Hili ni tamko la madaktari bingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam. Hawa wanahusisha hospitali za umma za Muhimbili (MNH), MOI, Ocean Road na Hospitali za manispaa katika mkoa huo.

 

Kutokana na kikao kilichofanyika tarehe Juni 29, 2012 madaktari bingwa tumeamua yafuatayo:

 

* Tunalaani kwa kauli moja kitendo alichofanyiwa daktari na kiongozi wa Jumuiya yetu, Dk Stephen Ulimboka cha kutekwa kuumizwa na kutupwa msitu wa Pande. Kitendo hiki kimetuhuzunisha, kimetufadhaisha na kutufanya kuishi katika hofu ya hali ya juu.   * Tunazitaka mamlaka husika kutuhakikishia mustakabali wa usalama wetu sasa na siku za mbeleni (za baadaye) katika nchi yetu.

 

* Tunalaani juhudi zinazofanywa na wathalimu (wadhalimu) wote katika fani ya udaktari.

 

* Tunalaani vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa madaktari wenzetu sehemu mbalimbali kama Bugando, Dodoma, Mbeya na kwingineko.

 

* Tunatamka wazi kuwa kitendo cha kuwafukuza, kuwanyima mshahara na haki nyingine za mwezi Juni ni udhalilishaji na kinyume na amri ya Mahakama.

 

* Kutokana na vitendo vyote hapo juu (yaani kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, unyanyasaji wa madaktari wenzetu) na pia kutoka na ukweli kwamba hali ya Dk. Ulimboka inazidi kudorora, vile vile kwa kuwa siku zote Serikali imekuwa ikikubali kuwa madai yetu ni ya msingi (lakini haiyatafutii ufumbuzi wowote), tumeamua kusitisha kutoa huduma katika hospitali zote tunazofanyia kazi, yaani Muhimbili, MOI, Ocean Road, Amana, Mwananyamala nk; hadi hapo madai yetu ya msingi yatakaposikilizwa na kutekelezwa.

 

* Tunaomba madaktari bingwa wote hapa nchini watuunge mkono katika harakati hizi za kuiboresha sekta nzima ya afya.

 

Imetolewa na Dk. C. Mng’ong’o

Mwenyekiti wa Madaktari Bingwa Kanda ya Dar es Salaam

By Jamhuri