David O. Oyedepo anatajwa kuwa ndiye mchungaji tajiri kuliko wote duniani. Ndiye mwanzilishi wa Kanisa la Winners Chapel International, kanisa ambalo linatajwa kumiliki jengo la kanisa kubwa kuliko yote duniani, likiingiza watu 50,400 kwa mara moja. Jengo hili Ota nje kidogo ya jiji la Lagos la Nigeria na ndiyo Makao Makuu ya Kanisa hilo duniani.

Mchungaji huyu pia anatajwa kumiliki ndege binafsi nne za kisasa. Kanisa lake linamiliki vyuo vikuu vitatu vikubwa na vya kisasa kuliko vyote vya binafsi nchini Nigeria, Covenant University, Crown University na Land Mark University. Wana hospitali, viwanda, shule za msingi na sekondari zinazofikia mia moja, vile vile wana mradi wa makazi (nyumba za kuishi) ambao ni mkubwa kuliko yote Afrika ukiwa unajenga nyumba laki moja na nusu kwa ajili ya waumini wake.

Mchungaji huyu ni mwandishi wa vitabu [vikiwemo vingi vya uchumi] na ameandika vitabu vinavyokaribia mia moja. Huwa nina utamaduni wa kusoma rekodi (biographies) za watu mbalimbali waliofanikiwa. Nilipokutana na habari za mchungaji huyu nilitaka kujifunza jambo moja kubwa kuhusu mafanikio yake.

Nilijiuliza, Je, ni nini anafanya cha ziada hadi amefikia mafanikio makubwa namna hii? Acha hayo mambo ya majengo na madege anayomiliki (ambayo wakosoaji wake wanaweza kuwa na mengi ya kusema) lakini [mimi nikiwa mwandishi wa makala na vitabu] nilitaka kugundua siri iliyomwezesha kuandika vitabu vingi namna hiyo na vyote vikiwa vinafanya vizuri sokoni.

Kuna mambo mengi nimejifunza kutoka kwake yaliyonithibitishia kuwa haiwezekani na haijatokea duniani pote mtu yeyote akafanikiwa kwa viwango vikubwa ama vidogo pasipo kuwepo na gharama aliyoilipia. Oyedepo analipa gharama nyingi lakini iliyonivutia na kunishangaza ni hii: mpaka sasa katika umri wa miaka 60 anafanya kazi kwa saa zisizopungua kumi na sita kila siku! Anasema ni jambo la kawaida sana kwake kutoka ofisini saa kumi alfajiri. Ameamua kulipa gharama ya kupunguza muda wa kulala ili kufanikisha majukumu, malengo na wito wake duniani.

Ukimuuliza kila mmoja wetu atakwambia anatamani mafanikio.  Mwanafunzi anatamani kufaulu, mfanyakazi anatamani kuwa na kipato kinachotosha, mfanyabiashara anatamani kupanua biashara zake kadiri iwezekanavyo na kuendelea kupata faida kubwa. Hata mimi Sanga natamani kuendelea kuandika makala na vitabu vyenye mvuto na msaada kwa watu wengi ninaowafikia.

Kukosa usingizi na kulazimika kusoma usiku kucha hiyo itakuwa ni gharama ambayo mwanafunzi atalazimika kuilipa ili aweze kufaulu. Kujinyima kunaweza kuwa gharama anayotakiwa kuilipa mfanyakazi ili mshahara wake usikate kabla ya tarehe nyingine ya mshahara. Kupunguza kuangalia TV ili niweze kusoma vitabu vingi zaidi, kufanya utafiti wa kina, kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi nikisamehe saa za kulala na kupumzika; hiyo itakuwa ni gharama ninayolazimika kuilipa ili niendelee kuandika makala na vitabu vyenye nguvu ya kusaidia na kuyabadilisha maisha ya wasomaji.

Ukweli ni kwamba chochote cha thamani maishani hakipatikani kwa njia ya mkato. Chochote unachokipata kiurahisi uwe na uhakika kwamba kitaondoka kwa namna hiyo hiyo iliyo rahisi. Usichokitolea jasho sio rahisi kukipa thamani. Na chochote usichokipatia thamani ni rahisi kukipoteza.

Kulipa gharama ingawa kuna wakati huambatana na maumivu na mateso lakini kuna maana kubwa katika kufanikiwa kwako. Jambo la kwanza kunakupa kuyathamini mafanikio unayoyapata. Jambo la pili linakusaidia kuyatunza mafanikio yako.

Kuna mambo mengi ambayo huwa yanasababisha watu wengi washindwe kabisa kulipa gharama. Adui namba moja wa mafanikio ya watu ni hadhi zao, (iwe amejipatia ama amepewa). Kwa kushikilia hadhi zao watu wengi huwa hawapo tayari kulipa gharama zinazostahili ili waweze kufanikiwa.

Mathalani; sehemu kubwa ya jamii na hata wasomi wenyewe wanaamini kuwa msomi ni “lazima” apate kazi za ofisini na kama ni kujiajiri basi inabidi awe na biashara kubwa zenye hadhi ya kuajiri wengine. Lakini sayansi ya mafanikio inatufundisha kuwa vikubwa huanza na vidogo. Hakuna aliye juu ambaye hakuanzia chini.

Kuanza na kidogo kunahitaji gharama ya uvumilivu, kuanzia chini maana yake utatakiwa ulipe gharama ya kusota. Sasa, wasomi wengi kwa sababu ya hadhi zao, wanakosa utayari wa kulipa gharama za kusota na kukubali kuvumilia. Hata kama akiambiwa biashara ya kuuza maji ina faida kubwa hawezi kuthubutu kuifuatilia kwa sababu anajiuliza swali baya sana katika mafanikio liitwalo, “Watanionaje?”

Jambo la pili ni kutokuwa tayari kujikana na kujizuia. Kimsingi katika hatua fulani ya maisha kama unataka kujikwamua ama kupiga hatua utalazimika kujizuia kwa mambo fulani. Kujizuia na kujikana kuna mantiki mbili. Mosi ni kuhakikisha unajibana kufanya jambo moja ili ufanikishe jambo fulani. Mathalani unaweza kuahirisha kula nyama kila siku badala yake ukageukia maharage. Gharama unazookoa ukazipeleka kwenye ujenzi.

Lakini pili kujizuia kunasaidia kuutiisha na kuuwajibisha mwili ili uwe katika mkao fulani wenye maamuzi na mifumo imara ya kukusaidia. Nitakupa mfano: wakati fulani nimewahi kuvaa mkanda mmoja tu wa suruali kwa mwaka mzima. Sio kwamba nilikuwa nayo mingine, la hasha! Ulikuwa ni huo huo pekee na niliamua kuwa sitanunua mkanda mwingine. Sio tu mkanda lakini wakati huo huo nilikua na pea moja tu ya kiatu, suruali mbili na mashati yasiyozidi matatu kwa karibu mwaka na ushee, nilikivaa kiatu hadi kikatoboka sore.

Sio kwamba sikuwa nikipata fedha ya kuweza kununua mkanda wa suruali ama kiatu, isipokuwa nilitaka kutengeneza mfumo wa fikra ambao utaniwezesha kuutiisha na sio matakwa ya mwili kunipelekesha. Mtu anaweza kuniona kana kwamba nilikuwa na ubahili ama maisha magumu yaliyopitiliza kwa kuamua kuvaa mkanda mmoja, kiatu pea moja na suruali mbili pekee mwaka mzima!

Ukweli ni kwamba kilichonisukuma kufanya hivyo yalikuwa ni majukumu. Wakati huo familia yetu ya kiyatima (baba yangu alishafariki kitambo) ilikuwa inapita katika wakati mgumu sana kiuchumi. Mimi nikiwa ndiye kaka mkubwa, nyuma yangu kulikuwa na rundo la wadogo zangu ambao walihitaji sio tu kusoma bali kuanzia chakula na kila kitu.

Mimi mwenyewe nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato cha sita kwanza nilikuwa katika mbinyo wa kujisomesha na wakati huo huo nilitakiwa kubeba majukumu mazito na makubwa ya kuiokoa familia. Katika hali kama hii kila senti niliyokuwa nikipata katika kufanya vibarua na kazi za hapa na pale ilikuwa kama lulu.

Ningekumbukaje kununua kiatu wakati kuna wadogo nyuma wanahitaji ada na kandambili kwa ajili ya shule? Ningepata wapi muda wa kukumbuka kwenda ‘shopping’ za nguo wakati hata chakula ni cha kubangaiza nyumbani. Leo hii nina wadogo waliofanikiwa kimasomo na wanayaendea vema maisha lakini nililipa gharama!

Nimekupa uzoefu wangu huo ili ubaini siri ya kukusaidia. Siri ni hii: Ili uwepo msukumo wa kulipa gharama kwa mafanikio ni lazima kuwepo na jambo la thamani mbele yako. Jambo la thamani unalipataje? Jambo la thamani unalipata katika maeneo mawili: majukumu na malengo!

Kwa kadiri unavyoyatambua na kuamua kuyabeba majukumu iwe ya kifamilia, kindoa, kijamii ama kikazi ndivyo utayari wako wa kulipa gharama unavyoongezeka. Kama huna majukumu yanayokukabili ni rahisi sana kuchezea fedha na ni rahisi mno kuchezea muda.

Pia kujiwekea malengo yanayokukereketa, yanayokujengea hamu kubwa kutakusaidia kulipa gharama inayohitajika kufikia malengo husika. Hapa nazungumzia yale malengo ambayo yanatanua uwezo wako na kukupeleka hatua ya mbele. Kama wewe ni mfanyakazi unayelipwa shilingi laki tano ama milioni moja kwa mwezi ile dakika unapoweka malengo ya kujenga nyumba ya milioni hamsini, utajikuta unaanza kulipa gharama ‘automatically’.

Huwezi kwenda baa na ukatumia laki nzima wakati mafundi wanahitaji sementi mifuko kumi. Kama wewe ni mwanamke huwezi kushinda madukani ukibadilisha viwalo vya malaki wakati saiti kunahitajika lori la mchanga. Bila shaka utajizuia dhidi ya matanuzi na starehe na kisha utaelekeza mshahara wako kwenye ujenzi. Huwezi kutumia mshahara wako wote katika ‘matanuzi’ halafu utarajie maendeleo, haiwezekani!

Amini nakwambia, suala la kufanikiwa halihitaji demokrasia, halihitaji usubiri kuungwa mkono na kila mtu. Kuna wakati utalazimika kulipa gharama ya kuwa mpweke kwa sababu hakuna wa kukusapoti katika mawazo yako lakini kwa ndani unaona kunachemka kutenda hilo jambo.

Kuna saa itakubidi ulipe gharama ya kubezwa kwa sababu wanaokuzunguka wanaona unachofanya hakiwezekani. Kuna muda pia itakulazimu ulipe gharama ya vikwazo na upinzani kutoka kwa washindani ama wanaokupinga kuhusu unalolifanya. Kuna wakati ili ufanikiwe ni lazima uwe kama “kichaa hivi”, upambane kama mwehu, usiangalie nyuma bali uangalie malengo yako.

Kama ambavyo vijana wa bodaboda wanasema, “Kuna vingi vya kuokota, lakini huwezi kuokota nyumba,” ndivyo nami ninavyokuthibitishia kwamba huwezi kuokota mafanikio yenye maana, bali kufanikiwa katika jambo lolote lenye thamani itakulazimu ulipe gharama, hakuna mkato kwa sababu mkato katika mafanikio hugeuka kuwa mzunguko na aibu!

2263 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!