SHINYANGA

Na Antony Sollo

Mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Rahim Mwita mkazi wa Sarawe mkoani hapa, anadaiwa kumuua mkewe, Monica Lucas, kisha kutokomea kusikojulikana na mtoto wa mama huyo ajulikanaye kwa jina la Prince.

Ndugu wa mama huyo, Mabula Lucas, ameliambia JAMHURI kuwa mauaji hayo ya kikatili yalitokea Agosti 11, mwaka huu.

Mmoja wa majirani anasema siku ya tukio, Mwita, Monica na Prince waliwasili nyumbani kwao kwa pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Mwita.
“Walipokaribia chumba alichokuwa amepanga Mwita, Monica alidondoka kutoka kwenye pikipiki kisha Mwita akambeba kumuingiza ndani.
“Muda mfupi baadaye Mwita akatoka nje akiwa amembeba mtoto, akafunga mlango na kusema anakwenda polisi kuripoti kuwa mkewe anataka kulipua nyumba,” anasema jirani huyo akiomba hifadhi ya jina lake.
Anasema baada ya Mwita na mtoto kuondoka na pikipiki, ukatokea mlipuko mkubwa, nyumba ikaanza kuteketea.
Taarifa zinasema majirani walifanikiwa kuvunja mlango na kumkuta Monica akiwa amekwisha kufariki dunia, huku akiwa amerundikiwa nguo, hivyo kushindwa kujiokoa.
Ndugu wa Monica wanadai kuwapo kwa utata katika tukio, wakisema mamlaka za usalama zinamkingia kifua mtuhumiwa zikimsaidia kukwepa mkono wa dola.
“Polisi wanasema Monica alijilipua mwenyewe kwa kuwa mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, hoja inayokinzana na ya majirani waliofika mapema eneo la tukio,” anasema Mabula, ndugu wa Monica.

Anasema Jeshi la Polisi halijamkamata Mwita likidai kutokuwapo sababu, kwa kuwa Monica alifanya uamuzi mwenyewe wa kujiua.
Mabula anaainisha hoja zinazopaswa kutolewa ufafanuzi na polisi baada ya ripoti ya daktari kuwa ni kwanza, mlango kufungwa kwa ndani.
“Waliovunja mlango si polisi, bali majirani. Majirani wanadai mlango ulikuwa umefungwa kwa nje. Kwa jinsi ilivyoonekana, Monica hakuwa hata na uwezo wa kusogea mlangoni kujifungia,” anasema Mabula.
Mashuhuda wa awali wameliambia JAMHURI kuwa majibu ya polisi katika hoja hiyo ni mepesi na hayana mashiko.
Kuhusu taarifa ya daktari, ndugu wa Monica wakiongozwa na Mabula wanasema maelezo waliyopewa na daktari yanatofautiana na taarifa iliyopo Kituo cha Polisi.

“Polisi wanasema sababu ya kifo ni moto, lakini daktari anasema Monica aliuawa kabla hata ya kufikishwa nyumbani. Anasema inaonekana kwamba alipigwa kwa kuwa mkono wake wa kushoto umevunjika.
“Inaonekana alinyongwa na ili kupoteza ushahidi, mtuhumiwa akaamua kumchoma moto,” anasema.

Ndugu hao wanatilia shaka sababu za polisi kutojishughulisha kabisa na Mwita wala hata kumtilia shaka, wakati ni yeye ndiye mtu wa mwisho kuwa na Monica kabla mauti hayajamkumba.

Wanasema polisi walipaswa kumuuliza iwapo kulikuwa na ugomvi kati yao na kusababisha uamuzi wa Monica kujiua.

Taarifa zinadai kuwa Mwita, ambaye hakuhudhuria mazishi ya Monica, ni mwajiriwa wa mmoja wa askari polisi wa Salawe kama dereva wa magari yake.

Uhusiano huo wa kikazi unawatia shaka ndugu na majirani kuwa huenda ndiyo sababu hadi leo hajakamatwa.
“Lakini hofu ya ziada ni kwa mtoto, Prince, yupo hai au na yeye amekwisha kuuawa? Kama bado yupo hai, anaishi katika mazingira gani? Kwa nini polisi wasifuatilie kujua usalama wa Prince?” wanahoji ndugu hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, George Kyando, ameliambia JAMHURI kuwa hana taarifa za tukio hilo na kuwataka wanafamilia kumpelekea taarifa kamili azifanyie kazi mara moja.

“Wananchi wanapaswa kwanza kutoa taarifa kwa makamanda wa polisi wa mikoa husika kwanza badala ya kupeleka taarifa taasisi nyingine.

“Askari anayedaiwa kuingilia mchakato wa kuficha tukio hilo ni mdogo sana na sisi kama viongozi wa Jeshi la Polisi tuna wajibu wa kumkamata, kumhoji na kuhakikisha sheria inafuata mkondo,” anasema RPC Kyando.

342 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!