“K

una namna tatu za kuendeleza usawa (Ujamaa) zaidi nchini mwetu. Kwanza ni kupunguza tofauti ya kipato baina ya watu. Ya pili ni jinsi huduma (afya, elimu nk) za jumuiya zinavyomfikia kila mtu, na kiasi ambacho huduma hizo ambazo hugharamiwa kwa kodi za wote, zinawafaa watu wote, na siyo kikundi cha watu wachache tu. Na ya tatu ni wananchi kushirikishwa katika uamuzi.”

 – Mwalimu J. K. Nyerere – Miaka 10 ya Azimio la Arusha.

Wakati Tanganyika inapata Uhuru mwaka 1961, nchi ya Malaya ilikuwa tayari ina uhuru miaka minne kabla, ikipata uhuru wake mwaka 1957. Malaya ilijiunga na Singapore, Sabah na Sarawak Septemba 16, 1963 kuunda nchi ya Malaysia. 

Tanganyika ilijiunga na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania miezi saba baadaye. Hata hivyo, Singapore ilifukuzwa kutoka katika Muungano wa Malaysia mwezi Agosti 1965 kutokana na kutofautiana kwa sera kuhusu watu wa asili na namna ya kuwalinda kiuchumi. 

Viongozi wa Kuala Lumpur walitaka kuweka sera za kusaidia wazawa kwa kuwapa upendeleo maalumu wakati viongozi wa Singapore, chini ya Lee Kuan Yew, walitaka kuwepo na Malaysia moja kwa wote bila upendeleo maalumu kwa Bumiputera (watu wa asili wa taifa hilo). Singapore ina wakazi wengi zaidi wahamiaji kutoka China, hivyo ilipinga wazo hilo na ikajitoa kwenye Muungano. Tanzania imeendelea kudumu na Muungano licha ya changamoto kadhaa zinazoukabili muungano wetu.

Tanzania na Malaysia zote zilitawaliwa na Mwingereza. Wakati Tanzania inaundwa mwaka 1964, pato la wastani la mtu mmoja lilikuwa dola za Marekani 63 (shilingi Laki moja na elfu thelathini), wakati Malaysia ilikuwa na pato la dola za Marekani 113 (shilingi laki mbili na nusu). Kimsingi, nchi hizi zilikuwa sawa kimaendeleo ingawa Tanzania ni kubwa kwa zaidi ya mara tatu ya Malaysia. 

Hivi sasa Malaysia kipato cha wastani cha mwananchi ni dola za Marekani 10,000 (shilingi milioni 22) na Tanzania ni dola za Marekani 600 (shilingi milioni 1.3). Kwa Tanzania pato la wastani limeongezeka mara kumi takribani na kwa Malaysia limeongezeka mara elfu moja. Nini tofauti ya mikakati ya maendeleo ya nchi hizi mbili?

Leo tutaangalia eneo moja tu la kilimo na namna kilimo kilivyoweza kuivusha nchi ya Malaysia na kilimo hicho hicho bado hakijaweza kuivusha Tanzania. 

Malaysia iliunda Shirika la Umma linaloitwa Federal Land Development Authority (FELDA) likiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha wananchi maskini wanapata ardhi, wanalima kisasa na kuongeza uzalishaji kisha kufuta umasikini.

Kila mwananchi maskini aligawiwa ardhi yenye ukubwa wa hekta 4.1, ardhi husika ikasafishwa na kuwekwa miundombinu yote muhimu ya kilimo, ikapandwa michikichi na mwananchi akapata huduma za ugani ili kukuza michikichi hiyo. 

Shughuli zote hizi zilifanywa kwa gharama za Serikali na wananchi wale wakapewa kama mkopo ambao walikuwa wanaulipa kidogo kidogo kila wanapovuna na kuuza migazi/mawese kwa Shirika hili la Serikali. Hivi sasa Shirika hili ni kubwa sana, lina thamani ya dola za Kimarekani bilioni 3.5 (takribani shilingi trilioni 7.7) na kupitia Ushirika wao wananchi hawa waliopewa ardhi ya kulima michikichi sasa wanamiliki asilimia 20 ya hisa za Shirika hilo.

Malaysia iliweza kuondoa umaskini kutoka asilimia 57 ya wananchi wanaoishi kwenye dimbwi la umaskini mwaka 1965 mpaka chini ya asilimia 3 mwaka 2012. FELDA sasa ni Shirika la kimataifa maana linaanza kuwekeza duniani kote. FELDA ilipouza hisa zake kwenye masoko ya mitaji, IPO (mauzo ya hisa hadharani kwa mara ya kwanza) yake ilikuwa ni ya tatu kwa ukubwa baada ya makampuni ya Facebook na Japanese Airlines.

Shirika la Umma linalomilikiwa na Serikali, wakulima na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (EPF) na linaloendeshwa kwa misingi ya utawala bora wa makampuni limeweza kufuta umaskini kwa zao moja tu la michikichi. Malaysia leo inaongoza kwa kuuza mawese duniani. Michikichi hiyo ilitoka Kigoma, Tanzania na kupelekwa Malaya na Waingereza kwenye miaka ya 1950.

Tanzania nasi tulikuwa na shirika la umma kwa ajili ya kilimo. Leo tuchukulie Shirika la Chakula na Kilimo-NAFCO. Kama FELDA, NAFCO walichukua ardhi kubwa maeneo kadhaa nchini. Tofauti na FELDA, wao NAFCO walilima wenyewe mashamba haya na kuweka miundombinu ya kilimo. Tuchukue mfano wa mashamba ya mpunga kule Kapunga, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya. Mwaka 1985, NAFCO walikwenda kijijini Kapunga kuwaomba wananchi wawape ardhi ya kulima mpunga. Wananchi wakawapa hekta 3,000 hivi kwa mujibu wa muhtasari wa Mkutano Mkuu wa Kijiji niliooneshwa mwaka 2009 nilipokwenda kutembelea mashamba haya kufuatia mgogoro wa ubinafsishaji.

NAFCO wakapata msaada kutoka Serikali ya Japan na uwekezaji mkubwa ukafanyika ikiwamo kuweka kinu cha kukoboa mpunga cha kisasa kabisa. Hata hivyo, NAFCO ilijiendesha kwa hasara (kwa sababu ambazo sitazieleza kwenye makala hii) na ilipofika katikati ya miaka ya 1990 ikaamuriwa kubinafsishwa. NAFCO ikauza mashamba yale kupitia Mpango wa Ubinafsishaji kwa Kampuni Binafsi. Katika uuzaji huo NAFCO waliuza hekta 3,500 badala ya 3,000 walizopewa na wananchi. Kwa maana hiyo Kijiji cha Kapunga nacho kiliuzwa.

Mifano hii miwili inaonesha tofauti kubwa za kifikra, kimaendeleo kati ya nchi zetu hizi mbili. Moja iliwezesha wananchi kumiliki ardhi na imefanikiwa. Nyingine iliamua kufanya kupitia shirika la umma na baada ya kushindwa, badala ya kurejesha ardhi kwa wananchi na kuwawezesha kulima, ardhi ile ikauzwa kwa kampuni ya mtu mmoja. 

Ujamaa wa Malaysia ulikuwa ni wa kumilikisha wananchi wao ardhi na kuwawezesha kuzalisha. Ujamaa wetu ulikuwa ni wa kumiliki kwa pamoja na faida ya mavuno kufaidisha wananchi wote. Njia iliyotumika Malaysia ilifanikiwa, njia yetu (kwa sababu ya ufisadi na kukosekana uwajibikaji) haikufanikiwa. Badala ya kuboresha kwa kujaribu njia ya kijamaa ya Malaysia tuliona ni bora kufuata njia ya kibepari ya kugawa ardhi hovyo kwa wakulima wakubwa wachache na kuwaacha wananchi wetu wakiwa mafukara kabisa. 

Jambo hili ni mfano hai kabisa wa miaka 25 ya kulitupa Azimio la Arusha na kuacha sera za kijamaa zilizolinda usawa wa kiuchumi kwa raia wote. Hivyo, juhudi za ACT-Wazalendo za kuhuisha Azimio la Arusha kupitia Azimio la Tabora na kutangaza itikadi ya Ujamaa wa Kidemokrasia, ni juhudi za kuungwa mkono na kila Mtanzania anayetaka maendeleo ya nchi hii.

MUHIMU: Machi 25 ACT-Wazalendo tutaadhimisha miaka 50 ya Azimio la Arusha kwa kufanya mkutano maalumu wa kidemokrasia jijini Arusha. Katika mkutano husika, mijadala juu ya nafasi ya Ujamaa wa Kidemokrasia duniani itafanyika na pia tathmini juu ya miaka 25 ya Azimio na Ujamaa pamoja na miaka 25 bila Azimio na Ujamaa itachambuliwa. Masuala mengi ya namna hii yanatarajiwa kujadiliwa. Karibuni sana.

 

Mwandishi wa makala hii ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge (Kigoma Mjini) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

By Jamhuri