Padre Dk Faustin Kamugisha

Kufanya kazi kwa bidii ni siri ya mafanikio. Kuchapa kazi ni siri ya mafanikio. Ndoto hazifanyi kazi mpaka uzifanyie kazi. Haitoshi kuwa na kipaji lazima kufanya kazi kwa bidii. “Kipaji bila kufanya kazi kwa bidii si kitu,”alisema Cristiano Ronaldo. Katika Kamusi ya Kiswahili neno “kazi” linatangulia neno “mafanikio.”  Si katika Kamusi ya Kiswahili hata katika ukweli wa maisha.

Andrew Carnegie, wa Marekani aliyejikita katika sekta ya viwanda alikuwa tajiri sana siku moja aliulizwa kipi muhimu kati ya vitu vitatu: kazi, akili, na mtaji. Kwa haraka alijibu, “Ni mguu upi muhimu kati ya miguu mitatu ya kiti kidogo au kigoda cha miguu mitatu?” Vyote vitatu ni muhimu: kazi, akili na mtaji. Louis Pasteur alipoambiwa na rafiki zake kuwa anafanya kazi kupita kiasi alisema, “Nahisi naiba kama ninaruhusu siku ipite bila kufanya kazi.”

Kuchapa kazi ili ufanikiwe hakuna mbadala. Mpiga jitaa alisema: pesa haitoki pepesi. Jitaa imeniunguza vidole. Wanaofanikiwa wanaiona kazi kama baraka ambao hawafanikiwi wanaiona kazi kama adhabu. Mchumia juani hulia kivulini. Mtu anayefanya kazi ngumu (juani) huishia kufurahia matunda ya kazi yake kwa raha –kivulini (kwenye mafanikio).

Mtaka cha uvunguni (mafanikio) sharti ainame (kuchapakazi.)  Katika mtazamo huu Wahaya wana methali isemayo: Zuri (mafanikio) lina gharama kubwa sana  – ‘akarungi kaseza’.  Kuna kitendawili cha Wahaya kisemacho: Limeiva, lakini liko miibani (jibu ni senene kwenye miiba).  Jambo zuri lazima kulifanyia kazi, lazima kulipigania ingawa unachomwa miiba.

Charlotte Chandler aliandika kitabu mwaka 1948 kinaitwa The Ultimate Seduction. Kinahusu mtazamo wa watu mashuhuri juu ya kazi. Unapomaliza kusoma kitabu hicho utagundua mambo makubwa mawili yanayozungumzwa. Kwanza, watu wengi mashuhuri walifanya kazi kwa bidii. Pili, motisha yao ya kufanya kazi haikuwa pesa. Motisha yao ilikuwa kuifanya ndoto yao iwe kweli na kuifanya dunia iwe mahali pazuri pa kukalika. Maono na ndoto ni motisha kubwa ya kufanya kazi. Katika mtazamo wa Charlotte Chandler Kwa watu wenye mafanikio makubwa kazi si jukumu bali shauku yaani unaifanya kwa shauku kubwa.

Kazi ifanyweje? Kwanza ni kupenda unachokifanya. “Njia pekee ya kufanya kazi kubwa ni kupenda unachokifanya,” alisema Steve Jobs. Kufanya kazi ambayo hauipendi kunaleta msongo wa mawazo. Kufanya kazi unayoipenda kuna shauku. Pili ni kuzishinda changamoto za kazini. Changamoto zinafanya maisha yavutie. Kuzishinda kunafanya maisha yawe na maana.

Tatu, fanya kazi kama kwamba utaishi milele. Sali kama kwamba utakufa kesho. Nne, fanya kazi kwa moyo wako wote. “Fanya kazi kana kwamba huitaji pesa. Penda kana kwamba hujawaji kuumizwa. Dansi kana kwamba hakuna anayekutazama,” alisema Satchel Paige. Tano, fanya kazi kwa namna ambayo kazi itakutambulisha. Baba yangu anaitwa “Shughuli.” Hili ni jina la utani. Anatambulishwa na kazi. “Fanya kazi kiasi kwamba hauhitaji kujitambulisha,” alisema Harvey Specter. Kazi ikutambulishe. Sita, unahitaji timu ya kufanya nayo kazi ambapo kuna kuaminiana.

Kazi ina changamoto zake. Kuna profesa aliyetembelewa na wanafunzi wake wa zamani. Walikua na wake zao au waume zao na watoto. Walimweleza wanavyopatwa na msongo wa mawazo kazini, pengine wanaona wenzao wana kazi nzuri kuzidi wao.

Aliwakaribisha kunywa kahawa. Ilikuwa imewekwa kwenye vikombe mbalimbali: vya rangi ya dhahabu, vya chuma, vya madini ya shaba, vya udongo kutaja aina chache. Walipigana vikumbo kuchukua vya rangi ya dhahabu.

Aliwaambia kuwa kama walivyopigana vikumbo kuchukua vikombe bya dhahabu hili ndilo linawaletea msongo wa mawazo hata kazini. Hoja si rangi ya kikombe bali kilichomo. Hoja si aina ya kazi au cheo bali kilichomo. Yote yakiishasemwa nasisitiza fanya kazi kwa bidii. Ingawa kufanya kazi kwa bidii hakukuhakishii mafanikio asilimia 100, kunakupa fursa ya mafanikio.

1380 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!