Hebu leo tubadilishe upepo kidogo kwa kutafuta majibu ya kwa nini watu waovu wanaongezeka licha ya wingi wa makanisa, misikiti hata magareza? 

Kwa nini matukio ya uovu wa binadamu yanazidi licha ya juhudi kubwa zifanywazo na ulimwengu kudhibiti matukio hayo?

Inawezekana kabisa ni makosa yanayotokana na aina ya malezi ambayo watoto wanapatiwa siku hizi. Tunaambiwa kuwa taasisi ya kwanza kubwa, imara, sahihi na muhimu kuliko zote katika malezi na kumtengeneza binadamu ni familia. Huku ndiko binadamu anapoharibika au kuimarika.

Hakuna mzazi anayeharibu mtoto wake kwa makusudi. Kila mzazi angependa kuwa na mtoto mwenye maadili na tabia njema mbele ya jamii. Lakini wakati mwingine, watoto wanaharibika kupitia mikono ya wazazi ambao wanadhani wanawatengeneza kumbe ni tofauti.

Mathalani, kuna wakati wazazi huwafundisha watoto wao uongo bila kujijua. Halafu baadaye watoto hao wakianza kuwaongopea wazazi, wazazi wanabaki wakishangaa wameitoa wapi tabia hiyo ya uongo?

Kwa namna gani tunawafundisha watoto wetu uongo? Soma kisa hiki kifupi.

Alikuwepo msichana mmoja mwenye umri wa miaka sita. Siku moja kwa bahati mbaya alivunja sahani ya udongo pale nyumbani. Baada ya mama yake kurudi msichana akamwambia jambo hili bila kuficha.

Mama yake alimpiga makofi mengi sana. Mashavu yote yalipata tabu. Baada ya kipigo kile, binti yule akafahamu gharama ya ukweli.

Siku kadhaa baadaye akavunja kikombe. Mama yake aliporejea hakusema kama amevunja. Mama alipogundua akamuuliza kwa ukali: “Nani amevunja kikombe?” Akajibu: “Sijui mama, labda atakuwa paka, maana kuna muda nilimuona amepanda juu ya kabati la vyombo.” Mama hakumchapa. Binti akaonja utamu wa kusema uongo.

Ilipofika likizo nyumba ikapokea watoto wengine wa ndugu waliokuja likizo. Katika kipindi hicho kila kosa alilofanya binti alisingizia wenzake. Tangu hapo hakuona tena thamani  ya ukweli. Mara moja aliyopigwa na mama yake kwa kusema ukweli ilitosha kumfanya aamini uongo ni jambo la maana sana. Tangu binti yule aonje utamu bandia wa kudanganya hakuwahi kuamini kama ukweli humuweka mtu huru.

Kuna wakati ndani ya nia zetu nzuri tunasababisha matokeo mabaya. Hivi ndivyo wazazi wengi wanavyowafundisha watoto wao uongo bila kukusudia.

Kisaikolojia, mara baada ya mtoto kuzaliwa na kuanza kujifunza lugha kutoka kwa watu wanaomzunguka, anapofikisha miezi tisa huanza kuiga matendo kadhaa na anapofikia umri wa miezi 14 anaweza kuiga mambo na vitendo anavyoviona katika mazingira yake au kutoka katika picha, simu au runinga. Watoto hujifunza zaidi kwa kuona yanayofanyika kuliko kusikia  yanayozungumzwa.

Watoto wanaelewa mambo mengi sana tunayotenda kuliko yale tunayosema. Huwezi ukawa mzazi huendi kanisani wala msikitini halafu mtoto wako akakuelewa ukimfundisha kuhusu Mungu na dini. Hajawahi kukuona ukishika Biblia wala Quran na kusoma halafu akuelewe kuhusu somo lolote la imani.

Watoto wetu hawajawahi kufaulu somo la kutusikiliza wazazi na walezi wao kwa alama 100. Lakini hawajawahi kufeli kuiga tuyafanyayo. Usidhani utoto wake unafanya asiige chochote kwenye matendo yako. Anaiga na utakuja kuyaona kwenye ukubwa wake.

Mtu ambaye ana mtoto, anapaswa kuwa na tabia kama mtoto anapokuwa pamoja naye. Yeyote ambaye anaye mtoto, anapaswa, kwa ajili ya mafunzo yake, kujishusha mwenyewe mpaka kwenye kiwango chake cha utotoni.

Dk. Mayles Munroe anasema: “Marejeo mengi huweka wazi kuwa watoto hujifunza kila kitu wanachotaka kufunzwa katika miaka saba, kwa maana nyingine, kama haujamfundisha mtoto katika njia impasayo katika miaka saba ya kwanza na kama haujamuambukiza tabia yako, mwenendo wako na mambo yako katika wakati huo, ni vigumu sana hata neema ya Kristo isaidie baada ya miaka hiyo.”

Katika umri wa  miaka 0-11 (umri wa kupokea amri) utahisi anakuelewa sana kwa “mahubiri na  mawaidha” yako, lakini akifikisha miaka kati ya 14 na 18 (umri wa kuhoji na kuamua) hatakuwa yule uliyetaka kwa maneno yako, atakuwa yule uliyemjenga kwa matendo yako.

Ni katika kipindi hiki ndipo wazazi utawasikia wakilalamika: “Mtoto wangu amebadilika kabisa.” Hajui kuwa ni yeye ndiye aliyembadilisha kupitia matendo yake.

Lakini kiuhalisia mtoto hajabadilika. Plato anasema: “Chochote kipandwacho kwenye akili ya binadamu huota kwenye maisha yake.” Binadamu huelewa zaidi kwa vitendo kuliko nadharia, hivyo muda wote uliokuwa unamlazimisha aende kanisani au msikitini kinadharia, halafu kivitendo wewe huendi, alichoelewa ni kuwa kwenda au kutokwenda kanisani hakuna tofauti yoyote ile. Kama ingekuwa mzazi wake angekwenda, angeelewa kuwa kuna umuhimu wa kufanya hivyo. Anza kuwa wewe, vile unavyotaka mtoto wako awe.

Baba akiwa kazini anapiga simu kwa mkewe ambaye kwa wakati huo anapaswa kuwa nyumbani lakini hayupo hapo. Baada ya dakika chache za mazungumzo baba anaomba kumsalimia mtoto. Mama anamwambia mtoto wake wa kike: “Akikuuliza mpo wapi, mwambie tupo nyumbani.”

Binti anakua. Baada ya miaka kadhaa anaolewa na yeye. Mama analetewa kesi na mkwewe kwamba mwanae ni muongo sana. Anapenda kudanganya danganya. Mumewe akisafiri hatulii nyumbani, anaondoka bila kuaga halafu akiulizwa anasema yupo nyumbani. Marafiki wa mumewe wanakutana naye huko mitaani anakokuwa!

Mama anaanza kumlaumu binti yake bila kujua kuwa yeye ndiye chanzo cha tatizo lile. Ameshasahau kwamba yeye ndiye aliyemfundisha binti yake uongo. Anaanza kumsema: “Uwe na heshima kwa mume wako. Kama unataka kwenda sehemu kwa nini usiage ukasema ukweli mpaka udanganye?”

Ameshasahau kuwa alimfundisha uongo kwa vitendo. Uongo ambao unamshushia heshima yeye mwenyewe na kuhatarisha ndoa ya mtoto wake.

Muda wote uliokuwa unamfundisha asiwe mchoyo kwa maneno, alikuwa wakati ukirudi na zawadi unamfungia ndani, azitumie zawadi hizo kisha akimaliza atoke nje kucheza na watoto wenzake. Alichoelewa kupitia matendo yako ni kuwa uchoyo ni jambo bora sana.

Ulipomfundisha kuhusu heshima kwa wakubwa wakati anawaona mara kwa mara wazazi wake mkitukanana na kusutana bila staha, ameelewa hakuna sababu ya kuheshimu mtu. Haya yote ndiyo uliyoyapanda kwenye akili yake. Huja kuyatoa kuanzia miaka 14 na kuendelea.

Unadaiwa ada shuleni kwa mtoto wako nenda kalipe au nenda wewe mwenyewe kazungumze na uongozi wa shule. Si kumwambia mtoto: “Mwalimu akikuuliza mwambie baba amesafiri kaenda kwenye msiba wa babu.” Unakafundisha uongo hako kajamaa kako. Unapunguza thamani ya mtoto wako hata ndani ya nafsi yako wewe kama baba yake.

Unaweza kukaa na mtoto wako ana tabia mbaya mpaka shetani anapita pita kwenye mawazo yenu. Mtoto anawaza: “Dah, baba angekuwa Bakhresa, muda huu ningekuwa ninakunywa juice za ukwaju tu ndani ya Mark X.” Na wewe unawaza: “Dah, mwanangu angekuwa Mbwana Samatta, muda huu nipo zangu mitaa ya London.” Ukimlea mtoto wako vizuri, kila kitu kinawezekana. Anaweza kuwa Lionel Messi au Christian  Ronaldo.

Unamfundisha mtoto wako upendo wakati anakuona unavyowabagua watoto wengine wa ndugu zako na kumpendelea yeye. Hapa Unamfundisha ubaguzi na ubinafsi. Jinsi ya kumfundisha upendo ni kumtendea haki sawa sawa na watoto wengine kwenye nyumba yako.

Unamwambia mtoto fulani akija hapa mwambie sipo. Halafu akikudanganya wewe mwenyewe unamtia makofi. Namna mzazi anavyoishi ovyoovyo ndivyo anavyouambukiza u-ovyoovyo kwa mtoto wake.

Nitoe angalizo kidogo kwamba haimaniishi kuwa ukiyafanya yote yaliyoelezwa hapo juu yatakupa matokeo unayoyataka kwa mtoto wako. Unaweza kutimiza wajibu wako kwa malezi mema kama mzazi kwa asilimia 100, lakini bado mtoto wako akawa mwizi, mhuni, akapata mimba akiwa shuleni, akawa mvuta bangi na unga n.k.

Kwa sababu tu dunia haijawa sehemu iliyoshiba watu wema, ndiyo maana wenye lugha wakaiita ‘tambara bovu.’ Mtoto wako anapanda daladala, anakwenda dukani, anakwenda shuleni, anaingia mitandaoni anakutana na watu wengi wenye tabia tofauti huko. Kuna uwezakano wa kujifunza usiyoyataka kwa uhuru zaidi na kujinafasi bila wewe kufahamu.

Hapa ndipo Daktari mweusi wa Kimarekani wa kwanza kufanya operesheni ya kutenganisha watoto walioungana, Dk. Bern Carson kwenye kitabu chake cha ‘THINK BIG’ anatumbia: “Fanya uwezalo na yanayobakia mwachie Mungu.”

Mwanaharakati wa masuala ya kijamii na mwandishi wa Kimarekani, Frederick Douglas, anasema: “Ni rahisi sana kumtengeneza mtoto bora kuliko kumnyoosha mtoto aliyepinda.” Nafikiri anataka kufanana na Waswahili na msemo wao kuhusu muda wa kumkunja samaki. Wao wanasema usisubiri akauke, utamvunja.

0629500908

[email protected]

By Jamhuri