Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) unadaiwa kukwepa kulipa kodi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kiasi cha Sh bilioni 38.2 tangu mwaka 2007 hadi 2013.

Mgodi huo umekumbwa na kashfa hiyo baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubainisha ‘madudu’ hayo katika taarifa yake ya mwaka 2011/2012 iliyojadiliwa Julai 24, 2013 na Baraza la Madiwa wa Wilaya ya Geita.

 

CAG anabaisha kuwa kodi hizo zilitokana na mgodi huo kukataa kulipa dola za Kimarekani 1,400,000 (sawa na Sh 2,208,654,000) zikiwa ni deni ambalo GGM wanadaiwa na halmashauri kama malimbikizo ya kodi za Serikali tangu mwaka 2005 hadi 2009, ambapo mgodi huo unatakiwa kulipa dola za Kimarekani 200,000 kwa halmashauri hiyo kila mwaka.

 

Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliandika barua yenye Kumb. Namba GDC/F.10/64/17 ya tarehe 24/09/2012 kwenda GGM kudai malipo hayo  lakini mgodi haujalipa hadi sasa.

 

“Kwa vile M/S Geita Gold Mine haijatekeleza majukumu yake kulingana na makubaliano yaliyofikiwa tarehe 24 Juni, 2009, GGM inatakiwa kulipa riba,” inasema sehemu ya taarifa ya CAG.

 

CAG anapendekeza kuwa juhudi zaidi zinatakiwa ili kiasi hicho cha fedha kilipwe pamoja na riba yake huku akipendekeza hesabu zirekebishwe kulingana na viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (International Public Sector Acounting Standards-IPSAs) ili kupata picha yenye uhakika.

 

Pia CAG amesema mgodi huo umekataa kulipa Sh 36,067,000,000 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuanzia mwaka 2007 hadi sasa.

 

Mabilioni hayo ni kwa ajili ya ushuru wa utafutaji na  uchimbaji wa dhahabu katika hifadhi ya msitu wa akiba wa Geita, kwa mujibu wa sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002, kanuni namba 29 (1) na marekebisho ya kanuni za misitu mwaka 2011.

 

“Wakati wa ukaguzi tumebaini kuwa Hati ya Madai Namba 293642 ya tarehe 04/06/2012 iliyotolewa na Afisa Misitu wa Wilaya ya Geita na kupelekwa kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa GGM Ltd, kupitia S.L.P. 532, Geita.

 

“Hati ya madai vilevile inakumbushiwa na kusisitizwa kwa barua kumbukumbu namba GDC/23/3/VOL.II/157,” anasema CAG.

 

Kodi hiyo ambayo GGM imekataa kulipa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita inatajwa na CAG kama ifuatavyo kulingana na sheria ya misitu: Kuwa mwaka 2007 hadi 2010 zilipwe Sh 6,000,000 kwa miaka minne, ambayo GGM imekuwa ikifanya shughuli zake ndani ya msitu wa akiba na baada ya kanuni kuanza kutumika mwaka 2007, Sh 1,000,000 kila mwaka kwa Special Mining Licence (SML), Sh 500,000 kila mwaka za Prospecting Licence (PL).

 

Mwaka 2011 na 2012 walipe Sh 36,067,000,000 kulingana na kanuni za misitu zilizorekebishwa mwaka 2011 ikiwa ni Sh 1,000,000 kwa kila mwaka kwa hekta. Msitu wa akiba wa Geita huko kwenye hekta 15166 katika SML, yaani kodi ni jumla ya Sh 30,332,000,000 jumlisha hekta 5735 chini ya Prospecting License jumla ya Sh 5,735,000,000.

 

“Kwa nyongeza, ukaguzi unasisitiza kuwa riba na adhabu za kibiashara zilitakiwa zifanyiwe hesabu na zitumike kutokana na ucheleweshaji wa kulipa na kuwasilishwa kwa kiasi hicho katika halmashauri,” inasomeka sehemu nyingine ya taarifa ya CAG.

 

CAG anasema, “Kupitia barua ya tarehe 27 Juni, 2012, tumebaini kuwa GGM haitaki kulipa bill hii.”

 

Afisa Uhusiano wa mgodi huo, Joseph Mangillima, alipoulizwa na JAMHURI amesema taarifa hizo si za kweli, lakini alipotakiwa kutoa msimamo wa mgodi huo kutotambua taarifa ya CAG kwa madai kuwa ni uongo, alisema kwamba aulizwe mtu wa idara ya kodi mgodini.

 

“Hebu mtafute mtu wa idara ya kodi wa GGM anaweza kukusaidia,” alisema Mangillima.

 

Mgodi wa Dhahabu wa Geita unalalamikiwa na wananchi wengi wanaouzunguka kwa kutowatendea haki katika huduma mbalimbali za kijamii kama elimu, barabara, afya, maji na uhusiano mzuri.

 

Hivi karibuni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alitembelea mgodi huo na kusikiliza malalamiko ya wananchi ambao mgodi uliwahamisha katika mshamba yao ukaanza uchimbaji lakini umekataa kuwalipa fidia hadi sasa.

 

1189 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!