amefikisha umri wa miaka 52!

Komandoo Lady JayDee, mwaka 2002, alipigiwa kura kuwa msanii bora wa kike wa R&B kwenye mashindano ya Kora All Africa Designers.

Mwaka huo huo akapigiwa kura kuwa msanii bora wa kike wa R&B; akatuzwa kwa albamu bora ya R&B na Tanzania Music Awards mwaka 2004.

Agosti 6, 2004, Jide alinyakua tuzo ya albamu bora katika mashindano ya Tanzania Music Awards kama Julai 2005 alivyoshinda tuzo kwa upande wa wanawake ya video bora kwa Afrika Kusini.

Ndoa yake na Gardner Habash iliyodumu kwa miaka tisa, iliingia kwenye mgogoro mwaka 2014 na kutengana rasmi Februari 2016.

Jide ni msanii mzoefu anayetajwa na mashabiki kuwa na mvuto wa aina yake Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, akiwa mmoja wa wanawake wa kwanza kuimba nyimbo za R&B kwa Kiswahili.

Miongoni mwa albamu zake ni ‘Nasonga Mbele’, ‘Shukrani’, ‘The Best Of Lady Jaydee’, ‘Nasimama’, ‘Nakupenda’, ‘Siku Hazigandi’, ‘Nothing But The Truth’, ‘Woman’, ‘Binti’, ‘Moto’, ‘Siri Yangu’, ‘Ndindindi’, ‘I Love My Self’ na ‘One Time’.

Mama huyu ni fundi wa ‘kolabo’ Afrika Mashariki ambaye unapozungumzia wasanii waliofanya kolabo nyingi ndani na nje ya nchi, jina lake hauwezi kuliweka pembeni.

Lady Jaydee ni mwanamke mpambanaji; amekwepa mishale mingi ndani ya muziki wa Bongo Fleva, akapachikwa majina mengi yakiwamo ya Binti Machozi, Anakonda na Komandoo.

Ni zaidi ya miaka 20 sasa yupo ndani ya Bongo Fleva, amefanya vizuri na mpaka sasa hakuna msanii wa kike ambaye amevunja rekodi zake.

Mwanzoni kabisa amewahi kushirikishwa na mkali wa Hip Hop na Rap nchini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ katika wimbo wa ‘Mambo ya Fedha’; mmoja kati ya nyimbo kali za muda wote.

Pia amefanya kazi na Joseph Haule ‘Profesa Jay’ kwenye nyimbo za ‘Bongo Dar es Salaam’, ‘Ndio Mzee’ na ‘Niamini’.

Akishirikiana na Ambwene Yesaya ‘AY’, Jide aliimba katika wimbo ‘Machoni Kama Watu’ na kuleta mvuto wa aina yake.

Cheche za Jide zimesikika pia kwenye ‘Wanoknok’ ngoma ya wasanii wa Rap; Mandojo na Domokaya.

Wimbo wa ‘Sema’ aliufanya akiwa na Herry Sameer ‘Mr Blue’ nao umo kwenye orodha ya nyimbo kali alizoshiriki au kushirikishwa.

Akiwa na mkali wa Temeke, ‘Mtoto wa Mama Said’ Chige Chibunda, Jide alishiriki katika wimbo ‘Mambo Bado’ akiwa pia na Mike Mwakatundu ‘Mike Tee’ au Mnyalu.

Mvuto wa sauti yake ulisababisha Ally Kiba kuomba ‘msaada’ wa Komandoo katika ngoma ya ‘Single Boy’.

‘Zamani’ ni moja kati ya nyimbo bora kuwahi kutokea kwenye Bongo Fleva, unaomilikiwa na Abubakar Katwila ‘Q-Chief’, Jide naye amehusika humo.

‘Anita’ wa Matonya, uliwahi kuwa wimbo wa taifa kwa wakati fulani, ambapo kwenye kiitikio sauti tamu ya Lady Jaydee inasikika na kuufanya upande kwenye chati za Bongo Fleva.

Msanii Rich Longomba alimshirikisha Jide kwenye ngoma ya ‘Nimpate Wapi’ pia katika wimbo wa ‘Nitafanya’ alishirikiana vema na msanii kutoka Kenya, Kidumu.

Mkongwe huyu alitoka na wimbo wa ‘Sirimba’ akiwa na kundi la Ngoni na alishiriki katika wimbo wa ‘Njalo-Zumba’ ambao umeimbwa na Mina Nawe wa Afrika Kusini.

Nyimbo za ‘Sikiliza’ na ‘Mapenzi Gani’, alishirikiana na msanii kutoka Morogoro, Albert Magwea ‘Ngwair’, ‘Kuna Pesa’ alishirikiana na msanii wa Hip Hop, Langa Kileo ‘Langa’ na ‘Kuna Kilimanjaro’ alioshirikiana na Joh Makini.

Nyimbo za ‘Kadi’ na ‘Ua Rose’ alishirikiana na Fareed Kubanda ‘Fid Q’, ‘Sifai’ ni wimbo alioshirikishwa na TID na majuzi Jide ameshirikishwa katika wimbo ‘Wife’ wa Harmonize.

Jide amenukuliwa akisema mafanikio aliyonayo kwenye muziki yametokana na nidhamu kwa muziki ambao ni sehemu ya maisha yake.

“Ni kazi yangu. Ninauheshimu sana muziki. Ni kila kitu kwangu. Sijioni mimi bila muziki, hivyo ninauthamini sana,” anasema.

Baada ya ukimya wa kipindi fulani na kisha kuibuka na ‘Ndindindi’, wimbo uliopokewa vema wakati huo, Jide anasema:

“Baada ya kukaa kimya, sikuwa na hisia ya kuandika wimbo wowote. Nikakaa na watu. Seven, akaandika. Kuna mtu mwingine kutoka Uganda naye akaandika.

“Wote waliandika mashairi wakijua nitauvaa uhusika ipasavyo. Zikaandikwa na nyingine. Lakini ‘Ze NdiNdiNdi’ ndo ukapitishwa utoke. Hata sikufikiria ungekuwa mkubwa!”

Lady Jaydee anajieleza kama mwanamke mpole lakini mwenye hasira anapokosewa, akiwataka mashabiki wake wasiwe na hofu kwani ‘Komandoo wao’ yupo vitani, anapigana.

305 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!