Msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, amewalaani watu wanaofanya biashara ya kuuza dawa za kulevya nchini, akisema wanaharibu maisha ya vijana wengi.

Ray C, aliyewapata kuwika kwenye anga ya muziki wa kizazi kipya katika miaka ya nyuma na baadaye kupotea katika ramani ya muziki  huo kutokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, amesema kuwa wafanyabiashara hiyo wanapunguza kasi ya maendeleo kwa vijana wengi hapa nchini.

 

Msanii huyo ambaye kwa sasa anapata matibabu na ushauri nasaha dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, alikuwa akizungumza katika kipindi maalum kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds FM cha jijini Dar es Salaam.

 

Alisema kwamba alijikuta ameingia katika dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya baada ya kushawishiwa na rafiki yake.

 

“Mimi mwenyewe sikupenda kutumia dawa hizo ila nakumbuka nina rafiki yangu mmoja niliyekuwa naye kwa karibu sana, ndiye aliyenishawishi kijanjakijanja mpaka nikajikuta nimeanza kutumia.

 

“Nilikuwa naye kwa karibu sana si unajua, wakati mwingine ananipa sigara nivute kumbe kachanganya kwenye hiyo sigara, ila iliniuma sana kwani baadaye alikuja kuniambia ukweli kuwa zile sigara alizokuwa akinikipa zilikuwa na kitu ndani yake,” alisema.

 

Kwa sasa msanii huyo anapata tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Tiba hiyo muda wake ni miaka miwili ila yeye ana miezi sita tangu aanze kuipata bila malipo hapo Muhimbili na Mwananyamala, Dar es Salaam.

 

Alisema kwa sasa anaendelea vizuri na ana imani kuwa atapona na kurejea katika fani yake ili kuwapa burudani wapenzi wa muziki wa kizazi kipya.

 

“Nawapenda wanaopenda muziki wangu kwani bila wao mimi nisingeweza kuwa Ray C, nawaahidi kuwa kwa sasa nakuja upya na nina imani watafurahia ujio wangu mpya,” alisema.

 

Aidha, alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu wanaouza dawa za kulevya kutumia njia za kuwashawishi wasanii wazitumie ili waweze kuvuna pesa zao kwa njia hiyo.

 

“Kuna watu wanaona msanii kapanda stejini muda mfupi kapata hela zake nyingi tu, sasa wanataka kuzipata kupitia biashara yao ya dawa hizo, na ndipo wanapoanza kumshawishi ili atumie na hatimaye anakuwa mteja wao,” alisema.

 

Alisema kuna idadi kubwa ya watu ambao kwa sasa wanatumia dawa za kulevya. “Kuna wengine wanavaa suti lakini akijipinda kona wanatumia, wengine vijana wadogo, wanamuziki ndiyo usiseme, nina orodha kubwa sana ya wanamuziki wanaotumia. Kwa kweli matumizi ya dawa yapo kwa watu wengi sana,” alisema.

 

Ray C hakusita kukumbuka maisha yake ya awali kabla ya kutumia dawa za kulevya. “Nakumbuka maisha yangu yalikuwa mazuri sana, nilianza kufanya kazi nikiwa na umri wa miaka 17, nikaanza kujenga nikiwa na miaka 22, sasa inakuwaje sasa hivi eti mimi Ray C nakufa kwa matumizi ya dawa za kulevya, naomba Mungu anisaidie na nimekuwa nikiomba sana juu ya hili,” alisema.

By Jamhuri