Katika toleo lililopita sehemu ya kumi na moja tuliishia katika aya isemayo: “Noel, mimi ninaona utafanya mambo makubwa, wala usikate tamaa,” alisema profesa. Noel alikuwa amekaa kwa huzuni akiwa na mawazo tele, maana alikuwa akifikiria kuhusu umaskini aliouacha Tanzania. Umaskini ulikuwa ukimpa fikra nzito, hasa hali aliyokuwa ameiacha katika familia yake. Sasa endelea…

Wakaingia katika barabara za mji wa Moscow, Noel alikuwa akifurahia mazingira aliyokuwa anayaona katika Jiji la Moscow. “Mmh! Ila huku pazuri, si kama Tanzania,’’ Noel alikuwa akiwaza mwenyewe akilini mwake huku akiwa anatazama dirishani, shingo akiwa ameigeuzia kwenye dirisha. Profesa alikuwa akiendesha gari ili kuwahi chuoni.  

“Noel unatazama nini nje?’’ aliuliza profesa. “Ninaangalia namna Moscow kulivyo kuzuri tofauti na Tanzania,’’ alisema. Akiwa anaangalia barabarani, aliona askari wa barabarani wakiwa hawapo, taa pekee za barabarani ndizo zilikuwa ziki ongoza watu na magari. 

“Kadiri unavyokuwa ukitembea eneo moja kwenda jingine kuna mabadiliko,’’ alisema profesa. “Ni kweli,’’ alizungumza Noel, lakini macho yake yalikuwa nje bado akitazama huku na kule. Mandhari ya mji ilikuwa ikimvutia. 

“Noel, Mungu akusaidie uweze kuishi huku,’’ alisema profesa akiwa anamaanisha. “Mimi mwenyewe ninatamani iwe hivyo pia,’’ alisema. Mji wa Moscow ulikuwa ukimvutia Noel, asilimia kubwa ya watu aliokuwa akiwaona walikuwa ni Wazungu.

Meninda baada ya kufika ofisini na kufanya majukumu yake akatoka, akiwa anatoka mwenzake waliyekuwa wote ofisini akamuuliza: “Unakwenda wapi Meninda?’’ Meninda alimjibu: “Ninakwenda ofisini kwa….wa jarida,’’ mwenzake alimruhusu. 

Ulikuwa ni mwendo wa dakika tano, Meninda akafika akafungua mlango na kumkuta yule mtu aliyekuwa akihusika na jarida la wakimbizi akiwa amekaa peke yake ofisini. 

“Meninda karibu, halafu nilikuwa nimesahau.” Meninda akakaa kisha wakaanza kuongea: “Sasa tusipoteze muda, nina kijana nyumbani ametoka Afrika, ni mwandishi mzuri, hauwezi kumpa nafasi katika jarida letu hapa?’’ aliuliza Meninda huku akimtazama yule mtu. 

“Nimsaidie vipi?’’ aliuliza yule mtu kwa maana Meninda alikuwa hajatoa maelezo yanayoeleweka kwake. “Awe anaandika makala kuhusu wakimbizi hususan Afrika, atakuwa anatusaidia maana ndiko alikotokea,’’ alisema Meninda akiwa anaweka ushawishi mkubwa kwa yule mtu.

“Sawa, itabidi niongee na jopo la wahariri wetu, je, alikwisha kufanya au kuandikia sehemu yoyote ile?’’ Meninda alimjibu na kumwambia: “Ndiyo, alikuwa nchini Tanzania na alikuwa akiandikia magazeti ya huko.” Yule mtu ambaye alikuwa ni raia wa Marekani lakini alikuwa akiishi hapo Moscow, alimuuliza tena Meninda: “Huku Moscow amefuata nini?” Meninda akaendelea kumuweka bayana: “Amekuja kusoma shahada yake ya kwanza ya uandishi wa habari.” Yule ‘bosi’ akahamasika: “Safi, tunaweza kumpa ajira pia akawa ‘reporter’ wetu kisha tukamlipa.’’ Meninda aliposikia hivyo, alitamani iwe vile.

“Sasa lini mtakutana na hao wahariri?’’ aliuliza Meninda akiwa anataka uhakika. “Ninafikiri kesho njoo na hayo magazeti yake.” Meninda alijua wazi hilo litakuwa suala jepesi. “Ila leo hii nitaongea nao tuone,’’ alisema. Walipomaliza kuzungumza Meninda akasimama na kuanza kuondoka huku akiweka matarajio ya kufanikisha kile alichokuwa anakitaka. 

***

Profesa aliendesha gari, hatimaye alifika eneo la chuo, akaegesha gari lake. “Sikiliza Noel, twende kwanza ofisini kwangu nikasaini,’’ alisema profesa huku akiwa amesimama na kushikilia funguo za gari lake. 

“Sawa, profesa,’’ alikubali Noel, wakaambatana hadi ofisini kwa profesa. Noel akaingia, macho yake yalikuwa yakiangaza huku na kule.

“Karibu Noel,’’ alisema profesa huku akienda kukaa katika kiti chake. Noel akabaki amesimama. Profesa akamuelekeza akae katika kiti. “Noel kaa hapo, ninasaini kisha tutaondoka.”’ 

Noel akakaa profesa akasaini katika ofisi yake kisha akampa katibu wake. “Naondoka ninakuja mara moja,’’ alisema profesa akiwa anamwambia katibu wake. 

“Sawa profesa, kuna watu walikuwa wana shida na wewe pia.’’ Profesa akaangalia saa yake ya mkononi kisha akamwambia: “Wakija waambie baada ya dakika arobaini nitakuwa ofisini.’’ Alisema maneno hayo machache kisha wakatoka nje na kwenda katika jengo la utawala.

Katika jengo la utawala ndipo kulifanyika mambo yote yaliyokuwa yakihusu chuo. Profesa alipokuwa akitembea na Noel, Noel alikuwa akifurahia mandhari ya chuo, alikuwa akiona ghorofa ndefu zilizokuwa zimekwenda juu. 

“Na hizi ghorofa?’’ aliuliza Noel. “Hizo ghorofa ni madarasa ya wanafunzi na hostel.” Noel macho yalikuwa haya banduki katika kuziangalia zile ghorofa na mandhari ya pale chuoni.

Chuo kilikuwa na mandhari nzuri na ya kisasa. Wakafika kwenye jengo na kusimama kusubiri lifti. Noel alikuwa akiangaza macho yake huku na kule, punde lifti ikafika wakaingia ndani.   Lifti ilikuwa nzuri kwa ndani, Noel akatikisa kichwa chake, maana hakuzoea kuona vitu kama vile. 

“Noel usishangae, ndiyo chuo hiki, ukifaulu utakuwa ukisomea hapa,’’ alisema profesa huku akiwa anatazama chini. Profesa alikuwa mtu mwenye utu kwa watu. 

“Sawa profesa,’’ aliitika Noel kwa upole. Noel alikuwa akidadisi kuhusu maisha ya chuo kile. Kwenye lifti hawakuwa yeye na profesa pekee, kulikuwa na watu wengine pia ambao walikuwa ndani ya lifti hiyo. “Mbona kila tunapopita ni Wazungu!’’ aliwaza Noel. 

Tangu alipopita hakuonana na mtu mwenye rangi sawa na ya kwake. Wakafika ghorofa ya juu lifti ikasimama. Profesa na Noel wakatoka ndani ya lifti wakaingia katika sehemu iliyokuwa na mlango wa kioo. Walipofika karibu mlango ukajifungua wenyewe, Noel akabaki kuduwaa. “Mmmh! Hii teknolojia mbona kubwa sana?’’ Noel alikuwa akijiuliza mwenyewe moyoni.

***

Wakaingia na kumkuta Mzungu mmoja akiwa amekaa kwenye kiti cha kifahari. “Habari yako?’’ alisema profesa huku akiwa anampa mkono yule Mzungu mwenzake.  

“Salama profesa, za siku?’’ alionekana kumchangamkia profesa. Noel alijua pasi na shaka watakuwa wakifahamiana. “Nzuri, naona uko na kijana,’’ alisema profesa huku na yeye akiwa mwenye tabasamu lisilokuwa na kifani. “Ndiyo profesa,’’ alijibu yule Mzungu akiwa amekaa katika kiti. Profesa pasipokupoteza muda aliuliza:

“Hivi mitihani kwa watu wa mchujo wa Shahada ya Mawasiliano na Habari ni lini?” Yule Mzungu aliyekuwa amekaa kwenye kiti ndiye alikuwa akishughulika na mambo yote ya hiyo mitihani ya majaribio. 

“Kwani upo kwenye baraza hilo?’’ aliuliza yule Mzungu. Profesa akamjibu kwa kumwambia ukweli. “Nilikuwa na kijana wangu huyu hapa anatoka Afrika.’’ Alipozungumza vile mara yule Mzungu akaelekeza macho kwa Noel. 

“Anaitwa nani na ametoka taifa gani Afrika?’’ aliuliza. Profesa akawa na haraka kumtajia: “Anaitwa Noel, anatoka Tanzania.” Mzungu yule akapekua katika tanakilishi yake kisha akalikuta jina hilo.

“Ndiyo, yupo Noel Daniel kutoka Afrika nchini Tanzania.’’ Ikampa hamasa Noel baada ya kuona alikuwa akitambulika. “Mtihani ni juma lijalo, utakuwa wa kawaida tu, hapa ninaona amekidhi vigezo vyetu, ila ajitahidi na mtihani afaulu atapata nafasi,’’ alisema.

Profesa alishukuru kwa kuweza kupata taarifa zile zilizokuwa njema. “Asante sana,’’ Mzungu mwenzake profesa aliitikia. “Sawa profesa, naona hata hivyo kijana amejaza Shahada ya Mawasiliano na Habari, anataka kuwa mwanahabari mzuri,’’ alisema. 

Wakacheka kwa upendo, kisha wakapeana mikono na profesa akaondoka akiwa na Noel, wakasimama kusubiri lifti huku wakiwa wanaongea. 

“Noel umesikia lakini?’’ aliuliza profesa. Noel akaitikia: “Nimesikia profesa.’’ Profesa akaendelea kumtia moyo Noel.

Wakati profesa akiwa amesimama na Noel wakingoja lifti, mara akapita binti mmoja raia wa nchi ya Jamaica aliyekuwa akisoma katika chuo hicho. 

Alikuwa akisoma kitivo ambacho profesa alikuwa akifundisha. Akamuona profesa na kusalimiana naye. “Profesa habari?’’ Profesa akaitika: “Nzuri Penteratha.’’ Profesa alikuwa akimfahamu, maana alikuwa amemkariri jina lake.

Penteratha alikuwa anapenda sana kuandika riwaya ambazo zilikuwa zikilenga ukombozi wa fikra kwa Waafrika ulimwenguni. 

Alikuwa amefanikiwa kuchapisha riwaya mbili, alikuwa ni ‘Mwafrikasti’ kutoka Jamaica. Baba na mama yake walikuwa na asili ya Afrika. Babu zake wa pande zote mbili kwa baba na kwa mama walikuwa na asili ya Ghana. 

“Profesa, ninataka kuzindua riwaya yangu nyingine,’’ alisema Penteratha. Profesa akacheka na kumpongeza:  “Safi sana, halafu imekuwa bahati pia huyu kijana ni Mwafrika, naye ni mwandishi mzuri,’’ alisema profesa akiwa anawakutanisha vijana hao wawili. 

“Aisee! Anasoma hapa?’’ alionekana Penteratha kumchangamkia Noel huku wakipeana mikono.  “Hapana, ndiyo amekuja kufanya mtihani wa majaribio, endapo atapita atakuwa akisoma hapa,’’ alisema profesa. 

“Mungu atakusaidia Noel,” aliongea kwa tabasamu la upole. “Asante na itakuwa hivyo,’’ alisema Noel ambaye pia alikuwa na furaha ya kukutana na mtu mwenye rangi sawa na ya kwake. 

“Unaitwa nani?’’ aliuliza Penteratha. “Naitwa Noel,’’ alijibu Noel. Ikawa furaha kwa vijana hao wawili kuweza kufahamiana. 

“Mimi ninaitwa Penteratha,” alisema. Profesa alipokuwa akiwatazama nyuso zao akagundua walikuwa na furaha halisi kutoka mioyoni mwao.

66 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!