Madini yatishia amani Morogoro

Wananchi wa Kitongoji cha Epanko ‘A’, Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku wakilalamikia utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa madini ya graphite kwamba haukuzingatia mambo mengi yanayohusu maisha ya walengwa.

Baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho wameyakimbia makazi yao kutokana na kutishiwa maisha. Wakazi hao wanatafutwa na Jeshi la Polisi kutokana na kile kinachoitwa wamekuwa wakipinga kutekelezwa kwa mradi huo.

Wakizungumza na JAMHURI hivi karibuni, baadhi ya wananchi hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini, wanasema kumekuwa na ukiukwaji wa taratibu za kupata ardhi ya kijiji.

“Katika hali ya kawaida mwekezaji anapohitaji ardhi ya kijiji, anatakiwa kupitia ngazi zote. Kunakuwa na kikao cha Serikali ya Kijiji na baadaye mkutano mkuu wa kijiji. Serikali ya kijiji ilikaa na kuitisha mkutano mkuu wa kijiji ambao wananchi wengi walikataa kutokana na hoja za msingi kutojibiwa,” anasema mmoja wa wananchi hao.

Sehemu ya malalamiko ya wananchi hao ni pamoja na mradi huo wa uchimbaji graphite, kutozingatia suala la uharibifu wa mazingira. Wananchi hao wanasema kwamba eneo la mradi katika Kitongoji cha Epanko ‘A’, litatekelezwa katika eneo lenye chanzo cha maji yanayotumiwa na wananchi wa Ulanga.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti la JAMHURI limezipata, Januari 6, 2014 Kampuni ya Kibaran Resources Limited ilichapisha kwenye tovuti yao kuwa imepata kibali rasmi kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kufanya utambuzi wa athari za kimazingira katika mradi wa uchimbaji graphite huko Epanko, Ulanga, Morogoro.

Taarifa zaidi zinasema kandarasi ya kufanya utambuzi wa athari za mazingira ilikabidhiwa kwa kampuni ya ushauri ya MTL Consultant Company. Kumekuwa na wasiwasi mkubwa kutoka kwa wananchi endapo vigezo vya athari za mazingira vilifuatwa.

Septemba 30, 2014 Kampuni ya Kibarani Resources Limited ilichapisha tena kupitia tovuti yao kuwa imefikia hatua muhimu na za mwisho za utambuzi wa athari za kimazingira kwenye mradi wa uchumbaji madini ya graphite.

Kampuni hiyo ilitoa taarifa kwenye mtandao, Mei 2, 2015  kuwataarifu watu kununua hisa za mgodi wa graphite ulioko Epanko. Taarifa hiyo ilieleza kwamba kampuni iko mbioni kupata leseni ya uchimbaji wa madini.

Baada ya taratibu zote hizo mpaka matangazo kuwa zimekamilika, kampuni ya Kiberan Resources Limited ilitangaza mkutano wa wananchi wa dharura Agosti 20, 2015. Mkutano huo ulikataliwa na wananchi, uliahirishwa na kupangwa kufanyika Agosti 25, 2015 huku vikitolewa vitisho kadhaa kutoka kwa wawakilishi wa kampuni.

“Kulikuwa na vitisho kutoka kwa John Bosco, kwa kusema kama wananchi hawatakubali kufika kwenye mkutano atakuja na polisi ili afanye kazi hiyo ya utambuzi wa kaya siyo uelemishwaji wa athari za kimazingira,” wanalalamika wananchi hao katika sehemu ya taarifa yao.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilifanya sensa ya makazi na uhakiki wa mali za wananchi. Kinachoendelea kugomba mpaka sasa ni mrejesho wa kazi ya uthamini iliyofaywa na kampuni ya MTL kuhusu athari za kimazingira na kijamii za mradi wa graphite.

Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Steven Kebwe, ambaye ametuhumiwa na wananchi hao kuwatisha kwa maneno kwamba ‘risasi ikishatoka kwenye bunduki haiwezi kurudi’ anasema, maneno hayo aliyatoa kweli, lakini hakulenga kuwatisha wananchi hao na badala yake alilenga kuwaambia mradi lazima uendelee na hakuna wa kuukwamisha.

“Nilikwenda kwenye eneo la mradi kwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini, ambaye aliniletea ujumbe kuhusu mgogoro huo. Kikubwa hapa ni kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili waelewe faida za kuwapo kwa mradi huo,” anasema Dk. Kebwe.

Mkuu huyo wa mkoa anasema baada ya kuona kumekuwa na pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kitongoji cha Epanko ‘A’, aliamua kuunda kikosi kazi maalumu chenye wajumbe 12, wanne kutoka kila kitongoji. Vitongoji vilivyohusika ni pamoja na Epanko ‘A’, Kazimoto na Itatira.

“Huu mradi una hadhi ya kitaifa, hatuwezi kurudi nyuma… wananchi wa eneo la mradi wanayumbishwa na watu watatu. Wananchi hao watapatiwa huduma nzuri za hospitali, maji, shule, lakini hayo mbona hayasemwi?” anasema Dk. Kebwe.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga, anasema kumekuwapo na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya viongozi kuhusu mradi huo bila kuzingatia maslahi ya wananchi wengi.

Mbunge huyo anasema yeye binafasi anapingana na viongozi wenzake namna wanavyoshughulikia mradi huo wa uchimbaji wa graphite. Mlinga anasema si wananchi wala mbunge aliyeshirikishwa katika hatua zote za mradi huo.

“Hata mimi nausikia tu huo mradi. Mkuu wa Mkoa (Dk. Kebwe) pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya (Mndeme ambaye sasa amehamishiwa Dodoma) wamekuwa mawakala wa mwekezaji na kusahau kabisa maslahi ya wananchi wengi… sina tatizo na mradi isipokuwa nataka taratibu zifuatwe tu,” anasema Mlinga.

Anaongeza: “Wananchi wamekuwa na wasiwasi na mwekezaji tangu hatua za awali za utafiti. Nilimwandikia barua Waziri Mkuu kuhusu wananchi wangu kutishwa… wanabambikiziwa kesi zisizokuwa na msingi wowote na wanaachiwa.”

Mlinga anasema kutokana na historia mbaya iliyojitokeza sehemu mbalimbali nchini yanapogundulika madini, yeye ameamua kuungana na wananchi katika kuhoji, mambo muhimu, kama wakiondolewa kwenye maeneo yao watakwenda wapi? Huduma za afya pamoja na shule zitakuwaje?

Wananchi hao pamoja na mbunge wao, wanajenga hoja kutoka kwenye sheria ya mazingira ya mwaka 2004 (Act No. 20 of 2004) ambayo inasisitiza kufanyika kwa tathmini ya athari na madhara ya kimazingira na kijamii katika miradi mikubwa na midogo ambayo inatafsiriwa  kwenye kanuni na taratibu za tathmini za mazingira ya mwaka 2005.

Hivyo, ili kutekeleza sheria hii kuna ulazima mkubwa wa kuhusisha wananchi/jamii husika kama inavyoelekeza sheria ya mazingira kifungu namba 17 sambamba na hatua nzima ya utathmini wa kimazingira na kijamii amabao unaendelea.

Kifungu cha 17, kifungu kidogo namba 2 cha sheria ya mazingira ya mwaka 2004, kinaweka wazi kuwa ni muhimu kupata mawazo ya jamii husika katika mradi na tathimini. Mmiliki wa mgodi anatakiwa kutoa taarifa za madhara na faida za mradi huo kwa wanajamii husika ambayo itaathirika na mradi huo.

Kifungu Na. 17 na kifungu kidogo Na. 2a (ii) kinaeleza kutoa taarifa za wazi kwenye gazeti linalopatikana nchini kote kwa muda wa wiki mbili mfululizo.

Kifungu kidogo 2a (iii) kinaelekeza kutangaza taarifa za mradi huo kwa lugha zote mbili yaani Kiswahili na Kiingereza katika vyombo vya habari vya radio ambazo zinasikika nchi nzima angalau mara moja kwa wiki mbili mfululizo.

“Matakwa hayo ya kisheria hayakufanyika kabisa katika kuanzishwa kwa mradi huo wa graphite, badala yake kumekuwa na vitisho kwa wananchi tu. Hizi sheria zilitungwa na kupitishwa ili zifuatwe,” anasema mmoja wa wananchi waliozungumza na JAMHURI.

 Wananchi hao wanahoji kwa nini Baraza la Mazingira Tanzania halijaona au kujua taratibu zozote za utambuzi wa athari za kimazingira kuwa hazikufuatwa? Taarifa ya mrejesho wa tathmini za kimazingira kuhusu mradi wa graphite mbona hazipo wazi kwa wananchi na pia mtandao wa Baraza la Mazingira?

Hali iliyoshuhudiwa na JAMHURI Serikali Kuu inapaswa kuingilia kati tatizo hili na kulipatia ufumbuzi wa haraka, kwani kasi inayoendelea inaweza kuzaa uvunjifu wa amani.