Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Si nilikwambia mama, Noel watu mpaka sasa wanamkumbuka, nimetoka kuongea na mkurugenzi wa redio anamuulizia.’’ Mama yake akasimama na kuanza kumsikiliza Zawadi. “Heee! Si alimfukuza?’’ alishangaa Mama Noel. Tumaini lilikuwa limemjia mama yake Noel baada ya kuongea na mchungaji na kupewa mustakabali wa mipango vizuri. Mama Noel akajikuta kuhamasika Noel kwenda nchini Urusi kusoma. Sasa endelea…

“Mama, hata mimi ninashangaa imekuwaje wakati walimtaabisha Noel kipindi kile,” alisema Zawadi. Kwa namna mambo yalivyokuwa yakienda, Mama Noel alianza kuona nuru kwa mwanae ikianza kumulika. 

“Zawadi huu ni kama muujiza, inatupasa kumuombea Noel,’’ alisema mama yake Noel huku akitikisa kichwa chake. Imani na tumaini kuwa Noel anafanikiwa vilitawala katika familia yake.

Wakiwa wanazungumza ndani, nyuma ya nyumba yao wakapita vijana watatu wakawa wakiongea maneno ya ‘kusanifu’. “Nasikia tunajifanya waandishi,’’ kijana mwingine akadakia na kusema:

“Haya bhana tutakuona utafika wapi.’’ Walikuwa wakiongea wale vijana huku wakipita nyuma ya nyumba yao Noel. Mama Noel pamoja na Zawadi dada yake Noel wakasitisha maongezi yao na kuwasikiliza vijana hao ambao walikuwa hawana mafanikio yoyote katika maisha yao.

“Mama umesikia unafiki wa vijana wenzake Noel?’’ aliuliza Zawadi. Mama yake akakaa kimya kisha akamwambia: “Mwanangu nimegundua maisha ni vita na watu wapo kwa ajili ya kukatisha tamaa wengine. Kwa kuwa wanataka siku zote kutuona vile tulivyo,’’ yalikuwa maneno mazito kutoka kwa Mama Noel. 

“Lakini mama, Noel amehangaika sana hata kusoma kwake imekuwa shida, Mungu ampe wepesi tu,’’ alisema Zawadi. “Zawadi, Noel mimi ninahisi ni mbegu iliyopandwa, kuna wakati itachipua na kuonyesha mazao yake,’’ alisema Mama Noel. Ni kama nguvu fulani ya kuhamasika mchungaji alikuwa ameipandikiza akilini mwake.

Zawadi alikuwa akiwaza na kukumbuka namna Noel alivyokuwa akihangaika kipindi cha nyuma akibeba kreti za bia kupeleka dukani kwa bwana mmoja. Zawadi kumbukumbu zikamjia alipokutana na Noel akiwa amebeba kreti la bia akamsimamisha na kuanza kuongea naye: “Wewe Noel mbona kreti zito hivyo, utafika?’’

Zawadi akakumbuka aliongea kwa uchungu na alimuonea huruma Noel lakini alikuwa hana namna bali kumuacha Noel aendelee kufanya kazi kama hiyo. “Dada Zawadi niache tu, sasa nitafanyaje?’’ alisema Noel akiwa amesimama na kreti lake begani. “Haya nenda usije kuanguka hapa njiani,’’ alisema Zawadi. 

Akazidi kukumbuka Zawadi tukio hilo namna lilivyokuwa na uchungu alioupata kwa mdogo wake Noel kisha akamwambia mama yake: “Mungu atunusuru kutoka katika janga hili la umaskini,’’ aliongea Zawadi huku machozi yakimtiririka.

Maisha wakati huo yalikuwa si mabaya kama zilivyokuwa siku za nyuma. Mchungaji alikuwa akiwasaidia lakini pia Zawadi biashara ya samaki aliyokuwa amemuachia mama yake ilikuwa ikiendelea japokuwa ilikuwa si vema sana.

“Noel amehangaika mwenyewe, Mungu alikuwa akimuona, hakuna ndugu wala mtu wake wa karibu aliyemsaidia,’’ alisema Mama Noel.  “Mungu ni mwema, lakini anawaona watu wenye nia ya kweli,’’ alisema Zawadi huku akielekea alikokuwa amekaa muda uliopita ili kuendelea kuchora picha zake za kutuma magazetini.

Zawadi alikuwa ameshaanza kufahamika kwa wahariri kadhaa wa magazeti makubwa. Akiwa amekaa akichora mara mhariri wa gazeti akampigia simu, simu ya Zawadi ikaanza kuita akaichukua akakuta ni namba ya mhariri.

Zawadi akaipokea pasipokuwa na shaka. “Wewe tuma hivyo vibonzo kesho tunavihitaji kwenye gazeti,’’ alisema. Zawadi akamkubalia na kumwambia: “Bado ninachora, ndiyo ninamalizia nitatuma kesho,’’ Zawadi alisema. 

Mhariri anamkubalia. Uchoraji wa Zawadi ulikuwa si wa kisasa, maana alitumia njia duni ambayo ilikuwa ikimpa changamoto kuweza kuwasilisha vibonzo vyake gazetini.

Muda huo wa usiku katika chuo kikuu alichokuwa akifundisha profesa, chuo ambacho Noel alikuwa amekuja kufanya mtihani wa majaribio. Usiku huu jopo la maprofesa takriban kumi na tano kutoka vitivo mbalimbali walikuwa wamekusanyika ili kuandaa mitihani ya majaribio. Zilikuwa zimebaki siku nne kabla ya mitihani hiyo kuanza.

Maprofesa walikuwa makini katika shughuli hiyo, walikuwa wakipewa majina na idadi ya watu katika kila kitivo. Profesa mmoja aliyekuwa raia kutoka nchini Ghana alikuwa rafiki yake profesa ambaye Noel alipofikia, akajaribu kuangaza huku na kule lakini hakuweza kumuona. 

“Hivi ina maana prof… hayupo hapa au hawakumuweka mwaka huu kwenye hili baraza?’’ Alikuwa akijiuliza huku akiangaza kumuona. Alipomkosa akaamua kuchukua simu yake na kumpigia.

Profesa siku zote alipokuwa akipumzika simu yake aliiacha ikiwa haijazimwa, alikuwa amelala huku simu ikiita muda wa dakika tatu akiwa hapokei. Akashituka kutoka usingizini akasikia simu ikiendelea kuita. Profesa akafikicha macho yake, hakufikiri kama ni simu ya profesa mwenzake. Alijua itakuwa simu nyingine nje ya watu anaofanya nao kazi.

Akaichukua na kuipokea kisha akaiweka sikioni: “Haloo!’’ Sauti akaifahamu kuwa ni ya profesa mwenzake. “Mbona sikuoni, hauko kwenye baraza mwaka huu?’’ Profesa baada ya kusikia hivyo akashituka: “Kwani kuna baraza la mitihani gani hapo?’’ aliuliza profesa, maana alikuwa hajui kilichokuwa kikiendelea.

By Jamhuri