Umakini wa JAMHURI unapovuka mipaka ya nchi

Si jambo la kupendeza sana kwa mtu kujisifia au kuonekana unafagilia upande uliopo wewe, lakini pia sidhani kama ni kosa la jinai ukiamua kuonyesha yaliyo mema kwa upande wako. 

Ndiyo maana hata mimi ninaamua kuonyesha umakini wa Gazeti la JAMHURI niliouona siku chache zilizopita.

Si kwamba nilikuwa sijauona umakini huo kwa muda wote tangu gazeti hili liingie mitaani, isipokuwa ninataka niuonyeshe umakini niliouona kutoka kwa watu ambao hawawezi kuusema ila wanaufurahia. Na ukweli ni kwamba hawakatazwi kuusema, lakini walikuwa hawajapata mahali pa kuusemea, sasa wameuweka wazi kupitia kwangu.

Naam! Baada ya kufanya hivyo, nami nikaona nitakuwa sijawatendea haki wala kulitendea haki gazeti lenyewe kwa kukaa kimya bila kuueleza umakini huo.

Wakati fulani tulikuwa na warsha ya vyombo vya habari iliyoandaliwa na taasisi ya masuala ya kiuchumi ya Kenya, Inter Regional Economic Network (IREN KENYA) katika kuvifanya vyombo vya habari kuwafikishia wananchi habari za masuala ya kiuchumi, hasa yanayofanyiwa utafiti na taasisi hiyo.

Warsha hii ilifanyika mjini Bagamoyo ikiwa na washiriki kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini pamoja na wenyeji Tanzania.

Jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba upande wa wenyeji ndio uliokuwa na washiriki wachache kuliko wageni. Kwa mfano, wanahabari wa Kenya walikuwa kama 70, wakati Uganda walikuwa kama 60 na nchi nyingine walikuwa 20, pungufu sana watu 10 kwa kila nchi. Lakini Tanzania hatukuzidi watano.

Baada ya kuzoeana kuna waliokuwa na hamu ya kujifunza Kiswahili, hususan Wanyarwanda na Waganda. Niliwaambia kuwa kitu kilicho rahisi kujifunzia lugha ni kujitahidi kusoma maandishi yaliyo katika lugha husika.

Walitokea kama watu watatu, Waganda wawili na Mnyarwanda mmoja, ambao tumetokea kuwa marafiki zaidi kiasi cha Waganda hao kunikaribisha nyumbani kwao Kampala na yule Mnyarwanda kuja kunitembelea Dar.

Mnyarwanda aliyenitembelea Dar aliniomba nimzungushe kwenye baadhi ya vyombo vya habari na tukafanya hivyo. Tulipata nafasi ya kufika hata kwenye ofisi za Idara ya Habari – Maelezo, ambako alipata nafasi ya kuongea na wanahabari katika kubadilishana uzoefu.

Bahati mbaya kijana yule aliporudi kwao aliamuliwa kurudi Uganda, kwa madai kwamba ndiko kwao. Yeye ni Mnyarwanda aliyekulia na kusomea Uganda kama walivyo Wanyarwanda wengine wengi akiwemo hata rais wao.

Baada ya vuta – nikuvute akabahatika kupata  nchi ya kumpa hifadhi, Australia, ambako yupo mpaka sasa. Jambo la kushangaza ananimbia anavyosoma Gazeti la JAMHURI kupitia kwenye mtandao. Wakati mwingine ndiye anakuwa wa kwanza kuniambia kuwa nimeandika kitu fulani kwenye JAMHURI!

Fikiria mtu yuko Australia lakini ananishtua mimi niliye Tanzania kuwa kuna makala yangu imetoka kwenye gazeti wakati mimi hapa nyumbani nikiwa bado sijaiona, achilia mbali kuisoma!

Wakati huohuo rafiki zangu wa Uganda nao wananieleza namna wanavyolifuatilia gazeti hili bila kulikosa kila linapotoka, na wanalipongeza kwa kuwapandishia uelewa wao wa Kiswahili.

Nakumbuka hata baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani mara moja alitamka kuwa gazeti analoliona likifanya mambo kiumakini ni la JAMHURI. Lakini kwa kadiri ninavyoona, si Rais Magufuli peke yake anayeona hivyo, si ajabu marais wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaopendelea kusoma Kiswahili wanaona hivyo.

Maana rafiki yangu wa Uganda ameniambia kuwa Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo  ni mpenzi mkubwa wa maandishi ya Kiswahili na magazeti ya Tanzania anayasoma sana, kwa hiyo hata JAMHURI litakuwa miongoni mwa magazeti hayo.

Kitu kingine ni kwamba hata huku Bukoba Vijijini nimegundua kuwa JAMHURI linapendwa sana kuliko magazeti mengi ya kawaida, kwa sababu magazeti yanayopendelewa hasa na vijana ni magazeti ya michezo. Lakini wengi wakishayanunua hayo wanaongeza na JAMHURI. Nilipouliza kwa nini wanafanya hivyo, nikaambiwa kuwa gazeti  hilo ni darasa tosha!

Eti kuna mambo mengi wanayojifunza kwenye gazeti hilo. Kuna wakati rafiki yangu mmoja alinishawishi mpaka nikalazimika kumpigia Mhariri Mtendaji, Deodatus Balile, ili waweze kusalimiana. Nadhani Balile atakuwa bado anakumbuka tukio hilo, ingawa ni muda mrefu kidogo umepita.

Nimalizie kwa kusema kwamba umakini aliouona JPM kwa JAMHURI unazidi kujionyesha, kuandika bila uonevu wala upendeleo. Ni umakini, kama tulivyoona, uliovuka mipaka ya nchi.

Sina budi kulipongeza JAMHURI kwa umakini huo.

[email protected]

0654 031 701