Katika toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: “Unasemaje?’’ aliuliza Mama Noel kisha yule mlevi ambaye alikuwa mteja wake, akamjibu: “Niachie ya elfu mbili.’’ Mama Noel alimkubalia kwa kuwa siku zote mteja ni mfalme. “Haya mimi ninakwenda,’’ alisema mteja huyo huku akitembea kwa kuyumba.” Sasa endelea… 

Noel anapata umaarufu kupitia utangazaji 

Ni muda wa jioni Zawadi anarudi nyumbani kwao akiwa amebeba beseni lake la samaki lililokuwa limebaki tupu. Karibu samaki wote walikuwa wamekwisha na alichokuwa amebakiza ni madeni ya mtaani.

Zawadi alikuwa alitembea kichwa akiwa kainamisha chini, aliwaza namna ya kukuza biashara yake aliyokuwa akifanya. Zawadi alianza kuweka fikra zake katika biashara yake ndogo ambayo alikuwa nayo.

Akiwa njiani, Zawadi alimkuta mhubiri mkubwa kutoka nchi ya Marekani akiwa amesimama jukwaani akifundisha kuhusu kutokata tamaa. “Hatutakiwi kukata tamaa,  mtu anaye kata tama hufa mapema zaidi,’’ aliongea yule mhubiri. 

Zawadi akaamua kusimama na beseni lake alilokuwa amelibeba likiwa linatoa shombo la samaki “Maneno haya ni adimu sana kuyapata,’’ aliwaza moyoni mwake huku akiwa anatega masikio yake kuweza kusikiliza vizuri maneno yaliyokuwa yakitolewa na yule mhubiri. Mhubiri aliendelea kuongea akiwa amewalenga wale ambao walikuwa wakipitia katika mambo magumu na changamoto mbalimbali katika maisha.

Wakati Noel akiwa anapata umaarufu kupitia kazi yake ya utangazaji, mtaani watu ambao waliokuwa wakimdharau na kumuona hana thamani walikuwa wakimwangalia kwa muktadha mwingine. 

“Noel kawa mtangazaji,’’ alisema dada huyu ambaye alikuwa akipendwa kimapenzi na Noel lakini alimkatalia kutokana na umaskini aliokuwa nao. 

“Noel amekuwa maarufu sana,’’ waliongea kina dada hao ambao walikuwa wakiishi maisha ya juu. “Hivi Noel ametumia mbinu gani!’’ walibakia kushangaa na kujiuliza maswali mengi kiasi cha kukosa majibu.

Noel alibahatika kuchaguliwa kwenda kusoma chuo kikuu lakini alikosa mkopo kutoka bodi ya mikopo hivyo hakuweza kwenda chuo kikuu kwa wakati huo kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kumuda maisha na gharama za chuo kikuu.

Noel alikuwa anajua wazi kuwa yeye lazima aweze kupata mkopo na kuweza kusoma chuo kikuu, alijiaminisha kwa asilimia mia kwa mia.

“Ikiwa nilichaguliwa kwenda chuo kikuu kwanini mkopo nikose?’’ ndivyo alivyowaza katika akili yake kijana Noel. 

Alikuwa amewahi studio kama ilivyokuwa kawaida yake. Noel akiwa ofisini alipekuwa na kuangalia jina lake katika mtandao kama limetoka katika bodi ya mikopo, alihangaika kuweza kutafuta lakini hakuliona.

Mara Gilbeth akamtumia ujumbe katika simu ukisomeka: “Noel sijaliona jina lako.’’ Noel alizidi kuchanganyikiwa zaidi huku akijiuliza moyoni: “Sasa imekuwaje tena?’’ Akaamua kukaa mbali na tanakirishi yake kwa hasira na jaziba. 

Dada yake Gilbeth pamoja na ndugu wengine walikuwa wakifurahi pia walijua anakwenda kuwa msomi lakini walijua wazi kuwa suala la kumlipia ada kwao ndiyo limefikia ukomo.

Muda huu Gilbeth alikuwa na wazazi wake akiwa alishatoka kule mgodini baada ya maisha kumshinda. 

“Angalau aisee nilikuwa nikitaka kuuza mashamba,’’ alisema baba yake Gilbeth akiwa amekaa sebuleni na Gilbeth.

“Ukienda soma sana,’’ alisema mama yake. “Mama nitajituma kwa bidii,’’ aliongea kwa kuwahakikishia wazazi wake. “Na dini suala la msingi,’’ wazazi wake walizidi kumpa mawaidha kuhusu kile walichokuwa wakikisikia huko vyuoni ingawa walikuwa na elimu ndongo lakini walikuwa na ufahamu kuhusu mambo madogo madogo  ya huko vyuoni.

“Nitafuata kilicho nipeleka,’’ alisema Gilbeth huku akiwa anawatia moyo na faraja wazazi wake. “Fanya hivyo mwanangu utakuwa mtu wa maana sana,’’  Gilbeth aliwaaminisha kwa mambo mengi.

Furaha iliwatawala lakini ilikuwa tofauti kwa Noel, aliondoka mapema studio siku hiyo na kwenda katika eneo la ufukwe. Ulikuwa ufukwe wa Ziwa Victoria ili apunguze mawazo yaliyokuwa katika kichwa chake. Noel hakuwa mwenyewe, alikuwa na rafiki yake wa kike au mpenzi wake ambaye walianza naye mahusiano takriban mwezi mmoja tu.

Mapenzi yalianza kutokana tu na umaarufu wake wa kipindi cha redio alichokuwa akikifanya. Binti Tayana alikuwa msikilizaji mzuri wa kipindi cha Noel, walitafutana na mwanzo wa mapenzi ukawa umeanzia hapo kwa wawili hao. “Sitasoma chuo kikuu sasa,’’ alisema Noel akiwa anatembea na mpenzi wake Tayana katika ufukwe wa Ziwa Victoria.

“Utasoma tu maana wewe ni mtu maarufu lakini pia una akili,’’ alisema Tayana huku akiwa hataki kuona Noel akiwa katika msongo mkubwa wa mawazo kama ambavyo alikuwa. “Kitendo cha kuwa mtangazaji na hujawa mtaaluma ni mafanikio tosha,’’ aliendelea kuongea Tayana kwa lugha ya utaratibu huku mkono wake akiwa ameuegesha begani kwa Noel. Kwa kipindi cha mwezi mmoja Noel alikuwa ameridhika na mapenzi ya Tayana.

“Inaniuma sana mbona rafiki yangu Gilbeth kapata,’’ alisema Noel. “Usimwangalie yeye ni bahati yake,’’ alisema binti Tayana, ingawa mkurugenzi wa redio alikuwa amempa ahadi ya kumsomesha lakini Noel alionekana kutoridhika nayo. 

Yeye alikuwa akijua atasomeshwa na serikali yake, kushindwa kupata mkopo wa serikali na kufanya kazi redioni na kutolipwa kulimfanya Noel kuzidi kuwa katika wakati mgumu zaidi.

Baada ya Tayana kuweza kumpa maneno yenye faraja, Noel alipata furaha kisha akaamua kutulia na kumwambia: “Noel nikikwambia mimi waweza kulia,” alisema Tayana, maana yeye alikuwa na matatizo sawa na ya Noel. 

“Sawa nimekuelewa,’’ alisema Noel huku akiwa anaangalia chini kwakuinamisha kichwa chake. Kwa namna moja au nyingine, Tayana na Noel kihistoria walikuwa wanakaribia kufanana. “’Succes on my Mind’’, alitamka neno lake tena Noel huku anamuangalia Tayana usoni.

Tayana alitokea kuipenda kauli mbiu ya Noel kisha akamjibu: “Kama unapambana Yes, it can be in your mind.’’ 

Noel alikuwa amerudi katika hali yake ya kawaida ya mwanzoni kisha akamwambia: “Nitajitahidi kupambana na utangazaji utanitoa tu.’’ Tayana alimsikiliza kwa makini naye akamwambia: “Waza mawazo mazuri maana awazavyo mtu ndivyo itakavyokuwa.” 

Tayana alikuwa ni fundi mzuri wa kushona nguo. Aliamua kufanya ufundi kwa sababu alikosa ada ya kulipia chuoni nakujikita zaidi katika ujasiriamali, lengo likiwa ni kukusanya apate pesa za kurudi tena chuoni.

“Kijiweni kwako vipi?’’ aliuliza Noel. “Dah! Nasubiri oda zangu za maharusi,” alisema Tayana huku akiwa amemshika mkono Noel.

Ilikuwa ni muda wa usiku, Noel akiwa nyumbani anamuaga mama yake ili kurudi studioni. Noel alianza kufanya kazi yake kwa kujituma, alihurumiwa na kuanza kulipwa shilingi elfu tano. Walimlipa hivyo kwa sababu hakuwa mtaaluma katika fani ya utangazaji.

Noel alikuwa akiamka asubuhi mapema kuwahi studioni, usiku pia alikwenda kukesha studioni, ilikuwa si kazi nyepesi kwa kijana Noel kuweza kuacha usingizi wake na kwenda kukesha studioni.

Akiwa anafanya kazi ya kuandaa vipindi vingi redioni. “Mama narudi studioni,’’ alimwambia mama yake. “Leo mpaka usiku unakwenda?’’ alisema mama yake akiwa anamuonea huruma mwanae kwa kuwa na mazingira ya kufanya kazi mpaka usiku. “Inabidi iwe hivyo mama,’’ alisema Noel.

“Au ndiyo unatafuta pesa ya chuo?’’ alimuuliza mama yake Noel. “Ndilo ninalopigania mama,’’ alisema Noel huku suala la kukosa udhamini wa kusoma chuo kikuu akiwa amelitupia pembeni na kulisahau.

Kwa sasa alikuwa akiwaza kufanikiwa na kufanya mambo makubwa. “Uwe unatunza hela au bado hawakulipi bado?’’ aliuliza mama yake: “Wananilipa Sh 5,000.’’ Mama yake aliweza kumwambia kuwa ajitahidi kwani hakuna aliyeanzia juu. “Siku zote watu huanzia chini.” Maneno ya mama yake yaliweza kumpa faraja na hamasa. “Tunza elfu tatu, tumia shilingi elfu mbili,’’ aliendelea kumwambia na kumpa elimu ya maisha kwa ujumla.

Noel pamoja na kusoma kwake lakini alikuwa bado hajaweza kuwaza kile ambacho mama yake alikuwa akifikiria juu yake.

Akiwa anayafikiria maneno ya mama yake, mara wazo likamjia akilini mwake: “Haba na haba hujaza kibaba,’’ likawa limemuingia katika akili yake. Tena likamjia wazo jingine kuwa: “Siku zote kikubwa huanza na kidogo,’’ alijikuta akipata maneno mengi  papo kwa hapo, wazo lake la siku zote na kauli mbiu yake ikamjia akilini: “Oooh success is on my mind…success is on my mind’’ huku akijipigapiga kifuani kishujaa.

Ushauri wa mama yake aliuchukulia uzito na akaona ni zaidi ya vidato sita ambavyo alisoma “Mama umenifungua macho yangu,’’ aliongea huku akimpa mkono mama yake.

 “Tunza zitakusaidia,’’ alisema mama yake. Noel alijiona kama anasonga mbele  kutokana na mawazo aliyokuwa amepewa na mama yake. Mawazo ambayo Noel aliyaona ni ya kishujaa zaidi, Noel alirudi tena kumuaga mama yake na kisha akaondoka.

Mama Noel alimpa baraka na fanaka zote mwanae Noel katika kazi yake. Mama yake Noel alikuwa mhamasishaji mkubwa kwa Noel, ndugu pia walianza kuwa sehemu ya kuhamasisha kile alichokuwa akikifanya. Huku tumaini likiwa limemjaa Mama Noel alikuwa anajua mwanae atakwenda kuwa mtu mkubwa siku moja.

 Akiwa njiani alikutana na binti aliyekuwa amevaa nusu uchi, alikuwa amesimama barabarani. Walikuwa mabinti wengi wazuri, wengine walikuwa wazuri kwa macho. “Mmmh!’’ Kila mwanaume ambaye aliyekuwa akipita alimwangali yule binti na kutaka kuongea naye. 

Noel yeye alizidi kwenda mbele na mawazo yake alikuwa ameyahamishia studioni. Ghafla likapita gari mbele yake, lilikuwa limejaza watu wa jinsia ya kike. Wanawake hao pia walikuwa wamevaa nusu uchi. Dereva wa gari hilo pia alikuwa mwanamke, naye alikuwa amevaa sawa na wenzake. 

139 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!