Tukio hili tunalitafsirije? (2)

Mifano hai ya waliopata ‘rustication’ ni kama hivi (sitawataja majina humu), mmoja alikuwa ni chifu kutoka Usukumani kule Shinyanga. Chifu huyu alitimuliwa Shinyanga akapelekwa kuishi Tunduru, mahali ambako alikuwa hajawahi kufika wakati ule wa ukoloni. Mwingine alikuwa wakili, Mhindi wa Songea, yeye alipelekwa Mpanda, Rukwa.  

Spika na maofisa wengine wakiingia bungeni kwa ajili ya kuendesha vikao. Wabunge wanatarajiwa kuchochea maendeleo kwa kupitisha mipango ya serikali.

Kuna Mpare mmoja kutoka Same, huyu alitupwa Mafia na kuna mtu wa Lindi yeye alihamishiwa kule Mkomazi, Tanga akaishi na Wasambaa.

Wazawa wote hao walikuwa na mawazo ya kuichafua serikali. Lakini baada ya kupewa adhabu ile ya ‘rustication’, watu walifyata mikia na kufunga kabisa midomo yao. Walikomeshwa na adhabu ile kali.

Labda baadhi ya wasomaji wanakumbuka adhabu hii kwa vile miaka ile ya 1990 kuna  Wakurya wa Mara, wezi sugu wa ng’ombe na waporaji sugu wa mifugo walisafirishwa kwa makundi tena kwa ndege kutoka Mwanza mpaka Mtwara na pale walisombwa kwa mabasi kupelekwa Tunduru. (sijui Tunduru serikali ilikuonaje siku zile!) Adhabu ile kali iliwakomesha wakorofi wote.

Bado ninajiuliza kuhusu tukio hili, kweli huyu askari wa Operesheni Miaka 50 kutoka Kambi la JKT Mgambo – Kabuku, Tanga amewezaje kulifanya? Lakini kwa vile jambo lenyewe limefikishwa katika Bunge kama hoja binafsi, na Spika wa Bunge kamwambia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kulifuatilia sina haja ya kulisemea zaidi. Kichwani mwangu bado nina sintofahamu kimetokea nini kwa Mheshimiwa Zitto Kabwe hata akatenda vile.

Nadhani wananchi bado wanakumbuka jina la Mheshimiwa Zitto Kabwe kuhusiana na yale mambo ya madini na kuhusu kuzuiwa kwa ile ndege yetu ya Bombadier Q400-8 kule Canada mwaka juzi.

Gazeti la Mwananchi la Agosti 19, 2017 lilimnukuu Kabwe akitamka kwamba yeye kama mpinzani wajibu wake ni kuibua hoja na kuiuliza serikali maswali na wajibu wa serikali ni kutoa majibu. Iliandikwa hivi: “Wajibu wangu huo nimetimiza. Nilimuuliza waziri mwenye dhamana (Profesa Makame Mbarawa) kuhusu suala hili kwenye mtandao wa Tweeter, lakini majibu yake yalikuwa finyu. Haya yanayoendelea sasa ni propaganda za kuchafua na sihitaji kujihusisha nazo…”

Mheshimiwa Zitto Kabwe alikuja kusikika tena mtandaoni lilipoibuka suala la Acacia Mining. Sasa kutokana na kule kuanzishwa kwa kampuni ya ushirika baina ya Barrick na serikali iitwayo TWIGA, nafikiri hili limewaumiza sana wapinga maendeleo wote katika nchi yetu. Sijui!  Lakini ni wazo moja wapo, au kuna wasiwasi wa huu Uchaguzi Mkuu ujao mwishoni mwa mwaka unaweza kusukuma watu kutenda mambo yasiyofikirika. Mtu mwenye uzalendo kweli asingeweza kutenda vile, sioni kabisa sababu za kutokea hili hapa nchini.

Inajulikana ulimwenguni kote kuwa upinzani ndiyo kichocheo cha kuipa serikali changamoto kimaendeleo. Kwa lugha ya wataalamu wa kemia kuna kitu wanaita ‘catalyst’ yaani ‘kichocheo’.

Mimi nimekuwa nikiamini kabisa kuwa upinzani katika siasa ni kichocheo cha maendeleo.  Lakini inavyoonekana hapa kwetu hasa katika Bunge letu kuwa badala ya kuchochea maendeleo, limezuka hili la kuzuia fedha za miradi ya hayo maendeleo. Kitendo hiki hakikubaliki katika mila na utamaduni wa Kiafrika na ndipo kinaonekana kuwa hatarishi. Kwa mtazamo huo, kinastahili kuitwa uhaini kwa taifa, sivyo?

Huko sasa hakuwi tena kutimiza ule wajibu kama upinzani hata kidogo. Hapo unageuka kuwa tendo la kubomoa hayo maendeleo tuliyokwisha kujijengea katika miaka yetu 58 ya kujitawala kwetu. Upinzani si uadui wala si mapambano, bali ni kichocheo cha maendeleo katika nchi. Kwa maana hiyo, njia za kuendesha upinzani ziwe njia halali, si za kuvurugana. Kuna usemi duniani kuwa: “The end never justifies the means.” Ukiwa na maana kuwa lengo halihalalishi njia zinazotumika. Hapo lengo likiwa haramu, basi na njia zitumikazo kulifikia nazo zinakuwa batili.

Hivyo basi, kwa vile lengo la upinzani ni kuisimamia serikali, basi njia zile za kuikosoa zitumikazo ziwe halali na zisizokuwa na alama za uchochezi wala uvunjifu wa amani mahalia.

Ni wanasiasa wangapi wanajua hilo? Inakuwaje kunatokea hali ya chama kuwa ya ubabe na kutunishiana misuli kama wapiganaji masumbwi vile miongoni mwa wanasiasa kati ya chama tawala na vyama vya upinzani? Tujisahihishe na tujirekebishe, maana nchi hii ni yetu sote, likiharibika jambo, basi sote tutaathirika, na wewe uliyelianzisha hautapona asilani! Kwa mtazamo wa namna hiyo, kiongozi wa NCCR-Mageuzi amekuwa akitamka daima kauli ya ‘maridhiano’.

Napenda nikubaliane na maneno au maandiko ya yule Baba Askofu Bagonza kwenye mtandao wake pale aliposema: “Kila penye mitume 12, ‘Yuda Iskariote’ lazima awepo. U-Yuda daima umo ndani ya kundi, wala si nje. Bila Yuda, utume ule mwisho wa siku ni bora huyu aliyeandika kuliko wanaofikiri kama yeye na hawaandiki na wamo ndani ya serikali…”

Kwa kuyapima tu maneno haya unaweza kuona wazi haya ni maneno mazito sana na yanatoa tahadhari muhimu kwetu sote angalau tujue tunao miongoni mwetu kina ‘Yuda Iskariote’ – watu wasaliti katika nchi.

Tuwe macho na wanoililia Tanzania kwa machozi ya mamba kumbe wanafurahia matatizo ya walala hoi wale waliowapigia kura kuwapeleka katika Bunge.

Bado Mhe. Zitto Kabwe haeleweki. Eti anasema: “…Hoja ya msingi hapa ni kwamba una serikali, ambayo inatumia matrilioni ya fedha kununua ndege wakati ni asilimia moja tu ya wananchi wanatumia…” Tazama JAMHURI toleo No. 437 la tarehe 11-17 Feb. 2020 uk. 3.

Hapo ndipo panashangaza. Hizi ndege si ndiyo ‘flag carriers’ za taifa letu? Tulikuwa hoi hapa nchini. Shirika limefufuliwa na hizi ndege ndizo zinatuingizia fedha za kigeni kupitia watalii. Je, hilo nalo Zitto Kabwe kweli halijui?

Kiwanja cha ndege kule Kigoma kilikuwa cha manyasi, leo hii kimetiwa lami hata Bombadier inatua. Hufurahii hilo? Hajapata kupanda hizi ndege kuja huku Dar? Au tuamini, mheshimiwa huwa anaruka kwa ungo? Kule Kigoma kuna Mbuga ya Wanyama ya Gombe, imejaa masokwe, watalii wanakwenda kwa urahisi sasa na hilo linamchukiza? Hapo kweli mheshimiwa haeleweki – “mtu kwao” – “dulce domum” (kwa Kilatini, ikimaanisha “nyumbani kuzuri”). Lakini yeye anachukia maendeleo haya ya kwao! Hapo ndipo nisemapo haeleweki!

Rais wetu Magufuli hachoki kutuomba Watanzania tumtangulize Mwenyezi Mungu katika kulitumikia taifa. Ipo Zaburi katika Biblia inasema hivi: “Bwana ni nuru yangu, na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu.” (Zab.  27, mstari wa 1). Kama Watanzania wote wa imani na itikadi mbalimbali tukimtanguliza Mungu, naamini tutaishi kwa amani.

Basi, ninahitimisha makala hii kwa kukumbuka kuwa Mungu aliumba nchi hii kwa neno lake tu na akatukabidhi sisi wanadamu tuitumie. Nchi haimaliziki kamwe daima ipo pale pale lakini sisi viumbe tuishio katika nchi ndio tunakuja (kwa kuzaliwa) na tunatoweka (kwa kifo).

Sasa tunapojitengenezea mazingira mazuri ya kuishi kwa njia nzuri kama kwa elimu bora, afya bora na kadhalika tunapata faraja ya kuishi duniani. Kumbe kuzuia fedha za maendeleo ni ulofa usio na kifano. Unamkomoa nani? ‘World Bank’ kuna Wazungu waliokwisha kuendelea wao wanatuangalia tu na wanatucheka. Ni kujidhalilisha.

Naomba sote kwa sauti moja kama wazalendo wenye uchungu wa maendeleo katika nchi yetu tulikemee tendo hili. Kwa mbunge yeyote kujifanya kibaraka wa nchi za Magharibi, ni kukubali utumwa na huko ndiko kufilisika kiuzalendo.

Mungu ibariki Tanzania. Dumisha uhuru na umoja wetu.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).