London ina upepo, ubaridi wa haja na mvua kwa siku mbili tatu hizi, lakini kuna wanaotokwa na jasho. Kihoro kimewashika wanene wachache, kwa sababu ya kashfa ya kupanga viwango vya riba za kukopeshana kwa benki za hapa.

Wa kuumbuka wameshaanza. Baada ya kujiapiza mbele ya familia, marafiki na umma kwamba hataachia ngazi, mkuu wa Benki ya Barclays hapa, ameondoka baada ya Barclays kupigwa faini ya paundi milioni 451.

Bob Diamond hakuwa peke yake kujitetea, bali tuliona jinsi binti yake, Nell Diamond, alivyojiachia kwenye Twitter akiwashambulia wote waliokuwa wakimfuatafuata baba yake.

London imechafuka kabisa sasa, ni kihoro baada ya suala hili kuanza kujadiliwa bungeni, ambako mahasimu wa pande mbili – Conservative na Labour – wanarushiana mawe ya kisiasa. Nilicheka hadi nikawa sina mbavu nilipoona picha ya Bob Diamond na bintiye huyo Neill wakionyesha kile wanachokiita ‘Diamond Gesture’ wakati wa onyesho la mwanamuziki wa Kimarekani, Jay-Z.

Walisimama pamoja – baba kushoto na binti kulia – wakaangalia mbele, lakini kila mmoja akielekeza bega upande wa pili kidogo ili kufanya kama kaduara hivi, kisha wakanyoosha mikono kama wanamwekea mtu, lakini kiupande; hiyo ndiyo ‘Diamond Gesture’.

Hayo yalikuwa kabla ya baba mtu kukumbwa na kashfa, ambayo hata hivyo mkewe, Jenifer, amekuwa naye sambamba akimtia moyo. Kabla na baada ya kulazimika kuachia ngazi, binti mtu alifanya mashambulizi kwa kutumia mitandao ya jamii  hasa Twitter, pengine akidhani angeweza kumwokoa baba yake.

Huyu ni msichana anayetimiza umri wa miaka 24 mwaka huu na ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Princeton anayefanya kazi benki ya Kijerumani – Deutsche Bank. Binti huyu katika mashambulizi yake halengi watu wadogo, ni vigogo, kuanzia Waziri wa Fedha ambaye hapa Uingereza ni mtu mkubwa sana baada ya waziri mkuu na wote wanakaa mtaa maarufu wa London – Downing.

Amemshambulia pia Kiongozi Rasmi wa Upinzani, Ed Miliband, na kuwaambia wakipenda wanaweza kwenda kuzimu, badala ya kumchimba baba yake. Alitumia pia neno baya linalotumiwa na vijana wadogo wa Kimarekani dhidi ya viongozi hao wawili.

Neill hakuishia hapo, amemwaga maneno haya mwishoni mwa wiki iliyopita: “Hakuna mtu ninayemheshimu kama baba yangu duniani. Ametumia miaka 16 kuijenga Barclays, ni aibu kuna makosa ya wachache yanachafua kazi hii ngumu.”

Binti huyu ambaye amekuwa akiishi nchini Marekani, anatajwa kuwa mmoja wa vidosho wanaotamba kwenye mtaa maarufu – Wall Street jijini New York, Marekani. Awali alikuwa akiishi kwenye nyumba ya wazazi wake yenye vyumba sita vya kulala iliyopo Wycombe Square, Chelsea.

Hata hivyo, nyumba hiyo iliuzwa mwaka 2009 kwa kiasi cha fedha ambacho bado hatujakijua, japokuwa nyumba za jirani thamani yake ni kwenye paundi milioni sita.

Katika kuonyesha ukaribu wake na baba yake, kuna picha baba yake akiwa ameshika Kombe la Chelsea la ubingwa wa mashindano ya FA nchini Uingereza. Binti anasema kwamba baba yake alikwenda kupiga picha hiyo baada ya kumtumia picha yake akiwa kwenye sherehe za Chelsea kutwaa kombe la klabu bingwa Ulaya.

Binti anazidi kudai kwamba alimwomba baba yake asiwe anavaa tai yenye picha za wanyama anapoingia kwenye klabu ya burudani ya Soho House. Klabu hiyo ni maarufu kwa vibopa na ina matawi London na New York.

Binti huyo pia alikwenda na baba yake kwenye harambee ya kuchangia hospitali jijini New York mwaka jana ambako zilichangwa dola milioni 9.7. Neill ni balozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Wengine waliohudhuria harambee hiyo ni watu wazito wa aina ya Gary Cohn, Rais wa Benki ya Goldman Sachs. Alikwenda pia Larry Fink, Mwenyekiti wa Taasisi ya Ukaguzi wa Mali ya BlackRock.

Kwenye hafla hiyo binti mtu alijipamba kwa mabawa ya mbuni na bata, na baba yake akatania wageni akisema; “Ukiialika benki ya Kiingereza (yaani yeye ndiye Barclays) mtapata hali ya hewa ya Kiingereza.”

Aprili mwaka huu binti huyo alikuwa akipinga msimamo na mwelekeo wa kifedha wa Gavana wa Benki Kuu ya Marekani, Ben Bernanke, akidai kwamba kesho yake angeweza (binti) kutabiri mwelekeo bora zaidi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Neill aliandika hili kuwabeza watu fulani; “Watu wanaokunywa maji kutoka kwenye vifaa visivyo vya kuwekea maji kama chupa za malimau ni wanyama.”

Huyu ndiye binti ambaye siku baba yake alipofutwa, samahani, alipojifuta kazi, alichukua off (mapumziko) kazini kwake, na nadhani ndipo akaanza kufanya mashambulizi ya uhakika.

Bob Diamond anaondoka, lakini huenda akapata hadi paundi milioni 30 kama mafao yake, ukichanganya hisa, mishahara na pensheni. Kashfa hii inayozungukwa na vituko vya binti huyu inahusu viwango vya riba benki zinapokopeshana kuokoana kwenye udhia.

Kimsingi zinatakiwa kulipana riba (iliyokubalia)  na Chama cha Benki cha Uingereza (BBA) na si njia za uchochoroni kama walivyofanya Barclays. Inaaminika zipo benki nyingine zinazofanya hivyo.

Kibaya zaidi ni kwamba imeelezwa palikuwa na maagizo kutoka ngazi za juu Benki Kuu na serikalini, kupanga riba hizo wanavyotaka wakubwa badala ya kufuata utaratibu uliowekwa.

Hii ndiyo sababu wanasiasa nao wameingizwa humo, wakinyoosheana kidole huku binti wa mkurugenzi akinunua kesi ya baba yake, na ngoja tuone ataishiaje.

Ngoja nikadundulize nilichovuna kazini kwenye akaunti yangu Barclays, maana vita ya wakubwa na binti huyu hainiathiri mimi katika amana yangu.

[email protected]


By Jamhuri